KISWAHILI KINA WENYEWE

‘Mgogoro’ katika ushairi wa Kiswahili

Mgogoro” katika ushairi wa Kiswahili umekuwapo kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Una misingi yake katika utata wa mambo mawili:

(i) Maana ya jumla ya shairi
(ii) Maana ya shairi la Kiswahili.

Mvutano huu, sawa na uk tulioutaja katika nchi za Ufaransa, Uingereza na Marekani, una pande kuu mbili. Upande mmoja wapo wanamapokeo ambao wanasisitiza kuwa vina na urari wa mizani ni roho ya ushairi wa Kiswahili.2 Upande wa pili wako wanamabadiliko, washairi wa kisasa, ambao wanaeleza na kuthibitisha kuwa si lazima shairi liwe na vina na urari wa mizani ndipo liitwe la Kiswahili.

“Tatizo” lilianza rasmi katika miaka ya mwisho ya sitini na mwanzoni mwa miaka ya sabini walipotokea “watundu” watatu: Ebrahim Hussein, Euphrase Kezilahabi na Jared Angira. Hawa waliandika na kusoma mashairi kwa lugba ya Kiswahili bila kujali kanuni zilizo “uti wa mgongo” wa ushairi wa Kiswahili kwa wanamapokeo. Baadaye waliungwa mkono na washairi wengine kama akina M.M. Mulokozi, K.K. Kahigi, na hivi karibuni Henry Muhanika na Theobald Mvungi. Baadhi ya wanamabadiliko hawa hali kadhalika wameandika nadharia za ushairi za kuonyesha kuwa si lazima shairi la Kiswahili libanwe na kanuni na sheria hizo. Jambo ambalo wanamapokeo kama vile Jumanne Mayoka na Abdilatif Abdalla hawakuzingatia katika vita vya maneno baina yao na wanamabadiliko ni kwamba akina Kezilahabi, Kahigi, Mulokozi na wenzao hawana vita na ushairi wa Kiswahili unaofuata hizo sheria. Kwa mfano, katika diwani ya Mulokozi na Kahigi ya Malenga wa Bara3 zaidi ya nusu ya mashairi yao ni ya kimapokeo yafuatayo “sheria” za vina na mizani! Jambo walilolisisitiza watundu hawa ni kuwa kila kitu na kila kiumbe duniani daima kiko katika mwendo wa mabadiliko; na kuwa fani ya ushairi wa Kiswahili pia isingesimama tisti tu katika mzingo wa “sheria” daima dumu. Walilotilia mkazo basi, ni kuwa uwanja wa ushairi wa Kiswahili uyakubali mabadiliko ya fani zilizotumiwa na washairi kueleza maudhui mapya.

Kwa kueleleza kiini cha mgogoro huu, tutatoa maana za ushairi zilivyoelezwa na wanamapokeo na zile za wanamabadiliko. Baada ya hapo tutazichuja zote na kutoa maana tuonayo kuwa inafaa zaidi.

Shaaban Robert, ambaye tunaweza kumchukua kuwa kielelezo cha waumini wa ushairi wa kimapokeo, alitoa maana ifuatayo ya ushairi:

Ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa sanaa ya vina ushairi una ufasana wa maneno machache au muhutasari… Wimbo ni shairi dogo, sbairi ni wimbo mkubwa na utenzi ni upeo wa ushairi… kina ni mlingano wa sauti za herufi. Kwa maneno mengine huitwa mizani ya sauti, na ufasaha ni uzuri wa lugha. Mawazo, maono na fikira za ndani zinapoelezwa kwa muhtasari wa ushairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu.4

Kabla ya kuichambua maana hii ya ushairi, tuangalie maana zingine zilizo na welekeo sawa na wa hiyo ya Shaaban Robert.

Mathias Mnyampala, ambaye aliishi enzi za Shaaban Robert pia, aliueleza ushairi hivi:

Ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kaie. Ndicho kitu kilicho bora sana katika maongozi ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalumu kwa shairi.5

Nayte Abdilatif Abdalla kaueleza ushairi kuwa:

Utungo ambao katika kila ubeti wake kuna ulinganifu wa vina vitukufu vilivyopangwa kimoja baada ya chenziye; wenye vipande vilivyo na ulinganifu wa mizani zisizo pungufu wala zilizo zaidi; na vipande hivyo viwe vimetandwa na maneno ya mkato maalum na yenye lugha nyofu, tamu na laini, lugha ambayo ni tetelezi kwa ulimi kwa kuitamka, lugha ambayo ina uzito wa fikra, tamu kwa mdomo wa kuisema, tumbuizi kwa masikio ya kuisikia na yenye kuathiri moyo uliokusudiwa na kama ulivyokusudiwa.*

Katika maana hizi za ushairi kuna mambo kadhaa yanayoibuka. Kwanza kabisa, kipengele cha lugha kinatiliwa mkazo na washairi wote hao waliojaribu kueleza maana ya ushairi japo kwa mitazamo tofauti tofauti. Shaaban Robert anasisitiza kuwa shairi zuri halina budi kuwa na ufasaha wa lugha. Naye Mathias Mnyampala anakieleza kipengele hiki kwa kusema kuwa ushairi lazima utumie “maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata.” Abdilatif hatofautiani na wenawe kwani naye pia kasisitiza kuhusu “maneno ya mkato maalum na yenye lugha nyofu, tamu na laini.”

Kwa jumla basi, wanamapokeo hawana ugomvi wowote na washairi wa kisasa kuhusu kipengele cha lugha. Wote wanakubaliana kuwa lugha ya ushairi haina budi iwe ya mkato na ya ufasaha.

Jambo hili tunaliona tujaribupo kuchunguza maana za ushairi kama zilivyotolewa na wanamabadiliko. Tutadondoa maana hizo kama zilivyotolewa na M.M. Mulokozi na E. Kezilahabi, ambao tunaweza kuwachukulia kama wawakilishi wa wanamabadiliko. Kezilahabi anasema:

Ushairi ni tukio, hali au wazo ambalo limeonyeshwa kwetu kutokana na upangaji mzuri wa maneno ya fasihi yenye mizani kwa kifupi ili kuonyesha ukweli fulani wa maisha.7

Naye M.M. Mulokozi ametoa maana ya ushairi kuwa ni:

… mpangilio maalumu wa maneno fasaba yenye muwala, kwa lugha ya mkato, katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo, ili kueleza wazo au mawazo, kufunzaau kuelezajambo au hisi fulani kuhusu maisha ya binadamu kwa njia inayoburudisha na kugusa moyo. 8

Mgogoro uko katika matumizi ya urari wa mizani na vina, kwam wanamapokeo wanashikilia kuwa vipengele hivi ni vya lazima; kuwa ni sheria za kutumiwa katika ushairi, hususan ule wa Kiswahili. Kwao vina na urari wa mizani ni uti wa ushairi wa Kiswahili. Haya yamepigiwa muhuri na mfuasi mkuu wa tapo hili Jumanne M. Mayoka, ambaye akiwa kajawa na jazba alisema haya kuhusu mashairi ya kitabu chake cha Mgogoro Wa Ushairi na Diwani ya Mayoka:

Katika kitabu hiki, tungo kama za Kezilahabi, Kahigi, Mulokozi na wengineo watungao tungo tutumbi zisizokuwa na sanaa yoyote nimezitupa pembeni… Mwundo wa mashairi yote yaliyomo kitabuni humu ni wa asili ya Kibantu. Kila utungo wa shairi umefungika upande wa mistari: ni lazima kila ubeti wa shairi uwe na idadi maalumu ya mistari; umefungika upande wa vina: ni lazima mistari iwe na vina; umefungika upande wa mizani: ni lazima kila mstari uwe na idadi sawa ya mizani. Mashairi yote yaimbwa; yawcza pia kusomwa au kusemwa tu. Tungo zisizotimiza yote hayo si mashairi.9

Tumemdondoa Mayoka kwa kirefu kwa sababu matamko yake, na hasa lazima alizozisisitiza ni mfano mzuri wa sheria za kirasimi10 ambazo akina Kezilahabi, Kahigi, Mulokozi na wengineo wanaeleza kuwa si za lazima.

Labda kabla ya kuuingilia “mgogoro” huo, tuangalie vipengele vingine vijitokezavyo katika maana za ushairi tulizoziorodhesha.

Vina na urari wa mizani ni vipengele vya ushairi vilivyo na asili yake kama itakavyodhihirika baadaye. Ni udhaifu wa kianazuoni kusisitiza juu ya kipengcle kimoja au viwili vya fani ya kazi ya fasihi na kuviita ni uti wa kazi hiyo. Mathalani, ni wazi kuwa kuna mashairi na nyimbo mzo mzo katika fasihi andishi na simulizi ya Kiswahili ambazo hazifuati hivyo vipengele alivyoviwekea ulazima mtaalamu Mayoka, na ambazo hazina vina wala urari wa mizani, na bado – tupende au tusipende – ni kazi nzuri sana za sanaa.

Katika maana ya kwanza tuliyoiangalia, kwa kutaroka kuwa “wimbo ni shairi dogo” Shaaban Robert anaweza kumtatanisha mwalimu na mwanafunzi wa ushairi. Tujuavyo, si kila wimbo ni shairi. Sifa ya “udogo” ambayo kaitumia Shaaban Robert ina utata pia, le udogo huo ni wa kifani au kimaudhui?

Shaaban Robert aelezapo kuhusu “maono na fikra za ndani (ambazo) huvuta moyo kwa namna ya ajabu” anaungana na wengine kama Abdilatif anayeongelea juu ya nguvu ya ushairi katika kuathiri moyo uliokusudiwa, na hata Mulokozi ambaye amesisitiza kuwa ushairi unatoa maudhui yake “kwa njia inayoburudisha na kugusa moyo.”

Nadharia hizi zina udhaifu wake kwani katika ushairi hakuna maajabu yoyote yale. Ijapokuwa huenda wataalamu hawa walikusudia tu kueleza juu ya umuhimu wa ushairi kujaribu kunasa hisia za watu, unasaji huo si lazima uwe kwa upande wa ushairi tu bali, kwa hakika, ni unasaji wa lazima kwa kazi zote za sanaa.

Ziko nadharia dhanifu zilizopandikizwa kuhusu uwezo wa mshairi. Nadharia hizi humweka mshairi juu ya watu wengine, juu ya jamii; nazo humgeuza kuwa Mungu-mtu mwenye visima vya hekima na zamzam za mawazo na maeneno mazito yanayovuta mioyo ya watu “kwa namna ya ajabu.”

Imani hii ambayo imeenea basa katika nchi za kibepari ambako mwanasanaa ni mtu maalumu asiye mmoja wa watu anaoandika juu yao, imepata nafasi kubwa sana katika kuipotosha nadharia yote ya ushairi wa Kiswahili. Kwa kufuatana na nadharia hii, baadhi ya washairi wa Kiswahili wameshikilia kutumia maoeno magumu magumu-hasa ya Kiarabu katika mashairi yao. Kwao hao mapambo ya sheria za vina na urari wa mizani ni ya lazima kafika ushairi. Wasioweza kuzitimiza sheria hizo kali basi wasijitie kuwa ni washairi! Kuhusu msisitizo huu wa matumizi ya “mapambo”, M.M. Mulokozi kasema:

… Uozo na ubaradhuli wa maisha ya kiumwinyi, hasa wakati mfumo huo unapoanza kutetereka kutokana na mabadiliko ya nguvu za jamii na uchumi, huwafanya mamwinyi, katika maisha yao ya kizembe na kifasiki, wapendelee sana mambo ya kuvutia macho na kuliwaza pua, kama vile mapambo aina aina, wanawake wazuri, nakshi na marembo ya rangi za kuvutia katika makazi na malazi yao… marashi na manukato, udi na ubani, (nakadhalika…)11

Ni wazi kuwa baadhi ya washairi wetu wa Kiswahili wanaosisitiza mno kuhusu mapambo katika maana ya ushairi wanasisitiza tu mtazamo wa kimwinyi waliorithi na kuuchukua vivi hivi tu bila kutambua asili yake.

Mtazamo huo pia – kwa vile unahusu tabaka hilo nyonyaji la kimwinyi – huwania kuweka sheria na kanuni mbalimbali za kuulinda utamaduni wake. Ni mtazamo unaoumba sanaa na wanasanaa wenye kujitenga na janui, wajionao wao kuwa ndio tu wamejawa na hekima katika bongo zao – hekima na uwezo ambao ni siri yao tu. Ili kusisitiza kuhusu upekee wa wanasanaa wenye mtazamo huo, wengi wao huanza kazi zao kwa kumwita Mungu na kuongea naye. Twaelezwa kuwa huyu, huwaongezea hekima na vipawa. Haishangazi kuona kuwa washairi wetu wengi waliopokeatu “ada” hii ya kinafiki ya kujiona kuwa na kipaji na hekima yenye asili ya uwezo wa Mungu, daima huanza mashairi yao kwa dua. Leo hii hili jambo la kuanza shairi au utenzi kwa kumwita Mungu ni dhahiri kuwa ni njia dhaifu mno ya kuanzia kazi yoyote ya fasihi; ni kujidanganya kuwa ni mkongojo wa mpingo kumbe ni “wa bua” tupu!

Kwa Mayoka, maana ya “shairi” imeishia tu katika idadi ya mistari, vina, urari wa mizani na kule kuimbika kwa utungo. Utungo usiofuata “sheria” hizo basi kwa mtaalamu huyu haufai kwani hauna “sanaa yoyote.” Lakini labda swali la kuuliza hapa ni je, sanaa ni nini? Sanaa ni uoanishaji mzuri wa fani na maudhui katika kazi ya mwigo aifanyayo mtu. Tanzu za sanaa hukua, hubadilika, na hata wakati mwingine hupigwa vikumbo na nguvu za kijamii ikabaki kuwa historia katika kumbukumbu za nyaraka za kale. Tanzu hizi basi, daima huwa katika mwendo wa mabadiliko, na ijaribupo kusimama tu bila kuguswa na mwendo huo hujikuta imechacha. Hii ina maana kuwa mtu aiwekeapo sanaa sheria na kuziita takatifu zisizoguswa na wakati na aina ya jamii, anadunisha na hata kuudharau uhai wa sanaa hiyo!

Katika maana aitoayo Kezilahabi utata unajitokeza katika sehemu mbili: kwanza anapotaja ulazima wa mizani katika shairi, halafu pia anapotamka kuwa kila shairi linaonyesha “ukweli fulani wa maisha.”

Kuhusu mizani, inabidi kuzingatia kuwa Kezilahabi anaongelea kipengele ambacho ni tofauti na kile cha urari wa mizani. Urari wa mizani ni kulingana kwa silabi za kila mstari wa ubeti katika shairi, kila silabi moja ikiwa ndio mizani moja. Urari wa mizani hupambanuliwa na mizani tu katika msisitizo wa idadi sawa za silabi. Mizani aisisitizayo Kezilahabi ni mapigo (rhythm) ambayo ni muhimu katika kila shairi ijapokuwa si lazima yaws ya kufanana kwa kila mstari. Mapigo haya hujulikana pia kama wizani. Ni mapigo yanayosaidia kuainisha mwendo wa shairi. Kwa mfano, iwapo shairi linahusu kifo, lazima mwcndo wake utakuwa wa polepole na mapigo yake yataonyesha huzuni na majonzi. Vile vile, iwapo shairi linahusu mapenzi ni wazi kuwa litakuwa na wizani laini na nyororo inayooana na maudhui ya kimapenzi. Wizani pia huainishwa na mambo kama vile urefu wa mstari au sentensi, ucbaguzi wa maneno na jinsi hayo maneno yanavyohusiana yenyewe kwa yenyewe katika kujenga mstari, ubeti au hata shairi zima.

Kufaulu ama kushindwa kwa shairi kutoa maudhui yanayoeleweka vizuri akilini mwa msomaji au msikilizaji hutokana na ufundi wa mshairi wa kuchagua mwendo na mapigo yanayolandana na maudhui anayoyashughulikia katika shairi lake.

Wizani inajitokeza katika hali mbalimbali, na wala siyo lazima ibebwe na mizani minane au kumi na sita kama ambavyo yaelekea wanamapokeo wanataka iwe. Hali kadhalika siyo lazima wizani iletwe na vina vya kati na vya mwisho, na hata siyo lazima kuwepo na vina katika shairi ili kuleta wizani. Wakati mwingine msisitizo uletwao na marudiorudio ya maneno fulani fulani katika shairi huleta mapigo mahsusi katika mtiririko wa hilo shairi. Yako mashairi mengi katika fasihi ya Kiswahili ambayo yanatumia mbinu hii ya matumizi ya maneno yenye kurudiwarudiwa.

Kwa kifupi basi, tunaweza kusema kuwa wizani ni mpangilio wa urudiaji wa mapigo au mwendo tunaosikia katika tungo. Hata hivyo haimaanishi kuwa lazima wizani ijitokeze tu katika ushairi. Sentensi ifuatayo imedondolewa kutoka katika nathari (Rosa Mistika ya Kezilahabi) na bado ina wizani utokanao na ufupi na usambamba ndani yake. “Jualikatua. Gizalikaingia. Mwezi ulitokea.”

Wizani husaidia sana wasomaji au wasikilizaji wa shairi kwani hufungamana oa yale maudhui akusudiayo kuyatoa mshairi. Mathalani, katika shairi la “Wimbo wa Kunguni” tulilolidondoa katika Kitangulizi, mshairi kaamua kuwa mstari wa 12 uwe na neno moja tu, tena wa mizani mbili tu: “sasa.” Inambidi msomaji ajiulize kwa nini mshairi kafanya hivyo. Ielekeavyo, hapa mshairi alitaka kuwekea mkazo neno hili, na kulipa nguvu ya msisitizo kuwa mambo yote hayo yahusuyo matatizo na migogoro ya ndoa yanatokana na usasa kwani hayakuwapo zamani. Ni wazi kuwa neno hili lingepoteza nguvu yake ya kusisitizwa kama lingewekwa na maneno mengine.

Kwa hiyo basi, sheria za kuifunga wizani katika mapigo ya aina hiyohiyo na ya idadi hiyohiyo ya silabi kwa kila mstari zinaweza kuifanya sanaa ivie, na shairi kama hilo la “Wimbo wa Kunguni”, lisingeleta athari hiyo ya kimaudhui kama lingefungwa na sheria hizo.

Tamko la Kezilahabi alitoalo katika maana yake ya shairi, kuwa katika kila shairi mna ukweli fulani wa maisha linatatanisha, kwani hata maana ya “ukweli” ina utata pia. Labda kwa vile baadhi ya wanafalsafa wamesema kuwa kila uongo ni ukweli fulani wa maisha; lakini tamko la Kezitahabi linaibusha swali moja muhimu: Je, huu “ukwell wa maisha” ni kwa macho ya nani? Kwa mtano, ni wazi kuwa shairi au kazi yoyote ya fasihi ya kipinga maendeleo – tuseme fasihi iliyoandikwa na kaburu anayeabudu ubaguzi wa rangi – itajaa wongo mtupu kuhusu hali za wanaobaguliwa; na itanuia kuuimarisha uongo huo ili kuendeleza unyama wa ubaguzi wa watu kufuatana na rang zao. Yako mashairi mengi sana yaliyojaa wongo mwingi ndani yake!!

Tamko la Kezilahabi halitotautiana na lile la Jumanne Mayoka ambaye, kati ya mengi aliyoyasema, kahitimisha juu ya ushairi kwa kusema: “kamwe ushairi hauwezi kuwa na uhusiano wowote na ujinga wa binadamu. Kazi ya ushairi ni kuuzindua na kuuelimisha umma wa binadamu.”13

Tatizo kubwa la Mayoka ni kuwa ametoa matamko ya jumla jumia mno kutokana na imani yake ya “utakatifu” wa usbairi. Kazi ya ushairi ya “kuuzindua na kuuelimisha umma wa binadamu” hutegemea masuala mbalimbali ya kijamii, hasa ya maslahi ya kitabaka. Katika jamii za mfumo wa kibepari, kazi ya ushairi mara nyingi ni ya kuwalaza na kuwapumbaza watu ili waendelee na ujinga wao kuhusu hali zao. Kazi za namna hii ni zile zinazoeleza uzuri wa maua na machweo ya jua; utamu wa nyimbo za ndege na za mawimbi ya bahari; pamoja na mambo mengine ya kindotondoto wakati ambapo mamilioni ya watu katika jamii hiyo hiyo wanaendelea kuteswa na kugandamizwa. Kazi za namna hii za ushairi katika jamii hizi husiflwa sana na vyombo vya habari, majarida na wahakiki; na zile zinazojaribu kuwazindua oa kuwaelimisha wanyonge zinapigwa vita vikali. Ijapokuwa kwa Mayoka shairi ni lile tu linalozindua na kuuelimisha umma, lakini tujuavyo yamejaa mashairi chungu ozima ya kupumbaza na kuuzubaisha umma.

Mayoka angeihusisha nadharia yake ya ushairi na mifumo mbalimbali ya kijamii, pamoja na nguvu za kitabaka katika mifumo hiyo, angelupatia nadharia sahihi zaidi.14

Sehemu ya mwisho ya maana aitoayo Mulokozi nayo ina matalizo kidogo. Siyo lazima kila shairi lieleze mambo yake “kwa njia inayoburudisha moyo,” kwani yako mashairi mengi mno yanayotoa maudhui vake kwa niia inayokasirisha na hata kukera moyo.

Abdilaut Abdalia naye atuelezapo juu ya “lugha nyofu, tamu na laini,” tena lugha “tetelezi kwa ulimi kuitamka” anatetereka kwani matumizi ya lugha hutegemea maudhui ya shairi. Lugha “nyoofu, tamu na laini” huweza kutumiwa kwenye maudbui kama yale ya mapenzi; wakati ambapo iwapo shairi linahusu vita au hasira lugha itakayotumika ni kali, chungu, na ya kukatakata.

Baada ya kuchunguza kwa kifupi kuhusu maana za ushairi kufuatana na mawazo ya wataalamu wa fasihi ya Kiswahili, sasa tunaweza kutoa maana tuonayo inasadifu kuueleza ushairi.

Ushairi ni utanzu wa fasihi utumiao mpangilio wa lugha ya mkato, ya kipicha na iliyopangwa kwa njia iletayo mapigo mahsusi kufuatana na maudhui yahusikayo.

USHAIRI WA KISWAHILI

Zamani sana lugha ya Kiswahili ilikuwa ya watu wa pwani ya Afrika ya Mashariki tu. Lakini leo hii hutumika Afrika ya Mashariki yote pamoja na nchi za jirani kama vile Zaire, Burundi, Somalia na Malawi. Kwa hiyo ni wazi kuwa wakati tukiongelea kuhusu ushairi wa Kiswahili mara nyingi tunamaanisha ule ushairi uliotungwa kwa lugha ya Kiswahili, na ambao unawahusu watu watumiao lugha ya Kiswahili maishani mwao.

Kwa sababu tunajua wazi kuwa historia ya ushairi wa Kiswahili haianzi na matumizi ya vina na mizani – kwam tuna ushairi mwingi wa Kiswahili kutoka katika fasihi simulizi ambao haufuati “sheria” za vina na mizani15 – sisi hatutachukulia vina na mizani kuwa ni uti wa ushairi wa Kiswahili. Pia tunajua wazi kuwa kuita vina na mizani kuwa ni roho ya ushairi wa Kiswahili ni kosa kwani ushairi wa Kiarabu na mataifa mbalimbali ya Ulaya pia una mizani na vina kama atuelezavyo mtaalamu Lyndon Harries:

…kwa mujibu wa arudhi ya Kiarabu ilishikiliwa kuwa, bila kujali urefu wa shairi, vina vya mwisho katika kila ubeti lazima vipatane tangu mwanzo hadi mwisho wa shairi. Kwa hiyo, hata katika tungo zenye vina vya kati, mtunzi akishaamua tu kutumia kina fulani katika kipande cha kwanza, ilibidi akitumie kina hicho hicho hadi mwisho… utaratibu wa namna hii bado unafuatwa katika mashairi mengi ya Kiswahili…16

Kumbe basi hicho wakntacho “roho” ya ushairi wa Kiswahili kipo katika ushairi wa Kiarabu na mataifa mengine. Je, ushairi wa Kiarabu ni ushairi wa Kiswahili kwa sababu kote ipo “roho” hiyo?

Si nia ya kitabu hiki kujaribu kupuuza sanaa ya urari wa vina na mizani katika ushairi wa Kiswahili. Ni wazi kuwa sanaa hii ikitumiwa vizuri ni pambo zuri sana katika ushairi. Hata hivyo jambo linalosisitizwa hapa ni kuwa vina na mizani sio yipengele pekee katika sanaa ya ushairi wa Kiswahili; wala sio lazima vina na urari wa mizani utumiwe katika utungaji wa ushairi wa Kiswahili.

Usanii katika kazi ya fasihi huamuliwa na mambo yaliyomo katika kazi hiyo. Yaani kutumia au kutotumia mambo kama vile tamathali, vma, mizani, na kadhalika, hutegemea jambo linaloongelewa katika kazi ya fasihi. Kwa kifupi fani ya kazi ya fasihi huamuliwa na nwudhui ya kazi hiyo. Sasa basi, ushairi wa Kiswahili ni upi?

Mwanzoni tulitaja uhusiano wa fasihi na utamaduni wa jamji inayohusika. Uhusiano huu utatusaidia hapa katika kueleza ushairi wa Kiswahili. Tutaamua kuwa kazi fulani ni ya fasihi ya Kiswahili au la kutokana na jinsi ilivyojitambulisha na ilivyojihusisha na utamaduni wa Waswahili. Hapa neno Waswahili halimaanishi kabila la Waswahili kwani kabila la namna hiyo halipo leo. Waswahili hapa ni wananchi wa Afrika ya Mashariki na Kati kwa ujumla na wala si wale tu wanaoishi katika pwani ya nchi hizi.

Sasa basi, utamaduni huo wa Waswahili ni upi? Huu ni ule unaohusu mila na jadi za Waswahili; sanaa zao, siasa, sayansi na uchumi wao; pamoja na mambo mengineyo yanayokamilisha maisha ya watu hao. Kwa hiyo ushairi wa Kiswahili ni dhahiri kuwa utakuwa na wahusika, mawazo, maudhui, falsafa, historia, dhamira na mambo mengineyo yanayoambatana na maisha ya Waswahili. Kutokana na mambo yote haya, hata kama shairi lina vina na mizani, kama halitekelezi mambo hayo ya kiutamaduni, basi hatuwezi kuliita la Kiswahili!

Maelezo

1. Wazo hili la kuwa chanzo cha ushairi ni uchawi limcelezwa kwa kirefu na mtaalamu George Thomson katika Studies in Ancient Greek Society: The pre-historic Aegean (Lawrence and Wishart, London, 1961). Katika Kiswahili wazo hili limeendelezwa na wahakiki kama vile K.K. Kahigi katika makala yake “Ushairi (Mtazamo wa Kisayansi)” katika Kiswahili, Tol. 411, (Machi 1975). Baadhi ya wataalamu wa ushairi wa Kiswahili wameligusia jambo hili – labda bila wao wenyewe kuwa na habari – kwa kuupa ushairi Sifa ya kuuathiri moyo kwa “namna ya ajabu,” ijapokuwahawakulipanua. Ila Jumanne Mayoka, katika kitabu chake cha Mgogoro wa Ushairi na Diwani ya Mayoka, (Dar es Salaam, TPH, 1986), ameielewa vibaya nadharia hii akadhania kuwa akina George Thomson na Kahigi waongeleapo “uchawi” wana maana ya “tunguli za kichawi” na uramali. Nguvu za kishairi zinazoweza kumfanya mtu alie, ahuzunike, apate moyo wa ujasiri, na kadhalika, ndizo zilizokusudiwa hapa na wataalamu hawa; kwa hiyo “uchawi” ni neno ambalo limetumiwa kishairi zaidi kuliko kwa maana ya ulozi.

2. Dai hili la kwamba vina na mizani ni uti wa ushairi wa Kiswahili linajitokeza katika matamko mengi ya wanamapokeo. Mathalani, katika kitabu cha Jumanne Mayoka, Mgogoro wa Ushairi na Diwani ya Mayoka, (uk. 28), mwandishi anadai hivi:

Vina na urari wa mizani ni uhai, roho na uti wa ushairi wa Kiswahili. Iwapo vitaepukwa au kubezwa hatutaweza kutambua kuwa hili ni shairi au la.

Dai kama hili linalochukua vipengele viwili au vitatu vya fani na kuviita kuwa ni robo na uhai wa kazi fulani ya saoaa linaua sanaa!!

Yakaenda na kwa kasi
Ni kukanda bila rasi
Na mikanda kuiasi
Hebu basi pigilia.

Utungo huu nimeutunga harakaharaka tu kwa kutumia maneno ya Kiswahili yaliyojipanga katika vina vya kati oa urari mzuri wa mizani. Lakini maneno yenyewe hayana maana wala mantiki, ijapokuwa hiyo roho na uhai audaio Mayoka upo. Huu ni ubeti kibudu, hauna ubai wowote! Uhai wa kazi yoyote ya sanaa hutokana na uwiano mzuri baina ya fani na maudhui, na kamwe hauwezi kutokana na vipengele viwili au vitatu tu vya fani!

3. M.M. Mulokozi, na K.K. Kahigi: Malenga wa Bara, (Dar es Salaam/Kamnala/Nairobi: East African Literature Bureau, 1976).

4. Shaaban Robert, “Hotuba Juu ya Ushairi,” Journal of The East African Swahili Committee, 28/1 (1958).

5. Mathias Mnyampala, Diwani ya Mnyampala, (Dar es Salaam Kampala/Nairobi: East African Literature Bureau, 1970); “Dibaji.”

6. A. Abdalia, “Tanzu za Ushairi na Maendeleo Yake.” Makala, (Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, 1974).

7. E. Kezilahabi, “Ushairi wa Mapokeo na Wakati Ujao,” katika kitabu cha J.P. Mbunda (Mhariri), Uandishi wa Tanzania: Insha, (Nairobi/Kampala/Dar es Salaam: East African Literature Bureau, 1975), uk. 23.

8. M.M. Mulukozi, “Ushairi wa Kiswahili ni Nini?” Lugha Yetu, Na. 26 (1975), uk. 12

9. J. Mayoka, Mgogoro wa Ushairi, uk. x

10. Ili kuelewa zaidi kuhusu matapo ya fasihi za Ughaibuni na yale ya fasihi ya Kiswahili ya urasimi mkongwe, urasimi mpya, ulimbwende na uhalisia, soma sura za 1 na 2 za kitabu cha F.E.M.K. Senkoro, Fasihi na Jamii (Das es Salaam: Press and Publicity 1987).

11. Mulokozi, “Ushairi na Kiswahili ni Nini?” uk. 12

12. Yafuatayo ni baadhi ya marejeo kwa wenye nia ya kusoina zaidi KUHUSU wizani: C. Kugh Holman (Mhariri), A Handbook to Literature (Indianapolis: Odyssey, 1975), hasa kurasa za 4456-457; William R. Bascon na Melwile J. Herskovits (Wahariri), Continuity and Change in African Cultures (Chicago & London: The Univ, of Chicago Press, 1959); Ruth Finnegan, Oral Poetry (Cambridge: Cambridge Univ. Press, 1977); Desmond Graham, Introductin to Poetry (London: Oxford Univ. Press, 1968); na A.M. JONES, African Rhythm.” Africa 24 (1954)

13. Kezilahabi, “Ushairi wa Mapokeo.” uk. 5

14. Nimejaribu kuainisha fasihi katika mifumo tofauti ya jamii tangu jamii ya mwanzo hadi ya sasa katika Sura ya Kwanza (“Fasihi Katika Mifumo Tofauti ya Jamii”) ya Fasihi ya Jamii.

15. Huu ulikuwa katika umbo la cyimbo za ngoma, za kazi, majigambo, na kadhalika. Kuhusu jambo hili, Mnyampala alisema haya: “… Mashairi ya Kiswahili, kabla ya watu hawajajua kuandika, yalikuwa yanatungwa na kuimbwa katika ngoma, majando, nyago, harusi na kadhalika; kwani mashairi si kitu kingine, ni nyimbo, na waliokuwa wakizitunga nyimbo hizo au kuziimbisha katika ngoma waliitwa ‘Manju’ au ‘Malenga’, nazo ziliendelea kuimbwa na kukumbukwa namna hiyo…” (Waadhi wa Ushairi, East African kuwa “mashairi si kitu kingine ni nyimbo” kwani si lazima kila shairi liimbike – na tujuavyo bila kuimbika maneno hayaitwe wimbo – hata hivyo Mnyampala anapoelezea kuhusu ushairi wa Kiswahili kabla ya maandishi anatudhihihshia wazo letu la awali kuhusu vina na nuzani. Kwani, si kila wimbo ulikuwa na vina na mizani kati ya hizo za majaodo, oyago, ngoma, na kadhalika.

16. Lyndon Harries, Swahili Poetry, (London, 1966) uk. 186. Msisitizo wangu.

TANBIHI: Kutoka kitabu cha Ushairi – Nadharia na Tahakiki (Dar Es Salaam University Press, 1988, 168 p.) cha F.E.M. K. Senkoro

4 thoughts on “‘Mgogoro’ katika ushairi wa Kiswahili”

    1. Ni kazi nzuri, kila kitu kina taratibu zake, shairi za mapokeo ndiyo haswa kwani zitamtaka mtungaji atumie maarifa kufikisha ujumbe tofauti na ya mabadiliko

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.