Kifua chetu ki mbele, twatembea na kuringa
Kifua hakina pele, chang’ara amba upanga
Kifua hiki ki mbele, kina uzio na kinga
Hata kilenge mshale, haudungi utadunda
Kifua twakitanua, kwa madaha na kuringa
Kifua cha kishujaa, kilichovunja upanga
Kifua chatandawaa, wakikimbia wajinga
Wasema hwepataona, kifua chenye mashina
Kifua ni kile kile, mbili tano kilounga
Kifua kimaumbile, mbili nane tukijenga
Kifua chaenda mbele, kila siku ikisonga
Kifua mbele kwa mbele, wacha wapige kelele
Kifua chetu murua, twashangaa mwakipinga
Kifua mwakitofoa, kwa marungu na mapanga
Kifua kichatulia, hakiumi kina kinga
Bure nguvu mwaziua, kifua kimejijenga
Kifua tembea mbele, ‘siogopee mzinga
Kifua we’ songa mbele, u mgumu ja mkonga
Kifua u mule mule, wache wapige kipenga
Usishituke na wale, akili walozirenga
Amour Hadji
Haile Selassie School
Zanzibar
5 Februari 2016