Uzito wa dhambi hii, u juu yake kichwani
Wamtesa yuko hai, hajatiwa kaburini
Kila mahala hakai, asijione motoni
Chumbani anapongia, ‘kajibwaga kitandani
Jinamizi humjia, naye yu usingizini
Silisili ‘kamtia, toka juu hadi chini
‘Kisema akaye macho, njozi awe hazioni
Humjalia makocho, ‘kamuenea mwilini
Hapo kila asemacho, huwa hakisikikani
Pale nje atokapo, kusudi awe kundini
Huzinga watu walipo, walakini hawaoni
Na hata awaonapo, si watu bali majini
Dhambi yaja juu yake, kwa sauti yenye kani
Yaimba makosa yake, kwa hasira si kughani
‘Kitubu kwa Mola wake, hwamba haiwezekani
Mohammed K Ghassani
Bonn
8 Januari 2016