KISWAHILI KINA WENYEWE

Machozi Yamenishiya: Msafiri Safarini

MSHAIRI NA DIWANI YAKE

Linapokuja suala la kutaja mafanikio ya mshairi fulani, inatubidi kwanza tulikabili suala gumu la ki-ontolojia: ‘shairi ni nini’? Kwa vile suala hili hukosa jibu mwafaka, mimi hulipa fasili rahisi tu – yaani shairi ni umbo la sanaa-lugha linalojitofautisha na maumbo mengine ya sanaa-lugha kwa jinsi linavyosikika likisomwa kimoyomoyo au kinywa kipana. Shairi kwa hivyo, huvutia kwa utamu wake kimasikizi au kimaandishi kwa namna maneno ya kawaida yalivyoteuliwa na kupangwa kujenga hisia na kutoa taathira ya kiujumi na ujumbe.

Kwa fasili hii, shairi huwa shairi tunapokutana nalo uso kwa macho au mdomo kwa sikio, bila ya kufikiria kanuni kandamizi zinazowekwa na washairi wenyewe au wahakiki wao. Tunapolisikia au kulisoma shairi na kulifahamu bila ya kuteswa na maneno au picha ngumu zinazochorwa ndani yake; tunapolifahamu bila ya kutoka jasho katika kupenya jazanda na ishara zake; tunapolikuta shairi katika bayana yake; pale linapotugusa na kutuingia kwanza kwenye hisia, na baadaye katika mbongo zetu kutukabidhi ujumbe au maana fulani. Shairi ambalo ni shairi kweli, hukupandisha madadi na kumwiinua msikilizaji au msomaji juu kwa ujumi wake kabla  ya kumpa ujumbe unaotolewa. Kwa maana nyingine shairi huathiri hisia za msikilizaji au msomaji kwanza, kabla halijaathiri akili yake.

Na Said A. Mohamed
Na Said A. Mohamed

Miaka kadhaa iliyopita, Mohammed Ghassani aliniletea mswada wake wa mashairi niupitie, niuhariri, niuandikie utangulizi na baadaye nimsaidie kuwashawishi watoa-vitabu kuuchapisha. Nilipoanza tu kulisoma shairi lake la mwanzo, nilijikuta nimetekwa kwa uchawi wa ujumi wake, hasa kwa namna anavyoyatumia na kuyapanga maneno kwa namna ya ajabu. Maneno rahisi tu, yenye kuibua utamu, hisia na tafkira wakati mmoja, utamu na tafkira inayomwingia mtu moyoni na akilini kwa nguvu kubwa za kisanaa. Sikiliza kwa mfano, ubeti mmoja wa shairi lake analoliita Nikupendavyo (uk. 2), linavyomkuna mtu akilisoma kimyakimya au kwa sauti:

Kwa sababu wanipenda, ndipo hakupenda vivyo
Sababu umeniganda, na ndivyo nikugandavyo
Na siku ya kukushinda, sitatenda vyenginevyo
Vyovyote nikupendavyo, sipendi usipopenda

Siri ya utamu wa ubeti huu imo, kama nilivyosema, kwenye jinsi maneno yanavyotumika; maneno ya kawaida, maneno yanayotumika katika maisha yetu ya kila siku, maneno yale kwa yale mshairi anayocheza nayo kimpangilio wa usambamba na uradidi, unaoleta pamoja visawe vinavyokamilishana, na vinyume vinavyotofautiana na visawe na vinavyotofautiana vyenyewe kwa vyenyewe. Mshairi anafanya hivyo ili kujenga taathira fulani kimuziki na kisha kusisitiza maana ya ukubalifu na ukinzanifu.

Vilevile, uchawi wa mashairi katika diwani hii, umo katika kutumia ‘neno moja’ lilelile linalobadilishwa maumbo na maumbile yake tofauti, yenye msisitizo uleule, ingawa una mkengeuko katika ukamilishaji wa maana inayotakiwa kujengwa: wanipenda inapofuataishwa na hakupenda au umeniganda inakaambishwa kuwa nikugandavyo; kisha kinyume cha maneno haya: “Na siku yakikushinda” (yaani mapenzi), “Sitatenda vyenginevyo (yaani na yeye mshairi hatafanya vingine ila kushindwa na mapenzi).

Na mwisho, kinyume cha mambo  kinatochotoa ‘shuruti’, ‘pindipo’ na ‘iwapo’, ambapo ‘shuruti’, ‘pindipo’ na ‘iwapo’ zikivunjwa, basi matokeo ni kinyume cha mambo, kama asemavyo Mohammed Ghassani (Vyovyote nikupendavyo, sipendi ‘siponipenda). Msisitizo huu unakubaliana na ukweli wa mambo, maana ‘mapenzi’ hutarajiwa kulipwa kwa ‘mapenzi’, ingawa, kama wasemavyo Waswahili, ‘mapenzi’ huwa na ‘kuwiza’ (kuchukia) pia.

Mbali na hayo, kuna usambamba unaosimamia mlinganisho na mkinzano, kwa upande mmoja, na urari wa sauti {–nda} na {–vyo} kwa upande mwingine. Mizani hii ya usambamba inajenga taathira kubwa ya kimuziki huku ikitilia mkazo ukweli na matarajio ya ujumbe wenyewe katika  ubeti huu wa shairi la Mohammed Ghassani.

Baada ya kwisha kusoma kimyakimya shairi hili la mwanzo, sikuweza kujizuia. Nilijikuta nafululiza kuusoma mswada mzima, huku nimejaa hamu ya kuendelea, nikiongozwa na utamu wa kila shairi nililolisogelea. Na bila shaka, chambilecho wa kwetu, kila shairi lilimwambia mwenzake sogea huko kwa ufundi, utamu na tafkira zilizojaa.

Kusema kweli, sikuwa na haja ya upekuzi mkubwa. Tangu hapo nikagundua kuwa nimekutana na mshairi chipukizi gwiji, mwenye kipawa kikubwa chenye mwangwi wa kazi za washairi maarufu wa Kiswahili. Kazi za akina Muyaka bin Haji Al-Ghassany, Abdilatif Abdalla,  Ahmad Nassir wa Mvita, na akina Kamange na Sarahani wa Pemba7. Nilipokuwa, nikisoma mashairi hayo, nilihisi, kwa utani tu, nimwite Mohammed Ghassani ‘kinyinginy’a’ cha Muyaka bin Haji Al-Ghassany, na isingelikuwa ajabu maana wote wawili wana asili moja ya  Al-Ghassany.

Lakini kwa kufanya hivyo, labda yeye mwenyewe Mohammed Ghassani na akina Kamange na Sarahani wenye asili ya Pemba, wangeniteta kwamba nimeisaliti hadhi ya ushairi wa Pemba kwa kumhusisha Mohammed Ghassani wa Pemba na Muyaka bin Haji Al-Ghassany wa Mvita. Mohammed Ghassani ni Mpemba ‘fyoko’, anayejinasibu na u-Pemba wake, kwa hivyo Kamange, Sarahani na Wapemba wengine wangedai hadhi kivyao, ingawa wakati ule wa akina Kamange na Sarahani, Pemba na Mvita zilikuwa kitu kimoja na pua na mdomo zaidi kuliko leo. Zilikuwa zikiogelea bahari moja karibu karibu, na utambi wa mbari na kabila mara nyingi ulikuwa uleule ingawa taa mbili zilimulika kwa mianga tofauti katika maeneo mbalimbali. Ukaribu wa Pemba na Mvita wakati ule ulikuwa wa kiasi cha kupigiana kelele tu: ”Ohaaa, nakuja.” Na ndu wa Mvita kujibu: ”Ndoo akhi.” Nina hakika Mohammed Ghassani atadai ‘uvyake’ au, kwa uchache, atadai mwangwi wa ki-Pemba kwanza kabla wa ki-Mvita.

‘Tatizo kubwa’ la mashairi haya ya Mohammed Ghassani ni kwamba mengi yao ni yale yaliyojaa msisimko wa kisiasa wenye mielekeo mbalimbali: yenye kuomboleza mateso na maumivu, yenye kuvukuta hamasa za kina cha ndani kabisa za mshairi, hamasa ambazo hatimaye anazitoa nje ili wengine wazisikie, hamasa zenye mchemko wa potelea-mbali kwa nia ya kuufedhehi ukandamizaji, uonevu na uvunjaji wa haki za kibinadamu – ‘potelea mbali’ ambayo  mtu angeweza kusema ina mwangwi wa uzalendo wa akina Muyaka bin Haji Al-Ghassany na Abdilatif Abdalla.

Nimetumia maneno ‘tatizo kubwa’ hapo juu, kwa sababu si rahisi kwa mshairi mtetea haki ya nafsi yake, na haki ya wananchi wenzake, kuweka uzani wa mazungumzo pande mbili (dialogue) baina ya sanaa na mateso, sanaa na maumivu, sanaa na siasa (Dawes 1997:12). Mara zote sanaa humkaba mshairi abaki katika ulingo fulani, kwani akitoka nje ya ulingo huo, kazi yake itakuwa chapwa au isiyohimili maweko au mabadiliko ya muda mrefu. Kwa bahati mbaya lakini, mateso, maumivu na siasa ni mambo yaliyojaa uchochezi mkali unaomsukuma mshairi kuzungumza waziwazi na kinagaubaga na hatimaye kumfanya mwandishi apandwe na jazba zinazofanya kazi fulani itoke nje ya kingo za ulingo wa kisanaa.

Katika hali kama hii mshairi lazima atunge wimbo unaoimbika ndani ya nafsi yake mwenyewe kwanza, wimbo utakaomwezesha kunyanyuka kitandani asubuhi huku akijua hayuko pweke, ana wenzake wenye maumivu kama au kuliko yake, wimbo utaomfanya mshairi autambue kuwa ni dawa ya kuondosha kiasi cha maumivu, si yote, ingawa kwa muda mchache tu. Kama asemavyo Dawes (13-14):

[…] uzuri wa muziki (‘au ushairi’: msisitizo wangu), ukikugonga huhisi maumivu. Si muhimu kwetu nini muziki hutufunza, muhimu ni kile kinachojazwa nyoyoni mwetu na muziki, na vipi (muziki) unavyoweza kutugusa kwa namna ambayo inaweza kuelezewa tu kwa uzuri na ufundi wa kutumia maneno.

Mohammed Ghassani ana weledi huu wa kubaki ndani ya kingo za ulingo wa kisanaa, weledi wa kuichenga siasa kwa namna ya kuipa nguvu kubwa zinazoficha na kuzimua unagaubaga na hata ukali wake. Sikiliza Mohammed Ghassani anavyoombeleza kisiasa maumivu yake. Mwanzo kama kwamba mtu kafikwa na maafa ya kawaida na kumbe nyuma ya maneno yake kuna uzito mkubwa wa kisiasa. Na kisha, ukiigundua siasa iliyomo ndani ya maneno yake, usije ukasema hii ni siasa inayomwathiri mtu binafsi tu, la. Mara moja utagundua kwamba Mohammed Ghassani halii wala haombolezi peke yake anaposema katika shairi lake Machozi Yamenishiya (uk. 1):

Ni mimi mwana kuliya, ni mlizi tangu hapo
Tangu hapo naso’neya, kamwe sijanyamazapo
Hata hisita tiki’ya, hufanywa nisisitepo
Sasa machozi hayapo, na sauti ‘shafuiya

Kwa kusoma ubeti mmoja, msomaji anaweza kuona kwamba shairi la Mohammed Ghassani linakosa ushujaa wa kisiasa na kivita, lakini lisome hadi mwisho, utaukuta mwingi wa ujabari na uteto wa mshairi huyu:

Japo chozi ‘menishiya, wanilizao wa papo
Hawaachi nifanyiya, mdomo usifumbepo
Basi ninawaapiya, kamwe tena sililipo
Lakini sisahaupo, lazima watafidiya

Ingawa dhamira ya uzalendo na siasa ndiyo inayotawala katika diwani yake hii Mohammed Ghassani anaonekana pia kujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha ya mwanadamu kama vile ‘mapenzi’ na ‘unyumba’ (Nikupendavyo; uk. 2, Siwati uk. 10), ‘mkabala wa mtu na mtu’ hasa juu ya wema na ubaya (Akianza Umalize; uk. 3), na ‘nasaha kwa wenzi’ (Akhlaki; uk. 17). Labda si ajabu hata kwa washairi wawili wanaotengana mno kiwakati, kutunga mashairi ya mapenzi, na unyumba kwani dhamira hizi zimo ndani ya ubinadamu wetu. Lilo ajabu ni namna gani tungo zenyewe zinavyoathiri namna moja kwa uteuzi na mpangilio wa maneno tofauti unaogonga vyema kwenye sikio letu na nje na la ndani.

Katika shairi la Muyaka bin Haji Al Ghassany Ndia Haimeli Mani (64) na Mohammed Ghassani Bila ya Wewe (uk. 23), kuna tofauti ya usanii na ujumi ndiyo, lakini hatimaye taathira ya utamu na ujumbe ni ileile. Muyaka, yumo kubembeleza kupata, wakati Mohammed, yumo kubembeleza kubaki na mapenzi aliyokwishapewa. Kimaana tofauti ipo ndogo tu kati yao. Kwa maneno mengine wanakokwenda washairi hawa ni kwahala kulekule kumoja, lakini njia wanazopita ni tofauti. Wote wawili kwa mfano, wanazungumza moja kwa moja na wandani wao; lakini Muyaka anatuonyesha usumbufu wa kuandama njia bila ya kusita au kuchoka, na ndani ya msisitizo huu tunakutana na ajabu ya mapenzi kwa anayependa – yaani Muyaka bin Haji Al Ghassany. Na kuhusu Mohammed Ghassani, yeye anasisitiza uchapwa wa kutokuwa pamoja na mwandani na uchangamfu wa kuwa naye kama chanda na pete. Ndani ya hali hizi mbili, kuna dhiki na raha ya maisha ya duniani. Hebu tudondoe beti mbilimbili ili kuimarisha madai yetu. Kwanza tumfuate Muyaka ndani ya kiguu na njia chake kwenye Ndia Haimeli Mani:

Sengekuja, sengekuja, asubuhi na jioni
Kwamba mimi sina huja, kwako mbeja wa shani
Nikidhia yangu haja, unitowe mashakani
Ndia haimeli mani, na nijialo ni wewe!

Laiti! Kwamba wajua,  lililo mwangu moyoni
Usingelinisumbua, mwandani wangu mwandani
Apendaye hana dawa, mwenyi kupenda haoni
Ndia haimeli mani, na nijialo ni wewe!

Kisha tumsikilize Mohammed Ghassani pachapacha na mwandani wake kwenye Bila ya Wewe:

Bila ya wewe, ni chapwa duniya, haina thamani
Bila ya wewe, maisha huviya, nisiyatamani
Bila ya wewe, nyota hukimbiya, hawa sizioni
Bila ya wewe, hunitumbukiya, huzuni moyoni

Nikiwa nawe, anga hutuliya, likatamakani
Nikiwa nawe, mwezi husogeya, ‘kawa viganjani
Nikiwa nawe, ndege hutwimbiya, nyimbo za kughani
Mimi na wewe, tukawasikiya, kama tu peponi               

Pia, katika dhamira hii hii ya mapenzi na unyumba, washairi hawa wana mlingano mmoja wa taathira na matokeo ya utunzi unaozungumzia utiifu wa mapenzi ingawa kwa njia mbili tofauti. Katika Naradhiwa Kufa Naye (93-94), Muyaka bin Haji Al-Ghassany anatuchorea upeo wa utiifu kwa kuwakana wale wanaotaka aachane na mwandani wake; na katika Omba Chengine (uk. 27), Mohammed Ghassani anamkatisha tamaa yule anayetaka kuchukua nafasi ya mwandani wake, wakati huo huo akisisitiza dhati ya: Simuwati. Mgandamo wa Mohammed Ghassani na mwanadani wake umo katika kumwambia mtu mwingine kwamba yuko tayari kumpa chochote kile anachoomba, lakini vitu vingine havigaiwi – vitu kama mapenzi ya mwandani hayawezi kuombwa hasa mtu mwaminifu kwa mwandani wake. Huyu hapa Mohammed Ghassani hafichami maneno yake katika Omba Chingine:

Omba haja niombwayo, nitakuridhiya
Nitaikidhi hajayo, sitakuringiya
‘Siniombe haja siyo, ‘takuwa mbaya
Hilo sitakuridhiya

Nambie niambiwacho, nitakusikiya
‘Tasikiza usemacho, ‘takuitikiya
‘Sinambiye kitu sicho, nisichozoweya
Hilo sitakusikiya

Mfanano wa shairi hili la Omba Chengine la Mohammed na Naradhiwa Kufa Naye la Muyaka umo katika msisitizo wa usuhuba na mapenzi ya kufa na kupona. Mtu akikwambia Omba Chengine maana alivyoomba zamani ameshapewa, na pana nini chingine kilichoombwa kama si muhali wa kutoa mapenzi?

Omba Chengine maana yake ni kuhakikisha kwamba aliyeomba atapewa, ingawa hapa Muhammed Ghassani anatoa shuruti kwamba ama “…’Siniombe haja siyo, ‘takuwa mbayaHilo sitaridhiya”, “…’Sinambiye kitu sicho, nisichozoweyaHilo sitakusikiya”, “…’Sinitume kwenda siko, n’nakochukiya…Huko nitakukimbiya”, “…Nisicho uwezo nacho, vyema kukweleyaKwamba sitagaiya”.

Mohammed Ghassani anaweka mipaka katika mapenzi yake. Anatoa fasili na maana ya mapenzi anayoijua yeye, fasili na maana ya kutoa mapenzi au kitu chochote chingine kwa mwanadani wake, chochote ambacho kina kadiri kwa mtoaji, vinginevyo inakuwa kutoa inakuwa muhali.

Kwa Muyaka tafsiri ya mapenzi ni ya aina nyingine, kama ilivyo namna ya kuyachora mapenzi hayo katika wito wa shairi ambamo anawataka wale wanaomhimiza amwache muwatiwa wake.: Yeye anawakatisha tamaa na kuwaambia wasahau kabisa jambo hilo, maana yeye yuko tayari kukikabili kifo kuliko kumwacha muwatiwa wake. Tumsikilize Muyaka anavyokuja kinagaubaga, hana kificho katika kuweka wazi mapenzi yake na maana ya mapenzi yake katika shairi hili la Naridhawa Kufa Naye! (93-94):

Tautekeleza uwe, wasia nalousiwa
Viumbe vyote vijuwe, mzidi kufunukiwa
Wenye maninga muvuwe, muone kutoonewa
Simuwati, muwatiwa, naradhiwa kufa naye!

Tamuataje ni wangu, mikononi nimepawa
Anagnikusa matungu, kwa hivyo ‘tamtukuwa
Mambo Mtenzi ni Mungu, Muumba mwezi na juwa
Simuwati, muwatiwa, naradhiwa kufa naye!

Simuwati, hawatiki, bali atakavyokuwa
Nimuwene halichiki, halichwa kwa kulichiwa
Hata kama hanitaki, si mwenye kuliya ngowa
Simuwati, muwatiwa, naridhawa kufa naye!

Katika Naradhiwa Kufa Naye, Muyaka anapofua macho na kusema na moyo wake ukubali mapenzi kwa hali yoyote ile hata kama kuchagua kifo! Ingawa haianishwi kwenye shairi lenyewe, lakini mtu akisoma baina ya mistari anakuta kwamba Muyaka yuko tayari kuomba na kutoa kila aombwacho, hata roho yake, mradi tu aliyeomba ni muwatiwa wake. Hapa pia mapenzi ya dhati yanaelezewa kwa namna yake, lakini yapo dhahiri. Hapana anayeweza kumshuku Muyaka kupenda, tena mapenzi ya ajabu, mapenzi ya kuchagua kufa pindi suala likiwa ‘kumwata muwatiwa.’

Na hili bila ya shaka ni lile lile suala la kutangamana na mwenzi au mwandani lililosisitizwa na Mohammed kwa njia nyingine kabisa, lakini katika ugo uleule wa mapenzi ya kuridhishana. Isipokuwa tu, fasili na maana ya mapenzi kwa Muyaka, kinyume na Mohammed, ni kujua dosari ya unayempenda na bado uko tayari kumstahamilia “Hata kama hanitaki, si mwenye kuliya ngowa.” Haya hutokea, kwani ndiyo kibinadamu. Waliimba watiribu wa Ikhwan Swafaa huko Unguja: “Ishallah yatamfika, Apende us’omtaka, Nimwone anicheke.”

Tukija upande wa siasa, ushujaa wa washairi hawa wawili wanaotengana kwa mwanya mkubwa kiwakati unajionyesha si katika maneno tu wanaoyatumia kujinasibu na kujigamba katika mashairi yao, bali katika kutoogopa kuthubutu kusema kweli mbele ya watawala wao wakali wenye vitisho vikubwa kwa wale wasiozifyata ndimi zao. Kwa mara nyingine tena tunawakuta washairi hawa wanazungumzia mada moja ileile katika mitazamo tofauti. Muyaka yeye hamwelekezi mtu yeyote moja kwa moja bali anajinasibu na kujigamba kinywa kipana ili kila adui yake amsikie. Huyu hapa Muyaka katika Simba wa Maji (59-60):

Ndimi tazo nembetele,  majini ndimi mbuaji
Nishikapo nishikile, nyama ndimi mshikaji
Ndipo nami wasinile, nimewashinda walaji
Kiwiji, simba wa maji, msonijua juani!

Maji yakijaa tele, huandama maleleji
Pepo za nyuma na mbele, hawinda wangu windaji
Huzamia maji male, male yasofika mbiji
Kiwiji, simba wa maji, msonijua juani!

Nawiapo mawindoni, nenda kama mwenendaji
Nisi hamu na huzuni, sitishwi ni watishaji
Welevu siwezekani, kutenepo na wambuji
Kiwiji simba wa maji, msonijia juani!

Shani yangu ya urembo, nipeweo ni Mpaji
Sina tua wala kombo, hiwa na wangu wandaji
Ndimi muolesha sambo, na kuzua maji mbiji
Kiwaji simba wa maji, msonijua juani

Mohammed Ghassani yeye anajinasibu na kujigamba kwa namna yake. Moja ya namna yake ni vile kujanasibisha kwa nguvu za wingi, ingawa ni yeye tu anayemkabili mteta wake mkali na katili. Kwa maneno mengine Mohammed Ghassani anatumia kiwakilishi cha wingi ili kuwashirikisha wenyeji wenzake dhidi na mgeni waliyempa nguvu za kutawala wao wenyewe. Kwa maneno mengine majigambo ya Mohammed hayako wazi, kwa upande mmoja yanasikika kama masimango na kwa upande mwingine yanabeba ujasiri unaomshutu kiongozi wa juu kabisa katika jamii yake, na kwa hivyo kujenga sifa ya majigambo ya ndani kwa ndani mwa shairi lenyewe.  Tumsikilize Mohammed asiyetaka kuyatafunia maneno yake anapohoji Hukumbuki Ihisani? (uk. 4):

Wiji
hapa u mgeni, tukakupa uwenyeji
Wiji hata huna dini, leo hii Al Haji
Kushasahau zamani, sasa u mtukanaji?
Lau fadhila haiji, basi hata ihisani?

Wiji hapa ujusini, kinyaa kitujituji
Ukishii mapajani, nasi ‘kikutia maji
Leo wenda mnadani, wazinga mnunuaji
Hujijuwi u mjaji, wauza kunarithini?

Wekuja huna hunani, sisi ‘kakupa malaji
Wiji hapa masikini, nasi ‘kakupa mtaji
Wekuja u msibani, wewe tukakufariji
Huo ndio ulipaji, wenyeji kutufitini?

Tulikutia jandoni, mke tukakuziwaji
Na neemaze Manani, zija kwako kama maji
Tukakupa usukani, tukakuvika na taji
Leo watusi wenyeji, jaza hii jaza gani?

Kwa kuwa u mtu duni, ha’ko alokuhitaji
Sisi tukakuani, kwa chakula na kwa maji
Tena tukakuthamini, tukakukabidhi mji
Na leo siye wenyeji, watutia utumwani?

Mjinga wa ihisani, mwerevu wa ukopaji
Umesahau zamani, hukumbuki kichwamaji
Hujijuwi sasa nani, kushajifanya mwenyeji
Wewe mkando wa Mbiji, ‘sijigeze hufanani

Ewe mkosa imani, jua tunalokuhoji
Hatukuhoji madeni, twajuwa hu mlipaji
Twakuhoji ihisani, walau ukumbukaji
Fadhila hatuhitaji, bali kumbuka hisani

Tunaweza kuzungumzia pasi na ukomo juu ya mshabihiano, dhamira na mitindo kati ya Mohammed Ghassani na malenga wengine wa Uswahilini kama Muyaka bin Haji Al-Ghassany, Ahamad Nassir Juma Bhalo na Abdilatif Abdalla. Hata hivyo, Mohammed Ghassani anajipambanua kiasi kikubwa kwa uyeye wake katika utungaji na umalenga wa ushairi.

Moja ya sifa kubwa ya mashairi yake ni ile mbinu ya kumchezea msomaji kudhani kwamba shairi linaelekea kuzungumzia hili, kumbe linazungumzia jambo jingine kabisa – na pia upana wa ulinganifu baina kilichodhaniwa kinazungumziwa mwanzo na kile ambacho msomaji anakigundua hatimaye ni chenye mwanya mpana mno kimaana. Mbinu hii imedharauliwa sana katika utunzi na uhakiki wa maishairi ya Kiswahili, ingawa ni mbinu muhimu sana inayofanya shairi liwe shairi katika fasihi za wenzetu, na wala si vina na mizani tu. Hii ina maana kuwa, kwa sababu tumeegemea mno na kutilia mkazo vina na mizani katika ushairi wa Kiswahili, basi tumeishia kudhani kwamba iwapo kuna urari wa mizani na vina, shairi limekamilika.

Tazama natija ya mbinu hii, pale Mohammed anapocheza na akili zetu katika shairi la N’kitakacho N’chicho (uk. 12), linalotupelekea kudhani kwamba akitakacho mshairi ni mapenzi au mwili wa mwanammke, kumbe sivyo kabisa. Kumbe anayoitaka ni ‘haki’:

Waniu’za n’takacho, amba usiyekijuwa
Kunakishika unacho, kitu hicho wakigawa
Basi sasa kuwa macho, ku’ kwamba nishaamuwa
Si  jambo kubwa la kuwa, chenyewe n’kitakacho

Sikuombi kitu sicho, sicho unachokitowa
Mimi kwako nizingacho, si wa mwanzo kukipewa
Nakuomba uombwacho, ukakubali kigawa
Nipa kama wanopewa, uwapao kitu hicho

Ni hicho ugaiacho, watu wakabarikiwa
Ni hicho si chenginecho, nihitajicho kupewa
Nadai udaiwacho, na mwenyewe ukatowa
Wala sitakusumbuwa, unipapo kitu hicho

Si kigeni niombacho, na ombi langu ni sawa
Ni kitu ukigawacho, kwa wenzangu kikatwawa
Na bado ungalinacho, wendapo wakichukuwa
Jinalo sijachafuwa, kwa hichi nikuombacho

‘Sininyime kitu hicho, ndicho mie cha kupewa
Nipa ninogewe nacho, kama wanaonogewa
Madhali wale wanacho, nawe ndiye ‘liyegawa
Nami nataka ‘megewa, kitu hicho niwe nacho

Zaidi ya kitu hicho, zaidi ya unotowa
Nikitakacho sinacho, kwako cha kukichukuwa
Lakini nihitajicho, ni haki yangu kupewa
Walonacho nami sawa, vije nami ‘siwe nacho?

Au tazama Mohammed anavyotupeleka kwenye mitindo wa dansi (bluzi), mtindo wa dansi ya kigeni katika shairi lake Kivyetuvyetu (uk. 17), na jinsi ambavyo baadaye kufumbukiwa na fikra kwamba si bluzi anayoizungumzia bali ni uchaguzi ambao pia una uasili wa kigeni kwetu:

Bluzi ina wenyewe, Ging’ingi si ngoma yetu
Nasi tukitaka iwe, bluzi ichezwe patu
Yatubidi tuamuwe, natuwe kama wenzetu
Isiwe kivyetuvyetu, kwa kutaka tuambiwe

Hivi sasa tuchezavyo, ni kivyetu peke yetu
Bluzi twacheza sivyo, ichezwavyo kwa wenzetu
Inachezwa vyenginevyo, tofauti na vya kwetu
Tukiyataka ya watu, tutake na yafanywayo

Bluzi haina shambi, za kuteuwana watu
Wala  haina ukumbi, maneno kama upatu
Haichezwi kwenye kambi, kukanyagana viatu
Bluzi raha  ya watu, huchezwa panye ukumbi

Wala haichezwi peke, yachezwa mtu na mtu
Haichezwi kwa makeke, au kakatukakatu!
Ina taratibu zake, zisizo hizi za petu
Yetu siye ni papatu, bluzi si jila lake

Bluzi tuipigavyo, twapiga kama wenzetu
Lakini tuichezavyo, tunaicheza kikwetu
Tusikiye tufokavyo, makali maneno yetu
Twataka mambo ya watu, ambayo hatuyawezi

Neno hili narudia, bluzi si ngoma yetu
Yetu siye ni kumbwaya, mkobele mwana kwetu
Ikiwa tumeridhiya, ngoma hii hapa petu
Tucheze kama wenzetu, tucheze vinofalia

Akiwa fanani aliyepevuka tayari, Mohammed Ghassani anafahamu sana umuhimu wa upya katika fani ya kazi yoyote ile ya kisanaa. Mbali na uteuzi wa maneno na jinsi maneno yanavyopewa upya kimaana, kiumbo na jinsi yanavyoonekana kiumbile, mashairi yake kadha yana mkengeuko mpya kama ule  wa mikeketo mitatu <—–na          —–pa —–ka>,  yenye vibwagizo vya mwanzo wa kila ubeti (kama katika Mbona?; uk. 8, Hatari Tupu; uk. 33 na Siwachi; uk. 45), au vibwagizo vya mwanzo na mwisho katika kila ubeti (kama katika Zama Mauti Yakija; 58). Au shairi moja linaweza kuchukua mpangilio wa vina vya kati na mwisho katika ubeti mmoja na halafu katika ubeti mwingine vina vya aina hiyo moja vikafululiza mwisho tu (kama katika  Mambo Kibao; 54). Machache ya mashairi yake hata yanaelekea kuwa huru (kama katika Vilio Tu!; 20).

KISWAHILI SANIFU NA LAHAJA YA KIPEMBA

Kwa muda mrefu, fikra ya Kiswahili Sanifu imetawala katika fasihi ya Kiswahili – fikra ya kwamba fasihi inayostahiki kusomwa miongoni mwa watu wetu wa Afrika Mashariki nzima ni ile inayoandikwa kwa Kiswahili Sanifu. Jambo hili linasisitizwa mno hata baadhi yetu huwa tunashindwa kuelezea kwa ufasaha Kiswahili Sanifu ni kipi. Je, ni Kiswahili chenye msingi wa lahaja ya Kiunguja Mjini? Au ni Kiswahili cha lahaja ya Mrima, Tanzania Bara? Au ni lugha dhahania iliyotengenezwa makusudi na wakoloni kwa madhumuni ya kufanikisha sajili ya elimu, hasa kimaandishi? Kama kweli msingi wa Kiswahili Sanifu mmojawapo miongoni mwa yote hii ulikuwepo tokea mwanzo, je, bado msingi huo unafuatwa mpaka leo kama kigezo cha Kiswahili kinachotumiwa katika shughuli rasmi na kueleweka na watu wote?

Tukipeleleza sana, na tukiacha siasa ya nchi kwa nchi au eneo kwa eneo, tunataona kwamba hakuna Kiswahili Sanifu kinachotawala janibu zote za Afrika ya Mashariki namna hiyo. Kile kilichopo ni misingi fulani tu ya Kiswahili Sanifu inayoishia pahala fulani, na mbele ya hapo, kuna kuingiza maneno na hata sarufi ya viswahili vya maeneo mbalimbali, na wakati mwingine, hata misamiati na sarufi za lugha nyingine za Kibantu. Mimi binafsi silalamiki hata kidogo kuwepo mchango wa lahaja mbalimbali za Kiswahili au hata wa lugha za Kibantu za Afrika ya Mashariki. Siwezi kulalamika kwa jambo hilo, kwa sababu Kiswahili Sanifu kama kilivyo hakina upana wa kumpa mwandishi, hasa wa fasihi, kuweza kujifaragua apendavyo kwa mapana na marefu. Kwa hivyo kuingiza maneno, misemo, na mipangilio ya kisintaksia katika misingi ya Kiswahili sanifu kutokana na lahaja zake au hata kutokana na lugha za Kibantu, kutakipanua na kukikuza Kiswahili Sanifu. Kwa hivyo, Kiswahili Sanifu lazima  kikubali kubwia utajiri wa msamiati na ukunjufu wa kisarufi unaotokana na majilio mengine. Watu wanaoshughulika na elimu na mitaala ya masomo ya Kiswahili, pamoja na watoa vitabu wetu wa Afrika ya Mashariki, lazima wasaidie jambo hili, badala ya kudai mihuri rasmi ya kuingizwa vitabu shuleni.

Hapa, sharti ifahamike vizuri, hatusisitizi kuwepo uovyo na vurugu katika Kiswahili Sanifu, bali lazima kuwepo taratibu na mifumo maalumu ya ukubalifu wa uingizaji maneno na mipangilio yake na viwango mbalimbali vya matumizi ya baadhi ya maneno yanayotokana na Kimrima, Kiamu, Kimvita, Kimtang’ata, Kipemba. Kipate na hata Kikikuyu, Kihaya, Kikamba, Kikerewe na kadhalika.

Ni wazi kwamba upanuzi wa Kiswahili sanifu umefikia upeo mkubwa sana katika kiwango cha istilahi za fani na sayansi maalumu, hasa katika uwanja wa magazeti, sayansi jamii, sheria, sayansi ya taalaki za ubinadamu, isimu, lugha, fasihi, falasafa ya lugha na uandishi wa habari, bado lakini upanuzi wa Kiswahili bado unazorota katika matumizi ya maneno ya maisha ya kawaida. Kwa maneno mengine, makamusi yetu tuliyonayo yanaacha maneno ya msingi kutoka Viswahili mbalimbali, maneno na mipangilio ambayo inatumiwa katika janibu nyingi za Kenya, Tanzania na Uganda, licha Rwanda, Burundi na Kongo.

KISWAHILI SANIFU NA KAIDA ZA USHAIRI WA KIMAPOKEO

Katika utunzi wa ushairi wa kimapokeo unaofuata kaida za arudhi, mambo yanakuwa magumu zaidi kwa uteuzi wa vipashio vya maneno, maana kunaingia haja ya vipimo vya maneno kwa mujibu wa mizani. Vipimo hivi vya maneno, kwa upande mmoja, vinahitajia urefusho maumbo au maumbile ya maneno fulani (kama kauli fupi lisilotendeka inaweza kurefushwa kwa lahaja ya Kipemba kuwa lisijalotendeka) na, kwa upande mwengine, vinahitajia mbano wa maumbo na maumbile ya maneno husika (kama kauli ndefu alikuwa mzuri inaweza kufupishwa kwa misingi ya lahaja ya Kipemba iwe kauli ali mzuri). Pia kuna vipimo vya urari wa sauti na vina, uvokali na ukonsonanzi. Kwa mfano, iwapo mshairi anahitajia urari wa kina cha -po kutokana na kauli yenye mwelekeo wa Kiswahili Sanifu sisahau kamwe ambapo hakuna kina hicho -po, katika lahaja ya Kipemba tungeliweza kukipata kwa kugeuza umbile la neno sisahau kuwa sisahaupo na kupata kina cha -po tunachokihitajia.

Au mshairi angehitaji upachapacha wa uvokali unaopatikana kwa kuweka kwa ukaribu mfwatilizo wa vokali kama katika shairi la Aambaye la diwani ya Jicho la Ndani (84) ambamo neno nyamaa lenye uvokali mwishoni linatokana na lahaja ya Kipemba:

Aambaye aamba, aamba likazagaa
Aambaye aamba, aamba lenye kufaa
Aambaye aamba, aamba mawi balaa
Aambaye aamba, pasi na jema nyamaa

Katika diwani yake, kwa makusudi Mohammed Ghassani anaamua kutoka nje ya mstari wa matumizi ya Kiswahili Sanifu kwa sababu, akijua asijue, hatimaye anahisi uhuru wake wa uteuzi umefumbika. Kutokana na kuchota kutokana na lahaja ya Kipemba anajisalimisha na pingamizi nyingi sana za kujenga mizani kaidi, urari mkorofi na ujengaji wa kimuziki unaozuka kwa kujali mbinu ya uvokali na ukosonanti. Diwani hii imeingiza lahaja ya Kipemba kwenye mashairi mengi ili kuweza kufaulu katika utekelezaji wa mbinu hizi za arudhi katika ushairi wa Kiswahili. Tutatoa mfano mmoja ambao umesheheni, uvokali, ukonsonanti, urefusho na mkabo wa mizani, vina na usambamba – mbinu zote hizi zinatokana na shairi moja Akianza, Umalize. Ubeti mmoja tu wa shairi hili unatosheleza mbinu zote hizo:

Akutenzaye mtenze, ajuwe kutenzwa nini
Akuchezaye mcheze, muingize mchezoni
Mpuuzi mpuuze, hana haja ya thamni
Sivyo ‘takuja mwilini, akwanzaye mmalize

Kwa maneno mengine, mshairi anayeogelea kwenye Kiswahili Sanifu na lahaja nyengine anapata uhuru na wepesi mkubwa zaidi wa uteuzi wa maneno, mpangilio wa maneno na sauti kuliko yule ambaye anajikita kwenye Kiswahili Sanifu tu.

Katika hoja hii, tunaona kuwa Mohammed Ghassani kaelemea sana kwenye lahaja ya Kipemba, lahaja iliyomlea na kumkuza na ambayo inampa uhuru tuliouzungumza hapo juu. Katika kutia mkono ndani ya lahaja hii, tunaona anavyocheza na maneno ya kila siku lakini yenye sura tafauti, yenye msikiko adimu na yenye ladha ya kimuziki.

Hii lakini si kusema kwamba mshairi huyu anatoka nje ya Kiswahili Sanifu kwa ukamilifu – hasha. Mohammed Ghassani na washairi wa aina yake, kama vile Ahmad Nassir Juma Bhalo na Abdilatif Abdulla, wana mtindo wa kuchanganyisha Kiswahili Sanifu na lahaja. Lahaja inapohitajika lahaja na Kiswahili Sanifu kinapohitajika Kiswahili Sanifu inafanya usanii kuchapukia sana kiladha.

Profesa Said A. Mohamed
Mhariri

Kuagizia diwani hii, tafadhali bonyeza hapa.

MAREJEO

Abani, Chris. 2007. Kalakuta Republic. London/San Francisco/Beirut: Saqi.

Abdalla, Abdilatif (Mhariri) 1994. Utangulizi. Katika ‘Sikate Tamaa: Tungo za Said A. Mohamed. Nairobi: Longman Kenya.

Abdulaziz, Mohamed H. 1994. Muyaka 19th Century Swahili Popular Potery. Nairobi: Kenya Literature Bureau.

Alawy, Abdurrahman Saggaf & El-Maawy, Ali Abdalla. 2011. Kale ya Washairi wa Pemba: Kamange na Sarahani. Mkuki na Nyota, Dar-es-Salaam (Mhariri Abdilatif Abdalla)

Dawes, Kwame. 2007. Introduction. In Kalakuta Republic. London/San Francisco/Beirut: Saqi.

Hichens, W. (Mhariri) 1940. Diwani ya Muyaka bin Haji Al-Ghassany. Johannesburg: University of Witwatersrand Press.

Mohamed, Said A. 2001. Jicho la Ndani. Nairobi: Longhorn Publishers.

4 thoughts on “Machozi Yamenishiya: Msafiri Safarini”

 1. Nimeamini kwamba kiswahili zanzibar ni nyumbani, jinsi Muhammad Ghassan anavyocheza na misamiati ya kiswahili.
  Zaidi shairi “Hukumbuki ihisani” hili limenivutia sana:-

  “Wiji hapa u mgeni, tukakupa uenyeji
  Wiji hapa huna dini, leo hii Al Haji
  Kushasahau zamani, sasa u mtukanaji
  Lau fadhila haiji, basi hata ihisani”

  Ahsante Mungu akuweke akujaaliwa umri mrefu wenye Kheri uzidi kutangaza lugha yetu.

 2. nimependa mtindo anaotumia Ghassani kuwasilisha ujumbe wake. Mashairi yake yavutia kwelikweli! Heko Ghasani!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.