KISWAHILI KINA WENYEWE

N’na Kwetu: Sauti ya Mgeni Ugenini

Siku ilikuwa Jumatano. Tarehe ilikuwa 1 Septemba 2010. Majira yalikuwa ya saa 4:00 usiku. Mahala palikuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K. Nyerere jijini Dar es Salaam, mji mkuu wa kibiashara wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nakumbuka kila kitu kuhusu siku hiyo. Nikiwa kwenye sehemu ya kusafiria abiria waitwao wa kimataifa, nilitoa simu yangu ya mkononi nikawasiliana na watu kadhaa kwa nia ya kuwaaga. Kati yao ni mama zangu wawili, aliyenizaa Abeida bint Nassor na aliyenilea Salama bint Said, mke wangu Tauhida bint Mkwale na dada yangu Fatma bint Khelef.

Hayo yangelikuwa mazungumzo yangu ya mwisho kwa simu nao nikiwa kwenye ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha mwaka mmoja na  nusu baada ya hapo. Hicho, hapana shaka, kilikuja kuwa kipindi kikubwa kabisa kuwahi kuishi mfululizo nje ya nyumbani, Zanzibar, hadi wakati huo. Mazungumzo yangu nao hayakuwa ya kuagana tu, bali pia ya kutiana moyo. Watatu kati yao, yaani mama zangu na mke wangu, nilikuwa nimewaacha chini ya paa moja, nyumbani kwetu, Mwanyanya, Unguja, na kitoto chetu cha mwisho wakati huo, Abdunaeem, kilikuwa ndio kwanza kina wiki mbili baada ya kuzaliwa. Picha yake ilikuwa imeniganda akilini, huku hisia za kuwaacha wote nyumbani nami kuselemea ughaibuni, zikiwa zinaniandama. Nakumbuka mama yangu mzazi aliniambia: “Nenda baba, inshallah hapa hakuna litakaloharibika!” Mama yangu mlezi aliniambia: “Mungu akulinde mwanangu. Tu mikononimwe!” Mke wangu alikuwa analia huku akiniombea dua, mtoto wangu wa kike, Ghanima, aliniita: “Baba, baba!” Nilipomuitikia “Naam, mama!” Akaniuliza swali ambalo alikuja kuendelea kuniuliza kila siku ya Mungu ambayo ningelipiga simu baada ya hapo: “Kwani waja lini?” Na kila baada ya kulijibu swali hilo, ningeanguka chini nikalia.

Hisia hizi zimesalia nami, hata baada ya mke wangu na watoto wetu wanne kuja kuungana nami nchini Ujerumani, mwaka mmoja na nusu baadaye. Kila siku, kila saa, kila dakika, ndani ya kipindi chote hiki, nimekuwa nikiishi kwenye mateso ya nafsi – ya kujiumiza na kujihoji mwenyewe. Daima nimekuwa nikijikosoa kwa kuamua kwangu kuacha kuishi maisha ya uwenyeji nyumbani kwetu na kuradua kuishi maisha ya ugeni, huku ugenini niliko. Hisia za mkosaji zimekuwa nami.

Usiku mmoja, katikati ya giza na baridi kali, nikaamka kichumbani mwangu, nikalia peke yangu na huku nikijiuliza mwenyewe maswali yasiyo na majibu:

Nyumbani oo nyumbani, kwetu ninakukumbuka
Gizani humu gizani, machozi yamiminika
Kwa nini hivi kwa nini, kwetu miye nikauka?

Ukiwa oo ukiwa, guo lilonigubika
Wauwa huu wauwa, na punde utanizika
Lau kuwa lau kuwa, naweza kuuepuka (Uk.76)

Lakini je, ilikuwa sawa kwangu kuendelea kuishi kwenye mateso haya ya nafsi?  Nilijiuliza siku kadhaa baadaye kwa njia ya kujifariji mwenyewe, ingawa jibu la swali hili likazidi kuugawa moyo wangu badala ya kuuleta pamoja.

Upande mmoja, lilinionesha ukweli kuwa dunia hii tunayoishi ni ya kuhama na kuhamia. Tangu siku Mtume Nuh alipoamriwa kupanda kwenye safina akiwa na jozi ya viumbe hai vilivyokuwepo wakati huo, na kisha kushuka tena kwenye ardhi hii ya Mungu Muumba, ulimwengu umekuwa uwanja wa kuhama na kuhamia. Iwe wakati wa amani au wa vita, wa furaha au majonzi, kwenye utulivu wa kisiasa au machafuko ya kijamii, dunia yetu imejaa wahamao na wahamiao. Kila uchao, watu hutoka upande mmoja wa dunia kwenda mwengine.

Kwenye mifano kadhaa, nikajipa moyo, mtu huweza kukuona kule ambako yeye anakuhama, ndiko ambako wenzake wanakuhamia. Nina hakika kuwa ndani ya kipindi hiki cha miaka saba ya kuishi kwangu kwenye ardhi ya ugenini na kupageuza hapa kuwa nyumbani pangu na pa wanangu, kuna mamia ya wageni ambao nao pia wamekugeuza nyumbani kwetu, Zanzibar, kuwa nyumbani kwao na kwa wana wao. Kwa hivyo, angalau kwa upande huu, nami nimejikuta naingia tu kwenye kundi la ukawaida – ukawaida wa kibinaadamu, ukawaida wa kihistoria, ukawaida wa kimaumbile – wa kuhama na kuhamia.

Lakini upande huo nao una na upande wake mwengine kwangu, na ambao haunifariji hata kidogo. Nilishawahi kuwa muhamaji na muhamiaji – ikiwa ningeliweza kuitwa hivyo – ndani ya ardhi ya nchi yangu mwenyewe – Zanzibar. Linalonifanya nikubaliane na hiyo fasili ya uhamiaji na uhamaji ni uhalisia niliokumbana nao, kwenye pande zake zote mbili za jambo lenyewe, yaani uzuri na ubaya wake.

Hadithi yenyewe ni kuwa katikati ya mwaka 1996, mwaka mmoja na ushei baada ya baba yangu kufariki dunia, nilihama kisiwani Pemba nilikozaliwa na kukulia na nikahamia kisiwani Unguja kwa ajili ya masomo. Visiwa hivi viwili ndivyo vikuu vinavyoiunda Zanzibar vikiwa vimezungukwa na vyengine vingi vidogo vidogo. Nakumbuka, muda mchache kabla ya meli ya MV Serengeti haijang’oa nanga katika Bandari ya Mkoani, iliyo kusini mwa kisiwa cha Pemba, nilitoa kalamu na karatasi na kuandika shairi la kukiaga kisiwa changu – Khadhira Wangu Nyamaza:

Khadhira hii safari, leo hii niyendayo
Usidhani nahajiri, naselemea machweyo
Sienendei hiyari, nendea makadiriyo
Basi kiri pendo kiri, niuke nina radhiyo
Kisha utunge nadhari
Ni ya kurudi safari
Wala sitakughairi, kwa ya huko nikutayo. (Uk.65)

Bali katika uhalisia uhamaji huo ulinigeuza kuwa ‘mwana-kutokomea’, maana hadi leo sijawahi kurudi tena nikayaishi maisha yangu niliyokulia kisiwani Pemba. Tangu wakati huo, kurudi kwangu kumekuwa ni kwa matembezi ya muda mchache tu na, hivyo, ile ahadi yangu ya kutomuwacha ‘Khadhira’ wangu kwa yale niliyoyakuta nje yake, sikuitimiza.

Hata hivyo, nilifaidika kwa mengi ndani ya uhamaji na uhamiaji huo. Ndani ya kipindi cha miaka kumi na nne niliyoishi kisiwani Unguja, niliyafanikisha mengi kwenye kiwango cha maisha yangu binafsi – masomo, ajira, ndoa, na familia. Ndio muda nilioajiriwa na kampuni ya utalii ya Fisherman Tours & Travel Ltd na pia Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) kwa wakati mmoja. Ndio wakati niliojiunga na gazeti la kwanza huru la Dira Zanzibar na pia kuwa mwandishi wa mara kwa mara wa makala za uchambuzi katika magazeti kadhaa yanayotolewa jijini Dar es Salaam. Ndicho kipindi ambacho pia  nilijunga na Kurugenzi ya Habari ya Chama cha Wananchi (CUF) kama afisa dawati wa uchambuzi wa habari. Kwa hivyo, najihisabu kuwa uhamaji na uhamiaji wangu huo wa awali ulinifaidisha mimi na wale walionizunguka. Alhamdulillah, ulinipa fursa za kujiinua kimaisha hata katika mazingira ambapo maelfu ya vijana wa marika yangu hawakujaaliwa bahati hiyo. Katika mifano yote hiyo, sikuwa na muda wa kujifikiria kuwa muhamaji na muhamiaji, kwa hakika, kwa kuwa mambo yalikuwa yanakwenda upande wangu.

Lakini nilikuja kuuhisi ukweli mchungu wa uhamaji na uhamiaji huo ndani ya nchi yangu mwenyewe, pale haki zangu za kiraia zinazofungamana na msimamo wangu wa kisiasa zilipoingia kati. Nilipofika mahala pa kutaka kutumia haki yangu ya kupiga kura kwenye chaguzi zote kuu na ndogo ndogo baina ya mwaka 2000 na 2010, nikajikuta kwa mara ya mwanzo nakumbushwa na wenye mamlaka ya chaguzi zenyewe kuwa mimi ni mhamiaji, na haki hiyo haikuwa yangu. Sheria za Zanzibar zinampa Mzanzibari aliyefikia umri wa miaka kumi na nane na mwenye kitambulisho cha ukaazi haki ya kupiga kura na akiwa ameishi kwenye eneo analopiga kura kwa miaka mitatu mtawaliya kabla ya siku ya kujiandikisha. Hata hivyo, uamuzi hasa wa nani apige kura haumo kwenye sheria hizo, bali mikononi mwa maafisa wa serikali waitwao masheha, ambao moja ya sifa zao ni kuwa kwao walinzi wa utawala. Matokeo yake, wenye haki ya kupiga kura wananyimwa kwa kuwa tu wao si sehemu ya walinzi wa watawala, na wasiokuwa na haki wanapewa, kwa kuwa wanaaminika kuwa ni walinzi wa watawala. Mimi nilikuwa upande ulio kinyume na watawala – yaani upinzani. Shairi Kipande cha Kura linaelezea muhtasari wa sehemu ya mkasa wenyewe ulivyonitokea likichanganya na mikasa iliyowakumba wengine kama mimi:

Jina langu hatamka, “Fulani bin Fulani”
Mara sheha akaruka: “Unakaa nyumba gani?”
Huyu sheha kwa hakika, mimi na yeye jirani
Hamwambia “Matuleni, nawe wapajuwa fika!”

Basi sheha kainuka, akenda mwake bukuni
Majina ‘limoandika, akasema hanioni
“Si wangu huyu hakika”, katangaza hadharani
Miaka yote tu jirani, bali akanikanuka (Uk. 96)

Ukweli mwengine kuhusu uhamaji na uhamiaji, ambao haunifariji, ni sababu zilizozoeleka na kuzoeleshwa akilini mwa wengi, pale muhamaji anapohama kutoka nchi zinazoitwa za Dunia ya Tatu – Afrika, Arabuni, Asia na Amerika ya Kusini – kuja kwenye nchi ziambiwazo ni za Dunia ya Kwanza, zinapolinganishwa na uhamiaji wa kinyume chake – yaani wa kutokea mataifa ya Dunia ya Kwanza kwenda ya Dunia ya Tatu.

Wakati mhamiaji wa kutoka Dunia ya Kwanza anafahamika kama muwekezaji, mtaalamu na mtalii, ufahamu wa jumla-jamala kwa mhamiaji kutoka Dunia ya Tatu ni kuwa amesukumwa na tamaa ya kuishi maisha mazuri na ya anasa yaliyoko kwenye Dunia ya Kwanza, akizikimbia dhiki, balaa na beluwa za kwao. Picha ya jumla ni kwamba yeye ni masikini anayekimbilia kwa tajiri, muhanga wa tawala za kibabe anayekimbilia usalama wa maisha yake, au msikwao anayekimbilia sitara. Na yumkini, ndani ya nafsi yake, hutakiwa ajikubalishe kuingia kwenye tafsiri hizo za kuhama kwake na autambuwe hivyo uhamiaji wake. Ndivyo pia mulivyo vichwani mwa wengi, sio tu miongoni mwa waliompokea ugenini, bali hata wale aliowaacha nyumbani anakotokea.

Hayo ukijumlisha na ukweli mwengine mchungu: kwamba sasa wahamiaji wengi wanaoingia au kuwania kuingia kwenye mataifa ya Dunia ya Kwanza wanatokea kwenye mataifa ya Arabuni na Afrika ya Kaskazini ambayo yamesambaratishwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, basi pumu huwa imepata mkohozi. Haitoshi hayo, bali pia kuna ukweli kuwa mashambulizi mengi yanayoitwa ya kigaidi katika mataifa ya Dunia ya Kwanza – kutoka Marekani hadi Ufaransa, Ubelgiji hadi Uingereza na Uhispania – yanasemekana kufanywa na aidha wahamiaji au vizazi vya wahamiaji hao. Haya yametosha kuwatia wahamiaji wote kwenye kundi moja la watu hatari wanaotoka hatarini na wasambazaji hatari, na sasa siasa kali za mrengo wa kulia zinaibuka na kupata kasi kote kwenye mataifa ya Dunia ya Kwanza, kupinga ujio wa wageni na wahamiaji!

Kichwa changu kimezikataa fasili hizi za muhamiaji wa Dunia ya Tatu kwenye ardhi za Dunia ya Kwanza. Sikatai ukweli kuwa nchi nyingi za Dunia ya Tatu, ikiwemo ya kwangu, Zanzibar, zina umasikini wa kipato na udhaifu wa kiuchumi. Sikatai pia kuwa  nyingi zinatawaliwa na tawala za kimabavu na zinazowanyima raia haki zao na uhuru wa kujiendeleza na kuziendeleza jamii zao. Lakini si kweli kuwa kila muhamaji kutoka nchi hizo aliye sasa kwenye Dunia ya Kwanza yupo hapo kwa kuwa ni muhanga wa madhila hayo. Badala yake, wako ambao kuhamia kwao Dunia ya Kwanza kumechochewa na sababu nyengine kando ya hizo, ikiwemo kusaka elimu, kuuona ulimwengu na hata kuwekeza. Hawa si kwamba hawana makwao kunakokalika, bali ni kwa kuwa wamechukuwa uamuzi wa kuondoka kwao kuichanjaga dunia!

Jambo jengine muhimu kabisa ambalo linaisumbua nafsi yangu kwenye maisha ya ugenini ni namna ya kuwakuza watoto wangu. Hawa, kwa hakika, nawachukulia kuwa wahanga wa kwanza wa uamuzi ambao hawakuhusika nao hata kidogo. Si wao walioamua kuja kuishi nje ya ardhi iliyowazaa na kuzikiwa vitovu vyao. Ni mimi ndiye niliyewang’oa nyumbani kwetu wakiwa na umri mdogo wa kutoweza kuamua wapi wapaite pao na wapi yawe maisha yao. Sasa wakati wanakuwa wakubwa, nashuhudia kile ambacho nimewanyima maishani mwao na kile ambacho nimejaribu kuwapa kwa uamuzi wangu huo. Nimewanyima ulimi wa nyumbani – ufasaha wa lugha ya Kiswahili – na nimewapa ulimi mwengine usiokatwa utata – lugha ya Kijerumani wanayokuwa nayo. Nimewanyima ujananchi wa kujifakharishia na kwao ambako ndiko kwetu sote na nimewapa utata wa “kwao” kwengine ambako, hakika, ni kugeni nao, kungawa ndiko uwenyejini kwao. Dhamana hii ya kuwachagulia katika wakati ambapo hawana namna ila kufuata matakwa yangu, inanifanya nijione sina hakika na hiki nilichokifanya. Ndio maana mwaka mmoja baada ya wao kuungana nami huku ugenini, niliandika shairi Wanangu Nisameheni:

Musije mukanisuta, wanangu nifahamuni
Musije mukanibuta, nishakuwa kaburini
Musije kuniburuta, mabaya mukanidhani
Ya kheri nalotafuta
Wanangu mutayapata
Ila hata mukikosa, wanangu nisameheni (Uk. 87)

Kwa hivyo, diwani hii ya N’na Kwetu ni kiwakilishi cha vita ninavyopigana ndani ya nafsi yangu. Ni matokeo ya hisia za muhamiaji anayekesa macho usiku wa manane, akiyahoji maamuzi yake ya kuhama kwao na kuhamia ugenini. Ni ungamo la baba aliyezaliwa na kukulia kwenye utamaduni anaotaka ufuatwe na kizazi chake, lakini akawa anawaona watoto hao wakikuwa na kuuzowea utamaduni ambao yeye baba haufahamu na wala si wake. Ni hadithi ya tajiriba ya mgeni ambaye anaziishi dunia mbili, akijaribu kuziunganisha na kujiunganisha nazo, na kwa hivyo kuwaunganisha watoto wake kwenye vikuku vya mkufu wa tamaduni hizo, akiamini kuwa zinaweza kukutana na kuishi pamoja ndani yake na yao bila ya kukerana na kukosana, lakini akajikuta kutokujaa ndani yake.

Hata hivyo, jambo moja na la muhimu kulisema hapa ni kuwa nina shukrani za pekee na za hali ya juu kwa taifa la Ujerumani, ambalo lilinipokea miaka saba iliyopita na kuipokea familia yangu mwaka mmoja unusu baadaye, na sote kutupatia fursa za kujiendeleza na kuviendeleza vipawa na vipaji vyetu. Ndani ya kipindi hiki kifupi, tayari nimejifunza mengi sana ambayo sikuweza kujifunza ndani ya kipindi chote cha umri wangu wa hapo kabla nikiwa nyumbani kwetu. Ujerumani imenipa fursa za kuyatekeleza mengi na kwa imani kubwa kutoka kwa wenyeji wangu, kutoka kazini kwangu nilikoajiriwa hadi katika taasisi rasmi za nchi, pengine katika kiwango ambacho hata mamlaka za nchi yangu zisingeweza kuniamini, aidha kwa sababu ya msimamo wangu wa kisiasa au kwa sababu ya kutokuujuwa uwezo wangu kwenye mambo hayo, au hata kwa kutokuwa na mfumo unaotambua vipaji nilivyonavyo na kuvipa nafasi.

Kama kuna chochote nakijutia kwenye kuishi kwangu ugenini, basi hakimo kwenye kukosa fursa na imani, bali kimo kwenye kuiwacha nchi yangu wakati ikinihitajia na ambayo pamoja na yote iliyonayo na isiyokuwanayo, bado inaendelea kuwa yangu. Husemwa kuwa mama ni mama. Hakuna ambaye anaweza kulingana naye hata awaje. Lakini mimi nina uzoefu wa kuwa na mama wawili, wa kunizaa na kunilea na wote wakabakia kuwa mama zangu.
Jambo hili la kuhama pawa na miko kutoka ardhi iliyozikiwa kitovu changu na kuselelea mbali nako limenipa uzoefu wa pande zote ninazoishi, lakini bado kumbukumbu za nyumbani kwetu  zimeendelea kuwa maisha halisi ninayoyaita yangu  – angalau kwenye kiwango cha ukimya wa nafsi yangu. Ndio maana hadi hivi leo, hakuna siku ninayoota usingizini mwangu nisijione niko kwetu. Humo ndotoni, watu waliomo ni wale wale nilioshi nao katika miaka yangu 18 ya mwanzo wa uhai wangu. Maeneo yanayonijia, ni yale yale niliyokulia, kucheza na kuyazowea kwenye miaka hiyo. Hata ninapoota yanayonijiria hapa Ujerumani, basi picha zake huchanganyika na za nyumbani huko na kisha za nyumbani zikatawala sinema nzima ndotoni. Kwa mfano, ninaweza kuota nimo ndani ya treni linalotembea kwa mwendo wa kasi, lakini treni hilo huwa linakata misitu na vijiji vya Zanzibar – Pemba na Unguja.

Naamini, ni kwa kuwa N’na Kwetu. Kwetu inayoishi ndani yangu, popote niwapo, vyovyote nilivyo – na kwetu nako kunami!

Kununua diwani hii, tafadhali agizia hapa.

8 thoughts on “N’na Kwetu: Sauti ya Mgeni Ugenini”

  1. dahhh kuna vitu nimejifunza kupitia hapa hasa sisi tunao yaota maisha ya ughaibuni nakuanza kufikiria yapoje kama ningali nimepewa fursa ya kukuuliza ningali nimekuuliza ili nijifunze zaidi maswali niliyonayo

  2. Nimependa stori mwanzo mwisho, nimependa ulivyotumia mafumbo yenye uhalisia ndani yake.

  3. Masha allah kweli unakuja tna kwakasi kubwa mm nimpenzi wahadithi namashairi ata wakat nipo shule nilipenda sna hadithi yatakadini lkn kwahii hadithi yako yasafari yakwenda ugenini nicngeweza kuimaliza km cujacr maana wakati unaiaga familia yako hapo ndipo machozi yalinilenga machoni mwangu kwan nilikua najenga picha akilini mwangu. Hongera sana sana sana.

  4. Allah akubarik Sheikh Mohammed Ghassani wallah watufariji kujiona tuna wenza tulio ughaibuni, twalia kilio kimoja

  5. Nami nifarijika kwa usanii wako wa hali ya ju uliosheheni mashairi na lugha yenye mnato allah akubariki, awabariki wazanzibar wenye kwao karibu mwanyanya tupo tunasota karibu pba nakubali tunakwetuna si nnakwetu tu hongera

  6. Kwa kweli diwani hiyo ya nna kwetu inatufariji wengi tunatoka kisiwa cha pili ambao tunakusa haki zetu za MSngi kwasababu ya kisiasa.
    Allah akubariki

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.