Kwa nini?
Kwa nini iwe ni wao, iwe ni wao si siye
Iwe watakalo liwe
Lisiwe tutakalo siye
Watwae lisilo lao, la kwetu walichukuwe
Kisha twambwe siye nao, kweli mtu na nduguye
Kwa nini?
Kwa nini nguvu wapewe, nguvu hata wasonayo
Silaha wasaidiwe
Na vifaru waletewe
Kulindwa maovu yao, kusudi sisi tusiwe
Tusiwe walivyo wao, kisha bado tuambiwe –
Sote ndio hao hao
Kwa nini?
Kwa nini niulizayo, sambe sina jawabuye
Ningawa nauza leo
Yawapo kale kwa hayo
Ungajuwa hayo nawe, nayo mengi mengineyo
‘Kwa nini’ hii naiwe, kwetu na kwao zinduo
Tukikaa tutambuwe
Si huru siye na wao!
Mohammed K. Ghassani
22 Januari 2016
Bonn
Kazi njema kaka. Nashukuru