MIAKA mitano iliyopita nilipata kueleza namna ambavyo wanafunzi wa Chuo cha SOAS (School of Oriental and African Studies) cha nchini Uingereza wanavyofanya juhudi kubwa kujifunza lugha ya Kiswahili.
Nilisema lugha ya Kiswahili ni adhimu, katu haitakuja kuachwa nyuma katikati ya utandawazi. Kwamba ni vigumu kwa utandawazi kukifuta au kushusha ari ya kuenea na kujifunza lugha ya Kiswahili.
Watu mbalimbali duniani wanakusudia kukimanya Kiswahili na wamependa kumenyana na wale wanaoizungumza lugha hii. Juhudi ziazofanywa na watu kuongeza uwezo wa kuzungumza lugha hii ni utunzi wa mashairi.
Wazungumzaji wa lugha hii waliopo ughaibuni wanatumika katika vyuo na taasisi mbalimbali kuelimisha lugha ya Kiswahili. Niliposikiliza utunzi wa shairi la “N’na Kwetu” niliduwaa namna mtunzi Mohammed Ghassani alivyowasilisha kazi yake kwa ustadi. Ni kati ya watunzi wanaoelimisha lugha hii huko ughaibu.
Ghassani ni mwandishi wa habari wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW) ambaye kwa sasa ameingiza dukani kitabu chake cha ushairi kiitwacho “Andamo”. Kitabu hicho kimechapishwa na kampuni ya Buluu Publishing chini ya usimamizi wa Mathieu Roy wa mjini Paris nchini Ufaransa.
Andamo ni diwani ya tungo za ushairi zilizoandikwa kwa muongo mmoja kuanzia miaka ya mwanzoni ya 1990 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000. Ni tungo zinazoogelea pamoja naye kwenye bahari ya uzoefu wa mwanzo wa ujana kuelezea hadithi yake ya maisha, mtazamo wake juu ya yale yaliyokuwa yakitokea mbele ya macho yake na ufahamu wake kwa ulimwengu.
Aliyekuwa Katibu wa Kamati ya Fasihi na Utamaduni ya Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Bwana Abbas Mdungi, wakati akikabidhi ripoti ya muswada wa diwani hiyo mwezi Oktoba 2003, aliandika hivi:
“….Mshairi ameibuni kazi yake kwa ustadi mkubwa kama kwamba ni mweledi katika utunzi ilhali hii ndiyo kazi yake ya kwanza kabisa. Mitindo aliyotumia ni mingi na mizuri ambayo inatafautiana na wakati wengine kushabihiana….Kwenye lugha, ametumia lugha ya ushairi – nyoofu, nzuri na telezi…
Maudhui, bila shaka, ameyatumia vizuri kuweza kuelimisha jamii akijikita kwenye masuala ya utamaduni, siasa na uchumi, ingawa utamaduni umekuwa sura kubwa zaidi.
Kwa kawaida, washairi wa Afrika huzikita dhamira zao katika migogoro ya kimapenzi, kindoa, kidini, kikazi, kinyonyaji, kidemokrasia, uongozi mbaya, umangimeza, njaa, umasikini na maradhi, naye kwa ujumla amefanikiwa sana katika hilo….
Hivyo, ndani ya Andamo, sio tu mna mwangwi wa sauti ya kijana anayejaribu kuiwasilisha hadithi yake kwa hadhira kwa njia ya kishairi, lakini pia ishara ya kuibuka kwa kipaji cha aina yake kwenye uwanja wa fasihi ya Kiswahili.
Mmojawapo wa mifano ya mashairi yake makali ni hili;
Juu ya kaburi lako
Nangojea niicheze
Ngoma ya boso na soko
Sababu maisha yako
Uliyageuza kijinga
Kuwachomea wenzako!
Omba nife mwanzo miye
Kwa Mungu nitanguliye
Bali lau ‘tabakiya
Siku ikakufikiya
Miye sitakuliliya
‘Talipiga kaburilo
Mikwaju na mijeledi!
Ghassani ameandika mashairi yake kwa lugha inayovutia. Amejenga taswira ya wahusika kwa namna ya kipekee, anaonya, anaelekeza, anahimiza na kulinda maadili.
Mathalani katika shairi la “Upande wa Giza’ ambalo limetumika kumalizia katika diwani yake:
“Kula mmoja anao, upande wake wa giza
Wenye majambo kibao, asotaka yaeleza
Angayapiga ubao, fudi kayafudikiza
Kuu ni siku ambayo, yatajiwa na mwangaza!”
Ushairi ni sehemu inayowezesha kumvuta msomaji kwa kusikiliza. Lakini sasa vitabuni limekuwa jambo la maana kabisa kuchapishwa na kuhimiza usomaji.
GHASSANI NI NANI?
Mohammed Khelef Ghassani alizaliwa kisiwani Pemba, Zanzibar, mwaka 1977. Ana shahada ya uzamili katika Taaluma za Tafsiri kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania aliyoipata mwaka 2014.
Kabla ya hapo alisomea shahada ya kwanza ya Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam mwaka 2009, na pia diploma ya ualimu wa lugha kutoka iliyokuwa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Zanzibar mwaka 2001.
Kwa sasa ni mtangazaji na mhariri wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle nchini Ujerumani. Amekuwa akiandika tungo za ushairi na hadithi fupi fupi kwa zaidi ya miaka ishirini sasa, ambapo miongoni mwa kazi zake zilizokwishachapishwa zinapatikana kwenye mikusanyiko ya Damu Nyeusi (MacMillan Kenya, 2007), Masikini Milionea (Oxford University Press Nairobi, 2012), Diwani ya Waja Leo (Oxford University Press 2012) na Homa ya Nyumbani (Phoenix Publishers Nairobi 2016).
Mwaka 2015, alitunukiwa Tunzo ya Fasihi ya Kiswahili ya Mabati-Cornell kutokana na mswaada wake wa ushairi, N’na Kwetu, ni shairi hili ndilo nilaolipenda mno katika kazi kuliko mengine. Ndiyo N’na Kwetu miye.
Diwani ya Mohammed Ghassani ya ‘Andamo’ kwa sasa inapatikana kwenye mitandao ya Amazon, Google Play na iTunes. Ambapo unaweza kuandika neno “Andamo: Diwani ya Mohammed Ghassani.”
Nimalizie uchambuzi huu leo kwa kukuonjesha kipande chake hiki kinachonisisimua kila wakati, na aghalabu huwa ninakisoma bila kuchoka:
Raru pakwe n’jaani, si kwa fundi wa viraka
Hata awe fundi gani, haliwezi sarifika
Utavisha vyerehani, matomo hayazibika
Raru lishavyoraruka, hili halina nshoni.
TANBIHI: Makala hii iliandikwa na Markus Mpangala na kuchapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Mtanzania la tarehe 3 Juni 2016. Mwandishi anapatikana kwa barua-pepe: mawazoni15@gmail.com.