Unahitaji kukutana na Eddy Riyami mara moja, siku moja na takriban mkazungumza kwa kiasi cha dakika tano na atabaki kichwani kwako. Hakuna sehemu utayaoingia katika historia na siasa za Zanzibar ikawa yeye ni mwanafunzi. Allah amemjalia kuitumika nchi yake Zanzibar vilivyo katika uzalendo wa hali ya juu kabisa toka akiwa kijana mdogo sana. Siku nilipokutana nae kwa mara ya kwanza alinishangaza jinsi alivyokuwa anaijua historia ya Bara na wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine katika historia ambazo zinagusa pande zote mbili za Muungano. Alinishangaza sana jinsi anavyoweza kuunganisha matukio katika siasa za Visiwani na Bara kisha akafanya na utabiri ambao kwa mara nyingi inapotokea mimi huiambia nafsi yangu kuwa Eddy alipatapo kunigusia jambo hili.

Eddy Riyami ni bingwa wa ‘’Facts and Figures’. Hili niligundua siku mmoja tumekaa pamoja wakati wa uchaguzi uliopita nyakati za jioni. Kama kawaida kila tukikutana mazungumzo yetu ni maendeleo ya nchi yetu na nini kifanyike kujenga utengamano katika jamii. Aliyonieleza siku ile ndiyo yaliyokuja kutokea kuwa CCM haitashinda uchaguzi Zanzibar. Eddy akanipa na ‘’indicators,’’ yaani viashiria. Mimi nilimgusia “gerrymandering” iliyokuwa imepitika Zanzibar, yaani ukataji mpya wa majimbo ya uchaguzi. Jibu alonipa lilinishangaza sana. Eddy alinambia haitosaidia kubadilisha “pattern” ya upigaji kura. Lazima nikiri kuwa wakati mwingine ilibidi nijikunyate kama mwanafunzi makini anayetaka kulijua somo ili apasi mtihani wa profesa wake. Kwa nini nilikuwa wakati mwingine nakaa kimya kwa sababu nilikuwa kwa kweli sielewi ile mantiki ya ushindi katika “Gerrymandering” ya Zanzibar. Kilichionifanya mimi nifunge mdomo wangu ni kuwa nilikuwa najua nazungumza na mjuzi.
Nakumbuka alipatapo siku moja kunambia kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ndiyo dira itakayowaongoza Wazanzibari katika neema. Alinieleza mengi kuhusu juhudi zilizopitika hadi kufikia pale na vipi “referendum” ilivyofikiwa na vipi Wazanzibari kwa mara ya kwanza walipeleka ujumbe ulio wazi kwa viongozi wao nini walichokuwa wanakitaka na kutegemea kutoka kwao. Eddy “Master of Figures” pale pale akaniuliza: “Hivi unajua kwa Wazanzibari kupiga kura 66.7% kutoka SUK wewe unajua maana yake?” Nimetumbua macho namsikiliza mwalimu wangu ananisomesha. Hii itakuja kujiakisi katika hata upigaji kura katika uchaguzi mkuu unaokuja. Naweza kusema mengi sana kuhusu Eddy Riyami. Eddy ni mzalendo wa kweli na mtu shujaa na mwenye akili pevu na uwezo mkubwa sana wa kusimamia kile anachokiamini.
Eddy si mtu wa kuificha sura yake na kutoa matusi kuwatukana viongozi wa nchi. Vitu kama hivyo vya kujificha uso vinafanywa na watu waoga. Eddy hana sababu ya kutoa matusi. Huo uwanja wa matusi unao wenyewe. Huo si uwanja wa Eddy. Viwanja vya Eddy hakuna Mzanzibari asiyevijua. Eddy kasimama saa 7:00 mchana na kufanya aliyofanya kwa wazi kila mtu akishuhudia. Eddy hawezi kujifungia chumbani akamwaga matusi kwenye “digital recorder” kisha akairusha hewani.
Naamini katika dhati ya moyo wangu kuwa hakuna kitu kitachoma moyo wa Eddy kama ile kudhaniwa ati yeye ni mtoa matusi.
Chanzo: Mtandao wa Mohamed Said, mohammedsaid.com