UCHAMBUZI

Kikwete azungumza asichokiamini akitutaka tumuamini

Nimekua nikitafakari matamshi ya hivi juzi tu na hotuba ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jakaya Khalfani Mrisho Kikwete mkoani Singida alipokuwa akizungumza kwa kiburi na kusema uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa na dosari kubwa na baada ya kuzungumza na wenzake wakakubaliana na maamuzi ya Tume ya Uchaguzi (ZEC) kuwa eti uchaguzi urejewe. Nilitikisa kichwa na kucheka. Nikicheka kwa sababu nikijiuliza hivi kweli katika dunia hii ya leo, kiongozi anaweza kujidanganya, kuudanganya umma na jumuiya ya kimataifa na kuamini kwamba matamshi yake yamepokewa kuwa ni sahihi?

Hakuna asiyejuwa uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa huru na haki. Kwa mara ya kwanza katika historia ya chaguzi za Afrika ambako tume za uchaguzi sio huru, wametokeza waangalizi wote wa ndani na nje wakiwa na kauli moja. Ndiyo kusema kwa kauli yake hiyo, Kikwete anawasuta hata waangalizi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika na hata Umoja wa Madola (Commonwealth), jumuiya ambazo Tanzania ni mwanachama.

Alichokionesha Kikwete ni kwamba alihusika moja kwa moja na kilichotokea Zanzibar, ambacho mimi nakiita Mapinduzi. Sio tu kuwa akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi la Ulinzi na Usalama hakuwa na ubavu wa kuwaambia CCM Zanzibar kwamba wameshindwa na wajiimarishe kwa 2020 na kuipa nafasi demokrasia na matakwa ya Wazanzibari yatekelezwe, bali pia mwenyewe akiwa mwenyekiti wa CCM Taifa alilazimisha kukiukwa kwa matakwa ya Wazanzibari ili kulinda masilahi yake binafsi.

Kisha kuna kichekesho chengine. Umoja wa Afrika, ambao uliufuatilia uchaguzi huo na kuutangaza kuwa huru na wa haki, ndio huo huo uliomteuwa Kikwete hivi karibuni kuwa mjumbe maalum kuhusu Libya.

Yaani mtu ambaye hauamini Umoja wa Afrika kwenye hukumu yake ya Uchaguzi ndani ya nchi yake na aliyekandamiza demokrasia nyumbani kwake anatumwa akaisimamie kwengineko. Hivi Walibya watakuwa tayari kupatanishwa na kiongozi ambaye alitumia vyombo vya dola kukandamiza sauti ya umma ndani ya nchi yake mwenyewe?

Viongozi wa CCM wanashindwa kutazama dunia ilikotoka na historia inatupa funzo gani. Udikteta una mwisho. Mifano hai ni Urusi na mamlaka ya Chama cha Kikoministi tokea 1917 baaada ya mapinduzi yalioongozwa na Vladimir Ilych Lenin hadi 1989. Alau Mikhael Gorbachov alisoma alama za nyakati na kuleta siasa ya uwazi na mabadiliko – Glasnost na Perestroika. Lakini ukandamizaji ulifikia mwisho wake. Umma katika jamhuri nyengine zilizounga Muungano wa Jamhuri za Kisovieti, kila moja ikadai mamlaka yake na nyengine zikajumuika upya katika kile kinachoitwa Umoja wa Madola ya iliokuwa Urusi, kila moja ikiwa na haki sawa, zaidi ukiwa ni ushirikiano wa kiuchumi. Iko wapi Yugoslavia ya zamani iliyozikusanya pamoja jamhuri zaidi ya saba chini ya Marshall Josef Broz Tito?

Wahafidhina wanapodhania wakati ndio huu

Mbali na wahafidhina walioyapindua matakwa ya Wazanzibari walio wengi Oktoba 25 kwa kumshinikiza Jecha Salum Jecha, hawa wakiwa kina Vuai Ali Vuai, Balozi Seif Ali Iddi, Shamsi Nahodha na Pandu Kificho, hivi karibuni walijitokeza wale waliokuwa wakishamiri enzi ya Dk. Salmin Amour, wakiongozwa na Amina Salum Ali, kujionesha kuwa nao wapo na wana usemi kwenye siasa za nchi. Wanachokisambaza ni kuwa Maalim Seif Sharif Hamad ni mtu anayetaka sana madaraka. Walichosahau ni kwamba mwanasiasa yeyote lengo lake ni kuongoza, kuwa na madaraka, lakini kubwa ni madaraka kwa faida ya nani. Ukimlinganisha Maalim Seif na wengine, jawabu walilitoa Wazanzibari wengi katika uchaguzi wa Oktoba 25.

Inasikitisha na kukirihisha kumsikia Amina Salim Ali, aliyekuwa Balozi wa Umoja wa Afrika mjini Washington, akitoa matamshi ya aina hiyo ya kukejeli demokrasia. Nilifikiri akiwa Marekani, alifunuka macho na kujifunza kutokana na nchi hiyo kuwa mojawapo ya zilizopiga hatua katika suala la demokrasia. Lakini licha ya hayo aliifanyia nini Afrika, alizungumza lipi la kuipiga jeki Afrika katika katika siasa za kimataifa? Hitimisho langu na nionavyo ni kuwa aliondoka na fikra finyu na kurudi na fikra zile zile. Sikumbuki kama hata kwengineko Afrika wakijuwa bara lao lina mwakilishi Marekani. Daima Amina alikuwa likizo na sasa akina yeye ndio wanataka Zanzibar iwe na matumaini nao.

Hata watu aliofuatana nao katika mazungumzo na gazeti la Mwananchi akina Mohamed Hija (aliyekuwa naibu mkuu wa usalama wakati wa utawala wa Salmin) na Abdullah Rashid (mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib kipindi hicho hicho) ni watu ambao utendaji wao unajulikana kwa Wazanzibari. Amina anafikiri ataweza kuutumia mpasuko huu na vurumai ya sasa ndani ya CCM kupenya na kurudi tena madarakani. Sisemi haliwezekani kwani ndani ya CCM iliyokosa dira kila kitu kinawezekana, lakini ni siasa zilizokosa uadilifu, na hawa ni watu waliokwisha kisiasa na wasio na jipya la kuwapa matumaini Wazanzibari. Kama uchaguzi wa Machi 20 utafanyika kama walivyodhamiria, hatima ya Zanzibar ni mbaya.

Magufuli na utatuzi wa mgogoro

Matarajio ya kwamba Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaweza kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya kisiasa Zanzibar sasa yamefifia kabisa. Magufuli amedhihirisha kwamba hata kama alikuwa na nia hiyo, lakini mwenye kuukamata mpini ni CCM na mtangulizi wake ni Kikwete. Hilo limejiotokeza dhahiri katika kauli ya Mwenyekiti Kikwete aliyoitoa Singida kuhusu Zanzibar.

Pengine Maalim Seif sasa amejithibitishia dhahiri kwamba aliokuwa akizungumza nao kutoka upande wa CCM hawakuwa na nia njema. CCM ni ile ile iwe Bara au Visiwani. Magufuli au Kikwete ni wale wale wasio tayari kuona demokrasia inatekelezwa sio Bara wala zanzibar. Na sasa swali wanalojiuliza Watanzania wapenda haki ni je haya yataendelea hadi lini? CCM inajenga msingi gani kwa mustakbali wa vizazi vijavyo na, juu ya yote, nani hasa mwenye ufumbuzi?

Tunaiombea amani Tanzania, lakini subira ina mwisho sawa na ukandamizaji ulivyo na mwisho. Nguvu za dola zilitumika Urusi, Yugoslavia, Burkina Faso na kwengineko, lakini hakuna nguvu kubwa kama nguvu ya umma. Tunapaswa kufumbua macho na kusikiliza kilio sio tu cha Wazanzibari, bali pia jumuiya ya kimataifa kuhusiana na matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25.

Kikwete anasema uchaguzi ulikuwa na dosari kubwa. Siku mbili baadaye wamejitokeza wajumbe wawili wa tume hiyo ya ZEC wakiitaka jumuiya ya kimataifa ijiingize kati kuutatua mgogoro wa Zanzibar, la sivyo visiwa hivyo vinaweza kuelekea pabaya. Hii tayari inaonesha Tume imegawika na kwa maana hiyo haifai, ina dosari. Je kuna uhalali wa uchaguzi huo wa marudio katika hali hii ya Tume? Wakati tume ina dosari hizi, vipi uchaguzi utakuwa na uhalali?

Wakati matumaini ya Wazanzibari na Watanzania wapenda amani ni kuwa suluhisho litapatikana kwa kutumiwa busara, la kukumbusha ni kwamba viongozi mpo lakini hakuna lisilokuwa na mwisho. Udikteta una mwisho, madikteta kuna siku wataondoka, lakini taifa linabakia na taifa ni watu. Historia itawaweka nafasi yenu na kuwahukumu. Na hilo halitakuwa na maana kwenu wala kwa familia zenu mutakazoziwacha baada yenu.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na mtu aliyejitambulisha kama msomaji wa Zanzibar Daima

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.