UCHAMBUZI

Inapopwerewa hoja ya Simai ikainuka ya Zitto

Labda kwa kuwa naonekana sana kwenye mijadala inayohusu, makhsusi, siasa za Zanzibar na za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa ujumla wake, si watu wengi wanaojuwa kuwa nilianza maisha yangu ya kujipatia riziki nyumbani kwetu Zanzibar kupitia utalii mwezi Mei 2001, na nikadumu kwenye kazi hiyo hadi Agosti 2010 nilipojiunga rasmi na Idhaa ya Kiswahili ya DW, Bonn Ujerumani.

Hapana shaka, nilikuwa najituma kwenye kazi nyengine ndani ya kipindi hicho, lakini ukiacha kipindi cha Septemba 2006 hadi Julai 2009 nilipokuwa masomoni Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, miaka yote kumi ya mwanzoni mwa kuajiriwa kwangu ilikuwa kwenye utalii.

_DSC2566Nilikuwa mwajiriwa wa kampuni ya utalii ya Fisherman Tours & Travel Ltd yenye makao yake Vuga, nilikoanzia kama mtembeza wageni na kumalizia nikiwa mwakilishi wa kampuni hiyo kwa mahoteli ya ukanda wa Kusini Mashariki mwa kisiwa cha Unguja.

Hadi hivi leo, kumbukumbu zangu njema za ajira nyumbani kwetu zimo kwenye utalii na kila nikifika nyumbani lazima nitembelee maeneo niliyokuwa nikiyafanyia kazi na kukutana na watu niliofanya nao kazi hiyo. Hivyo usishangae kuwa nazungumzia biashara ya utalii, ukasema “Ghassani kaingia choo cha kike“ kwa msemo wa vijana wa mjini.

Nimesoma maoni ya mmoja wa wamiliki wa maeneo yanayotembelewa sana na watalii, mkahawa wa Mercury, Bwana Simai Mohammed, ambaye aligombea na kushinda uwakilishi wa jimbo la Tunguu kwenye uchaguzi uliofutwa KIHUNI kupitia sauti ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha. Maoni yake yanatokana na kauli ya Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, juu ya hali ya uchumi visiwani Zanzibar (hasa kwenye biashara ya utalii, katika wakati huu ambapo nchi yetu tukufu ni mwathirika namba moja wa UHUNI huo.

Mimi ni miongoni mwa vijana wanaomuheshimu sana Simai kwa sababu ya kuwa kwake mjasiriamali wa Kizanzibari, ambaye anauthibitishia ulimwengu kuwa uwekezaji kwenye utalii unaweza kufanywa na kuendelezwa vyema na vijana wadogo wa Kizanzibari. Namuheshimu sana pia Zitto kwa sababu ya kile ninachoona kuwa uwezo wake mkubwa wa kisiasa na uchambuzi wa masuala ya kiuchumi. Kwa wasiojuwa, Zitto ni mchumi kwa fani yake, na ni mchumi wa kimataifa. Ninatafautiana na wote wawili kwenye masuala fulani ya kisiasa, lakini hilo haliondoshi heshima yangu kwao.

Kauli ya Zitto ilitokana na tamko la chama chake baada ya mkutano ya mkutano wa hali ya tathmini visiwani Zanzibar uliofanyika tarehe 19 na 20 Disemba mjini Unguja. Baada ya tamko hilo, Zitto aliandika hivi:

‘..Hakijaeleweka sababu ya uchaguzi. Wazungu waoga. Mtanziko ukiisha tutapata wateja wengi. Sio hivi unaona hamna watu “. Mfanyakazi wa Mercury Bar akinielezea sababu za wateja wachache katika Bar ya Mercury. Natumai mmiliki wa Bar hii atahimiza kumalizika kwa mtanziko wa kisiasa ili mshindi wa Urais atangazwe na Serikali ya Umoja wa Kitaifa iundwe.

Kama nilivyosema, mmiliki wa baa hiyo ni Simai na yumkini kwa kuwa Zitto anamjuwa kuwa Simai ni mwanasiasa visiwani Zanzibar pia, akawa amempa changamoto hiyo, ambayo Simai aliijibu hivi hapo hapo jana (tarehe 20 Disemba 2015:

“Kauli aliyoitoa Mh Zitto Kabwe haina mashiko juu ya swala zima la Utalii na hali halisi ya Utalii hapa Zanzibar. Kwanza atambue kuwa ni vigezo vyake alivyovitumia havina uhalisia. Kimsingi, swala la biashara nzima ya Utalii na Usafiri (Global International Travel) limepata changamoto. Kuna mambo ambayo yanatuhusu au kusababishwa na sisi wenyewe ndani (Internal factors) na kuna mengine yanasababishwa na mambo yapo nje ya uwezo wetu (external factors).”

Jibu linaendelea hadi kwenye sababu sita ambazo Simai anaamini ndizo hasa zilizoiporomoa biashara ya utalii kama hivi ifuatavyo:

  1. Matatizo ya Kigaidi yaliotokea West Gate Mall ambayo pia baadae yakasababisha kampuni nyingi za ulaya (Travel Agents and Tour Operators) kufunga kuleta wageni Mombasa na Kenya na hili likatugusa and sisi.
  2. Wasichana wawili wa Kiengereza kumwagiwa Tindi Kali.
  3. Sarafu ya Kimarekani kupata nguvu kuliko Pound na Euro na sisi wageni wetu wengi tunategemea kutoka Ulaya,
  4. Miripuko iliyotokea Arusha mjini na kusababisha vifo na watu kuumia pamoja na mali zao kuharibika,
  5. Ushindani wa kibiashara na Tanzania kushindwa kuallocate fedha za kutosha kwa ajili ya marketing na matangazo,
  6. Maandamano na zogo la ndani yaliyotokea miaka nyuma hapa Zanzibar juu ya hali ya Kisiasa yaliosababishwa na Uamsho.

Katika mjadala huu, mimi nasimama upande wa Zitto na napingana na upande wa Simai kwa sababu zifuatazo:

Kwanza, kinyume na anavyosema Simai, matukio ya kigaidi nchini Kenya hayakusababisha kuzorota kwa utalii visiwani Zanzibar ingawa yaliuzorotesha kwenye sehemu ya mwambao wa nchi hiyo. Kwa mfano, tukio la Westgate alilolitaja lilisababisha nchi nyingi zinazopeleka wageni Kenya kutoa onyo la kutosafiri kwa raia wao huko na hivyo waendeshaji makampuni ya utalii wakaamua kutafuta mbadala wa Mombasa na ndipo wakaanza kuwaleta wageni wao Zanzibar. Inaitwa “Kufa Kufaana”. Ndio maana katika mwaka 2014, wageni waliongezeka kwa 41% Zanzibar ambapo ilipokea wageni 311,891, ikilinganishwa na wageni 181,301 wa mwaka 2013. Hii ni dhahiri kuwa matukio ya kigaidi nchini Kenya yalitupa ongezeko la watalii na sio upungufu kama anavyodai Simai.

Pili, ni kweli kuwa tarehe 07 Agosti 2013, wasichana wawili wa Kiingereza waliokuwa wakijitolea visiwani Zanzibar, Katie Gee na Kirstie Trup, walimwagiwa tindikali eneo la Mji Mkongwe na watu wasiojulikana na ni kweli kuwa uingiaji watalii ulitikisika kidogo kipindi hicho, lakini kuanzia mwaka huo huo ndipo pia tunaona ongezeko la watalii kuingia Zanzibar, ikilinganishwa na mwaka 2012, ambao waliingia watalii 169,223. Hata idadi ya watalii kutoka Uingereza, ambayo ndiyo nchi waliyotokea wasichana hao, ilipanda mwaka 2013 kwa kuingia watalii 10,056 wakati mwaka uliotangulia waliingia 8,887.

Hivyo, haitokuwa sahihi kuuungunisha tukio hili na upunguaji wa watalii hivi sasa miaka mitatu baadaye, maana hata kwenye mwaka wenyewe idadi ilianza kupanda tena baada ya mtikisiko mdogo uliotokea.

Jengine ni kwenye suala la sarafu inayotumika kuuzia utalii na watalii. Hapa Ulaya, makampuni ya watalii yanauza “holiday packages“ kwa kutumia sarafu zao na kamwe hawatumii dola ya Kimarekani. Hivyo kupanda kwa thamani ya dola kunaweza kwa kiasi fulani kuongeza bei ya “holidays“ kwa wasafirishaji watalii ambao hawafungi mikataba yao kwa kutumia sarafu ya Euro tu na ambao si wengi barani Ulaya. Ukiachia Uingereza, wasafirishaji watalii wengi huingia mikataba na makampuni ya Zanzibar kwa kutumia Euro. Kwa hivyo, si sahihi kabisa kuunganisha kupanda thamani ya dola au kushuka thamani ya Euro kwa upungufu wa wageni katika kipindi cha uchaguzi na baada ya kufutwa kwa uchaguzi.

Simai ametaja pia suala la mashambulizi ya Arusha ya Julai 2014 kama sababu, ambayo nayo kama ilivyokuwa kwa wasichana waliomwagiwa tindikali Zanzibar, haikuathiri ongezeko la watalii kama ilivyooneshwa hapo juu na, hivyo, hatuwezi kuiingiza hivi sasa kuwa ni sababu ya kupungua watalii. Katika kusaka kwangu takwimu, nimekosa data zinazoonesha kushuka kwa utalii kwa sababu hii. Labda kama anazo atuoneshe.

Hata hivyo, nakubaliana na Simai kuwa ushindani wa kibiashara unachangia sana kushuka kwa idadi ya uingiaji wa watalii, lakini napenda kutanabahisha pia ushindani sio kile tunachokiita kwenye sekta hii “marketing“ pekee, yaani utangazaji wa biashara kwa wateja, bali pia (na zaidi hasa) utulivu wa kisiasa na kiusalama katika nchi husika. Utulivu wa kisiasa una mchango mkubwa mno katika biashara hii kuliko hata “marketing“. Kama nchi ina utata wa kisiasa na kiusalama, hata utumie mabilioni ya dola kuitangaza, hayawezi kuleta faida yoyote.

Kama Simai ataangalia rikodi zake vizuri, ataona kuwa maandamano na zogo la kisiasa la Januari 2001 ndiyo yaliyosabisha kushuka kwa watalii hadi kufikia zero. Mwaka 2000, waliingia watalii 97,165 lakini mwaka 2001 wakaingia 76,329.

Huenda Uamsho walisababisha wasiwasi mkubwa miongoni mwa wanaoleta watalii, lakini ni baada tu ya serikali kutumia vyombo vyake vya dola dhidi yao na sio kabla ya hapo, kwani hawakuwa na athari yoyote kwa utalii. Ukiangalia data utaona kuwa mwaka ambao Uamsho walipamba moto kwa mihadhara na maandamano yao, yaani mwaka 2011, idadi ya watalii ilikuwa 175,067 lakini baada ya serikali kuanza kuwaandama mwaka 2012 idadi ikashuka hadi 169,223. Zogo la vyombo vya dola lilipokwisha, utalii ukashamiri tena mwaka 2013 na 2014 kwa kupata watalii 181,301 na 311,891.

Mwenye akili angelijiulita kulikoni hivi sasa? Katika utafiti wangu mdogo, nilishindwa kupata data za uingiaji watalii baina ya Oktoba na Novemba 2013 na 2014, lakini
kutokana na ujumla ni wazi kuwa waliongezeka.

Unaweza ukakaa kimya hivi sasa pasi na kusema sababu hasa ya ushukaji watalii ni nini, lakini pia huwezi kukubaliana na Simai anayepuuzia kabisa suala la mzozo wa makusudi iliyoingizwa Zanzibar.

Kwa hivyo, kimantiki, ni rahisi zaidi kuzingatia matukio na matokeo ya matukio kama haya ya wasiwasi wa kisiasa huko nyuma na kuhitimisha kuwa kuwa mgogoro uliopo sasa unachangia kuwatia hofu wasafirishaji wageni na hata wageni wanaokuja kwa njia zao binafsi bila kupitia makampuni ya kitalii nchini mwao.

Na hapo ndipo changamoto ya Zitto inaposimama na hoja ya Simai inapoporomoka.

1 thought on “Inapopwerewa hoja ya Simai ikainuka ya Zitto”

  1. Mohamed khelf kwanza nishukuru kwa maelezo yako na namna safari ya maisha ilivyoanza mpaka ukafika dw na kunifanya nijifunze mengi kupitia kwako kwa maelezo yako nanamna ulivyoelezea ufahamu wako Juu ya utalii wa Zanzibar nimejifunza mengi kwa hoja ya zitto na simai nidhahiri mkwamo uliopo Zanzibar ndio utakaochochea watalii kupungua, na sababu anazoamini yeye ni chache zinaweza zikawa na mashiko na zingine zisiwe moja tu Juu ya kumwagiwa tindikali na mauaji ya Padri yule yanaweza yakawa na ukweli, lakini watalii hawakupungua kiasi kikubwa kama mkwamo wa kisiasa. Unavyoweza kuleta athari. Asante Mohammed khelf wasalim Bonn Germany ni mie mdau wenu wa dw na mwono wangu Juu ya Zanzibar.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.