UCHAMBUZI

Maafa ya Januari 2001: Busara iienzi damu ile

Kwa hakika, kuondokewa ni kugumu mno. Ugumu huu wa kuondokewa huzidi kuumiza panapoangaliwa huo muondoko wenyewe ambao waondokaji wameondoka. Ugumu huzidi kuchochota kwa kuwaangalia hao waondokewa wenyewe.

Ghassany2003

Na ugumu huzidi kupwita kwa kuzichunguza hizo sababu za kuondoka kwa hao waliondoka. Alimradi katika kila msamiati tutakaotumia hapa, tutakuta kuwa kuondokewa ni kuchungu na kunaumiza. Na ni kuondokewa huko ndiko kunakozaa makala hii ya leo, ambayo ni sehemu ya maombolezo ya maafa yaliyoikumba Zanzibar Januari, 2001.

Naandika kwa masikitiko, na kwa ombwe na kilio, lengo likiwa ni kuwaenzi wahanga wote wa maafa haya kwa stahiki na stahili yao . Kuomboleza kwangu huku, naomba kusichukulike kuwa ni zao la chuki kwa yoyote yule. Wala sitaki ichukulike kuwa naomboleza hivi ili kuwafanya watu wakumbuke na wateseke kwa mateso ya kumbukumbu hizo.

Badala yake, nataka ifahamike kuwa kuomboleza kwangu huku kunatokana na desturi ya muondokewa, maana mwenye kutenzwa hutenzeka! Kwamba naomboleza kama vile ambavyo Mzanzibari mwengine yoyote yule angelistahiki kufanya, maana kwa hakika iliyeondokewa ni Zanzibar na walioondoka ni Wazanzibari, nami ni katika hao!

Naam, Zanzibar imeondokewa! Pengine kulikuwa na watu ambao pale mwanzoni walijihisi kutokuguswa na simanzi za msiba ule, labda kutokana na mitazamo yao ya kisiasa, na hivyo wakayafurahikia maafa yale. Lakini hivi sasa, miaka miwili baadaye, nina imani kuwa wengi miongoni mwao wameshagunduwa hilo lilikuwa ni koseo na kwamba kama hawakumwaga chozi wakati ule, basi leo hii yanawatiririka michirizi michirizi!

Leo hii tunalia pamoja, maana na wao pia wameshang’amuwa kwamba yale yalikuwa ni maafa yaliyotia doa jeusi kwenye utu, heshima na utukufu wa Zanzibar , Uzanzibari na Wazanzibari wote popote pale walipo na katika imani yoyote ile waliyonayo.

Kwamba ile ilikuwa ni alama ya udhalilifu na udunifu wetu sisi Wazanzibari na viongozi wetu. Pia ilikuwa ni tusi kubwa kwa stara na staha ya mpenzi Mama yetu, Zanzibar! Basi nataka ijulikane kuwa hilo ndilo lililonisukuma kuomboleza huku na si jenginelo.

Katika wakati mgumu kama huu, tunapaswa sote kujifuta machozi ya kuondokewa na kutenzwa kwetu kwa kuyatafakari maafa haya kwa akili zetu na sio kwa hisia zetu. Kwa makusudi kabisa tunatakiwa tujiepushe na kuyakumbushia na kuyashadidia yale yaliyotokea, maana kufanya hivyo hakutasaidia jambo ila kuushindilia msumari mmoto juu ya donda bichi. Na kwa hilo hakuna mmoja miongoni mwetu ambaye atafaidika nalo.

Busara ya kiutu inatuelekeza kuwa huu si wakati wa kuulizana “Vipi maafa haya yalitokezea?”. Suali kama hili si mwafaka kwa wakati kama huu, maana jibu lake linatupelekea kusasambura nani alitufanya nini, na kwa staili gani. Jibu hili linazichokonoa hisia za kutendwa na hamu ya kulipiza.

Linaibuwa visa na mikasa vilivyofundikwa katika mivungu ya nafsi zetu na, baada ya yote, linahalalisha dhamira ya kisasi na kutendana. Utu hautuhimizi hivyo! Hakuna mnada hata mmoja utakaothubutu kuitia thamani damu ile iliyomwagwa katika maafa yale. Hakuna chochote kiwezacho kuirudisha heshima iliyovunjwa katika maafa yale. Hakuna dawa yoyote itakayoweza kulitibu jeraha lililozipata nyoyo zetu kwa pigo lile.

Hakuna chochote kiwezacho kufanya hayo, isipokuwa tafakuri ya kina na akili iliyotulia. Hakuna ila busara, kwamba ndiyo pekee itakayoweza kuienzi damu ya wahanga wetu iliyodidimizwa ardhini.

Maana ya busara ni uoni wa mbali, uwezo wa kukisia kiwezacho kuwa cha pili na cha tatu, ama kabla au hata baada ya kile cha kwanza kwisha kutokezea. Ndiyo maana ikawahi kusemwa kuwa busara ya tendo hilo haikamiliki mpaka pale mtendaji atakapofanikiwa kujiuliza na kujijibu: “Kwa Nini?”anatenda anayoyatenda.

Inawezekana kuwa busara ilikwisha kukiukwa huko mwanzo kabisa wakati wa kutendwa yaliyotendwa hata ikasababisha tupatwe na yaliyotupata na kutufanya leo hii tutote machozi kwa kuomboleza! Lakini hilo halikutia ukomo kwa Wazanzibari kutumia busara zao katika mambo yatakayofuatia baada ya yale!

Miongoni wa vitu vioneshavyo kuwa busara haikufa hata baada ya masaibu yote yale ni huku kupatikana kwa Muwafaka.

Basi wakati huu wa kuomboleza msiba ule mzito uliozisinzima nyoyo zetu, nauwe pia wakati wa kuipa busara nafasi yake kwa kujiuliza:” Hivi kwa nini wale watu wetu walikuwa wahanga wa maafa haya? Kwa nini damu ilimwagwa? Kwa nini miiko ilikiukwa na kwa nini heshima ilivunjwa? Suali hili KWA NINI? Ndilo liwe ombolezo kuu katika kuwaenzi wahanga wetu.

Tujiulizeni suali hili kusudi tupate kuupa maana msiba huu katika maisha yetu sisi tuliobakia. Tujiulize suali hili ili tupate kujuwa kuwa damu ile iliyomwagwa ilikukwa ikipigania mabadiliko katika nchi yake, maana haikuwa ikiridhika na hali ilivyo. Ilimwagika wakati ikitafauta haki zaidi, ustawi zaidi na uhuru zaidi.

Tutajuwa kuwa sababu kubwa ya udhalilifu ule wa Zanzibar na Wazanzibari ilikuwa ni katiba, zote mbili. Kwamba watu wale walikuwa wanatumia haki yao ya kikatiba katika kutowa mawazo yao, lakini wakati huo huo wakaambiwa kuwa walikuwa wanakiuka katiba. Ndiyo! Maana katiba zetu zina kigeugeu, hukupa kwa mkono huu na kwa mkono ule zikakupokonya! Kwamba katiba inayoitwa ya Muungano inaipa mamlaka makubwa Tanganyika kuyaingilia mambo ya Zanzibar na kuyaendesha mchafu koge, hata ikabidi kuzishurutisha roho zitoke!

Tutajuwa kuwa wahanga wale walikuwa ni watu waliopigania nguvu ya kura yao , maana walikuwa wakiamini kuwa kila mara kura yao haithaminiwi. Kwa ufupi jibu la suali “Kwa Nini”litatupa wasaaa wa kufungukana vichwa vyetu, na hivyo kututaka tutafute majibu mazuri kwalo. Litatupa njia nzuri zaidi ya kuienzi damu ile iliyomwagika.

Wakati huu wa kuomboleza maafa haya ni wakati unaotowa changamoto kwetu kama watendwa. Na hapa nataka nirejee tena na tena kwamba ninapozungumzia ombolezo la maafa haya sielekezi kalamu yangu kwa watu Fulani tu au chama Fulani tu, bali kwa Wazanzibari wote popote pale walipo. Hili ni letu, bila ya kujali uzawa wetu au vyama vyetu. Madhali sisi sote tu Wazanzibari, basi msiba huu ni wetu. Tumepatwa, tumeondokewa!

Basi huu ni wakati wa changamoto kwetu, ambao unatutaka tukabiliane na ukweli uliopo mbele yetu kwa tafakari kubwa na pana zaidi. Kwa raia, hili ni somo kwamba safari ya kuelekea ustawi wa kweli wa kibinaadamu na kiutu inakabiliwa na vikwazo vingi, lakini njia bora ya kupita katika kufika huko ni kushikamana pamoja kwa subira na matumaini. Mara moja, Willy Brandt, aliyewahi kuwa Kansela wa Ujerumani, alitamka: Hinter allen Ueberwindungen, es lebt sich Leben und Auschwung. Aber, der weg dorthin ist sehr schwierig, schmutzig und unentmuetig!”Kwamba “Baada ya kila mapambano kuna maisha na kujirudi (kufanikiwa). Lakini njia inayoelekea (kwenye maisha na ushindi huo) ni ngumu kupitika, chafu mno na yenye kuvunja moyo!”

Kwa hivyo, kwetu raia ni kuomboleza huku tukijuwa kuwa hao waliojitowa muhanga walifanya hivyo kwa ajili ya sisi tuliobakia hai. Ikiwa tuna mapenzi ya kweli kwao na ikiwa tunaithamini juhudi yao waliyokwisha kuipitisha, basi tuna jukumu la kuendeleza azma njema waliyoipigania.

Tunapaswa kujiuliza ikiwa hadi sasa, miaka miwili baada ya muhanga huu kutolewa, kuna maendeleo yoyote kwa lile walilolipigania watu wetu. Kama lipo, tuliendeleze lizidi kuwepo na kama halipo tulitafute lije. Huko ndiko kuwaenzi na kuwakumbuka watu wetu hawa.

Tutakuwa wachache wa ubinaadamu ikiwa tatarudi nyuma baada ya wenzetu kusonga mbele kwa ajili yetu. Tuna wajibu wa kuwaenzi wahanga hawa kwa kufanikisha malengo ya kheri waliyojitolea kwayo, ingawa nataka ifahamike kuwa kufanya hivyo kusije kukashawishi tena kuruhusu damu nyengine kumwagika.

Damu haienziwi kwa damu, na tayari Zanzibar imeshakuwa nyekundu, si fakhari tena kuiona damu nyengine ikimwagika!

Kwa serikali, hii ni changamoto kwake inayohimiza kuchunga na kuidumisha misingi ya demokrasia na haki za watu. Panaweza kutajwa sababu nyingi tu za raia wale kuamuwa kuingia barabarani, ilhali wakijuwa kuwa jambo hilo halingelipata jawabu njema kutoka kwa watawala, lakini walishafika pahala pa kusema: “Iwavyo, naiwe!”

Kwa serikali, kuwafikisha raia wake pahala pa kujiapia kiapo hicho ni kinyume na mantiki nzima ya userikali wa serikali hiyo. Hivi sasa miaka miwili baadaye, serikali zetu zinapaswa kuuhakiki uadilifu wao kwa raia. Je, inafahamu kuwa ile damu iliyomwagika pale ni ya raia wake yenyewe? Je, imejitahidi kwa kiasi gani kuhakikisha kuwa damu nyengine kama ili haitomwagika hapo baadaye?

Na hilo halifanyiki kwa kuongeza vikosi vya askari, maana kilichosababisha kutokea kwa yale yaliyotokea si upungufu wa askari, bali upungufu wa demokrasia. Na wala hilo halifanyiki kwa kuongeza vifungu vya sheria vya kupambana na ugaidi na kuvibana vikundi vya hiari kwa jina la utawala bora, maana yale hayakutokezea kwa kutokuwapo na sheria kama hizo,lakini ni kwa ajili ya kuzipinga sheria.

Mfano wa hizo ni zile ambazo zinalenga katika kujenga sheria ya kiutawala na sio utawala wa kisheria. Kwa ufupi ni kuwa katika wakati huu wa maombolezo, serikali inapaswa kupokea changamoto ya nini imekisoma kutokana na kadhia ile.

Basi sote naturudini kwenye busara, na tuitumie busara hiyo kuienzi ile damu iliyomwagika wakati wa maafa yale yaliyoanzia Januari 26, 2001 na kundelea kwa siku kadhaa baadaye.

Najuwa kuwa katika wakati kama huu wa maombolezo, wanaadamu huwa wana kawaida ya kutawaliwa na hisia zao na kuzitenga kando fikira zao. Wengine husema kuwa: “Wakati wa simanzi, ni wakati wa kuhisi si wakati wa kufikiri “. Lakini mimi nasema kuwa kila wakati ni wakati wa kufikiri. Naufahamu uzito wa kuondokewa, lakini tujaribuni kuwa na nyoyo zenye ujabari wa kupambana na gole gole hili la kuondokewa hadi tulishinde, lisitushinde. Tusiotezane vodole Sisi kwa Sisi ( kama lilivyo jina la mtaa mmoja), maana kufanya hivyo kutajenga mduara wa visa na mikasa.

Miaka 10 ijayo watakuja tena wale wale, watufanye tena yale yale, pahala pale pale na kwa sababu zile zile! Sishauri hilo kwa woga, bali nashauri hilo kwa mantiki. Kwamba twapaswa kujiuliza ikiwa tutajenga mduara kama huo wa kutendana na kulipiziana, tutautoka lini ili tupate kwenda mbele na safari hii ya kuijenga nchi yetu? Hili ni kwa watendwa.

Lakini kwa watenda, wanastahiki pia kuomboleza utendi wao. Hakuna la kujionea fahari kwa hayo waliyoyatenda, kwamba walilolifanya lilikuwa ni kosa kwa ubinaadamu wao wenyewe, ambao nina hakika unawasuta. Lakini pia, nina amini kuwa ikiwa watakusudia kikwelikweli kuyakiri makosa yao na kutubu, basi hakuna la kuwafanya wajione wakosa wasiostahili kusamehewa kwa haya.

Ni muhimu sana kwa wale wote waloshiriki kwa namna moja ama nyengine katika kuyatekeleza maafa yale, wajirudi wenyewe na wajute kwa makosa yao . Wasijikubalishe kamwe kujengwa na kiburi nafsini mwao au kuteswa na mateso ya kumbukumbu zile.

Ni kweli kuwa katika ulimwengu huu wa kistaarabu, kuimwaga damu ya mpinzani wako sio tena staili ya kujisifia wala ya kujisafishia. Ni aibu na ni fedheha. Lakini ikiwa lilitokezea ndio lishatokezea, hatuna namna ya kurejesha maisha nyuma na kufanya liwe halikutokezea. Tunaloweza kufanya, hata hivyo, ni kufunzika kwa makosa yetu na kukubali kujirekebisha.

Mimi nadhani haitakuwa vibaya hata kidogo, ikiwa kuna yoyote anayejijuwa kuwa alichangia mkono wake, mdomo wake au kalamu yake katika maafa yale, akaomba radhi kwa ukosefu wake na akakubali kuipokea jaala yake.

Pamoja na hayo, itakuwa vyema kama atadhamiria katika nafsi yake kuwa kamwe hatoshiriki tena maishani mwake kuchangia hilaki za wanaadamu wenzake. Hili litakuwa tendo la kishujaa kabisa na ambalo litamuepusha na mengi. Maana, kwa hakika ushujaa haukuwa ule kuchukuwa mtutu wa bunduki na kuwaelekezea raia wasio na silaha wala hatia akawamiminia risasi vifuani mwao.

Ule ulikuwa woga na upotofu, bali ushujaa utakuwa ni huu wa kuwaelekea mayatima aliowapokonya baba zao, wajane aliowanyang’anya waume zao, wanawake aliowachafulia staha yao au wazazi aliowatwalia watoto wao, na kuwaambia kuwa: “Mimi ndiye mbaya wenu, nakiri kwa makosa yangu, nahitaji msamaha wenu na naapa sitorejea tena!”

Jambo kama hilo likafanywa na yule aliyetumia mdomo wake kueneza fitna au yule aliyetumia kalamu yake kuyaeleza yasiyo na kuwacha yaliyo, ikiwa watu hawa watafanya hivi, naamini kuwa kutawaepusha na mengi hapa duniani kuandamwa na jinamizi la makosa yao na huko kaburini kutwekwa zigo la madhambi yao.

Chanzo: Gazeti la Dira Zanzibar la tarehe 24 – 30 Januari 2003.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.