Ushairi unatambuliwa kuwa miongoni mwa sanaa kongwe kabisa kwa mwanaadamu. Jamii yoyote inayojitambuwa kwa ukale na ukongwe wake, basi utaikuta ndani yake ikiwa na sanaa ya ushairi kama moja ya dalili za uwepo wake wa zama na zama. Haitoshi hayo, ushairi pia unachukuliwa na wasomi wa taaluma za kibinaadamu, kuwa moja ya nguzo kuu za ilimu ya falsafa. Kwa ujumla, fasihi – ambayo yenyewe ndiyo mama wa maarifa ya mwanaadamu – inabebwa na tanzu nyingi, na kongwe yao ni ushairi.
Mwaka 2011, nilianzisha ukurasa maalum wa mtandaoni kwa ajili ya kuuhifadhi na kuusambaza ushairi wa Kiswahili. Hiyo ni baada ya kutembelewa na ndugu yangu, Hamad Omar Hamad, ambaye kwa wakati huo alikuwa mwanafunzi wa shahada ya uzamili nchini Denmark. Ingawa wawili sisi tulizaliwa na kukulia Zanzibar, ilikuwa ni kuhamia kwetu ugenini ndiko kulikotufanya tujuwane na tuwe karibu zaidi. Yeye akiwa masomoni Denmark, mimi nikiwa mafunzoni Ujerumani, tukaanzisha jukwaa la mtandaoni liitwalo Kurasa Mpya.
Kuzichapisha na kuzisambaza tungo zetu kwenye mitandao ya kijamii, hasa ukurasa wa Facebook, kukanikutanisha na wengine wawili waliomo humu – Nassor Hilal Kharus na Ali Hilal Ali. Kwa kukiona kipaji chao cha utungaji na upevu wa mawazo yao, nikawa mara kwa mara nawasiliana nao kuwatia moyo na baadhi ya wakati kuwaomba waniruhusu niyachapishe mashairi yao kwenye jukwaa la Kurasa Mpya. Wote wawili, kwa nyakati tafauti, wakavutiwa na mawazo yangu. Wakawa sehemu ya mtandao wa malenga wa Kurasa Mpya, kabla ya hata kukutana nao uso kwa macho. Kwa hakika, hadi diwani hii inatoka, hatujawahi kukutana ana kwa ana na Ali Hilal, na nimewahi kukutana mara moja tu na Nassor Hilal mwishoni mwa mwaka 2015, Mjini Unguja.
Wengine wawili, yaani Maalim Mussa Shehe na Maalim Ahmad Kipacha (uk. 95), nilikutana nao kwenye mazingira tafauti na hao watatu waliotangulia. Kwa upande wa Maalim Mussa, nilijuwana naye tangu nikiwa mwanafunzi wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Zanzibar kuanzia mwaka 1996 hadi 2001. Wakati huo, yeye alikuwa ni mwalimu wa masomo ya ziada katika madarasa ya lugha na fasihi, nami nilikuwa mmoja wa wanafunzi wake. Kisha baada ya masomo, tukapoteana kwa muda na kuja kukutana tena kwenye shughuli za kisiasa – sasa yeye akiwakilisha Ubalozi wa Marekani kufanya utafiti wa siasa za Zanzibar, nami nikihusika na uchambuzi wa habari kwenye Chama cha Wananchi (CUF). Baada ya kuhamia Ujerumani na kuanzisha jukwaa la Kurasa Mpya, akawa mara kwa mara ananitumia mashairi yake, nami nayachapisha na kuyasambaza.
Ama, Maalim Ahmad Kipacha tulikutana siku moja na mara moja tu uso kwa macho, kwenye Kongamano la Kiswahili la Bayreuth, kusini mwa Ujerumani, mwezi Mei 2016. Yeye alikuwa anahudhuria kama mtaalamu wa lugha na fasihi, nami kama mwandishi wa habari na mshairi. Baada ya kushuka jukwaani, nilipokuwa nimesoma mashairi kutoka diwani yangu N’na Kwetu: Sauti ya Mgeni Ugenini, Maalim Ahmad alinifuata na kuniambia kuwa naye ni mshairi na ana mashairi ambayo angelipenda niyaone, niyahariri na nikiridhika nayo, basi niyatafutie uwezekano wa kuchapishwa.
Namna hii ndivyo mkusanyiko huu wa Kurasa Mpya ulivyokuwa kutoka jukwaa la mtandaoni na kuwa diwani kamili. Ndivyo ulivyokuja kuwafungamanisha pamoja washairi watano wa Kiswahili kwenye kitabu kimoja.
Namna nilivyokutana na washairi hawa na namna nilivyozikusanya tungo zao kuna maana kubwa sana panapohusika ile dhana iliyofungua utanguzi huu, yaani ukongwe wa sanaa ya ushairi na uzito wake. Kwamba licha ya kuonekana kwake kuwa sanaa kongwe na ya vikongwe, ushairi ni sanaa pia ya kisasa na ya watu wa sasa, ambayo imeweza kuhimili mageuzi yanayoingia na kutoka kwenye jamii ya Waswahili. Ni sanaa inayokata mipaka na kuunganisha mapande ya dunia tafauti – kutoka za kiwakati hadi kitaaluma, kijiografia hadi kihisia. Watano hawa wana historia tafauti, wana elimu tafauti, wana umri tafauti, lakini wote wameukumbatia ushairi kama njia yao ya mawasiliano – ama angalau kama mojawapo wa njia za kuwasilisha mawazo yao!
Jengine ni kuwa kwa ushairi kuhamishiwa jukwaa, kwa mfano, kutoka kutambwa kwenye hadhara za furaha na misiba au mitengoni na uwani hadi kuandikwa na kupachikwa mitandaoni, hakukuupunguzia ladha na nafasi yake. Ule utamu wa lugha, uteuzi wa maneno, utumiaji wa tamathali za semi, mpangilio wa vina na mizani, na hata ubinifu wa bahari na mikondo – yote yakiwa muhimu mno kwenye sanaa ya ushairi – umesalia pale pale kama ulivyokuwa zama za Fumo Liyongo, Muyaka al-Ghassani, Kamange na Sarahani na Shaaban bin Robert, miongoni mwa magwiji wa ushairi wa Kiswahili.
Msikilize, mathalan, Mussa Shehe, akimsuta nahodha anayetaka kutweka chombo chake hali ya kuwa hakuna upepo kwenye shairi Kutweka Bila Upepo:
‘Kitweka bila upepo, juwa hakuna safari
Hutaondoka ulipo, hali ikiwa shuwari
Utamaliza viapo, ujuba na ujabari
Upepo ndio muhimu, ili safari isonge
Hili bwana lifahamu, wacha vituko na finge
Hunalo wewe muhimu, nenda kacheze uringe
Tanga lote halijai, upepo tukaondoka
Foromali haikai, na kamba zikakazika
Huu wako ulaghai, jua utamalizika
Unataka tuondoke, na maji yanatusonga
Kila kitu kiko kwake, na mipango hujapanga
Sitweki jahazi kake, nikenda pata majanga
Utamu wa upangaji wa maneno na uteuzi kama huu umo pia kwenye uandishi wa mashairi ya Hamad Omar, ambaye anapenda sana kutumia muundo wa utandawili, ambao unaweza kumbabaisha msomaji, akayafumbua mashairi hayo ndivyo sivyo au sivyo ndivyo. Baadhi ya wakati kuyasoma na kuyaelewa mashairi yake, inakupasa kumtaka mwenyewe akupe tarjumi za mashairi hayo, na kawaida yake huwa hapendi kuitoa na hivyo anakuwacha uendelee kueleya, bila dira, lakini bila kuzama, katika bahari ya lugha ya kishairi, na ambao kwa wengine tunaamini ndio mafanikio ya ushairi. Msikilize kwenye shairi Kiti (uk. 39), uone jinsi anavyokubembeleza na wakati huo huo kukufunga kwenye bahari ya lugha, akitumia kwa undani lahaja yake ya Kipemba:
Kiti kye miliki yangu, akaja dhalimu
Akaniondosha
Akaiba hadhi yangu, na pya majukumu
Akanivulisha
Kwa nguvu za walimwengu, na sauti ya kalamu
Akajikalisha
Akitumilia
Kiti kye na maguu mane, akakihujumu
Kunidhalilisha
Akataka asimame, kwa yake isimu
Yangu kufutisha
Ndipo akafanya shime, na yake kaumu
Akajisimisha
Aking’ang’ania
Kiti kye uthibitisho, wa wangu uhuru
Kuuhalalisha
Kye ni kitambulisho, kwa walio huru
Hijitambulisha
Changu tena sicho, kashanikusuru
Chini nakalishwa
Hebu kiachia
Washairi hawa watano, ingawa wanatafautiana kwa mengi ya binafsi, wanalingana kwenye uwezo wao wa kuitumia lugha na upevu wa mantiki wanayoiwasilisha. Hata wanapozungumzia maudhui ambazo zinatafautiana, bado wanashikana kwenye fungamano la uweledi wa lugha. Ali Hilal, kwa mfano, ndiye mdogo kwa umri miongoni mwa watano hawa, lakini unapoyasoma mashairi yake hutaweza kuliona hilo la udogo wa umri. Hii ni kwa sababu, kama inavyohojika na wataalamu wa falsafa, ushairi peke yake ni alama ya upevu wa fikra, haidhuru uwe umetolewa na kinyandu cha umri. Shairi la Gonjwa Sugu Lina Dawa linathibitisha ukweli huu:
Tutafika tutakako
Tutafika tuendako
Tutafika na chereko
Kilele kisogeapo, uzito hutia nanga
Kwani kuna lili mwanzo
Pia lisili vikwazo!
Mwisho wa maangamizo
Hukithiri changamoto, hapo hatumwi mtoto
Na ukuni wa masika
Mtoto ye hatumika
Mkubwa huhangaika
Mwishowe ni kupasuka, ngoma sana ivumayo
Dawa yataka suudi
Kuifanyia juhudi
Hakuna gonjwa kaidi
Lenye mwanzo lina mwisho, gonjwa sugu lina dawa
Uzito wa fikra iliyomo mwenye mawazo haya ya Ali Hilal ni kama uliomo kwenye kina cha fikra za Nassor Hilal (hawa si ndugu), ambaye kwa hakika amemtangulia Ali kwa miaka mingi ya kuzaliwa. Msikilize Nassor Hilal kwenye shairi Muungwana:
Mtu muungwana, hujipeleleza
Husema hapana, asiloliweza
Naye huyanena, yasiyochukiza
Hupenda halali, inayopendeza
Neno la ukweli, ndilo hueleza
Hujibu suali, ukimuuliza
Haipigi ngumi, kwenye kiambaza
Na mate hatemi, watu kuapiza
‘Tadhani hasemi, amejituliza
Siri ‘kimwambiya, yako ‘taitunza
Hutaisikiya, ikihanikiza
Roho maridhiya, yake huiweza
Duniya dhaifu, yeye kapuuza
Yake taklifu, hataki kuwaza
Moyo kinaifu, wenye maliwaza
Washairi hawa watano wameogelea kwenye maudhui kadhaa zinazogusa jamii zao, zikiwemo zile zilizozoeleka sana kwenye ukale wa ushairi, yaani mahusiano ya kifamilia na ya kimapenzi, siasa na maadili ya kijamii, hadi kwenye mada ambazo zinagusa maisha halisi ya sasa, kama pale mshairi Ahmad Kipacha anapozungumzia ukweli wa kuingia bidhaa za China kwenye soko la Afrika, ambazo licha ya urahisi wake kwa wanunuzi, huzuwa hasara kubwa kwa kuwa si za kudumu na nyingi zao ni za kughushi. Anasema hivi kwenye shairi lake Shamba la Bibi (uk. 102):
Wangwana na madubwana, yamenishinda nanena
Uchao “made in” China, ukionacho cha China
Nywele bandia za China, kufuli na sodo China
Sawa makalio China, hata mnyegezo China?
Misemezo toka China, udugu sasa ni jina
Tumebaki kuchanana, kama nywele na kitana
Tumeshakuwa watwana, China imeshatubana
Litokapo twajivuna, toleo jipya la China
Uchao “made in” China, ndiyo urithi wa wana?
Bongo labaki hamna, tupu akili hawana
Ni kipi tunachorina, kama sio kuzugana?
Ghorofa zimepandana, kumbe samani za China
Uchao “made in” China, vyetu vichwa vimechina?
Si juzi tulifanana, leo wenzetu mabwana?
Kiwafanyacho kufana, mipango yao mwanana
Siye twa “pool” mchana, usiku “top” banana
Mwenyewe nikiwa mshairi ambaye ndiyo kwanza nimemudu kuchapisha kazi zangu baada ya miaka 20 ya kudima, ninafahamu umuhimu wa mwandishi kuiona kazi yake ikitoka, bali pia umuhimu wa kazi za waandishi wazuri kusomwa. Kwa upande, mmoja kunampa mwandishi moyo wa kusonga mbele na uandishi wake, akiamini kuwa mawazo yake yanasikika na yanapewa nafasi ya kuwa sehemu ya mjadala unaoendelea kwenye jamii yake na, kwa upande mwengine, utajiri wa jamii kwenye fasihi huongezeka, maana jamii isiyohifadhi maandishi yake huwa fukara na dhalili.
Kwa hivyo, kwa heshima zote, nawawasilisha kwenu washairi hawa watano ili muyaone, muyasome, muyapime na muyape nafasi maandishi yao kwenye mazungumzo yenu, maana mcheza kwao hutuzwa, na hakuna nishani bora kwa mshairi kama ile ya kuuona ushairi wake ukighaniwa, maoni yake yakijadiliwa na mchango wake ukithaminiwa.
Kununua diwani hii, tafadhali agizia hapa.
Mohammed K. Ghassani
Bonn
Ujerumani