Ni muhimu, ya moyoni kuyanena
Ni jukumu, mayowe kupiga sana
Nekhitimu, ndio leo nikanena
Nalitote, sote tupate kuzama
Nalitote, mbao nazo tugawane
Sisi sote, kwa mapande tupeane
Pata wote, akosae tumuone
Nalitote, sote tupate kuzama
Bora hayo, kuliko wanoyafanya
Watendayo, dhahiri tunayaona
Na ambayo, yaliyofichikana
Nalitote, sote tupate kuzama
Litotapo, moja litajulikana
Kufa hapo, kwa chombo kwisha kuzama
Nami nipo, tazama nikijiona
Nalitote, sote tupate kuzama
Lizamuke, heshima kuekeana
Mume mke, haki wote kupeana
Changu chake, chake si pekeye tena
Nalitote, sote tupate kuzama
Ni mseto, us’o na ladha kinywani
Ni mmoto, si baridi ulimini
Kwangu joto, kwake baridi la shani
Nalitote, sote tupate kuzama
Ammar Ruwei Nassor
instagram:@ammarruweih
Facebook: Ammar Ruweih
Dar Es Salaam – Tanzania
24 Juni 2015