Maamuzi, kuikata, nikakukabidhi
Maamuzi, kuipata, njema yangu radhi
Maamuzi, kukamata, kubwa njema hadhi
Sasa kwa bakora yangu, umenitia kilema
Ulikuja, ukasema, maneno chungu nzima
Ulikuja, ukipuma, umejivisha huruma
Ulikuja, tonge nyama, kutulisha takirima
Bakora yanigeuka, najutia maamuzi
Uliponiona, ulisimama, hali ukaniuliza
Uliponiona, uliungama, shida zangu kupunguza
Uliponiona, nekuwa mwema, sifa tele ‘kanijaza
Sasa kwa bakora yangu, umenitia kilema
Ulipohamia, ninapasikia, mitaa ya vizito
Umenikimbia, ninakulilia, kitanda changu majuto
Ninakusikia, ukihutubia, kwa habari moto moto
Unajisifia, wajitangazia, umeshatimiza ndoto
Bakora yanigeuka, najutia maamuzi
Ally Hilal
Wete – Pemba
13 Mei 2015