Wakitwambia tusende, siye tutoke, twendeni
Wakisema tusiunde, ‘sikubali, tuundeni
Wakitaka watushinde, twinuke, tuwashindeni
Hii safari ni yetu
Si yao
Nafasi tusiwapeni
‘Kitwamba ‘sikutane, tujikusanye, tukutaneni
‘Kisema ‘siandamane, sikubali, tuandamaneni
Wakitaka ‘sishikane, tukamatane, tushikamaneni
Dhamira hii ni yetu
Si yao
Nguvu hiyo ‘siwapeni
Wakitwamba ‘siandike, kalamu tutwae, tuandikeni
‘Kisema tusitamke, simu tuchukuwe, tuambianeni
Wakitaka wasitake, nawajuwe, tusiwatiini
Mwaka huu ni wetu
Si wao
Khofu ‘siwaogopeni
Mohammed K. Ghassani
Bonn
24 Mei 2015