KISWAHILI KINA WENYEWE

Vita baina ya ukale na usasa kwenye ‘Kitumbua Kimeingia Mchanga’

Kitumbua Kimeingia Mchanga ni tamthilia ya kimageuzi iliyoandikwa na Said Ahmed Mohamed na kuchapishwa na Oxford University Press East Africa Ltd inayojaribu kuonesha mgongano uliopo kati ya ukale na usasa katika jamii, ambapo mpishano wa kimawazo na kimtazamo baina ya wazee na vijana unayaumba na kuyaumbua mahusiano yao ya siku kwa siku tangu kwenye mambo makubwa na hadi kwenye madogo.

Wazee wanachorwa kuwa wahafidhina wanaong’ang’ania ukale wao na vijana kama alama ya mabadiliko na mageuzi, ambao wanapigania kuishi maisha ya usasa. Kwenye gamba la nyuma la kitabu, kumeandikwa hivi:

“Fikirini hakubali kuchaguliwa mke na babaake, Bw. Mambo, na nyanyaake, Bi Haija.
Wazee wake wanaona kuwa jambo la kumchagulia mke ni jukumu lao.”

Hapa ndipo penye kiini cha mgogoro wote unaowasilishwa kwenye tamthilia hii, mgogoro ambao kwa hakika unawakilisha hali halisi ya jamii zilivyo katika nchi zetu hizi zinazojipapatuwa sasa kutoka maisha ya kijadi na kuingia katika maisha ya kisasa. Mtazamo wa vijana ni kuwa wanastahiki huwa huru katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao, lakini wazee wanaamini kuwa ile dhima ya kuwa kwao wazazi inawapa haki na mamlaka yasiyo ukomo kwa watoto wao katika hali yoyote waliyo na hata kwenye umri wowote walio nao. Kwao wao “Mwana hakuwi kwa mvyelewe!”

Tamthilia inatuonesha kuwa ingawa imani ya wazee kwenye hili inakosolewa na vijana, haimaanishi kuwa wanakuwa na dhamira mbaya kwa watoto wao. Uamuzi wa wazazi, kwa mfano katika kumuamulia kijana wao mke au mume wa kuwa naye kwenye ndoa, si lazima umaanishe kuwa wazazi hao hawajali hisia za kimapenzi za mtoto wao, bali huenda unatokana na mapenzi yao kwake kuwa makubwa kuliko hisia za kijana huyo. Wazee wanaamini kuwa “Kuishi kwingi kujuwa mengi”, na hivyo uzoefu wao kwenye maisha huwafanya kuwapa madaraka ya kudhania wanaijuwa ghaibu ya watoto wao.

Katika Onesho la Nne panapotokezea majibizano baina ya Fikirini na wazazi wake, Bw. Mambo na Bi Sikitu, tunayashuhudia haya:

Bw. Mambo: Unakiri na kukubali hayo? (kwamba mimi ni baba’ko na huyu ni mama’ko)
Fikirini: Ninakiri Baba.
Bw. Mambo: Ikiwa hivyo ndivyo, basi kwa nini sisi kukuchagulia dhahabu, wewe unaokota shaba? (Fikirini kimya, macho chini)
Kwa nini…kwa nini basi hujali desturi na heshima ya ukoo huu?
Bi Sikitu: Baba, mwanangu Fikirini, wazee wana sehemu ya kukutafutia wewe wema.
Unaona mabaya sasa hivi tu, lakini baadaye utakuja kujua kuwa hatukutakii maovu.

(Uk. 31-2)

Hivi ndivyo wazee wanavyoamini. Lakini kwa upande mwengine, vijana wanadhani kuwa wazee hawana haki ya kuwaingilia kwenye mambo yao kiasi hicho, hata kama kweli wanastahiki kupewa heshima kubwa. Wanadhani kuwa wanapowaingilia kwenye mambo yao, hawafanyi kwa sababu ya mapenzi yao tu kwao, bali pia kwa khofu na woga wa kuona nguvu na madaraka yao yanahatarishwa. Pia kwa kuwa wazee wana tabia ya kuyatilia wasiwasi kila yale yaliyo mageni kwao. Faki, rafikiye Fikirini, anamueleza sahibu yake huyo kwenye mazungumzo yao ya ufukweni:

“Wewe una homa ya uhuru wako kwamba utakuokowa na kukupeleka unakotaka. Wao wana homa ya kuudhibiti uhuru wako, kwa kuwa hawana hakika kwamba uhuru wako hwenda ukakandamiza uhuru wao. Yaani uhuru wako u dhidi ya uhuru wao.” (Uk. 36)

Katika tamthilia hii, mgogoro huu unamalizika kwa ushindi kwa vijana – ushindi wa usasa dhidi ya ukale. Hatimaye, Fikirini anakubaliwa kumuoa amtakaye, Hidaya. Lakini hilo halikuja bure bure. Ni baada ya shindikizo kubwa kutoka kwake na mama yake. Roho ya mama kila siku inaonekana kulainika mbele ya mwanawe kuliko ya baba. Ni ajabu kuwa baada ya maelezo haya kwenye Ukurasa wa 27, Bi Sikitu alikuja kupata upumzi wa kuyameza maneno yake na kulikubali pendo la mwanawe liwe ndoa:

“Si mara moja wala mbili, nimeshamuona katiwa kati na wanaume; huku watano na huku sita, kakumbatiwa kitikiti njiani wanapita wakiyumba na kupepesuka na kucheka….na ubaya zaidi, nimepata habari za kuaminika kwamba kwa Hidaya kitumbua….kime’ngia mchanga!”

Harusi ya Fikirini na Hidaya ilibainisha kuwa khofu za wazazi wake hazikuwa za ukweli. Kitumbua hakikuwa kimeingia mchanga kwa Hidaya, bali ni kwa Zubeda, binti aliyeolewa na Badi, mdogo wake Fikirini, na ambaye alikuwa amechaguliwa na wazazi wake. Huko ndiko mambo yalikokuwa yameharibika.

Dhamira za Familia, Utamaduni na Malezi

Mbali na dhamira ya mageuzi, tathmilia hii inaibua pia dhamira nyengine nyingi yakiwemo masuala ya familia, mila unafiki na utamaduni. Kwa mfano, jinsi mkasa mzima wa kitumbua kilichoingia mchanga ulivyowasilishwa kutoka Onesha la Kwanza hadi Onesha la Tatu, unasema mengi kuhusu familia zetu za Mwambao wa Afrika ya Mashariki – nafasi ya mabibi katika nyumba zetu, mapishi yetu, mjengeko wa familia zetu na ukarimu na njia zetu za kufundishana.

Katika tukio moja, Bi Haja anatengeneza vitumbua na kuwapelekea wanawe, lakini kwa makusudi kabisa anavitia mchanga ili waupate ujumbe anaotaka kuwafikishia, bila ya kuwaambia neno. Na kabla hajaondoka, anawalezea namna ilivyokuwa shida kukitayarisha kitumbua kilicho kitumbua hasa, na namna inavyotia uchungu kuwa baada ya matayarisho yote hayo, anatokea mtu anakutilia kitumbua chako mchanga. (Uk. 5-6).

Pia, ule ukweli kwamba kumbe yule aliyedhaniwa kuwa kitumbua chake kiko safi hakijatiwa mchanga, yaani Zubeda, na akawa ndiye chaguo la wazazi wa akina Fikirini na akaolewa na mtoto wao, Baddi, ndiye ambaye chake kilishatiwa mchanga, unaonesha kiwango cha unafiki kilichomo kwenye jamii zetu. Pengine tukio lenyewe halioneshi kuwa wazazi wameshindwa kulea, lakini linaoenesha namna mwana alivyoshinda kuleleka.

Hilo halitoshi. Bw. Mambo, ambaye ni mhafidhina mkubwa anayepigania kulinda heshima ya familia yake kwa kumkataa katakata Hidaya asiwe mkwewe, kumbe naye ana yake. Anaonekana mwisho wa tamthilia hii akikamatwa na polisi kwa kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya, kitu ambacho hakikuwa kikifanana kabisa na taswira yake. Kumbe alikuwa na sura nyengine aliyokuwa akiificha kwa mkewe na wanawe.

Ni hapo pia inapodhihirka kuwa kumbe siku zote hizo alikuwa na nyumba nyengine ya Bi Mosi, mke aliyemuoa tangu miezi sita iliyopita, huku mkewe wa kwanza, Bi Sikitu, akiwa hana taarifa nayo kabisa.

Yanapombainika mawili hayo, Bi Sikitu anazimia (Uk. 66).

1 thought on “Vita baina ya ukale na usasa kwenye ‘Kitumbua Kimeingia Mchanga’”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.