KISWAHILI KINA WENYEWE

Dunia kokwa ya furu: Amali ya Misemo ya KiPemba

Jitihada za ukusanyaji na uchambuzi wa data za kifoklo za launi za Kipemba si jambo geni (angalia Whiteley (1958) na Mlacha (1995:21-25). Lakini kadri, muda unavyopita jitihada hizo zinaelekea kupungua kasi. Suala la uhifadhi wa ‘bohari la hekima ya wahenga wetu kimaandishi’ ni la wajibu na halipaswi kusita. Katika mradi huu unaoendelea, tumeonelea kufanya mambo mawili makuu (a) kuorodhesha na kujadili data za kifoklo zenye kuweka wazi umahususi wa launi za Kipemba. (b) Kuorodhesha na kuchambua kiethnografia data hizo kwa mujibu wa mtazamo wa uchambuzi wa data za kifoklo kimuktadha (Hymes (1962).

Makala ya Ahmad Kipacha na Ibun Kombo wa Chuo Kikuu cha Dodoma iliyochapishwa kwa mara ya kwanza na Journal of Humanities, Toleo Na. 1 la mwaka 2009.

 1. 0 Utangulizi

Uhifadhi na uchambuzi wa mapokezi ya ’bohari la hekima’ katika jamii ya Waswahili na makabila ya Kitanzania kimaandishi ni jitihada zinazojidhihirisha katika kazi mbalimbali kama vile Steere (1870), Taylor (1891), Farsi (1958), Omari na wenzie (1975), Ifedha (1987), Petrenko (1988), Mlacha na Hurskainen (1995), Madumulla (1995),Wamitila (1999, 2001), Mauya (2006)n.k. Kila jamii zina hazina za kifoklo. Hazina hizo husawiri namna ya jamii hizo zinavyoutizama ulimwengu na hujiumbia njia za kuelezea namna wanavyouelewa ulimwengu huo kupitia kazi mbalimbali za kifoklo kama vile ngano, michezo, sanaa, nyimbo, akida, mapishi,uchoraji, uzalishaji mali, ada nk.( Palmer1996:113-114)

Kazi za kifoklo zinafanya kazi katika mzunguko mzima wa maisha ya mwanajamii kuanzia mazazi, makuzi, hadi umauti na hata baada ya umauti4 ambapo mara kadhaa tunaona wanajamii mbalimbali wanavyowasiliana na mizimu na hata mizuka. Kwa namna kila jamii inavyosawiri maisha yake ndipo tunapata umahususi au mfanano wa jamii hizo, hivyo kazi za kifoklo si lazima zitofautiane kiutamaduni paweza kuwa na mfanano tunaoweza kuulinganisha (Hatch and Brown 1995).

Mpemba anapoamka asubuhi, mandhari yanayomzunguka, shughuli zake za kiuchumi, namna anavyosafiri kutoka kijiji kimoja hadi kingine, namna anavyofurahi, anavyohuzunika, anavyokabiliana na majanga, falsafa inayomwongoza, ibada, tekinolojia asili anayojiundia na kurithishana, na mahusiano ya kijamii ndiyo huzua mazingira ya uibukaji wa data za kifoklo. Tuchukulia kwa mfano Waswahili kwa ujumla wanavyoitazama dunia; Dunia kwao ni uwanja wa fujo au tambara bovu, Kwa Mpemba huenda mbali zaidi na kufuatana na mazingira yake Dunia kwake ni kokwa ya furu/fuu.

Furu ni tunda linalopendelewa na watoto na huliwa zaidi wakati wa njaa. Baada ya kuliwa na mwanadamu mara nyingi kokwa yake hutupwa na hapo fungo, kuku, popo na wanyama wengine hujilia kokwa hiyo na si lazima isagike tumboni, hivyo yaweza kutoka kwa njia ya kinyesi na kuendelea kugugunwa na vinyama vya kila aina. Hii ndiyo dunia kwa mtazamo wa Mpemba. Kila mmoja anaitumia kivyake na kuiacha. Dunia si tunda lenye thamani sana, kama ilivyo kokwa ya furu unalazimika kuila kutokana na njaa. Hakuna aliyeomba kuja duniani kila mmoja anajistukizia amefika na hana budi kuondoka na kuiacha dunia. Tunachoweza kufanya duniani kwa kila mmoja wetu ni ‘kuguguna’ kokwa ya furu. Maisha kwa ujumla kwa Mpemba ni mbio za chumbani ziishiao ukutani yaani Dunia ni Duara! au Lomhlaba Unzima, Lohmhlaba ‘Dunia ni fujo tu’ chembilecho Wazulu.

2. Kisiwa cha Pemba

Eneo la utafiti ni kisiwa cha Pemba ambacho pamoja na kisiwa cha Unguja huunda Zanzibari kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kina ukubwa wa kilometa za mraba 1000 na wakazi takriban 413, 3861(Sensa 2002). Kimegawanyika katika mikoa miwili ya Kaskazini na Kusini Pemba. Mkoa wa Kaskazini una wilaya mbili za Wete na Micheweni na hali kadhalika mkoa wa kusini una wilaya mbili za mkoa wa Kusini na Chakechake. Vipo visiwa vidogovidogo visivyopungua saba na vina wakazi wapatao 2,683. Moja ya kisiwa kikubwa ni Kojani chenye watu wasiopungua 3,976 (Sensa 2002).

Vipo visiwa visivyokaliwa watu vya Misali na Kokota bali vina utajiri mkubwa wa maliasili na ambavyo kwa sasa hupendelewa kutembelewa na watalii. Kisiwa cha Pemba kinamsitu maarufu uitwao msitu wa Ngezi katika eneo la ngezi wilaya ya mkoani kusini Pemba. Pia kuna upwa au fukwe la kupendeza liitwalo Vumawimbi ambayo ni sehemu watu hupendelea kutembelea na kufaidika na mandhari ya bahari. Historia ya Pemba haitoshi bila kutaja eneo la Pujini katika wilaya ya Chakechake mkoa wa kusini ambapo kuna eneo mashuhuri la makumbusho ya kihistoria liitwalo Mkamandume.

3Shughuli za Kiuchumi na kijamii

Wapemba hujishughulisha na kilimo, uvuvi na ufugaji. Mazao makuu yalimwayo ni kama vile muhogo, mpunga, viazi, migomba, mtama na mbogamboga. Zao kuu la biashara ni karafuu. Wapemba pia ni wafugaji wa wanyama kama vile ngombe, mbuzi, kuku na bata. Idadi kubwa ya Wapemba ni waumini ya dini ya Kiislamu ingawa imani na tiba za jadi na hata pungwa zingali hai. Upo msemo kama vile gae ni chombo siku za homa na nyimbo ya wavuvi wa Pemba kaskazini isemayo:

 • Nimpe mwanangu nahoza kombo,
  Nimpe kigae na ubani moto.

Msemo na nyimbo hiyo zinadokeza utabibu wa jadi kupitia taswira ya vigae na mafusho. Wapemba hutumia tiba za jadi ya kuchoma mafusho ili kumpa mgonjwa afueni aondokane na homa au hata kuondoa mkosi wa kukosa samaki baharini. Zipo data za Kifoklo zinazoambatana na michezo ya jadi kama vile mchezo wa ng’ombe haswa sehemu za Chwale (Ingrams 1931 : 422), nyemi na kiumbizi michezo ya sherehe za mwaka-kogwa, mashindano ya ngarawa, mchezo wa watoto uitwao kipalepale na hata mchezo wa wanawake pekee sehemu za Kojani uitwao mwanda. Hayo ni maeneo ya chimbuko na uhifadhi wa data za kifoklo.

 • Nadharia za Uchambuzi wa data za Kifoklo

Uchambuzi wa data za kifoklo umepitia mikondo yenye mitazamo mbalimbali: kidini, kitamaduni, kijamii, kipragmatiki, kiutambuzi nk Mtazamo wa kiutambuzi unaruhusu kuibua sifa za kiubia za utambuzi wa kumbo mbalimbali za kifoklo. Mtazamo wa kijamii na ule wa kipragmatiki unaruhusu kuchambua mazingira na itikadi zilizozusha kumbo mbalimbali za kifoklo zaidi ya kuangalia muundo wa kiisimu wa kumbo hizo. Aina ya kumbo tunayokusudia kuishughulikia katika kazi hii ni ile ya misemo. Kwa mujibu wa Mulokozi (1996:35) ‘semi ni tungo au kauli fupifupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo muhimu ya kijamii’. Semi zaweza kuwa methali, vitendawili, potominia nk.

Kiutambuzi, semi huhusisha usitiari na uhamishaji wa maana au sifa ya kitu kimoja na kukihamishia katika mazingira mengine (Lakoff na Johnson 1980). Tendo hilo linapelekea kuunda skema ya kisitiari (Lakoff na Turner (1989: 193-194). Tunaweza kuhamisha mawanda ya maisha ya viumbe vinavyotuzunguka katika mazingira yetu na kuyatumia mawanda hayo kwa kutanabaisha wanadamu. Sungura ni mnyama mjanja; Simba mtumia maguvu na mwenye utawala na hata ubabe; nyoka kiumbe asiyeaminika na msaliti; punda mtumishi au ‘mtwana’ mbeba mizigo; Pono mlala hovyo n.k Inakuwa rahisi kwa wanajamii kubandika sifa za uanadamu kwa viumbe wasio wanadamu kama kwamba hiyo ndiyo hali halisi ya mambo ilivyo hali ya kuwa huo ni ulinganifu wa kisitiari tu (Lakoff & Turner (1989: 194).

Ieleweke kwamba ingawaje mara nyingi tunadhani misemo hujinasibisha na tamaduni za jamii fulani tu, uoni huo unatokana na ufinyu wa kutokujishughulisha kuangaza katika jamii mbalimbali na kuibua visawe vya semi katika jamii mbalimbali.

Hatch and Brown (1995) wanadai kuwa hata kama hatuna semi za aina moja katika jamii mbalimbali, bado tunaweza kupata misemo ifananayo na yenye kusudio au dhima ya aina moja kwa vile wanadamu wana michakato ya kiumilisi ifafanayo dunia nzima (kiubia). Misemo ya ‘mtoto wa nyoka ni nyoka’ au ‘wema hauozi’ unathibitisha ubia wa kiumilisi katika jamii mbalimbali kwa kule kutapakaa katika jamii mbalimbali.

Hali hii inapelekea kuwa na misemo ya aina mbili (i) yenye sifa za kiubia za kuadabisha walimwengu kidhima na si lazima iwe kimaumbo. (ii) misemo mahususi iliyozuka kufuatana na matukio maalumu ya kihistoria, desturi mahsusi za wanajamii fulani, au tukio maalumu lisilo na sifa za ubia.

Hivyo hutokea jamii fulani ikawa na vibandiko au alama zao mahsusi zinazoelezea umahali, tukio au usuli binafsi.wa jamii husika. Misemo ni zao la jamii, na ili kuitafsiri itakiwavyo hakuna budi kuzingatia muktadha. Tunajifunza utamaduni na ada za jamii husika kwa kuchambua misemo yao.

Kwa mujibu wa Hymes (1962) ipo haja kwa wanaethnografia na (hata Wanalahajia) kujiingiza katika kazi za uchambuzi wa data za kifoklo ikiwemo misemo kama wafanyavyo katika uchambuzi wa data za lugha asilia. Data zote zina uwiano kwani zote zina vipengele vya kijamii vyenye ruwaza mahsusi. Huo ni mtazamo unaopelekea kuchambua data za kifoklo kama msimbo maalumu. Mtazamo huo unapendekeza kuwa iwapo lugha inaweza kuchambuliwa kimuundo basi na data za kifoklo nazo hazina budi kufuata mkondo huo.

Wapo walioitikia wito huo hususani kazi mashuhuri, ingawa ya kitambo kidogo, ya Arewa na Dundes (1964) ambayo ilichambua methali za Kiyoruba kiethnographia kwa kuzingatia kipengele cha muktadha.. Data waliyochagua ya methali za Kiyoruba ni zile zihusuzo malezi ya watoto tu. Hivyo walichagua mifano 12 yamethali za Kiyoruba zihusuzo malezi ya watoto ikiwemo ile methali mashuhuri ya ‘asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu’ ambapo wayoruba wao husema:

(2) ‘mtoto mtukutu na aliyekosa malezi basi atafunzwa na wasio wazazi’ (tafsiri ni yetu).

Tumekusudia kufuata mtindo wa Arewa na Dundes katika kuchambua amali ya misemo mahsusi ya Kipemba kwa kuzingatia muktadha wa shughuli za Uvuvi na ule unaohusu Kilimo. Shughuli hizi mbili za Kiuchumi ndizo zinazowashughulisha wenyeji zaidi kuliko shughuli nyengine yeyote kisiwani hapo.

Tutaangalia ni kwa namna gani taswira za uvuvi na kilimo zimeibusha misemo na hata leksimu mahsusi za launi mbalimbali za Kipemba. Kwa mujibu wa Lakoff na Johnson (1980: 14-17) dhana zitokanazo na mazingira na tamaduni zetu hujenga sitiari na fikra za kimetonimia tuzitumiazo kwenye kuunda misemo.

Mbali ya kuchambua misemo kwa kuzingatia muktadha, Evelyne Brouzeng (1984) ametushauri katika “Stylistique comparée de la traduction de proverbes anglais et français” kwamba iko haja ya kufafanua misemo kwa kulinganisha visawe vya misemo katika lugha mbalimbali kama njia ya kufasiri misemo bila kujali utofauti wa miundo ya misemo hiyo katika lugha mbalimbali.

Mfanano wa misemo katika lugha mbili au zaidi hutoa picha ya uoni na fikra za mwanadamu.kwa ujumla. Tumezingatia hilo katika uchambuzi wa baadhi ya misemo mahsusi ya Kipemba § 4.0. 3.0 Data za Kifoklo za Kisiwani Pemba Katika kila nyanja za kimaisha ya Wapemba tunaweza kuibua na kubainisha data za kifoklo. Mfano mzuri ni pale tunapoona wavuvi kama wale wa Maziwang’ombe na Chwale (Pemba–kaskazini) walivyo na nyimbo mahsusi za kutiana moyo wanapokosa samaki, wanapoona samaki baharini, wanaporudi baharini na nyakati wanapovuwa. Siajabu kusikia wavuvi wakiimba:

(3) dadee tukavue ngogo maji yajara
sebu wee nguo yangu ndogo kutiliwa vumba.

Wavuvi na wanajamii kwa ujumla hutiana moyo kuwa mwenda kende hakosi japo guotenge, sawa na Waswahili wasemavyo kuwa mgaagaa na upwa hali wali mkavu, ni usemi maarufu sehemu za Pemba kaskazini. Mintarafu ya usemi huo ni kuwa iwe isiwe ajitoae kutafuta basi hawezi kuula wa chuya’. Wavuvi na wanajamii wengine pia huhimizana kumtegemea Mungu katika kazi zao kwani msafiri ni ndi pwani. Shughuli nyengine kubwa inayowashughulisha wakazi waliowengi wa Pemba ni Kilimo. Umuhimu wa kilimo unadhihirishwa na usemi wa achanikae kwenye mpini hafi njaa. Wenyeji waliowengi hujishughulisha na kilimo cha kawaida cha jembe la mkononi katika makonde. Huko makondeni kuna kazi mbalimbali za kifoklo zinazoendana na shughuli hizo za kilimo.

Upo usemi usemao ungepiga teo mtama waliwa, na nyimbo ihamasishao kulinda mpunga:

(4) Kamange mambo ni mpayo
Yamuemeza mambo mengine
Mwinyiwi nbalozi tayatengenza
Kuna njiwa esha mpunga ngwa, hebu kuruza
Siku ya leo tampiga ndifu tamuumiza

Hoja kuu hapa ni kuhakikisha kuwa ndege waharibifu kama njiwa au chechele hashambulii mazao kama ya mpunga au mtama na kuisababishia jamii hiyo kuambulia kazi ya ‘kijungu meko’ au ‘bwaganchagase’. Mpemba ‘halisi’ kapambwaje kimisemo?; mpemba akipata gogo! hanyi chini; mpemba hakimbii mvua ndogo. Hii inamaanisha kuwa Mpemba halisi ana hulka zake nazo si ajabu kujitokeza apatapo maisha mazuri na huweza kujidhihirisha kwa hilo kwa namna ya mabadiliko ya tabia, hulka, migoko na hata vitimbwi. Je, Pemba kuna sifa gani? Kwa vile Pemba ni kisiwa kidogo, ujaji wa wageni haukwepeki haswa kutokana na mahitaji ya wahudumiaji mikarafuu katika kipindi cha uchumaji wa karafuu (Gray 1962 :63). Baadhi ya wageni mashuhuru tunaodokezwa kwenye nyimbo za bembezi za kinamama wa KiPemba walikuwa ni Wanyamwezi.

(5) Nilisafiri na bwana akanitupa malezi
Hashinda nchana kutwa nami njaa siiwezi
Hatamani kujiuza kwa Songoro mnyamwezi

Songoro Mnyamwezi imetumika kama taswira ya ‘jitu’ (la bara) lifanyalo kazi na lenye mafao ambalo mlalamikaji hakustahili (mke wa mtu) kujiuza kwake ili ajikimu kwa chakula kutokana na mumewe (mzawa) kutomuwajibikia. Katika uga wa ngano za Kipemba nako kuna hazina kubwa inayohitajia kufanyiwa kazi za kitaaluma. Ni sehemu ya mradi huu kulishughulikia hilo kwa siku za karibuni. Makusanyo yetu ya awali hususani sehemu za Micheweni yamedhihirisha utajiri wa ngano za Kipemba. Hata namna ya ufunguzi wa vigano upo kwa namna yake pale tunapoona fanani na hadhira (kwenye mabano) kuwasiliana kwa mtindo ufuatao:

(6) Paukwa (Pakawa)
Mwana wa kasa (Hutakasa)
Ukiwa nalo (Pasha)
Ukitakua nalo (Pashua)

Mwisho wa kigano huishia na ‘hadithi yangu insozea hapo’. Vipo vigano mashuhuri kama vile Kanlola na Kinyangaa, Hamad na Hamad, Harudiki n.k ambavyo ndani yake kuna utajiri na maki ya misamiati mahsusi ya Kipemba yenye faida kubwa katika taaluma ya Lahajia na Isimu-ethnografia.

Pengine mchango mkubwa wa data za kifoklo za Kipemba kimaandishi ni kazi ya kitoponimia au fumbojina ya Mlacha (1995:21-25) yenye kubainisha etimolojia na usuli wa majina ya maeneo mbalimbali ya kisiwa cha Pemba. Kuna mfanano wa mtindo wa uwasilishaji wake na ule wa kazi mashuhuri ya Webb Garrison (2007) iitwayo Why you say it yenye kuonyesha vyanzo vya misemo ya Kiingereza inayotumika kwa sasa. Tumeonelea ni vyema tuifupishe kazi ya Mlacha (1995) kwa njia ya jedwali la kimatriksi kama inavyoonyeshwa katika Jedwali 1.

Hili eneo la potonimia linahitaji kuendelezwa zaidi ili jamii ifaidike na hazina ya kihistoria iliyojifumbata ndani ya majina hayo. Majina yaliyoorodheshwa katika Jedwali la 1 ni sehemu ndogo tu ya hazina inayosubiri utafiti zaidi. Je, vyanzo vya majina ya Chakechake, Wete, Maziwa Ng’ombe, Micheweni, Kivumoni, Mitundafumoni, Majimbuta, Mkilindini n.k ni vipi? Mpemba anaposema enzi za chochoni au mibie ni matukio gani katika tarikhi za wenyeji yalizuka hadi kipindi hicho kuitwa enzi za mibie?18 Utafiti wa aina hii unastahili pia kushughulikiwa kama sehemu ya Isimu-Jiografia hususani tawi linaloinukia la Isimu Sura-Nchi (Linguistic Landscaping).

Jadweli Namba 1
Jadweli Namba 1

Kwa namna tulivyoziangalia data za awali za kifoklo za Kipemba tunashawishika kuunga mkono usemi maarafu wa mwanaisimu wa Kijerumani, Hugo Schuchardt, kwamba ‘kila neno lina historia yake’. Hivyo kila hadhari tumeichukua kufuatilia etimolojia na usuli wa maneno mbalimbali ya Kipemba kama yanavyojitokeza katika semi tunazozishughulikia katika makala haya.

 • Misemo ya Kipemba katika Muktadha wa Shughuli za Uzalishaji Mali (Uchumi)

Kama tulivyoona katika § 1.1.1 shughuli kuu za kiuchumi kisiwani Pemba ni uvuvi na kilimo. Tunakusudia kuainisha na kuchambua misemo inayotokana na shughuli hizo. Tutazingatia ubainishaji wa sifa za kiubia na zile mahsusi kwa kujaribu kufafanua au kufasiri misemo ya Kipemba na visawe vyake katika jamii mbalimbali duniani. Tutazingatia pia umahususi wa misemo ya Kipemba kwa kubainisha leksikoni mahsusi na mazingira yaliyopeleka kuibuka kwake.

4.1 Misemo katika muktadha wa Uvuvi na Shughuli za Bahari

(i) Mgeni hachomi pweza akanuka

Pweza (Octopus) samaki wa baharini mwenye minywiri minane (mikia minane) anapokauka akachomwa harufu yake hufika mbali sana. Lakini kwa mujibu wa mafundisho ya usemi huu mgeni ni mtu wa kuvumiliwa iwapo atafanya jambo lolote lile hata la kukerehesha mithili ya ‘harufu ya pweza’. Wenyeji hawana budi kuvumilia na kumsitiri hadi mgeni huyo aondoke. Lakini iwapo hataondoka na akawa wa kuishi milele basi ndipo wanajamii wanakumbushwa kuwa Pemba peremba ukienda na joho utarudi na kilemba. Wazawa wanakumbushwa na usemi huo kuwa wasiingie hofu na wageni kuwa pengine watazua kizaazaa kwa kuleta mila na hulka faafu. Hivyo kwa usemi huo, wenyeji wanaaswa kuwavumilia wageni hata kama atakuwa barobaro wa kupindukia kwani kadri muda unavyopita silsila za kipemba ‘zitamnyoosha’ na tabiai zake zitalandana na desturi maridhawa za wenyeji. Hivyo harufu ya pweza ni taswira ya kero ya mgeni inayoweza kuvumilika. Katika kipindi hiki cha maingiliano ya watalii na wageni usemi huu waweza kutumika pale wenyeji wawaonapo mfano watalii ‘wakizungu’ wakiwa na taratibu tofauti za mavazi au hata malaji. Si ajabu kuwaona wageni wajinsia mbili wakikumbatiana hadharani. Jambo kama hilo ni mwiko kwa wenyeji kulitenda hadharani. Kwa vile, mgeni ni kuku mweupe hivyo kingiacho mjini si haramu. Mbali ya pweza, Mauya (2006: 2) ameonyesha kuwa jamii ya waswahili wamemtumia ‘nguru’ kwani naye anayo harufu isiyofichika sawa na ile ya pweza. Tuna wasiwasi kuwa taswira ya nguru yaweza kupotea kwani kwa sasa uvundikaji wa ‘nguru’ si biashara yenye umaarufu. Samaki wamekuwa adimu kiasi kwamba ubanikaji badala ya uvundikaji ndio mbinu ya haraka ya kuzalisha ng’onda badala ya nguru. Upo msemo wa Kirusi unaoshadidia hali hiyo kwa kusema kuwa ‘kama umekubali kuwa mwenyeji wa mgeni wako basi na pia ukubali kuwa mwenyeji wa mbwa wake’.

(ii) Papa akipea mafuta huwapa wanawe

Papa ni simba wa baharini. Hupendelea kukaa bahari kuu iitwayo mweza. Mbali ya kuwa ni samaki aogopwaye lakini anafaida nyingi licha ya kuwa na uwezo wa kumjeruhi na hata kumuua mvuvi baharini. Kila kiungo cha papa kinaliwa, kuanzia mapezi hadi utemba/chisha (utumbo). Hali hii inapelekea kuwepo kwa msemo wa Kiswahili usemao avumaye baharini papa ingawa wengine wapo. Hivyo taswira ya ukubwa na mabavu ya papa bado inaendelea pale inapotegemewa kuwa angalau wanadamu au viumbe wengine wangefaidika na mafuta ya papa yanapomzidia haswa baada ya kuwala samaki wengine na hivyo kujitengenezea ziada ya mafuta mwilini. Katika hali isiyotegemewa, papa anawagaiya wanawe mafuta hayo. Ukweli juu ya usemi huu unadhihirishwa na vitendo vya wabadhirifu wa mali na ‘mafisadi’, ambao baada ya kuwanyonya wanyonge faida ipatikanayo wanatumia kwa maslahi yao na watoto au ndugu zao. Usemi huu unamaanisha kuwa ‘kwa kila mtafutaji manufaa basi hula na wakwao’ na pengine hata ‘ukichuma janga basi utawaponzea nduguzo’. Usemi huu husemwa na wanyonge pale wanapokumbushana kwamba wasijihangaishe kuwabembeleza walionacho kwani hawatakumbukwa kamwe.

(iii) Kuvua na kuvuvuga

Kuvuvuguka ni kuwatunga samaki hali yakuwa bado wapo chomboni huku ukiendelea na shughuli za uvuvi. Wavuvi huko Pemba hupendelea kuwahifadhi hao samaki waliotungwa katika chombo maalumu kiitwacho mkajasi. Usemi huu unatoa tahadhari kuwa unapowavua samaki hakikisha umewatunga kwani dau laweza pigwa wimbi na chombo kikaenda mrama hadi kuparaganisha samaki chomboni na kutumbukia majini ukawa umepata hasara kwani ulishawavua na hivyo kujikuta umeambulia patupu. Iwapo umewadunga kwenye mtungo, basi inakuwa rahisi kuwadhibiti inapotokea mushkeli.Upo usemi unaoendana na huo kwa Waswahili: ‘Usiache kunanua kwa kutega’. Iwapo umewakamata ndege usiache kuwadhibiti kwa kutegemea mtego ambao haujanasa wengine. Msemo wa Kiswidishi unasema kuwa ‘Usitupe ndoo ya zamani kabla hujajua iwapo ndoo mpya inaweza kuzuia maji (haina tundu)’. Waairishi nao wao wanausemi usemao kuwa ‘si samaki mpaka kafikishwa kwenye upwa’ sawa na ‘pesa iliyo kibindoni ni ile iliyochumwa’ (msemo wa Kiskotishi) au kwa Waswahili tunakuta usemi wa Hamadi kibindoni silaha iliyomkononi. Dhima ya ubia ya kudhibiti kile ulichokipata kwanza kabla ya kutoka kwenda kutafuta kingine inajitokeza katka jamii mbalimbali na si Pemba peke yake. Tofauti iliyopo hapa ni ya kifani tu na muktadha ulioibusha dhana ya kuelezea haja ya kudhibiti kile ulichokwisha kitia kibindoni.

(iv) Lishalo vuusha si dau?

Dau ni chombo kikuu kitumikacho kwa uvuvi katika ‘ukanda wa Waswahili’ (Swahili corridor). Wavuvi wengi hawana uwezo wa kiuchumi kuwa na vyombo vikubwa kama vile majahazi na hata meli. Hivyo madau hutumika kwa shughuli za uvuvi na hata usafiri. Ingawa kuna vyombo vingine kama vile mtumbwi au mchoo ambavyo wavuvi wadogowadogo wanavimudu kuvimiliki. Katika mazingira ya ukanda huu wa pwani, siajabu kusikia pia majina ya watu kama vile Mwandau au Dau yanayotokana na chombo hicho. Mbali ya usemi huo kuna usemi mashuhuru katika ukanda wa uswahili usemao Dau la mnyonge haliendi joshi. Jina la Dau linawakilisha vyombo mbalimbali vitembeavyo kama vile gari au jahazi.

Usemi wa lishalo vuusha si dau? Ni kauli-swali (rhetoric) inayokusudia kuonyesha kuwa dau likishakuvusha basi faida yake haipo tena waliacha hapohapo na kuendelea na safari. Usemi huu una kisawe chake katika Kiswahili sanifu nacho ni ‘pema si japo pema ukipema si pema tena’. Shauku ya jambo ni pale ambapo hujalitambua au kulionja lakini ukifanikiwa huwi na shauku kama ile ya mwanzo. Hutokea katika jamii ya zetu mwanaume akafanya jitihada kubwa kumgombea binti kigoli lakini anapomnasa na kumweka katika himaya yake basi vitimbi vinaanza na sasa anamkalifu kwa vitendo vya kupunguza pendo kutokana na kuchujuka kwa pendo. Wanawake wa Pemba huwaimbia watoto wao nyimbo ya bembezi ilalamikayo kuhusu kupungua kwa thamani kwa waume zao:

 1. Ulipo ukinitaka habarí zefika Wete
  Wepita ukitangaza madawani na nkote,
  sasa hunitaki tena hitajwa watema mate.

Mwimbaji amemtumia mtoto kama njia ya kufikishia malalamiko yake kwa mumewe kuwa thamani yake imepungua kwa vile yeye dau (mke) lishamvuusha yule mume. Mume hana abarrí naye tena bali yuangalia mbele tu na safari yake, pengine yuko njiani kumletea mke wa pili kama si kumtaliki kabisa.

 1. v) Mwenda tezi na omo hurejea ngamani.

Dau au ngarawa linavijisehemu ndani yake vyenye majina maalumu. Omo ni sehemu ya mbele. Ngamani ni katikati na tezi ni mwishoni mwa dau. Katika shughuli za uvuvi na hata kuliendesha dau lenyewe, mabaharia wataenda mbele na nyuma lakini hatimae wataishia katikati au ngamani. Usemi huu ni sawa na usemao ivunjikayo ondo hurejea zizini au ng’ombe akiumia mguu malishoni hurejea zizini kulelewa. Usemi huu unakumbusha kuwa ‘uwende kusini au kaskazini nyumbani ni nyumbani tu’ utarejea kulelewa pale mtu akiharibikiwa kimaisha au kupata maradhi ugenini. Hivyo wapemba na wanajamii kwa ujumla wanaasana kuwa usisahau kitovu chako au usisahau ubaharia kwa sababu ya unahodha.

(vii) Mtu huapa na bamvua haapi na bahari

Shughuli za uvuvi hufanyika baharini. Kisiwa cha Pemba kimezungukwa na bahari. Shughuli za baharini mara nyingi hutegemea pepo. Zipo aina mbalimbali za pepo kama vile kusi, kaskazi au matlai. Pepo hizo huwaongoza wavuvi katika shughuli zao. Nyakati zote bahari ipo tu kinachobadilika ni nyakati za pepo. Hivyo kinachotakiwa kwa mvuvi na watu mbalimbali kuangalia zaidi ni nyakati hizo za pepo katika kupanga shughuli zao za uvuvi na usafiri. Hivyo kuapa ni sawa na kupanga ratiba ya shughuli za baharini. Nyakati za pepo zimezua semi mbalimbali kama vile usichezee kusi kwa tanga bovu. Nyakati za kusi kunakuwa na upepo mkali hivyo uwapo utakuwa na tanga bovu linaweza kuchanika na chombo kikaenda mrama na pengine kupotea baharini na kupata madhara kwa wavuvi au abiria. Kusi huweza kusababisha muja yaani mawimbi makubwa. Mara nyingi wavuvi hukutwa na ajali za baharini na inapotokea kuwa tu wamekumbwa na maafa baharini na hivyo kuzama, pale maiti ipatikanapo huwa muhali kwa muda mrefu hivyo mazoea yamekuwa ni kuwazika haraka maiti hao mara tu wapatikanapo. Kutokana na hali hiyo usemi ukazuka usemao maiti wa maji halazwi. Hii inamaanisha kuwa kwa vile maiti wa maji anakuwa ameharibika sana haiswihi kumweka kwa muda mrefu pengine kungojea ndugu zake katika hali hiyo ya kuharibika. Ni kawaida kwa waliofiwa kuangalia hali ya maiti na iwapo itagundulika kuwa hawezi kuendelea kuwekwa ili ndugu wajikusanye basi huzikwa mara moja. Ujumbe uliopo katika usemi huo ni kuwa yapo mambo ambayo hayatakiwi kucheleweshwa yanapotokea. Kuna aina ya mchele ukipikwa unatakiwa uliwe ukiwa bado mmotomoto kwani mkiuchelewesha unakuwa unatawanyika na hivyo kutokupendeza. Iwapo mwanamali ametokea kupata mchumba nanyi mmeridhika nae basi msicheleweshe harusi kwa kisingizio cha kujitayarisha kwa muda ili mfanye harusi ya kujinaki. Katika ngojangoja hiyo paweza kutokea madhara au uharibifu mkakosa mwana na maji ya moto. Hivyo taswira za bahari na pepo (bamvua, kusi) zake zimetumika kimetonimia kuzalisha misemo mbalimbali.

(vii) Mcha maago hanyele huenda akauya papo.

‘Ago’, ‘yago’au ‘dago’ ni kambi ya muda mfupi ya wavuvi ambayo hutumika kwa ajili ya kufanyia shughuli zao, huweza pia kuwa ni kambi ya kuchuma karafuu au kwenda shamba baada ya bamvua au mavuno. Shughuli zinapokwisha watu huhama, hivyo inashauriwa kutokuichafua au kuiharibu kwani huenda mkarudi tena papo. Sehemu nyingi za pwani au hata visiwa visivyokaliwa vatu huanzishwa aga au madago. Wavuvi hulazimika kuhama makwao kutegemea na misimu na upatikanaji wa samaki. Wavuvi wa Pemba huweza kupiga dago Mafia au Kunduchi. Hali hii wakati mwengine imeanzisha mitala. Wavuvi wengi wanakawaida ya kuwa na wake zaidi ya mmoja kutegemeana na pwani wanapofikilia. Wavuvi wa Ununio huweza kuoa Unguja na wale wa Unguja kuwa na wake pwani ya bara. Sababu ya msingi ya kukaa katika madago ni upunguzaji wa gharama hasa ya pango katika miji ya ugenini. Madago huwa ni ya wanaume pekee. Usemi huu unaungwa mkono na ule usemao ‘usihadaliwe na usiku wa kiza ukanya njiani’ au pale Waswahili wasemapo ‘usitukane wakunga na uzazi ungalipo’. Lile jambo linalokusitiri basi huna budi kuliheshimu hata kama laweza kuonekana thamani yake imepitwa na wakati. Dago ni ‘nyumba’ iliyombali na nyumba halisi hivyo haina budi kuachwa katika mazingira mazuri huenda ukarudia papo kuendana na mazingira ya bahari na upatikanaji wa samaki.

4.2 Misemo katika muktadha wa Kilimo na Ufugaji

(i) Msitu mpya na komba wapya

Shughuli za kilimo kisiwani Pemba zina hatua mbalimbali. Kilimo kinaanzia na utayarishaji wa mashamba. Katika hali ya kutayarisha mashamba mkulima anaweza kujikuta amechomwa na mwiba na hivyo anashauriwa utoe wa tako ndio utoe wa guu. Iwapo umechomwa na mwiba mmoja ukiwa matakoni na mwengine mguuni basi washauriwa uutoe ule wa matakoni kabla ya ule wa miguuni. Mantiki yake hapa ni kuwa ukifanya hivyo utajipa urahisi wa kujihudumia vyema badala ya kukimbilia kutoa mwiba wa mguuuni. Kila jambo lazima lifuate hatua kutoka chini hadi kulekea juu. Usemi huo unafanana na ule wa Kiswahili sanifu usemao kabla ya ‘kutoa kibanzi katika jicho la mwenzio ondoa boriti jichoni mwako’. Mara kadhaa katika mashamba au hata karibu na majumba ya watu huweza kutokea nyoka. Mara aonekapo nyoka huuliwa mara moja. Ingawaje nyoka mdudu asiyetakiwa na karibu kila mwanajamii, yawezekana akatokea msamaria mmoja akawasihi au kuwaomba watu wamwachie atokomee porini asaidie kula panya. Hivyo Wapemba wanaamini kuwa pauliwapo nyoka hapakosi ndombezi. Hali hii inatokea katika jamii zetu haswa pale tunapomkamata mwizi na pakatokea makundi yanataka kumuua kabisa na wengine kutaka apelekwe polisi ili sheria ichukuwe mkondo wake.

Shughuli za uandaaji mashamba hupelekea kusafisha misitu na vichaka. Pemba kuna misita kadhaa kama vile msitu maarufu wa Ngezi. Kwa vile misitu hiyo inakaliwa na vinyama kama vile komba., wakati wa kusafisha misitu hiyo, komba nao hutokomea. Mara baada ya msitu kurudia upya, vinyama vipya navyo hurudia. Hivyo usemi wa msitu mpya na komba wapya twaweza kuulinganisha na wa Waswahili usemao ‘hakuna masika yasiyokuwa na mbu’. Masika inapoondoka na kuja nyakati zingine huondoka na mbu wake.

Katika maisha yetu ya kila siku tunashuhudia mabadiliko ya kisiasa ambapo viongozi wapya na mawaziri wapya wanachagulia katika vipindi fulani fulani. Watu wanaweza kufurahi mabadiliko hayo kwa kuondokea na adha fulani iliyokuwa ikiambatana na uongozi wa zamani lakini pengine matatizo mapya yanaweza kuzuka na hivyo matumaini yetu ya hali bora yakafifia. Tunatahadharishwa kuwa ingawa ni msitu mpya ‘uongozi mpya’ waharibifu nao ni wapya.

Taswira ya ‘msitu’ imetumika katika usemi mwingine wa Kipemba usemao msitu hawishi jengo. Mantiki ya usemi huo ni kuwa katika msitu kuna kawaida ya kujizalisha miti hata kama tutakata baadhi yake kwa kujengea. Muktadha wa usemi huu nipale ambapo mzazi anaweza kumwambia mwanawe wa kiume au hata wa kike asihuzunike anapokuwa amemkosa mtu aliyemtaka kumuoa au kumposa kwani msitu hawishi jengo utampata mwingine na kila situ wazuri wanazaliwa.

(ii) Udongo upate uli maji

Kazi ya kuandaaa mashamba inakuwa rahisi iwapo udongo umelainika. Hali ya udongo wa Pemba hutegemea mvua. Vipindi vya mvua vya vuli na masika hufuatana na shughuli za uandaji mashamba na upandaji. Hivyo, wakulima wanashauriwa kwamba udongo upate uli maji. Anza kushughulikia utifuaji wa ardhi nyakati zile ambazo udongo uko majimaji. Jamii za wafugaji wao badala ya kutumia taswira ya udongo hutumia taswaira ya ngozi ndipo usemi wa Ngozi ivute ili maji hutumika. Waswahili nao husema ‘samaki mkunje angali mbichi’ haswa wanapotaka kuasa kumpa mafunzo mtoto mapema ili kuepuka hatari ya kushindwa kumbadilisha tabia ukubwani.

(iii) Usitafunwe na nyuvi ukaonea tumba

Miongoni mwa mazao yanayotegemewa na wakulima wa Pemba ni uzalishaji wa asali misituni. Nyuki huzalisha asali katika tumba au mizinga. Usemi wa usitafunwe na nyuvi ukaonea tumba unaonya kuwa iwapo umekerwa na mkeo au mumeo jizuie kupeleka hasira yako kwa watoto. Kwa upande wa Waswahili wanashauri kuwa Usimlaumu mwewe, kipanga yuwesha kuku, au usigombe na mkwezi, nazi imeliwa na mwezi. Nae Lakoff na Turner (1989: 162) anasema kuwa hayo ni mazingira ya kipofu kulaumu dimbwi (Blind blames the ditch). Kipofu anaweza kulaumu dimbwi alilotumbukia akasahau kuwa sababu ya kuliingia dimbwi hilo ni kushindwa kuliona hivyo makosa ni kukosa macho na si kuwepo kwa dimbwi.

(iv) Kanda laikwa mpeto

Mazao yanapovunwa huwekwa katika kanda au ‘gunia’. Hata hivyo wapemba wanavigunia au mifuko midogomidogo iitwayo peto. Usemi huu unatuasa kuwa tusidharau peto kwa vile tuna kanda. Hii ni sawa na waswahili wasemavyo usiache mbachao kwa msala upitao. Istilahi za kanda na peto ni mahususi kwa lahaja ya Kipemba.

(vi) Ndama ndama ndio ngombe

Kisiwa cha Pemba ni maarufu kwa ufugaji wa ng’ombe. Msemo wa ndama ndama ndio ng’ombe umezingatia shughuli za mifugo iliyomaarufu kisiwani hapo. Usemi huo unamaana iliyosawa na ule usemao haba na haba hujaza kibaba au kupacha pacha wajaza pakacha.

Taswira ya uchungaji inaendelea kujitokeza katika usemi mwngine usemao hala hala mchungao ng’ombe usije mpiga huyoo? kwa kawaida ng’ombe anakuwa hampigi mchungawe, lakini kuna baadhi ya wakati ngombe huweza kumpiga mchungawe. Upo usemi usemao usicheze na simba, ukamtia mkono kinywani au anayefikiri amesimama, aangalie asianguke. Semi zote hizo zina dhima ya kuhadharisha kutokujiamini sana kwa lile jambo tulilolizoea. Tunatahadharishwa kutokujiamini kupita kiasi na kuacha kuchukua tahadhari. Katika jamii za wafuga ngamia kama vile Wairani wao badala ya ‘ng’ombe’ wanausemi wao tunaoweza kuulinganisha na semi zilizotangulia za Kipemba kuwa ‘Mwamini Mungu lakini mfunge ngamia wako’. Hapa wanamaainsha kuwa ingawa umezoa au umemzowesha mnyama wako iwe kwenye malisho au kwenye mchezo wa sarakasi basi uchukuwe tahadhari kwani yaweza kutokea madhara makubwa..

5.0 Hitimisho

Kazi hii imegusia kwa uchache misemo mahususi ya Kipemba. Si nia ya makala haya kuainisha misemo yote tuliyokusanya katika makala haya. Tumekusudia kugusia maeneo muhimu ya kinadharia yanayodhihirisha ufanano wa kidhima na uoni wa wanadamu kiubia duniani. Zipo tofauti za mazingira yanayozua misemo hiyo na hivyo sitiari na metonomia zinatumika kifani tu lakini ujumbe unaokusudiwa ukawa na malengo yaliyosawia. Kimsingi sitiari na misemo (au fani) hubeba historia ya jamii husika. Tunaweza kuchora mazingira, mfumo wa uzalishaji mali, ibada na itikadi, na uoni na falsafa ya maisha ya wanajamii kwa kuchambua na kuaninisha sitiari na metonomia zilizotumika. Mazingira ya bahari na Kilimo huko Pemba yamechangia katika kuunda misemo na data mbalimbali za kifoklo. Uchambuzi wa semi za Kipemba umepelekea kuonyesha ni kwa kiasi gani tunaweza kubainisha umahususi na ulinganifu wa misemo ya Kipemba na ile ya jamii nyenginezo duniani. Matokeo awali ya uchambuzi wa misemo ya Kipemba ni ushahidi wa ukweli na udhibati wa hoja za Evelyne Brouzeng (1984)na Hatch na Brown (1995) katika uchambuzi wa data za kifoklo kimuktadha.

Marejeo

Arewa, E na A. Dundes. (1964) Proverbs and the Ethnography of Speaking Folklore katika Gumperz, J na D. Hymes. (Wah) American Anthropologist: The ethnography of communication Vol 66(6) 70-85 CARE Tanzania and Department of Commercial Crops, Fruits and Forestry (2005).

Ngezi-Vumawimbi Forest Reserves Biodiversity Inventory Report Zanzibar :. Evelyne, B. (1984) Stylistique comparée de la traduction de proverbes anglais et français katika Richesse du proverbe, études réunies par François Suard et Claude: Typologie et Fonctions Jarida la (2):162-275 Université de Lille.

Farsi, S. (1958) Swahili Sayings from Zanzibar . Juzuu.1: Proverbs. Arusha: Eastern Africa Publications Limited.

Finnegan, R. (1970) Oral literature in Africa Oxford at the Clanderon Press.

Ghassany.(2003) Kheri ya Ruhani kuliko Subiani Dira (Zanzibar), 26 (30 Mei – 5 Juni), uk. 4.

Giles, L. (1987) Possession Cults on the Swahili Coast: A reexamination of theories of marginality katika Africa 57(2) 234-258

Gray, J. (1962) History of Zanzibar from the Middle Ages to 1856. London : Oxford University Press.

Gray, J. (1980) Bull-baiting in Pemba , Azania, 15, pp. 121-132 Hatch, E na Brown, Cl (1995).

Vocabulary, Semantics and Language Education. Hymes, D. (1972) The ethnography of speaking. Katika Anthropology and Human behavior, Gladwin T na W Sturtevant (Wah) Washington, Anthropological Society of Washington Uk 13-53.

Ifedha, A. (1987) Semi za Kiswahili Maana na Matumizi. Oxford University Press Eastern Africa.

Ingrams, W. (1931) Zanzibar : Its History and People. London : H. F. & G. Wither by. Lakoff,

G na M. Turner. (1980) Metaphors We Live By. Chicago: University of Chicago Press.

Lakoff, Georg and Turner, Mark. 1989. More than Cool Reason: A Field Guide to Poetic Metaphor.Chicago: University of Chicago Press.

 

 

3 thoughts on “Dunia kokwa ya furu: Amali ya Misemo ya KiPemba”

 1. Mashaallah nimefurah kuona jinsi mulivofanya uchambuz ijapo kwa muhtasari,mapenzi yangu ni kuona twarudisha hadhi ya lugha yetu,matumizi ya maneno sahihi yasokuwa yakuzuka.
  Tujitahidi kiswahili hichi kifunzwe kwa wanafunzi ili tusipoteze asili ya lugha yetu.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.