KISWAHILI KINA WENYEWE

Ushairi: Hisabati zinazotumia maneno badala ya nambari

Ushairi ni sanaa kongwe na pevu. Ni kongwe kwa kuwa ndiyo njia ya kwanza aliyoitumia mwanaadamu kuelezea hisia zake kupitia lugha na sauti hata kabla hajaanza kutumia njia nyengine za kujieleza. Ni pevu kwa kuwa ni bahari iliyobeba kiwango cha juu cha maarifa.

Lakini humu kwenye sifa zake ndimo pia mwenye ila zake. Uzoefu wangu wa  miaka 25 unaniambia kwamba kile ambacho mwengine angelikichukulia ni sifa za ushairi, ndicho hicho hicho kilicho ila yake.

Moja ya sifa za ushairi ni uwezo wake wa kuyasema mengi kwa maneno machache. Kile ambacho mwandishi wa riwaya angelihitajia kurasa 100 kukielezea, mshairi huhitaji mistari minne tu.

Kwa mfano, mtazamo wa wale wasioyaamini matokeo ya wanaokisia au kuagua mambo yajayo niliueleza hivi majuzi kwa ubeti huu mmoja tu:

Kukusanya makuhani, na wapigaji ramli
Wasomao kiganjani, wakakupa taawili
Hakulishindi tufani, mja linokukabili
Analotaka Jalali, huwa kun-fayakuni

Mara baada ya kuuweka ubeti huo kwenye ukurasa wa Facebook, maoni mbalimbali yakamiminika kufafanua, kukosoa, kutilia mkazo na hata kuongezea kilichomo kwenye ubeti huo. Kwangu, ubeti huu ulishatosha kulitoa joto lote nililokuwanalo na, baada ya kuuandika na kuubwaga, sikuwa tena na haja ya kusema zaidi kuhusiana na mada hiyo.

Lakini kwa kuwa sifa hii pia ndiyo ila ya ushairi, ubeti huu ukachochea pia wengine kuyatafsiri mawazo yangu kwa muktadha wa wanayoyadhani wao, na mengine hata hayakuwamo kabisa kwenye mtima wangu wakati nilipouandika.

Nilipoweka ubeti huu mwengine ufuatao kwenye huo huo ukurasa wangu wa Facebook, maoni mengi nilopokea yalikwenda mbali sana na pale mimi nilipokusudia:

Ninataka unitoke, unyonge nilionao
Ufukara ukopoke, nyumbani nisiwe nao
Bali nisidhalilike, heshima nibaki nayo

Mmojawapo, simba mwenzangu, Ahmad Omar, aliniandikia:

Ufukara ni silaha, subira ukiwa nayo
Hata mbele ya Wadudi, hisaba huwa hunayo
Kwa uwezo wa Rabbana, pepo ndio mafikio

Hapana shaka, yeye alidhani kuwa nazungumzia ufukara wa mali na hali kwenye nyumba yangu binafsi, jambo ambalo silo nililokusudia.

Mwengine, Mamlaka Tupumue, akaenda mbali zaidi ya alipofika Ahmad Omar, akinihoji kuwa nimefilisika vibaya vibaya:

Yaonyesha umechoka, dhoflhali haliyo
Hadi unalalamika, mazito uliyonayo
Hadi unalalamik, wakosa hata chajio?

Sifa yake nyengine ni kuwa ushairi ni kulisema neno zaidi ya neno na katika kulisema huko likazua maneno mengine mengi mno hata yakakuzidi kimo wewe msemaji, na huko njiani ukajikuta kama tiara inayoelea kwenye anga la maneno ukiuwacha upepo ukupeleke utakako. Hebu angalia hapa majadiliano ya beti baada ya mimi kuandika:

Iki Kinana kinani, kunena maneno yano?
Yasonenwa na waneni, wenye ya ndani maono
Kicho chayanena kwani, kwa inda na matukano –
Ama chazibeba kuni, za moto wa farakano?

Medis Khalfan akaja:

Kinana ‘tanena sana, ela siye tuwa pano
Kwa KAFU tun’shonana, twataka maridhiano
Na kwao siye hapana, tun‘choka majivuno
Kama kunena, nena tena, Kinana domo unalo!

Mussa Hamad akaingia na:

Kinana chajichanganya, kwa kisemayo mchana
Wala busara hakina, ingawa kizee sana
Nakionea huruma, kisije kufa chaona
Vijana wamekichoka, wasije kukitafuna!

Ismaili Islam akajikuta anaelea kwenye anga la maneno kama tiara:

Kinana kinene nini, zaidi ya ufitini?
Ndio mana hakineni, wayanenayo waneni
Kingewa kweli kineni, kingelinena zamani
Waloyanena waneni, walotupwa gerezani

Hakina kinokinena, mbele ya walionena
Kama Kinana chanena, uneniwe ni fitina
Wakweli walionena, wamekinena Kinana
Ati nacho kingenena, uneni uso maana

Bora n‘sinene sana, nami hajawa mneni
Yalowapata wanena, haishia gerezani
Nisijekuwa Kinana, kwa kwa uneni wa fitini
Sheria zao zabana, za humu mtandaoni

Abdallah Al-Alawy Baafarajiy  akaamua kuchapuka zaidi:

Kinana kwani ni nani, kututia ufutini?
Hiki kina nini kwani, kigeni pa duniani?
Mambo haya si mageni, yalidumu tu zamani
Kinana nae ni jini, swahibawe Firauni

Alimradi kila mmoja akalikuza neno la ‘kinana’ hadi kinana kikawa neno zaidi ya neno. Kwa hivyo, licha ya uwezo wake wa kuligeuza neno kuwa zaidi ya neno, ila yake ni kuwa wakati mwengine ni rahisi sana kujiona unachukuliwa na ukubwa wa maneno yako mwenyewe na kuanza kuwa mtumwa wake. Yakakupeperusha angani kisha yakakuangusha mahala tafauti au hata kukupoteza kabisa.

Sifa yake ya tatu ni kutumia kwake falsafa kubwa ya maana, mantiki, na viasi. Angalia ubeti huu ambao pia niliuweka kwenye ukurasa wa Facebook na ukavutia michango mingi kutoka kwa washairi wengine:

Nilipokufungulia, mlango wa nyumba yangu
Kumbuka uliridhia, kutii shuruti zangu
Yamini ukanilia, kumshuhudisha Mungu
Mbona leo wanambia, sina haki ndani mwangu?

Ismaili Islam alikuwa na haya ya kuniambia:

Lau hukumridhia, nyumbaniko ‘singengia
Yeye aliweka nia, nyumbanimo kukuotoa
Lengo lake ‘metimia, baada ya ndani kungia
Lau ‘singemridhia, kamwe hangefanikiwa

Zaid Taufik akaja na wimbo wa zamani wa Taarab usemao:

Ulisema uwe wangu, hadi mwisho wa dunia
Ukaapa jina la Mungu, hutoibadili nia
Sasa kama si mwenzangu, mbona unanikimbia

Mamlaka Tupumue akanielemea kwa lawama mfano wa zile za Zaid Taufik:

Kaka nawe ni mwepesi, kosa lako kuridhia
Usingetoa nafasi, mlango kuufungua
Ona sasa akughasi, vituko akuletea!

Wengetafuta shauri; kabla ya kufungua
Sasa waona hatari, ishayo kuelekea
Sasa ni yako hiari, mlango kumfungia!

Shara Khamis akanijia na wazo lililochanganyika na suto kwamba yote ni kusudi yangu mwenyewe:

Fikira nimzunguko, zikija zinatembea
Kubatilisha tamko, mimi najiamulia
Ni huo wepesi wako, leo unakuchongea
Utapata muamko, siku ya pili ‘tajua

Ahmad Omar kwa mara nyengine tena akanivamia kama kwa ile ya kwanza:

Uliwakusanya watu, na masheikh wamtaa
Ili kukusindiza, na ushahidi kukaa
Leo wamtelekeza, sababu zisizofaa

Huruma umepunguza, kama kwamba ‘mepumbaa
Hata nikikuweleza, wanena yasiofaa
Leo waomowa lio, wasema unaonewa?

Lakini Abdallah Al-Alawy Baafarajiy akaja kunifariji kama jina lake lilivyo:

Kosa ni la seramala, fundi mchonga mlango
Hakufanya muamala, wapitao kwa malengo
Ikawa na mabalaala, nyumba wakafanya pango
Ipo haja ya kulala, yakamtoka maringo

Naye Saeed Mohammed akamalizia kwa nasaha hii ya kunitaka nikipigwa kibao shavu moja, nigeuze na la pili nimaliziwe:

Cha muhimu cha muhimu, kaka ninakushauri
Salimu amri salimu, ili uepuke shari
Kama ‘taweza jikimu, basi muage kwaheri

Namna mjadala wa kishairi ulivyokuwa unakwenda, ukamfanya mmoja wa wachangiaji, Rabiya Aqsa aulize ikiwa: “Imetokea tu au mlijipanga!?” na jibu akapewa na Mamlaka Tupumue akiambiwa:

Rabiya ninakujibu, suala ulouliza
Sisi haitupi tabu, kusema tunayoweza
Wala hatuna sababu, muda mwingi kupoteza
Malenga tunajuwana, ukianza twamaliza!

Na malenga wanajuwana na upevu wa sanaa hii ni mkubwa sana kiasi cha kwamba wasiokuwa wamalenga mara kadhaa huwachwa kando. Ni hisabati inayotumia maneno badala ya nambari. Ndiyo sifa na aibu yake.

 

1 thought on “Ushairi: Hisabati zinazotumia maneno badala ya nambari”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.