
“Linganish! Mitazamo Linganishi Juu ya Matumizi ya Kiswahili Kiisimu, Kifasihi na Kiutamaduni” ndio maudhui kuu kwenye Kongamano la 28 la Kiswahili hapa kwenye mji wa Bayreuth, kusini mwa Ujerumani, ambalo limeanza Jumapili ya tarehe 31 Mei na litaendelea hadi Jumanne ya tarehe 2 Juni 2015 kwenye jengo la Iwalewa Haus.

Katika siku ya kwanza ya ufunguzi wa kongamano, kivutio cha awali ilikuwa ni kusomwa upya kwa kazi ya gwiji wa Kiswahili, Abdilatif Abdalla, ambayo aliichapisha takribani miaka 50 iliyopita, Kenya Twendapi. Mwasilishaji mada alikuwa Kai Kresse wa Chuo Kikuu cha Carlifornia.
Kabla ya Profesa Kresse kuwasilisha kazi yake juu ya maandishi ya Kenya Twandapi, gwiji mwengine wa lugha ya Kiswahili kutoka Kenya, Profesa Ken Walibora, alitupa swali la kitaalamu juu ya mustakabali wa Kiswahili kwenye ulimwengu wa sasa, hasa akilalamikia matumizi ya lugha hiyo kwenye vyombo vya habari. Swali lake kuu lilikuwa ni “Kiswahili chendapi?” akiakisi swali la Abdilatif Abdalla juu ya khatima ya Kenya.

Miongoni mwa mada nyengine zilizowasilishwa katika siku hii ya kwanza ya kongamano hili, ni “Changamoto za Uanishaji wa Fasihi katika Zama za TEHAMA” ya Angelus Mnenuka wa Chuo Kikuu cha Leipzig, ambaye amehoji juu ya uhalali wa kuendelea kuzigawa kazi za fasihi kwenye tanzu mbili tu za andishi na simulizi katika wakati ambapo kazi za kifasihi zinazowasilishwa kupitia mitandao ya kijamii zinatumia au zinapuuzia baadhi ya vijenzi muhimu vya kazi za fasihi kama vile dhana ya uhusika wa fanani na hadhira.

Jamie A. Thomas wa Chuo Kikuu cha Swarthmore cha Marekani alizungumzia namna wazungumzaji wapya wa Kiswahili kutoka miji ya Accra (Ghana), Beijing (China) na Naples (Marekani) wanavyojaribu kuzipa sura mpya hadithi wanazosimulia wakiwa jijini Dar es Salaam (Tanzania) kwa kuzipa uhusika na maudhui ya Kiswahili.

Siku hii ya kwanza ya kongamano hili la siku mbili ilishuhudia pia mjadala juu ya dhima ya riwaya za Kiswahili kwenye kuzungumzia suala la unyanyasaji wa kijinsia kupitia mada “Unyanyasaji wa Kijinsia: Ulinganishi wa Riwaya za Kiswahili za Miaka ya 1970 – 1980 na 1990 – 2000” iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ernesta S. Mosha, sambamba na “Matumizi ya Tashtiti katika Ulimwengu wa Waswahili” ya Zawadi Limbe Daniel pia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyejikita zaidi kwenye kulinganisha mawasiliano ya tashtiti katika mitandao ya kijamii.


Na kama bado una wasiwasi juu ya Ubantu wa lugha ya Chimiini inayozungumzwa kwenye mji wa Barawa nchini Somalia na ikiwa unaichukulia kuwa ni katika lahaja za Kiswahili, Meikal Mumin wa Chuo Kikuu cha Cologne nchini Ujerumani ana mtazamo mpya kuhusiana na lugha hii, akihoji kwamba si Kiswahili moja kwa moja wala si Kisomali peke yake, Bali iitwe tu kuwa ni lugha ya Somalia kupitia mada yake “Chimiini as a language of Somalia.”

Siku hii ya awali ya kongamano ilifungwa kwa taanzia ya bingwa wa lugha ya Kiswahili, Omar Babu Marjan, ambaye alifariki dunia tarehe 20 Januari 2015 nyumbani kwao Kenya, baada ya kuugua kwa muda mfupi. Prof. Ken Walibora ambaye ni sahibu wa siku nyingi wa Marehemu Omar Babu alilifunga kongamano kwa siku hii ya kwanza akighani wimbo ambao mwendakwao huyo alikuwa akipenda kuuimba maishani mwake: “Ilahi nipe nusura, uniruzuke na pepo!”

Ukumbi mzima ulisimama kwa dakika moja kwa heshima na kumtukuza mshairi, mwanafasihi, mwalimu na mchambuzi wa lugha, Omar Babu Marijan.