Nasikia mwasemani, mungalijinong’onea
Nasikia kwa yakini, njama mnonipangia
Nasikia tambueni, kama mwataka nibwia
Mwanong’ona kitu gani, na yote nayasikia?
Mbona yaja sikioni, si kushoto la kulia
Sauti zingawa chini, kelele zinanijia
Mwanong’ona ndani ndani, madili kunipangia
Mwanong’ona kitu gani, na yote nayasikia?
Naona muko shidani, mungalikinishikilia
Mikono nitawapeni, pingu mupate nitia
Sikio langu kichwani, hamuwezi lipatia
Mwanong’ona kitu gani, na yote nayasikia?
Mwanong’ona ja shetani, chano anohitajia
Mwadai mufanye nini, roho zipate tulia
Sikizeni kwa makini, kazi bure mwajitia
Mwanong’ona kitu gani, na yote nayasikia?
Nong’ono zinong’oneni, lugha zote nazijua
Kipate kitongoeni, na Kikaye natambua
Sikio halinikhini, vizuri ladadavua
Mwanong’ona kitu gani, na yote nayasikia?
Amour Hadji
25 Februari 2016
Zanzibar