KISWAHILI KINA WENYEWE

Athari ya lugha za asili katika Kiswahili

Niliwahi kueleza katika makala zangu za hapo awali na kusisitiza kuwa bado wako waandishi wengi wanaoendelea kufanya makosa ya hapa na pale bila kuzingatia ufasaha na usanifu wa lugha ya Kiswahili. Nilitilia mkazo katika uandishi hasa kwa upande wa sintaksia, mofolojia na semantiki katika Kiswahili. Niliwasihi waandishi wawe makini wanapoandika makala na taarifa za matukio mbalimbali. Watumie lugha sanifu na iliyo fasaha ili wasomaji wapate habari zilizo sahihi na za ukweli. Waandishi wasio makini wanaporuhusu neno ajari (malipo ya muda wa ziada-ovataimu) na ajali (tukio lenye kuleta madhara ambalo linatokea ghafla) kutumika bila uangalifu hupotosha maana iliyokusudiwa.

Katika makala ya leo nitajikita zaidi katika matumizi ya Kiswahili kwa watangazaji redioni na pia kwenye runinga.

Redio na runinga zimeanzishwa kwa lengo la kuelimisha, kuburudisha na kutoa taarifa kwa wananchi wa ngazi zote kuanzia watoto hadi watu wazima. Katika vyombo hasa vile vinavyoanzishwa na watu binafsi wako baadhi ya wafanyakazi ni vijana ambao baadhi yao hawakupatiwa mafunzo ya kutosha katika suala zima la utangazaji na hasa katika matamshi ya maneno, lafudhi sahihi ya Kiswahili, usomaji habari kwa kituo na kutilia mkazo maneno kulingana na misingi ya Kiswahili.

Watangazaji wengi vijana wameathirika kutokana na lugha za asili na hivyo hutamka maneno kama vile wanazungumza lugha zao kikabila. Wako baadhi wanatamka maneno ya Kiswahili kwa kutumia lafudhi ya lugha za kigeni kama Kiingereza au Kiarabu. Hawatambui kuwa Kiswahili kina mpangilio wake wa matamshi ya maneno ambao ni fauti na lugha nyingine. Baadhi yao hawatambui ni wapi wanapotakiwa kuweka mkazo katika neno.

Kwa mfano tukitamka neno ‘barabara ni tofauti na bara’bara. ‘Barabara (ni nomino), ni njia pana ya magari. Mkazo unakuwa katika silabi ya pili wa neno hilo. Hata hivyo, neno bara’bara (ni kielezi) na mkazo unakuwa katika silabi ya tatu ya neno hilo. Ni neno hili linaeleza jambo kuwa ni sawasawa kabisa au bila kasoro. Tunapokubali jambo tunasema barabara, naam, hasa, sawa. Maana ya tatu ya barabara ni aina ya ndege kama hondohondo. Kama mtangazaji hataweza kutambua tofauti za matumizi ya neno barabara atawababaisha na kuwakanganya wasikilizaji wake.

Ili kuwaweka watangazaji wa habari wawe katika hali ya kuridhisha, hasa katika matumizi fasaha na sanifu ya Kiswahili, wanatakiwa waanze kupata mafunzo ya lugha tangu waiwa katika madarasa ya awali, shule za msingi na sekondari kwa kuanzia na walimu. Walimu wanatakiwa kupatiwe mafunzo katika stadi zote za lugha kama kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika. Stadi hizi zinasomeshwa katika vyuo vya ualimu katika somo la lugha kwenye darasa na pia katika maabara.

Matamshi sahihi ya Kiswahili yanatakiwa kufundishwa. Wanafunzi wengi kutoka vijijini wanatoka nyumbani kwao na hawajui Kiswahili cha kuridhisha. Wako wengine hata Kiswahili cha kuzungunza hawajui kabisa. Walimu wanatakiwa kuanza kuwafundisha kwa kutumia mbinu za ufundishaji hatua kwa hatua. Wanaanza na stadi za kusikiliza, kuzungumza, baadaye kusoma na kuandika. Stadi hizi hujengeka kwa walimu ili kuwa mfano bora wa kuigwa.

Ni kawaida kwa walimu kufanya uchunguzi wa matatizo yanayowakabili watoto wanapoanza kujifunza Kiswahili. Watambue herufi zinazowatatiza wenyeji wa eneo la shule wanakotoka wanafunzi kwa maana lugha zao za asili ili zifahamike. Kwa mfano, wako wazungumzaji wanaochanganya herufi kama /l/ na /r/, /b/ na /p/, /z/ na /s/, /z/na /dh/, n.k. Mwalimu akifahamu tatizo hili itakuwa ni rahisi kuwasaidia wanafunzi wake tangu mwanzo. Wakufunzi vyuoni wanapaswa kuwaandaa wanachuo wao katika taaluma ya fonolojia kwa kutumia maabara za lugha (Language Laboratories). Ni bahati mbaya kuwa baadhi ya wakufunzi wa vyuo vya ualimu hawana ujuzi wa kutosha katika suala la fonolojia na mofolojia na sarufi kwa jumla.

Vilevile baadhi ya vyuo hivi havina maabara kabisa. Mpaka sasa haijulikani ni hatua zipi zitachukuliwa ili kila chuo cha ualimu kiwe na maabara yake ya lugha. Hili ni tatizo kubwa ambalo linawathiri walimu wengi wa Daraja la A wanaoandaliwa kwenda kufundisha katika shule za msingi baada ya kumaliza mafunzo yao.

Katika vyuo vya uandishi wa habari suala la lugha halitiliwi mkazo kwa kiwango kinachotakiwa. Upo ushahidi tosha kuwa katika redio na kwenye runinga watangazaji wana udhaifu mkubwa wa lugha. Inasikitisha kuwasikia watangazaji wakikiboronga Kiswahili bila woga. Hawatambui kuwa taifa zima la Tanzania na hata nchi za jirani zinasikiliza redio zetu kama mfano wa kuigwa. Pamoja na matamshi na lafudhi isiyoridhisha, watangazaji wengi siyo makini. Nina maana kuwa wanazungumnza kama wako mtaani au kijiweni wakati sivyo.

Wako watangazaji wanaojitetea wakisema kuwa wanatangaza katika redio inayohudumia nchi za Afrika Mashariki kwa maana ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Kwa hiyo wanatumia lugha inayoeleweka katika nchi hizo ambayo ni Kiingereza. Wanachofanya ni kuwa wanachanganya Kiswahili na Kiingereza wakisema eti wakitumia Kiswahili baadhi ya wasikilizaji hawaelewi vizuri basi iwe ni Kiswahili na siyo vinginevyo.

Pamoja na udhaifu uliopo, yafaa vyombo vya habari viimarishwe katika kutoa mafunzo ya lugha. Vianze kwa kutoa mafunzo ya kujinoa katika utangazaji. Hii ina maana kuwa mafunzo yatolewe kwa walio kazini (in service trainng) kwa kipindi kifupi. Kozi hii inaweza kuandaliwa katika chuo kimojawapo cha uandishi wa habari kama ‘Tanzania School of Journalism (TSJ)’. Chuo hiki kina walimu waliobobea katika taaluma ya uandishi wa habari na pia kina vifaa vya kutosha vya kushughulikia taaluma hii. Wataalamu wa lugha wataweza kualikwa kutoa mihadhara ili kuinua kiwango cha watangazaji hawa.

Eneo la pili la kushughulikia ni kuhuisha mitalaa wa kufundisha waandishi wa habari kwa kuongezea vipengele vya sarufi ambavyo ni muhimu katika utangazaji. Mtalaa huu uwashirikishe wawakilishi wa wakufunzi kutoka katika vyuo mbalimbali vya uandishi wa habari pamoja na mabingwa wa sarufi kutoka katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hapa wako mabingwa ambao wanaweza kutumika kwa upande wa kuhuisha mtalaa wa uandishi wa habari uwe wa aina moja kwa vyuo vyote vya uandishi wa habari. Inashangaza kuona kuwa vyuo binafsi vinavyoanzishwa havina maandalizi ya kutosha kwa maana ya kuwa na walimu waliobobea katika uandishi wa habari, somo la Kiswahili na pia na vifaa vya kufundisha lugha. Matokeo yake ni kujidhalilisha wenyewe na pia nchi yao.

Jambo la msingi ni kuwatahadharisha watangazaji hasa katika runinga mpya zinazoanzishwa kuacha kuchanganya lugha ya Kiingereza wanapotangaza. Baadhi yao wanadhani kuwa kuweka maneno ya Kiingereza ni ufahari wakati sivyo. Yako maneno mengi ya Kiswahili yanayoweza kutumiwa na watangazaji wa aina hii. Hawa nawaita ni limbukeni.

Nikirejea katika suala la taaluma ya uandishi na utangazaji wa habari, napenda kushauri wahusika kuwa habari ni silaha muhimu sana katika maendeleo ya nchi. Ndiyo maana inasemekana kuwa ni muhimili wa nne katika nchi baada ya mihimili mingine kama Serikali, Bunge na Mahakama.

TANBIHI: Makala ya Stephen Maina kama ilivyonukuliwa kutoka mtandao wa ZIRPP Stephenjmaina1965@yahoo.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.