KISWAHILI KINA WENYEWE

Siwachi Kusema: Uhuru U Kifungoni

Kusema ni moja kati ya njia za kuwasiliana na kuwasiliana kwenyewe ni miongoni mwa tabia za viumbe hai, kwa mujibu wa wataalamu wa mawasiliano. Mtu ambaye hawasiliani, au hana uwezo wa kuwasiliana, huchukuliwa kuwa amekosa kitu muhimu sana kwenye maisha yake, kama vile ambavyo angelichukuliwa mtu asiyeweza kupumua, kutoa uchafu na ama kutembea.

Kusema kwenyewe nako kuna maana zaidi ya kufumbua mdomo tu na kuufanya ulimi kutamka maneno. Kunajumuisha pia kutoa kauli kwa njia ya maandishi, bali hata kutumia ishara. Ndio maana, pale wananchi wanapojitokeza kwenye vituo vya kura kuchaguwa wawakilishi wao kwenye ofisi za nchi, kwa mfano, huwa inasemwa “wananchi wamepaza sauti zao”, maana kipande cha kura walichokitumia ndio imekuwa sauti yao waliyosema.

Kusema, kwa hivyo, sio tu kuwa ni tabia ya kibinaadamu inayojenga na kulipamba jengo la utu wa mtu, bali pia ni haki ya binaadamu kama kiumbe hai. Hii ni haki isiyopaswa kupokonywa kutoka miliki ya mwanaadamu, isipokuwa tu yeye mwenyewe anapoamua kunyamaza. Hakuna mwenye haki ya kumnyamazisha mwengine asiseme. Mwanaadamu anayelazimishwa – kwa sababu yoyote ile – kutoa kauli yake juu ya yale yanayojiri mbele ya macho yake, basi huwa amezibwa pumzi, ametiwa jiti la roho, na lazima atasaka njia ya kulisakamua jiti hilo viwe viwavyo. Atapapatika huku na kule, arushe mateke na mapindi, hadi apate pa kupumulia – pa kusemea.

Siwachi Kusema
Siwachi Kusema: Uhuru U Kifungoni

Ndivyo ile hadithi mashuhuri ya Mfalme Ana Pembe inavyotufundisha. Siku kinyozi wa mfalme huyo – aliyekuwa akijuilikana kwa ukatili wake – aliposhindwa kuhimili siri ya mteja wake ya kuwa na pembe kichwani, lakini huku akiwa anayakhofia maisha yake, ilimbidi aende msituni akachimbe shimo refu, kisha ndani ya shimo hilo apige ukelele mkubwa: “Mfalme ana pembeee!” Baadaye akalifukia shimo hilo, na siku zikapita ikaota miti miwili ambayo kila ikikuwa inakaribiana na kuchuana, na pindi upepo unapovuma, ule mchuano wao ukawa unatoa sauti: “Mfalme ana pembe!” Kufumba na kufumbua nchi nzima ikajuwa kuwa mfalme wao ana pembe, na mfalme akaaibika sana, hadi akafa kwa kibuhuti.

Fani mbili ambazo ni sehemu muhimu ya maisha yangu – uandishi wa habari na ushairi – zinahusiana sana na kusema. Kwa hakika, kusema ndicho kiini cha fani hizi sio tu kama taaluma, lakini pia kama kazi za kuongoza maisha yangu. Kwa hivyo, mimi na kusema ni mithali ya mtu na mpenziwe: kila mahala tu pamoja, hatuachani, hatubandukani. Ninachokichelea ni kule kusema kwa kuonekana tu kuwa nimesema; maana huko ni kuropokwa.

Nikiwa mwandishi wa habari na mshairi, huwa ninataka niseme kwa kuwa pana la kulisema na hutaka pia kusema kwangu kuwe na maana kwa lile nilisemalo, kwa wale niwasemao na kwa yule nimsemaye. Na ambapo natambua mipaka iliyowekwa na sharia za mataifa, kanuni na maadili ya kijami kwenye kusema huko, sitaki zitumike kama kufuli za kukikomea kinywa changu ama pingu za kuifunga mikono yangu pale ninapoinuwa kalamu kusema.

Siwachi Kusema ni diwani yangu ya pili kuchapishwa baada ya Andamo (Buluu Publishing, 2016) ikiwa na tungo 70 zenye bahari na mitindo mbalimbali. Ambapo Andamo ni hadithi za maisha yangu ya mwanzoni mwa ujana baina ya 1993 na 2001, Siwachi Kusema ni muedelezo wa hadithi hizo baada ya mwaka 2001. Ni namna yangu ya kusema na kuyasemea yale yanayotokea mbele ya macho yangu – iwe kwenye uwanja wa siasa, jamii au hata katika kiwango cha binafsi – na yakaniathiri au kuacha alama kwa mazingira yaliyonizunguka.

Ninasema na sitaki kuwacha kusema kwa kuwa kusema ni haki yangu na kwa kuwa ni tabia muhimu kwenye jumla ya mambo yanayouumba utu na ubinaadamu wangu. Ninasema kwa kuwa kuna mambo yanahitaji kusemwa, ili nipumuwe na nijipapatuwe dhidi ya kabari ya roho.

Ninasema kwa furaha na kwa matumaini pale mambo yanapoonekana kwenda njia sahihi, lakini pia ninasema kwa hasira na kuvunjika moyo pale yanayopindishwa na kuchukuwa njia ya machakani; na kamwe sitaki kuacha kusema.

Nimeuchagua ushairi kuwa moja ya njia ambazo naweza kuyasema na kuyawasilisha hao na mengine kama hayo na bado nikabakia na nafasi na wakati na nishati ya kuyasema mengine. Na bado nikabakia mimi mwenyewe.

Kusoma diwani ya Siwachi Kusema, tafadhali tembelea hapa.

1 thought on “Siwachi Kusema: Uhuru U Kifungoni”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.