KISWAHILI KINA WENYEWE

Kalamu ya Mapinduzi: Mapambano Yanaendelea

Ni jambo gumu kuyazungumzia maandishi bila ya kumgusa mwandishi wake, khasa pale maandishi yenyewe yanapokugusa na kuchoma mithali ya hivi zilivyo tungo za Kalamu ya Mapinduzi na unapokuwa unamfahamu mwandishi binafsi.

Nimemjua Mohammed Ghassani kwa zaidi ya miaka kumi kupitia maandishi yake mbalimbali yanayochapishwa kwenye magazeti ya Kiswahili nchini Tanzania. Sehemu kubwa pia ya maandishi yake nimekuwa nikiyasoma kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandaoni. Ilichukua miaka zaidi ya minane, tokea kuanza kusoma anayoyaandika, kupata fursa ya kuonana uso kwa macho nyumbani kwake nchini Ujerumani, lakini nilipokutana naye ilikuwa nazungumza na mtu tunayefahamiana kitambo kutokana na maandishi yake hayo. Kwa hakika, nilivutiwa sana kwa umahiri uliomo kwenye maandishi yake, kwa ufundi wake wa lugha katika kuwasilisha mawazo yake na kwa uzito wa hoja zake.

Ndio maana, aliponiomba nimsaidie kumtafutia njia za kuichapisha diwani yake hii, nilikubali moja kwa moja. Msomaji atakayesoma tungo zilizomo humu atafahamu haraka uwezo wa Mohammed Ghassani kwenye bahari hii ya ushairi kwa kuuhusisha na maudhui anayoyashughulikia kwenye maandishi yake mengine – yawe maqala, ziwe tungo, ziwe hadithi fupi. Kila mara anaonekana ana jambo la kulisimulia na ambalo linaamsha sikio lolote lenye kumsikiliza, akitumia ufundi wake wa lugha.

Ndivyo ulivyo kila utungo kwenye diwani hii ya Kalamu ya Mapinduzi, ambapo kila ubeti wake mmoja unasimama kama silaha kali ya mapambano iliyokuwa tayari kumshambulia adui yake na kusimamisha dhamira yake. Hebu msikilize, kwa mfano, kwenye shairi lililobeba jina la diwani hii anavyonguruma:

Ya umma nguvu ya umma, itaung’oa mfumo, wa walaji manyakuzi
Nguvu itawasakama, iwaponde humo humo, iwazibe na pumzi
Nguvu itawaandama, iwatie kwenye shim, majizi haya majizi

Diwani hii inaweza kuwa ya kwanza na ya aina yake kuyasema waziwazi yale ambayo katika kazi nyengine za kifasihi husemwa kwa kificho na mizunguko. Uwazi huu haukuinyima utamu wala uzito wake wa kifasihi, isipokuwa tu umeipa urakhisi mkubwa zaidi wa kujiwasilisha na kujikurubisha kwa hadhira.

Kupitia diwani yake hii, Mohammed Ghassani anapaza sauti ya ukombozi wa haki kwa jamii yake, akitangaza vita vya kudumu dhidi ya dhuluma na ukosefu wa haki na hapohapo kiapo cha kusimamia dhamira yake hadi itimie.

Kwa hakika, ni diwani ambayo inapaswa kusomwa sio tu na wanafunzi vyuoni wanaosoma fasihi ya Kiswahili katika zama zetu, bali pia na wanaharakati wanaopigania mabadiliko ya kisiasa na kijamii, kwani hii kweli ni Kalamu ya Mapinduzi!

Kununua diwani hii, tafadhali agizia hapa.

Ibrahim Noor Shariff

 

2 thoughts on “Kalamu ya Mapinduzi: Mapambano Yanaendelea”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.