UCHAMBUZI

CCM Z’bar haina uhalali kujinasibisha na Mapinduzi

Ukizingatia hotuba za Marehemu Mzee Abeid Karume na matendo yake wakati wa uhai wake, ukazingatia marudio ya kauli za Marehemu Karume kupitia kwa mjane wake, Mama Fatma Karume, ukasikiliza hotuba moja tu ya Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha aliyoitoa katika moja ya mikutano yake na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), moja kwa moja unapata maana na malengo halisi ya Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964 na kisha unahitimisha kuwa mshirika mkuu kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, yaani CCM, yuko mbali kabisa na malengo ya Mapinduzi hayo na, hivyo, amepoteza kabisa uhalali wa kujinasibisha nayo.

Uhuru na Umoja. Bango la kampeni za uchaguzi la chama cha ASP.
Uhuru na Umoja. Bango la kampeni za uchaguzi la chama cha ASP.

Nitafafanua. Kwanza, wazee wetu waliamua kudai uhuru wa nchi yetu hii ya Zanzibar na walipoupata wakaona haujatosha wakafanya Mapinduzi kwa sababu za kimsingi ikiwemo, kwanza, kupata taifa huru pamoja na kuwafanya wananchi wake kuwa huru dhidi ya kutawaliwa na wakoloni. Pili, Mapinduzi haya yalikuwa na lengo la kuwajengea wananchi uwezo wa kumiliki mali – ikiwemo ardhi – na ndio maana baada ya Mapinduzi, Marehemu Karume aligawanya ekari tatu tatu za ardhi kwa watu waishio maeneo yaliyo na ardhi husika.

Tatu, Mapinduzi yalidhamiria kuwapatia wananchi makaazi bora, ndio maana Mzee Karume akawajengea majumba ya kisasa kwa wakati ule kama vile Michenzani, Kilimani, Mkoani, Wete na kwengineko.

Na Ali Mohamed
Na Ali Mohamed

Nne, kwa kuwa kabla ya Mapinduzi raia waliowengi wa nchi hii walikosa haki ya kupata elimu kwa sababu mbali mbali, ikiwemo kutomudu gharama za kulipia elimu hiyo, baada ya Mapinduzi kuliwekwa lengo la kumpatia kila Mzanzibari elimu na ndio maana Mzee Karume akatangaza na kuifanya elimu itolewe bure pamoja na vifaa vyake vyote kuanzia msingi, sekondari hadi Chuo Kikuu. Kwa wakati ule, Zanzibar bado hakukuwa na hata chuo kikuu kimoja, lakini iwapo raia wa nchi hii alifanikiwa na kulazimika kujipatia elimu ya chuo kikuu, basi Serikali ilikuwa ikilipia gharama katika chuo kikuu chochote kilichopo nchi yoyote.

Tano, kujenga umoja wa kitaifa, ambapo Mzee Karume alipiga marufuku chuki na ubaguzi uliojengwa na watawala wa wakati huo baina ya raia wamoja. Miongoni mwa njia alizoamini zingelisaidia kufikiwa lengo hilo ilikuwa ni kuchanganya damu kwa makabila mbalimbali yaliyopo Zanzibar, na ndio kisa cha akina Brigedia Yussuf Himid kumuona Bi Fatma Jinja, kwa mfano, kama ambavyo Marehemu Saidi Sindano alivyomuoa bibi yangu, Bi Fatma bint Juma, Mshirazi wa Kipemba.

Malengo hayo ya Mapinduzi yalikuwa ndio dira ya kuingoza nchi yetu kutoka kwa mwasisi wa Mapinduzi na Rais wa Kwanza wa Zanzibar huru na pia mmoja wa waasisi wa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, Hayati Mzee Karume. Kwa kuwa yeye alikuwa kiongozi wa chama kilichopindua, yaani Afro-Shirazi (ASP) na ambacho baada ya kifo chake kikaungana na TANU ya Tanganyika kuunda CCM, malengo yake yalikuwa ni ya ASP na malengo hayo ya ASP hayakutakiwa kupotea baada ya kuungana na TANU na kuzaliwa CCM.

Lakini kilichopo ni kinyume chake. Ingawa kila mwaka CCM hukusanyika kuadhimisha Mapinduzi hayo kwa sherehe na mapambo, kivitendo tayari dhamira na malengo ya Mapinduzi hayo hayapo tena- yameshapuuzwa na serikali za CCM. Sio tu kuwa chini ya CCM, Zanzibar haina uhuru wa kujitawala na kujiamulia mambo yake wenyewe (ambalo lilikuwa lengo nambari moja la Mapinduzi), bali sasa Zanzibar haina uwezo wa kuwatibu, kuwasomesha wala kuwalisha watu wake. CCM haina uthubutu hivi sasa wa kujinasibisha na Mapinduzi. Kwa hakika, chama hiki kinawakilisha kila kile kilicho kinyume na Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa kuyatupa au kuyaacha yale malengo mema ya Mapinduzi, ndio maana baadhi ya viongozi walipozinduka na kwao, ndio maana hata baadhi ya viongozi wa CCM wenyewe wanakiri kuwa endapo malengo hayo hayakutekelezwa, basi wananchi watakuwa na masuala ambayo yatahitaji majibu, na endapo majibu yatakosekana kiuhalisia, basi uhalali wa kuongoza nchi hii ya Zanzibar kwa CCM utakosekana pia.

Msikilize mwakilishi wa CCM jimbo la Mwanakwerekwe, Waziri Kiongozi Mstaafu wa Awamu ya Sita na pia Waziri wa Ulinzi Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano, Shamsi Vuai Nahodha, anapohoji kwenye moja ya mikutano ya hadhara ya CCM:  “Nawaomba viongozi wa CCM na wanachama na wapenda amani tujiulize masuala yafuatayo, la kwanza, Mzee karume aligawa ardhi heka tatu tatu kwa wanyonge ili wajiendeleze kwa kilimo, mimi nauliza kweupe,jee! Ardhi hizi zipo na kama hazipo zimekwenda wapi? La pili, Mzee Karume alifanya elimu bure mwaka 1972. Mimi nauliza leo elimu ni bure kama alivyoacha Marehemu Mzee Karume? Kama hapana, mimi na nyinyi tujiulizeni kwa nini imekuwa hivyo? La tatu, afya bora. Je, kwa sasa afya ni bora kama alivyoziacha Hayati Mzee Karume? Kama hapana, kwa nini? Haya ndio masuala ya watu wenye hekima na busara, wanachama na viongozi wa CCM wayapatie majibu. Tusipotoa majibu, siku moja tutapoteza uhalali wa kuongoza.”

Alichochelewa kidogo Nahodha ni kujuwa kuwa tayari Wazanzibari wameshajiuliza maswali haya kitambo na kujipatia majibu wenyewe. Yumkini hata naye Nahodha hakuyauliza kwa nia ya kusaka jawabu kwa wenzake, bali kuwaamsha kutoka usingizini na wayafanyie kazi haya, wazirejeshe zile dhana na dhamira za Mapinduzi katika utekelezaji wake. Swali ni kuwa, je CCM Zanzibar wanaweza kuamka tena na kujirudi wakayarudia malengo ambayo kitambo mno wameyapuuza na hata kuyakashifu?

Sidhani. Viongozi wa CCM wameendelea kulala licha ya kuamshwa na kelele nyingi, kwanza kutoka kwa vyama vya upinzani na baadaye kutoka kwa watu wake wenyewe, akiwemo huyu Shamsi Vuai Nahodha. Hapana shaka, usingiti wa CCM ni mzito mno kuweka kuamka na kujifuta uso. Ni usingizi huo mzito ndio unaowapa takaburi za kujiona wao ndio wamiliki pekee wa Zanzibar hata kama wataikanyagakanyaga na kuiponda misingi halisi ya Mapinduzi na kuyatupilia mbali malengo yake.

Na huko ndiko kunakoifanya CCM ikose kabisa uhalali wa kujinasibisha na Mapinduzi na, hivyo, wa kuitawala Zanzibar.

Na Wazanzibari wanalifahamu hilo.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.