Subiri kheri na shari
Subira ni ujabari
Ni woga kutosubiri
Nawe woga ‘siwe nao
Ziche za Mola amri
Siwe mja wa kiburi
Papara ni ufakiri
Nawe ujitenge nao
Nenda yandame safari
Na moyo wenye dhamiri
Utaifika bandari
Pole pole si kwa mbio
Kama waliosubiri
Subira nguvu ya siri
Kwenye vita na kikiri
Ndiyo silaha na ngao
Hutajuta ‘kisubiri
Subira haidhiri
Basi baki na dhamiri
Litatimu kusudio
Mohammed K. Ghassani
Agosti 2000
Zanzibar