KISWAHILI KINA WENYEWE

Dhana ya ‘Ukanushi’ kwenye Kiswahili

Katika maana ya kawaida, kukanusha ni kukataa lakini katika kiwango cha uchambuzi wa lugha, kunanusha ni zaidi ya kukataa. Kama kitenzi, kuna vitenzi vyengine ambavyo vinahusishwa na kitenzi ‘kanusha’ kama vile vitenzi ‘pinga’, ‘kaidi’, ‘bishia’ na ‘kadhibisha’.

Hata hivyo, pamoja na kuhusiana kwao, vitenzi hivi vinaelezea viwango tafauti vya ukanushaji kwa mujibu wa muktadha na matumizi yake. Kwa muhtasari, ukanushaji unaokusudiwa na kitenzi ‘pinga’ sio ule uliomo kwenye kitenzi ‘kadhibisha.’ Kwa mfano, tunasema “Kombo alipinga madai hayo mahakamani” lakini hatusemi “Kombo alikadhibisha madai hayo mahakamani”, kwa sababu katika kiwango hiki cha matumizi, ‘kupinga’ kunawakilisha vyema dhana ya kukanusha kuliko ‘kukadhibisha.’

Turudi kwenye kiini cha mada. Ukanushi ni hali ya kupunguza kiwango cha ukubalifu kwenye sentensi, na hapa sentensi inahesabika kama kifungu cha maneno chenye maana kamili. Kwa manufaa ya mjadala huu, nitaugawa upunguzaji huu wa kiwango cha ukubalifu katika makundi matatu ambayo nitayapa alama za A, B na C.

Ukanushi Kundi A

Huu hufanyika kwenye vitenzi moja kwa moja kwa kubadilisha vipashio vya kiwakilishi nafsi kutoka hali ya ukubalifu kuwa ukanushi. Kwa mfano:

Ukubalifu                                                                          Ukanushi

Mimi ninasomesha                                                         Mimi sisomeshi
Wewe unasomesha                                                        Wewe husomeshi
Yeye anasomesha                                                          Yeye hasomeshi
Sisi tunasomesha                                                           Sisi hatusomeshi
Nyinyi munasomesha                                                  Nyinyi hamusomeshi
Wao wanasomesha                                                      Wao hawasomeshi

Jambo la kuzingatia kwenye kundi hili la ukanushi ni kuwa vipashio vinavyotumika kukanusha hubadilika kutoka nafsi moja hadi nyengine na pia kutoka wakati mmoja hadi mwengine. Ndio maana tunasema “Mimi sisomeshi” kwa kupachika kiambishi awali si- kinachowakilisha nafsi ya kwanza umoja (mimi) na mwisho wa kitenzi tunaweka kiambishi -i cha ukanushi wa wakati uliopo. Kwenye nafsi ya tatu umoja (yeye), tunasema “Yeye hasomeshi” tukimwakilisha yeye kwa kiambishi awali ha- kinachowakilisha ukanushi, huku kile kiambishi tamati -i kikibakia kwenye nafsi zote katika wakati uliopo.

Ingelikuwa ni wakati ujao, ingelikuwa “Mimi sitasomesha” ambapo kiambishi cha wakati ujao -ta- kimewekwa baada ya kiambishi awali si- kinachowakilisha nafsi ya kwanza umoja (mimi) katika ukanushi. Hakuna mabadiliko kwenye sehemu nyengine ya kitenzi, kama ambavyo tumefanya kwenye ukanushi wa wakati uliopo, yaani hatusemi “sitasomeshi” kwa kuweka kiambishi tamati -i ila inabakia kuwa -a kama ilivyo kwenye ukubalifu.

Ingelikuwa wakati uliopita, kitenzi kizima kingelibakia kama kilivyo huku kikichota tu kiambishi awali cha nafsi. Tungelisema, kwa mfano, “Wewe hukusomesha” kwa kupachika kiambishi awali cha nafsi ya pili umoja (wewe) kinachowakilisha ukanushi, yaani hu-, kwenye kitenzi kizima kama kilivyo, yaani –kusomesha.

Tufike hapo kwa leo. Sehemu ijayo itagusia Ukanushi Kundi B.

 

6 thoughts on “Dhana ya ‘Ukanushi’ kwenye Kiswahili”

  1. Ahsante sana kwa maelezo yako mazuri. Ila sasa mbona Ukanushi katika kundi “B” na “C” hamjaweka!!??

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.