Si jipya nilinenalo, lilishanenwa dahari
Mote linanenwa lilo, na miye nalikariri
Jambo nikushaurilo, hupaswi kulighairi
Subiri akhi subiri
Kwamba kila lianzalo
Ndilo pia liishalo
Hakuna aliyejuta, kwa kuwa alisubiri
Hakuna aliyepata, kwa papatu na kikiri
Na kila anotafuta, hutafuta na saburi
Akhi na wewe subiri
Kushavyoanza nyonyota
Upandacho kitaota
Wala hupotezi kitu, akhi yangu ‘kisubiri
Wala hutakera mtu, moyowo ‘kiusitiri
Subira ni utu wetu, tumeumbwa kusubiri
Subiri akhi subiri
Kilokwenda jana yetu
Kitarudi kesho yetu
Nyuki asaliye tamu, ela yuna misumari
Na mkate wa ajemu, una joto la tanuri
Kupata haya lazimu, kuteswa uwe tayari
Tumai akhi subiri
Ndivyo kibinaadamu
Mwisho wa chungu ni tamu
Hu wa mwanzo kukupata, wala huwi wa akhiri
Yewapata walopita, na wajao yatajiri
Na wao hawakujuta, sababu walisubiri
Subira nawe subiri
Wasubirio hupata
Kama wanavyotafuta
‘Tasema nikirudia, sababu hii si siri
Hikuona ‘takwambia, na hata ukisafiri
Salamu ‘takutumia, na daima ‘tadhukuri
Wasia wangu subiri
Subiria kwa lolote
Uone mwisho wa yote
Mohammed K. Ghassani
Septemba 2000
Zanzibar
Nashukuru kaka Kwa kazi nzuri. Kila la heri katika mwaka wa 2016
Mosol Kandagor Chuo Kikuu cha moi Kenya
Sent from my iPhone
>