UCHAMBUZI

Makosa matatu ya kuepukwa na Magufuli kwa Zanzibar

Kwa mara nyengine tena, Zanzibar imo kwenye mzozo usioweza kuelezeka kwa msamiati wowote zaidi ya uhuni wa waroho wa madaraka, japokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Masuala ya Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga anatumia kijembe cha “utamaduni wa kisiasa wa Zanzibar”. Huu si utamaduni. Huu ni uhuni uliopewa sura ya kisiasa kwa kuwa unatendwa na wanaoitwa wanasiasa.

Ni jambo jema kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) sasa inaonekana kusaka suluhisho la uhuni huu, baada ya Rais John Magufuli kukutana kwa mara ya kwanza na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, mwanzoni mwa wiki hii. Mkutano huu ulichukuwa masaa mawili na ukaishia kwa taarifa fupi kwa waandishi wa habari, ikiwa ni mara ya kwanza tangu vikao vinavyoendelea ikulu ya Zanzibar vikiwashirikisha marais wastaafu wa Zanzibar pamoja na Maalim Seif na Balozi Seif Ali Iddi kuwa na taarifa kwa waandishi wa habari kutoka Ikulu.

Siasa za Muungano kuelekea Zanzibar

Licha ya kuupenda kwangu ‘Muungano’, mimi si muumini wa ‘siasa za Muungano‘ kuelekea Zanzibar. Kwa hakika, nina mziya na dhima ya viongozi wa SMT, nikiamini kuwa wanatumikia sera maalum dhidi ya Zanzibar ambayo, hata kama haikuandikwa popote, inasomeka hivi: “Muungano imara kwa Zanzibar dhaifu, Zanzibar imara kwa Muungano dhaifu.” Na kwa vile kuwa na Muungano imara ndilo lengo kubwa na la kipekee, basi kila hatua moja inayochukuliwa kuelekea kwenye lengo hilo huidhoofisha Zanzibar kwa makusudi.

Rais wa kwanza wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere
Kutoka kulia: Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Karume, Rais wa Hamhuri Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, na Waziri wa kwanza wa Sheria wa Muungano, Hassan Nassor Moyo.

Mafanikio ya sera hiyo yanawezeshwa kwa kiasi kikubwa sana na viongozi wa Zanzibar wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani kwao wao hiyo ndiyo njia pekee ya  kubakia madarakani. Nje ya mduara wa papo kwa papo wa kuitumikia na kutumiliwa na sera hiyo, viongozi wa CCM Zanzibar hawana pengine pa kushika.

Na Mohammed Ghassani
Na Mohammed Ghassani

Ile inayoitwa ‘migogoro ya kisiasa’ visiwani Zanzibar, ukiwemo huu uhuni wa tarehe 28 Oktoba 2015, ina mahusiano makubwa sana na mduara huu. Kwa hivyo, suluhisho la kudumu na la uhakika limo kwenye jitihada za kuuvunja mduara wenyewe kwa maslahi mapana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar.

Hapa ndipo penye kiini cha makala hii inayoongozwa na kile kinachoitwa ‘husnu-dhana’ (dhana njema), licha ya kuwa mwenyewe nina mziya nilioutaja hapo juu na, hivyo, ninaweza kuhojika na pia kukosoleka. Je, Magufuli si mwana-CCM? Je, naye si kiongozi wa SMT? Sasa kipi kinachonifanya niwe na dhana njema kwake? Jawabu ni moja tu – Rais Magufuli ameonesha kuwa ni ‘mwana-CCM asiye ule u-CCM tuliouzoea kupitia utendaji wake. Hivyo, dhana yangu njema itabakia hadi pale naye atakapobadilika. Akibadilika, sitakuwa nimepoteza jambo zaidi ya kurejea kwenye kile nilichokuwa nikikiamini tangu mwanzoni.

Niliwahi kuwa na msimamo dhidi ya Benjamin Mkapa na pia Jakaya Kikwete wakiwa marais wa SMT juu ya kile walichoitendea Zanzibar na kwa bahati mbaya sana kwangu ni kuwa hawakunisuta kwa kutenda kinyume na khofu zangu mpaka siku wanaondoka madarakani. Hawakubadilika, nami sikubadilisha msimamo wangu. Rais Magufuli asipobadilika, nami sitabadilisha, lakini akibadilika, nami nitabadilisha.

Kuna kitu kinaniambia kuwa Rais Magufuli ni kiongozi anayejaribu kupapasa kuongoza njia akiwa gizani. Anaweza kuwa anafanya makosa katika kupapasa huko, lakini ni kiongozi anayejaribua, nami kama raia nina wajibu wa kumsaidia kuepuka makosa ambayo niliyaona kwa watangulizi wake, ili ajuwe anapopapasa anaashika nini na nini humo gizani alimo na, hatimaye, endapo atafanikiwa, basi itakuwa imefanikiwa Tanzania, itakuwa imefanikiwa Zanzibar.

Unafiki wa Mkapa na Kikwete

Kosa la kwanza la Mkapa na Kikwete kuhusiana na Zanzibar lilikuwa ni unafiki wao wa kujidai wanaulinda Muungano kwa gharama za haki, uhuru na heshima ya Wazanzibari. Mwaka 2005 wakati Mkapa anaulizwa na waandishi wa habari wa kimataifa kwa nini alituma wanajeshi na silaha nzito visiwani huko, alijibu kwa kebehi: “Kwa nini hamuulizi kwa nini Bush amepeleka vifaru na majeshi Iraq!?” Mwaka mmoja nyuma, aliyekuwa waziri wake wa Ulinzi  na Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Phelomon Sarungi, alisema kwamba “Muungano na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ni watoto pacha na hivyo jeshi halitavumilia kuona Muungano unahatarishwa.”

Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa

Miaka 10 baadaye, Kikwete alifanya yale yale aliyofanya Mkapa. Nilikuwepo wakati ofisi za kutangazia matokeo za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Bwawani, zikivamiwa na luteka ya kijeshi siku moja kabla ya uchaguzi kufutwa kihuni na Jecha Salim Jecha tarehe 28 Oktoba. Jeshi liliendelea kuvikalia vituo na maeneo muhimu miezi takribani miwili baada ya hapo, hadi Maalim Seif alipokutana na Rais Magufuli tarehe 21 Disemba.

Rais Magufuli atafanikiwa pakubwa kama ataliangalia suala la Zanzibar kwenye uhalisia wake na bila kuzamisha kichwa mchangani. Ayaone mafungamano makubwa baina ya siasa za uchaguzi wa Zanzibar na sera ya Muungano kuelekea visiwa hivi. Alione tatizo lililomo ndani ya chama chake, ambacho bado hakijataka kuutambua uhalisia kuwa pande hizi mbili za Muungano zinaweza kutawaliwa na vyama viwili tafauti vya kisiasa.

Rais Magufuli auone mtego uliomo kwenye mduara wa papo kwa papo wa kutumiliana baina ya CCM Dodoma na CCM Kisiwandui kwa maslahi ya kikundi cha watu na sio chama kizima wala nchi nzima. Kikundi cha Dodoma kinajenga picha kuwa bila wenzao wa Zanzibar kukidhi matakwa yao, basi hawawezi kusalia madarakani, na kikundi cha Zanzibar kinatumia fursa hiyo kujenga vitisho kwa wenzao wa Tanganyika kwamba bila ya wao kuwapo madarakani, basi hakutakuwa tena na Muungano. Kosa hili ni la muda mrefu. Lilikuwa likitendwa hata na Mwalimu Julius Nyerere wakati akivumilia uimla wa serikali ya awamu ya kwanza visiwani Zanzibar.

Rais Magufuli anaweza kujifunza kwa kutokuingia kwenye mtego huu, na kama akiliendea vyema atagundua kuwa kiini cha yote kimo kwenye muundo wa Muungano na hapo, hapana shaka, ndipo atakapofahamu kuwa hataweza kulimaliza la Zanzibar salama usalimini na milele, kama hapakupatikana katiba mpya inayoakisi uhalisia huu.

Kukosa uthubutu wa kisiasa

Kosa la pili la watangulizi wake ni kukosa uthubutu na kukumbizia majukumu kwengine, ambalo yumkini linatokana na hilo la kwanza la kuwa wanafiki. Wote wawili, kwa nyakati tafauti, walitaka kuonesha kuwa matatizo ya Zanzibar yanasababishwa na kundi la wahafidhina wenye nguvu za ajabu ndani ya chama chao kwa upande wa Zanzibar.

Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete

Wakati akizungumza na mwandishi wa jarida la Prospect, Jonathan Power, mwishoni mwa utawala wake, Mkapa alielezea masikitiko yake jinsi wenzake Zanzibar walivyomzuwia kuleta mabadiliko ya kidemokrasia na heshima kwa haki za binaadamu. Naye Rais Kikwete hata alipokuwa bado waziri wa mambo ya nje wakati wa Mkapa, alinukuliwa akisema amechoka na kuuliziwauliziwa mgogoro wa Zanzibar kila anapokwenda duniani na sasa ulikuwa umefika muda wa kuumaliza kabisa kabisa, lakini ulipofika mkutano wa Butiama wa uliokuwa uwe Muafaka II, akasalimu amri mbele ya wahafidhina hao hao.

Kwa sababu ya kukosa kwao uthubutu wa kulikabili tatizo halisi, wakawageukia wapinzani kwa lugha za kibaguzi na dharau kama wao ndio wenye jukumu la matatizo yaliyopo Zanzibar.

Katika hotuba yake ya kwanza bungeni Disemba 2005, Kikwete alisema anasikitishwa na “mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar”, lakini kama alivyofanya mtangulizi wake Mkapa mwaka mmoja kabla ya hapo, naye akatupa lawama za mpasuko huo kwa kundi fulani tu la watu – Wapemba. Msimamo kama huu pia ulikuwa umeanza kufuatwa na utawala wa Rais Magufuli na, kwa hakika, ndio maana ya kauli ya Balozi Mahiga ya “utamaduni wa kisiasa wa Zanzibar.”

Matokeo ya kukosa uthubutu kwa Mkapa na Kikwete sio tu kwamba yameendelea kuwa muendelezo wa uhuni wa kila baada ya miaka mitano visiwani Zanzibar, bali pia wote wawili wameondoka na kuiwachia hali kuwa mbaya zaidi kuliko walivyoikuta. Wote waliyawachia makundi ya kihalifu yaundwe na yatekeleze hujuma dhidi ya maisha na mali za wananchi wa Zanzibar – majanjawidi yaliundwa wakati wa utawala wa Mkapa na Kikwete ameondoka akiyaacha mazombi na masoksi – huku wao wakiyaangalia hayo kuwa ni “matatizo ya Wazanzibari wenyewe.”

Lakini Rais Magufuli amejipatia mwenyewe jina la “mpasua majipu”, ambalo linamaanisha kuwa “mtu mwenye kuthubutu.” Ikiwa kweli upasuaji wake majipu utaakisika kwenye suala la Zanzibar, hapana shaka atafanikiwa. Na wala hapaswi kuchimba mbali sana. Kwa mfano, akiwa rais na amiri jeshi mkuu wa nchi, ana nyenzo na taasisi za kumpa taarifa zote za ukweli wa nini kilifanyika Zanzibar ndani ya miaka 10 iliyopita na nini kinaendelea sasa. Ndani ya ripoti hizo, muna mikasi ya kutosha ya kulipasua jipu la Zanzibar, sindano za kushonea, dawa za kulipaka na bendeji za kulifungia. Baada ya miaka mitano tu, kitakachobakia kitakuwa ni kovu na sio tena kidonda.

Kiburi dhidi ya upinzani

Kosa la tatu ambalo Rais Magufuli anapaswa kuliepuka ni kiburi cha kupuuzia nguvu za upinzani visiwani Zanzibar, akidhani kwamba unafiki na kukosa uthubutu kunatosha kuwatenga kando. Ukweli kwamba CCM imekaa madarakani muda mrefu na inadhibiti mihimili yote ya dola uliwalevya sana Mkapa na Kikwete, ambao daima walidhani upinzani visiwani Zanzibar hauna njia yoyote ya kukabiliana na dola zaidi ya kulilia mazungumzo, vikao na miafaka, ambayo wao ndio wanaoiamulia ajenda na hatima yake.

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Ni kweli kuwa uongozi wa CUF unaamini sana kwenye siasa za diplomasia, labda kwa kuzingatia pia mazingira hayo mbayo unakabiliana nayo. Kuelekea uchaguzi wa 2005, Maalim Seif alimuandikia mara kadhaa Mkapa wakutane, na hakuna siku Mkapa alijibu barua hizo. Kuelekea 2015, mara kadhaa Maalim Seif alimuandikia Kikwete waonane, lakini ilimchukuwa miezi kukubali na hata walipokutana mjini Dodoma mwezi mmoja kabla ya uchaguzi, mazungumzo yao hayakuchukuliwa hatua yoyote. Mmoja wa watu waliokutana na Kikwete baada ya hapo, aliniambia Kikwete aliwaambia anashangazwa na Maalim Seif kila siku anamuendea na matatizo tu na hakuna siku amemuendea angalau na “pendekezo la kupanda miembe kisiwani Pemba.”

Inafahamika kuwa hata mkutano wa tarehe 21 Disemba 2015 kati ya Maalim Seif na Rais Magufuli ulikuja baada ya barua saba tafauti kutoka kwa Maalim Seif kuomba mazungumzo hayo. Mkapa na Kikwete waliichukulia siasa ya diplomasia ya Maalim Seif kuwa ni udhaifu. Wakautumilia udhaifu huo. Wakadhani kwamba wanamuhujumu Maalim Seif na CUF yake. Matokeo yake ni kuwa sio tu CUF ilikibwaga chama chao kwenye uchaguzi wa 2015 visiwani Zanzibar, bali pia athari za nguvu yao zilivuuka maji na kuupa mbolea upinzani upande wa Tanganyika na kwa mara ya kwanza ukakaribia asilimia 40 ya kura za urais.

Siasa za diplomasia zafanya kazi

Hii inamaanisha kuwa siasa za diplomasia za upinzani visiwani Zanzibar zina nguvu kubwa na wala si alama ya udhaifu. Kuna faida ya kipekee kwa Magufuli kufanya kazi na watu ambao wanaamini kwenye diplomasia kuliko kuwaachia waje wageuke kuwa waumini na siasa za mapambano. Baada ya yote, wote ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naye ndiye mwenye dhamana ya kuwalinda na kuwatumikia.

Kwa hivyo, kama ni kiongozi wa kujifunza, makosa ni mwalimu mzuri na Rais Magufuli mahala pa kuanzia anapo. Vyenginevyo, miaka mitano au kumi ijayo, tunaweza kurudi tena hapa kuandika yale yale tuliyoyaandika kuhusu Mkapa na Kikwete. Huenda wenyewe  wanadhani kuwa yetu ni maneno ya chura mtoni tu yasiyomzuwia ndovu kunywa maji, lakini mambo yana zama na zamu na dunia inabadilika.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.