‘Mengia mashindanoni, japo sina mshindani
Mikono i kiunoni, nahema ni taabani
Nasema ni mzigoni, kumbe ni pweke mbioni
Nimeita marafiki, waje wanishuhudie
Nikapiga na mimiki, hadi Paje wasikie
Sikujua sisiki, nikaachwa niumie
Niliamuru marefa, sheria wazipuuze
Nikataka walokufa, wazuke wanipongeze
Lengo wanijaze sifa, kwenye mbio niongoze
Jingi jasho nikatoka, nikidhani nakimbia
Huku nikipapatika, wengine kuwazuia
Hamu imenikatika, mpweke hiangalia
Kwa kuogopa kukosa, Mungu nilimsahau
Nilitoa toka pesa, fuu hadi zambarau
Ushindi si huu sasa, bali mbona wa dharau?
Maalim Mussa
Zanzibar
21 Machi 2016