UCHAMBUZI

Miujiza ya busu la Jecha ilivyomgeuza chura kuwa Mwana Mfalme

Miongoni mwa ufahamu wa watu wa kawaida hapa Ulaya kuhusu nchi yangu, ni kuwa Zanzibar ni sehemu ya hadithini tu yenye mambo ya kushangaza na kufurahisha. Hata kuna hadithi kama ile riwaya ya kisayansi iitwayo Stand on Zanzibar iliyoandikwa na John Brunner mwaka 1968 na ikaja kujishindia tunzo kadhaa za kimataifa. Riwaya kama hizi husaidia kuujenga uwelewa wa watu wa kawaida ninaokutana nao, na matokeo yake si wengi wao wanaoijuwa Zanzibar ya kweli – nchi niliyozaliwa na kukulia na niliyoinua mguu wangu kuja hapa nikiwa mtu mzima saba na akili, tusemavyo kikwetu.

Kuna wakati ninapokutana nao, husema nijipe muda wa kuwaelezea. Na kwa kuwa siku hizi tuna ‘smartphones’ na Google, basi huwa rahisi kuifupisha hadithi refu ya taifa langu kwa sentensi chache, kisha nikawaachia wenyewe jukumu la kujisomea zaidi. Lakini kuna wakati hujiuliza mwenyewe: “Kwani hivi ni uongo kuwa yangu ni nchi ya maajabu na miujiza?”

Ghassani
Na Mohammed Ghassani

Ni ukweli mtupu. Miujiza ya karibuni kabisa ambayo nina hakika itakuja kuandikiwa riwaya kadhaa siku zijazo ni hii iliyoanzia tarehe 28 Oktoba 2015 na kuendelea hadi tarehe 21 Machi 2016, inayohusiana na kufutwa na kuitishwa kwa uchaguzi ndani ya miezi mitano.

Hapa nataka kuzungumzia zaidi matokeo ya unaoitwa “uchaguzi wa marudio” wa tarehe 20 Machi 2016 kama maajabu hayo. Kwenye utangazaji wa matokeo hayo, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) haikuwa imefanya kawaida yake ya kutaja kura za wagombea urais kwa utaratibu wa jimbo kwa jimbo, kama ambavyo ilikuwa ikifanya huko nyuma, na hivyo ilinibidi kutuma ombi maalum kwenye ukurasa wa Facebook kwa wale wenye fursa ya kuyapata matokeo hayo.

Namshukuru sana mtumiaji mmoja wa ukurasa huo, kwa jina Yussuf Juma, ambaye aliyatafuta na akachukuwa juhudi ya kunitumia matokeo ya majimbo yote 54 siku ya tarehe 22 Machi 2016, takribani saa 7:15 usiku kwa majira ya nyumbani.

Matokeo hayo yalinisaidia ‘kuyapiganisha’ na matokeo ya majimbo 31, ambayo binafsi nilikuwa nimeyakusanya kutoka kinywani mwa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, na Makamu wake, Jaji Abdulhakim Ameir Issa, baina ya tarehe 25 na 26 Oktoba 2015 kabla ya Jecha hajatangaza “kuufuta” uchaguzi huo tarehe 28 Oktoba.

Hii ni kwa sababu mimi mwenyewe nilikuwepo kwenye ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwanani mjini Unguja, kushuhudia utangazwaji wa matokeo hayo.

Sitaki kuingia kwenye ta’awili wala uchambuzi wa chochote ule, isipokuwa hapa naweka tu majadweli ya kulinganisha, kwanza, zile kura ambazo Jecha na Issa walizitangaza kwenda kwa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. Ali Mohamed Shein, katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba na zile ambazo ZEC inadai zilikwenda tena kwa Dk. Shein siku ya tarehe 20 Machi kwa majimbo 31 (namba 1 hadi 31). Kisha kuanzia namba 32 hadi 36, ni majimbo matano pia ya kisiwani Unguja (Donge, Tumbatu, Amani, Kijitoupele na Shaurimoyo) ambayo licha ya kuwa yalikuwa hayajakuja kutangazwa hadharani, majumuisho yake yalishakamilika na kukubalika ndani ya chumba cha majumuisho, ikawa tunasubiri kutangaziwa tu. Na mwisho kuna jadweli la tafauti ya kura kisiwani Pemba.

Tafauti ya kura kwa kila jimbo imeandikwa kwa wino mwekundu na kuwekewa alama ya + kumaanisha kuwa ni ongezeko lililozidi kwenye kura ya 20 Machi.

Ongezeko la kura za Dk. Shein kisiwani Unguja

Na. JIMBO OKT. 2015 MACHI 2016 TAFAUTI
1. CHWAKA 6,067 8,294 +2,227
2. UZINI 9,941 12,995 +3,054
3. DIMANI 4,818 7,122 +2,304
4. PANGAWE 3,009 5,168 +2,159
5. MTONI 5,336 7,977 +2,641
6. TUNGUU 7,589 10,589 +3,000
7. CHUMBUNI 4,892 8,954 +4,062
8. KIWENGWA 2,995 3,539 +544
9. MAHONDA 4,352 5,665 +1,313
10. NUNGWI 3,556 4,064 +508
11. MPENDAE 3,974 6,642 +2,668
12. MFENESINI 4,192 5,790 +1,598
13. KIJINI 2,396 2,787 +391
14. MAGOMENI 5,445 8,173 +2,728
15. MTOPEPO 3,671 6,788 +3,117
16. M/KWEREKWE 4,003 9,597 +5,594
17. MWERA 2,554 3,449 +895
18. BUBUBU 4,356 6,593 +2,237
19. CHAANI 4,120 5,208 +1,088
20. PAJE 5,585 7,099 +1,514
21. WELEZO 2,528 4,033 +1,505
22. BUMBWINI 2,351 3,490 +1,139
23. JANG’OMBE 6,216 8,810 +2,594
24. KIKWAJUNI 5,998 9,942 +3,944
25. CHUKWANI 3,571 5,922 +2,351
26. MKWAJUNI 4,285 4,351 +66
27. MAKUNDUCHI 8,161 9,800 +1,639
28. FUONI 889 1,386 +497
29. K/SAMAKI 4,413 6,976 +2,563
30. MALINDI 2,334 5,873 +3,539
31. KWAHANI 5,960 9,360 +3,400
32. DONGE 5,255 5,308 +53
33. TUMBATU 5,424 6,081 +657
34. AMANI 4,107 6,026 +1,919
35. KIJITOUPELE 4,373 6,911 +2,538
36 SHAURIMOYO 5,593 9,006 +3,413

Hapa tusifanye uchambuzi wala tusifanye majumuisho, bali tusome tu hizi nambari kwa kuzingatia tafauti iliyopo. Katika ongezeko hilo, unaweza kuona kuwa kwenye baadhi ya majimbo, siku ya tarehe 20 Machi, Dk. Shein alipigiwa kura na “watu” 3,000+ wa ziada kutoka wale wa 25 Oktoba. Hiyo ndiyo hadithi ya Uzini, Tunguu, Mtopepo, Kikwajuni, Kwahani na hata jimbo la Malindi ambalo ni ngome ya CUF.

Majimbo yaliyotia fora katika haya ni la Mwanakwerekwe, ambako watu 5,594 wa ziada walijitokeza ‘kumpigia’ kura Dk. Shein siku ya tarehe 20 Machi, ikilinganishwa na wale wa Oktoba 25. Jimbo hilo linafuatiwa na la Chumbuni, ambalo lina ongezeko la kura 4,062.

Jimbo pekee ambalo linaweza kusemwa kuwa na ongezeko dogo kabisa kwa kura za Dk. Shein katika haya 31, ni la Donge ambalo liliongeza 53 tu likifuatiwa na Mkwajuni ambalo lina kura 66 za ziada.

Ongezeko la kura za Dk. Shein kisiwani Unguja

Hiyo ni kesi ya kisiwani Unguja, ambako kisiasa kunasemekana CCM ina ufuasi mkubwa zaidi. Hata hivyo, hata hadithi ya kisiwani Pemba, ambako kunaambiwa ni ngome ya Chama cha Wananchi (CUF), nayo si tafauti hata kidogo, panapohusika ongezeko la kura ambazo ZEC inasema alipata Dk. Shein tarehe 20 Machi.

Ingawa Jecha hakuwahi kuyatangaza matokeo ya majimbo ya Pemba kabla ya hatua yake ya tarehe 28 Oktoba 2015 ya ‘kuufuta’ uchaguzi wa Oktoba 25, siku ya tarehe 26 Oktoba, CUF ilikuwa imetuita waandishi wa habari saa 3:00 asubuhi kwenye ofisi zake za Mtendeni na kutupa matokeo ya majimbo yote 54 kwa nafasi ya urais.

Unapoyalinganisha matokeo hayo waliyotoa CUF na yale ya majimbo 31 yaliyotangazwa na ZEC kati ya tarehe 25 na 26 Oktoba, huwezi kukuta tafauti yoyote ya kimsingi. Hiyo ni kusema kuwa – ingawa matokeo ya majimbo mengine hayakuwahi kutangazwa na ZEC kabla ya Jecha ‘kuufuta’ uchaguzi, kwa kuwa hesabu ya CUF na ZEC ilikuwa sawa sawa kwenye hayo ya awali, basi kuna uwezekano wa kuwa sawa kwenye haya yaliyobakia.

Kwa msingi huo, matokeo yaliyopo hapa yanalinganisha kura alizoambiwa amepata Dk. Shein katika uchaguzi wa Oktoba 25 na zile ambazo ZEC inasema alizipata tarehe 20 Machi kisiwani Pemba.

Na. JIMBO OKT. 2015 MACHI 2016 TAFAUTI
1. CHAMBANI 725 3,129 +2,404
2. MTAMBILE 798 3,093 +2,295
3. KIWANI 1,499 3,892 +2,393
4. MKOANI 3,110 6,407 +3,297
5. CHAKECHAKE 1,113 4,551 +3,438
6. CHONGA 1,515 3,598 +2,083
7. OLE 617 3,818 +3,201
8. WAWI 1,243 4,147 +2,904
9. ZIWANI 571 2,890 +2,319
10. GANDO 795 3,298 +2,503
11. MTAMBWE 320 1,789 +1,469
12. MGOGONI 637 3,395 +2,758
13. KOJANI 1,003 3,994 +2,991
14. WETE 863 3,737 +2,874
15. KONDE 691 1,606 +915
16. MICHEWENI 1,436 3,273 +1,837
17. TUMBE 372 1,520 +1,148
18. WINGWI 394 2,062 +1,668

Hapa napo unaona ongezeko kubwa lililopo kama ilivyokuwa kwa Unguja. Majimbo yaliyotia fora kwa ongezeko ni Chake Chake (3,438), Mkoani (3,297) na Ole (3,201), huku ziada ndogo kabisa ikiwa jimbo la Konde, ambapo Dk. Shein ameongeza kura 915, ikifuatiwa na jimbo jirani la Tumbe, ambako kuna ziada ya kura 1,148.

Matokeo haya ‘yamepatikana’ hata baada ya ripoti za waandishi wa habari na mashahidi waliokuwepo siku ya tarehe 20 Machi kote visiwani Unguja na Pemba kuelezea idadi ndogo kabisa ya wapiga kura vituoni, kufuatia CUF na vyama vyengine tisa kutangaza kuususia uchaguzi huo.

Matokeo haya ‘yamepatikana’ pia hata baada ya picha za mnato na za vidio kusambaa mitandaoni zikionesha namna baadhi ya wale waliojitokeza kupiga kura walivyozifanya kura hizo ndani ya vituo – kuchorachora kwa nia ya kuziharibu.

Lakini kama nilivyotangulia kusema, huu si uchambuzi wala tafsiri ya chochote kilichotokea, bali ni wasilisho tu la namna busu la kimiujiza la Bint Mfalme lilivyofanikiwa kumgeuza chura akawa Mwana Mfalme.

Watakaokuja kukitafiti kipindi cha miezi mitano, kuanzia 25 Oktoba 2015 hadi 22 Machi 2016, bila ya shaka watakuja kutupa majibu zaidi kwa masuala tunayojiuliza. Hata hivyo, kitu kimoja nina hakika nacho – Zanzibar yangu itaendelea kuongoza kwenye kuanzisha mambo na wengine kufuata.

Ni Zanzibar, kwa mfano, ambao Ukristo uliingia kwa mara ya kwanza kabla ya kusambaa kwenye maeneo yote ya ndani ya Afrika Mashariki na Kati. Hiyo ilikuwa mwaka 1448.

Ni Zanzibar ambayo ilijenga Jumba la Maajabu (jengo la Baitul-Ajab) la pale Forodhani, ambalo lilikuwa ajabu ya kweli wakati huo kwenye eneo lote la Afrika ya Mashariki na Kati. Hiyo ilikuwa mwaka 1833, ambapo hapakuwahi kuwepo na jengo kubwa la namna ile, likiwa na umeme na lifti zaidi ya jengo hili.

Ni Zanzibar ambayo ilikuwa ya kwanza kuwa na treni yake yenyewe. Hiyo ilikuwa mwaka 1879.

Ni Zanzibar ambako magazeti yalianza kuandikwa na kusambazwa kwa mara ya kwanza ndani ya eneo zima la Afrika Mashariki na Kati, ambapo gazeti la Samachar lilichapishwa mwaka 1903.

Kwenye siasa pia, ni Zanzibar iliyokuwa ya mwanzo katika Afrika ya Mashariki kufanya uchaguzi kamili mwaka 1957, ambapo chama cha Afro-Shiraz (ASP) kilishinda viti vitano kati ya sita vilivyowaniwa.

Hiyo ndiyo Zanzibar yangu. Sio Zanzibar ya kwenye riwaya wanaoijuwa wengi hapa Ulaya.

2 thoughts on “Miujiza ya busu la Jecha ilivyomgeuza chura kuwa Mwana Mfalme”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.