KISWAHILI KINA WENYEWE

Maisha ya Haji Gora: Msanii Atayedumu Milele

Moyo wangu una fakhari sana kwa Mola Mtukufu kuniwezesha kuwa ni mimi ambaye nimebahatika kuandika na kukamilisha kazi ya Maisha ya Haji Gora, msanii ambae ni alama ya Zanzibar.

Nilianza kumjua Haji Gora kipindi ambacho nyimbo zake zilianza kuimbwa katika Klabu ya Taarab ya Nadi Ikhwan Safaa. Vilevile nilipokuwa nafanyakazi Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI).

Wakati huo sikuwa nikijua kuwa bwana huyu, mbali na kuwa kwake hazina ya enzi, ana hazina kubwa. Na kipaji chake kikawa kinafunuka kila umri wake ulipokuwa unaongezeka, kwa shani yake Mola.

Kama anavyosema mwenyewe katika kitabu hiki kuwa alichelewa kugundulikana. Ingawa nyumbani kwao Tumbatu na kwa watu wa umri wake walioko mjini Unguja, Haji Gora alikuwa amefanya mengi katika fani ya ushairi kuanzia ngoma za kwao mpaka katika rubaa ya taarab.

gorafrontSifikirii kama atatokea mtu kumkamilisha Haji Gora maana ana sifa kama ya kitunguu. Kila ukitoa gamba, huzuka jengine jipya. Na ndiyo maana ninakiri kazi hii haiwakilishi kila alichokiandika, hata kidogo, isipokuwa ni sampuli tu inayoonesha kina cha hazina aliyonayo.

Watu wengi wamemtafiti na kumuandikia makala Haji Gora. Kazi zake nyingi zimechapishwa isipokuwa moja iliyokuwa ishazongwa sana na vumbi hadi nilipoigundua. Na hiyo sasa itakuwa kitabu kitachoitwa Moto wa Tumbatu. Aliandika mswada huu kiasi cha mwaka 1964 juu ya moto mkubwa uliotokea kijijini mwao.

Nilipojipa kazi ya kuuokoa mswada wa Moto wa Tumbatu na kuandika Maisha ya Haji Gora, kamwe sikufikiria suala la uchapishaji.  Kwa kweli nilisema madhali Mungu yupo, basi atatokea tu mtu wa kuchapisha.

Alhamdullilahi, bila ya kutarajia, Emerson’s Zanzibar Foundation (EZF); yaani Mfuko wa Emerson kwa manufaa ya Zanzibar, ukaamua kuchapisha kazi hii. Sasa nihangaike na moja ilobakia yaani ile ya Moto wa Tumbatu. Nilijisikia furaha iliyofanana na kimo cha kufikishwa mbingu ya saba.

Ilikuwa ni ndoto niliyokuwa nikiiota kila siku. Na dua niloomba kila wakati, kwamba kazi ya mshairi na gwiji huyu Haji Gora, mtunzi wa vitabu na mwanafalsafa zielezewe kwa jamii.  Ijuwe kuwa mwana wao mmoja amefikia kiasi hichi cha mafanikio bila ya kuingia katika mabanda ya skuli za kawaida.

Kwamba sio tu elimu ya dunia ndiyo yenye kuleta kila mafanikio, bali juhudi za mtu ndizo hasa zinazoleta kufikia pale wengine wasipotaraji kuwa wangefika. Lakini si vyema kuyaachia majaaliwa ya kupeleka mperampera, bali ni wajibu wako kuhakikisha kuwa kila mara unalenga kufika bandari yako ya mafanikio.

Nasema hayo kwa maana kuwa mtu akisoma kitabu hichi pamoja na kufurahi, pia atahuzunika kuhusu maisha ya mshairi huyu. Alianza kwa kazi ya kufanya tanu za chokaa na kuvunja kokoto; tena akaingia uvuvi na ubaharia na akamalizia kwa uchukuzi wa mizigo (upagazi).

Hakutunzwa kwa ujuzi wake wala hakukumbukwa kwa kipaji chake. Na ndani ya taifa hata hajatajwa katika wenye kustahiki tunza na heshima inayofanana na utukufu wa mchango wake katika Kiswahili kama lugha na Uswahili kama utamaduni.

Ndipo nikasema naona fakhari sana kuwa nimebahatika kuandika historia ya mbobezi huyu ili vizazi kwa vizazi vije vijuwe kuwa alikuwepo Haji Gora. Kwa kazi hii na kazi zake mwenyewe Haji Gora ataishi milele na milele.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.