KISWAHILI KINA WENYEWE

Msikia neno asinene neno, hapatwi ni neno

Umbeya, kwa maana ya tabia ya kuwasema watu wenyewe wasipokuwapo, ni sehemu mojawapo ya khulka za kibinaadamu. Si tabia nzuri, lakini ule ukweli kwamba imekuwa sehemu yetu isiyotenganishika nasi, umeifanya ijengewe vina na viasi.

Nakusudia kusema kuwa ingawa kwa ujumla wake umbeya ni jambo baya, ubaya wake huhisabika kwa viwango kutoka cha chini kabisa hadi cha juu kabisa na humo ndani yake munakuwa na aina fulani ya ukubalifu au angalau uvumilivu. Kwa mfano, tunamvumilia anayetusema kidogo au kwa jambo dogo kwa watu hata tunapojuwa kuwa ametusema, lakini hali inakuwa tafauti ikiwa umbeya ni mwingi na jambo linalohusika ni kubwa.

Tuje kwenye msemo wetu wa leo ambao nao una uhusiano wa moja kwa moja na dibaji hiyo hapo juu. Nao pia niliambiwa na swahibu na mwandani wangu katika mazungumzo yetu kwenye chakula cha mchana. Hapana shaka, palikuwa na jambo lililotangulia na akalihusisha na msemo wenyewe. Hapa si pahala pake kulielezea lakini itoshe kwetu kuzama kwenye hekima iliyomo kwenye msemo “Msikia neno asinene neno, hapatwi ni neno” ambao onyo lake limo kwenye kinyume chake. Nalo ni kuwa “Msikia neno akanena neno, hupatwa ni neno.” Kumbuka kuwa neno “neno” kwenye Kiswahili lina maana zaidi ya neno. Tazama sentensi hizi kujuwa baadhi ya maana za neno “neno”:

  1. Sijakuona siku nyingi. Lete maneno (habari mpya)
  2. Muambie mama yako kwangu yamekwisha. Miye sina neno (sina tatizo)
  3. Ruzuna muogope. Ni mtu wa vinenoneno (mtu asiyeweza mdomo wake)
  4. Hujambo? Miye mzima, sina neno (sina ugonjwa)
  5. Kama una maneno kweli, njoo hapa nikuone (kama unataka ugomvi)
  6. Je, kuna chochote? Hapana, hakuna neno (jambo)

Hizo ni baadhi ya maana za neno “neno” kama linavyotumiwa na Waswahili. Hapana shaka, ziko nyengine nyingi, ukiwacha hiyo ya neno kuwa ni neno tu kama neno lilivyo. Swahibu wangu aliponikumbushia kauli hii ya wahenga, alikuwa anakokozoa maana kadhaa za neno “neno” na kuniwekea kwenye kapu moja la hekima za Kiswahili.

Upande mmoja alikuwa ananifahamisha kuwa kuko kusikia maneno miongoni mwetu waja, kwa sababu kama dibaji ilivyojieleza jambo la umbeya ni sehemu mbaya ya khulka zetu ambayo haitaki kutengana nasi. Lakini la kusikia neno ni jambo moja, la kunena wakati wa kulisikia na baada ya kulisikia neno hilo nalo ni jambo jengine. Kwa nini?

Kwa kuwa maneno yana tabia ya kusafiri na upepo, wasemavyo Waswahili. Wanaamini kuwa upepo unaoyasafirisha maneno mabaya yanenwayo hupeperushwa na shetani, ambaye lengo lake ni kushuhudia machafuko miongoni mwa wanaadamu. Na kisha ukayafikisha kusikopaswa kufika, yakazuka ya kuzuka.

Katika uhalisia, hapana upepo wala hapana shetani anayeyasafirisha maneno yanayonenwa dhidi ya mmoja wetu, bali sanaa yenyewe ya mazungumzo ya mdomo ni sanaa ya usimulizi. Kwenye fasihi simulizi, huwa tunasema kuwa hadithi ina ncha saba kwa kuwa ilisafirishwa kutoka kizazi hadi kizazi, eneo hadi eneo, matokeo yake ni kuwa kila inapotua hutua na yaliyoongezwa na yaliyopunguzwa kuakisi mazingira, hadhira na dhamira husika. Hapo ndipo mnena neno anapojikuta neno lake limegeuka neno naye akakumbwa ni neno.

Ikiwa unaweza kujiepusha usisikie neno ni vyema zaidi ingawa udadisi wa kibinaadamu unaweza kukutia majaribuni. Lakini, majaribu zaidi ni kunena neno baada ya huko kusikia neno. Unaweza ukawa wewe ndiye mwenye ncha ya saba ya neno unalolisimulia, na likakugeuka mwenyewe.

Ulimi ‘kizidi meno, mdomo ukavuuka
Ukayanena maneno, na maneno ‘kaneneka
Huwa si tena nong’ono, huwa kwenzi na kufoka
Na punde ukaumbuka, na muumbuziwo neno.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.