KISWAHILI KINA WENYEWE

Kiswahili kinatushinda, tujivunie nini Watanzania?

Natazama marudio ya taarifa ya habari ya kituo kimoja cha televisheni nchini. Usiku wangu siku hiyo unaingia ‘nuksi’ ninapofuatilia habari ya Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi aliyekuwa katika ziara katika Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Si nuksi tu bali pia napatwa na masikitiko pale nilipomtazama rais huyo akitumia lugha ya taifa ya nchi yake, yaani Kireno huku mkalimani akitafsiri kwa Kiingereza.

Ungeweza kufikiri hadhira ile ni ya wazungumzaji wa Kiingereza katika nchi fulani inayotumia Kiingereza.

Haikuwa hivyo, ilikuwa ni katika ardhi ya Tanzania, nchi yenye lugha yake ya Taifa. Mgeni anayejua thamani ya lugha yake hata kama nayo bado ni ya kikoloni alikuwa ‘akitiririka’ kwa lugha yake, huku Watanzania kama kawaida yetu tukiendelea kukipa Kiingereza nafasi.

Si bure Watanzania tumerogwa! Najua nitawaudhi mawakala wa Kiingereza lakini sitaki kuuma maneno. Nasema tena kwa kupaza sauti kuwa huu ni ulimbukeni na utumwa. Ni aibu iliyoje kutothamini chetu na kukimbilia cha mwingine.

Katika hadhira ile hata kama walikuwapo wasiojua Kiswahili, hakukuwa na sababu ya kutafsiri kwa Kiingereza. Kwanza maudhui ya mazungumzo rais Nyusi siku ile wala hayakulenga kwa kiasi kikubwa jumuiya ya kimataifa ambapo pengine tungeweza kutoa hoja kuwa lugha ya Kiingereza ilikuwa mwafaka kutumika kutafsiri.

Kwa kiwango kikubwa, ujumbe ulilenga kudumishwa kwa ushirikiano baina ya Tanzania ma Msumbiji. Sehemu kubwa ya hadhira ilijumuisha wanafunzi, wahadhiri, viongozi wa Serikali na wananchi ambao naamini wengi wana ufahamu mzuri wa lugha ya Kiswahili.

Lakini kwa kasumba ileile ya kuridhisha wageni wachache, Watanzania hasa walomtazama kupitia matangazo ya runinga hawakupata ujumbe zaidi ya maelezo mafupi ya watangazaji.

Niliwahi kusema Watanzania tuna vioja; si ajabu kuona katika mkutano wa waswahili 200 na mzungu mmoja, washiriki watajikomba kumridhisha mgeni huyo hata kama mijadala ya mkutano inahusu maendeleo ya Waswahili. Huu ni utumwa wa fikra uliofurutu ada.

Tunaposhindwa kukithamini Kiswahili ndani ya ardhi yetu, Watanzania turingie jambo gani? Kwenye michezo tupo hoi, uchumi hata kodi tunashindwa kukusanya tunabai kuwakamua wafanyakazi na wanywaji wa vileo.

Wapi tunapofanya vizuri? Kwenye siasa, mtindo ndiyo huu wa siasa za majitaka, elimu yetu nayo tia maji tia maji, rasilimali tunawapa wageni; basi hata Kiswahili nacho kinatushinda?

Kuna wakati Kiswahili kilipanda chati Afrika baada ya rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano kukitumia katika moja ya vikao vya Umoja wa Afrika.

Mgeni ambaye Kiswahili huenda ni lugha yake ya pili au ya tatu, anakithamini kuliko wazungumzaji wazawa. Huzuni ilioje!

Hivi sasa Wakenya pamoja na Kiswahili chao kibovu wanatamba katika soko la ajira la kufundisha Kiswahili duniani, sisi tunaishia porojo za kutangaza fursa za Kiswahili badala ya kuweka mifumo ya kuwawezesha wataalamu wetu kunufaika na fursa hizo?

Hata hivyo, tutawezaje kuwa na mifumo, ilhali waandaaji wake ndiyo watu walio mstari wa mbele kukipiga Kiswahili?

Uko udhaifu kuanzia kwa viongozi na nimewahi kusema siku viongozi wetu watakapoamua kuwa na utashi wa kukithamini Kiswahili, lugha hii itatamba ndani na nje ya nchi.

Kama Kiingereza kinachotetemekewa leo kilipanda chati kwa juhudi za mfalme wa Uingereza, viongozi wetu wanashindwaje?

Chanzo: Gazeti la Mwananchi la tarehe 18 Juni 2015.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.