
Kama wewe ni mwanamageuzi visiwani Zanzibar ambaye una dhamira ya kuufanya mwaka 2015 kuwa kweli mwaka wa maamuzi, huna sababu ya kuvunjika moyo licha ya kuibuliwa kwa madudu ya Tume ya Uchaguzi (ZEC) kwa kushirikiana na mtandao mpana wa waharibifu uchaguzi unaoihusisha Idara ya Vitambulisho, vyombo vya dola, wakuu wa mikoa, wilaya na masheha, anasema Foum Kimara.
Baada ya kusoma malalamiko ya wanamageuzi juu ya suala zima la uchaguzi unavyoendeshwa visiwani Zanzibar, naamini wananchi wanayo dhima kubwa katika kukabiliana na ufujaji wa haki unaoendeshwa na kuwapa viburi wachache wa kuwaita wengine mabwege. Bado karata iko mikononi mwa wanamageuzi na wala sio kwa wahafidhina. Na hapa naeleza kwa nini ushindi uko mikononi mwa wanaopigania mabadiliko.
Kwanza majina ya walioandikisha mara mbili mbili inafaa kabisa yatolewe wazi wazi na wananchi waweze kuwajuwa wizi wa haki na wanavyotumika. Kuanzia sasa majina, picha na vituo walimojiandikisha vifanyiwe kampeni maalum ya mwezi mzima kila mahala. Picha zao zibandikwe katika kuta za kila mtaa na kila kijiji ili wananchi waweze kuwafahamu vizuri na kuwatazama kwa macho mawili. Kama ni vipeperushi basi ni vya kuwaumbua hawa wanaotumika kuharibu zoezi la msingi wa haki ya kiraia na uwepo wa nchi yetu.
Pili, wanamageuzi waanze haraka sana zoezi maalum la kushughulika na hawa watu 10,000 walioandikishwa kinyume na sheria na kuwafungulia mashitaka katika mahakama za Zanzibar na zile za Muungano kwa vile hawa hupiga kura zote mbili – za Muungano na za Zanzibar. Hili si suala la kuachwa madhali ushahidi upo. Makosa haya lazima yapelekwe mahakamani ili tuweze kuhakikisha hawatakuwa tena watumwa wa dhulma inayofanyika. Kuna watakaokebehi hili kwa kusema vipi kesi ya ngedere umpelekee ngedere? Lakini naamini watuhumiwa hawa wanaoendelea kuvunja sheria na kuachwa wakiendelea kukebehi sheria za nchi ikiwa mahakama zitawatia hatiani au hata ikiwa tutaweza kutafuta njia za kuwafungulia mashitaka moja kwa moja basi hakuna mwengine ataejitokeza na kufikiri ubabe una nafasi katika ulimwengu wa sasa.
Tatu ni kuhakikisha mawakala wa vyama wanapewa elimu madhubuti ya namna ya kukabiliana na vitisho vya polisi katika vituo vya upigaji kura. Elimu iweze kuwajenga mawakala katika masuala ya sheria, haki zao na haki za wananchi wapiga kura. Nimetazama baadhi ya vidio zilizopita na namna ya mawakala walivyokuwa wakiburuzwa na polisi wa vituo kwa vitisho bila ya kusikilizwa madai yao juu ya vitendo vya baadhi ya waratibu wa Tume. Kama mawakala wale wangelipewa elimu nzuri ya kukabiliana na polisi kwa misingi ya sheria kungeliweza kupunguza vitendo vya namna ile katika chaguzi.
Tumebakiza miezi mitano. Kama tutaweza kuwapata mapema mawakala wa vituo vyote na kuanza kuwanoa katika elimu ya mikakati ya kulinda wizi wa kura basi tutapiga hatua kubwa zaidi. Kubwa ni kutowapa nafasi ya kuyafanya wakiwa na convinience, tuwekeze katika teknolojia na kuwa na mtanado mzuri wa kutoa ushahidi moja kwa moja na hadharani penye wizi, hadaa, matumizi ya nguvu na uvunjwaji wa haki.
Mawakala kuweza kupatiwa mapema vitendea kazi, kwa mfano mmoja wa wakala alikuwa akipiga kelele kwamba maofisa wa Tume walikuwa wakiziharibu kura za wapinzani kwa kuzitoboa na kuzifanya ziwe “invalid” – hazifai. Lakini tunarudi kule kule kwamba maofisa wa aina hii hawawezi kubanwa na sheria bila ya ushahidi, na ndio maana wakatuita “mabwege” kwa vile jeuri yao imevuka mpaka ikifikiri hakuna arubaini ya mwizi.
Ushahidi wa MANENO hautoshi, ukisikiliza ile maelezo ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) ya juzi mbele ya waandishi wa habari, utakuta hoja kubwa kwamba wizi ukifanyika huko nyuma lakini ushahidi ulikuwa haujapatikana. Nionavyo mimi kwa hili la mawakala namna ya kukabiliana nalo ni kuhakikisha vitendo kama hivi vinapatiwa vitendea kazi ilimkuweza kuonyesha ulimwengu namna ya Tume ya Uchaguzi inavyochangia katika kuharibu amani ya nchi. tusiingie katika uchaguzi bila ya elimu nzuri kwa mawakala na nyenzo za kileo zitazoweza kutumika kuonyesha kwa UWAZI uchafu wa maofisa wa Tume.
Wananchi bado wana nafasi nzuri sana ya kuzuia madudu haya yasifanyike. Zanzibar ni ndogo na karibu sote tunajuana. Wale wanaotoka uzini wakaandikishwa pia na mjini majina yao yanayotumika yatolewe, pamoja na picha zao kuwekwa hadharani. Kampeni kabambe ya kuhakikisha jamii nzima inawatenga wale wote wanaohusika na matendo haya machafu kutokana na dhulma wanayoifanya kama tulivyowatenga vibaraka wa ukoloni huko nyuma. Kampeni ianze kwa kila mtaa, kijiji, wodi, kuhakikisha haki inasimama. Wengi wa hawa watu hawajalazimishwa, ila njaa ndio inayotumika kuwahadaa, mbali ya chama kujipanga katika mikakati yake ya kupambana na Tume, wananchi waanze moja kwa moja kujipanga kulinda maslahi ya nchi yetu moja kwa moja kwa kukabiliana na wahalifu hawa kwa misingi ya kisheria. Tuanze katika majimbo yetu kuanzia Pemba na Unguja Kote.
Wakati umefika sasa kwa kulitoa hadharani daftari la wapiga kura na kuliweka wazi kila ward na kila panapo mashaka kuwekwa wazi ili jamii nzima ifahamu ukweli ulivyo. Naamini kila mmoja anauwezo wa kuzia uchafu huu usifanyike. Kama wewe mwananchi mpenda mabadiliko, hakikisha kidogo kidogo unajipanga katika teknolojia ya kuwaumbua wizi wa haki yako. Hakuna kitu kama taswira ya mwizi akiwa kwenye zoezi lake la wizi. Fikiri, ikiwa na madudu yote yanayofanyika na mshindi anatangazwa kwa kura 3000 tu dhidi ya mwenzake, jee kama tutaweza kuzuia kura haramu 100 tu kwa kila jimbo, hatutaweza kusimamisha haki? Jimbo lina ward karibu 5, hivyo unapoweza kuzuia wapiga kura haramu 20 tu kwa kila wodi jee hujaweza kuzuia kukuwa kwa zoezi haramu?
Kinga ya wanamageuzi ni daftari la wapiga kura na idadi yao ya jumla ya wapiga kura. Tume haiwezi kuruhusu watu wapige kura bila ya kujuwa hesabu za wingi wao kwa vile tutakuja kuhesabu kura zikiwa nyingi kuliko walioandikishwa. Hapo ndipo ulipo ushindi wa wanamageuzi kuhakikisha wizi unaopangwa unaparaganywa kiasi kwamba mawili yatafanyika, ima kura zitazidi wapiga kura au mshindi halali atatajwa.
Jianze kujipanga katika utetezi wa nchi yako kwa kuwajuwa majirani zako na wakaazi wa mtaa wako. Pitia majina yaliomo katika daftari la wodi yako na hakikisha yaliyooredheshwa mara mbili unawatambua wahusika na kuwafichua kwanza jamii iwajue. Jambo la pili ni kuundwa kwa baraza za wanasheria katika kila wodi ili tuanze kazi ya kuwapeleka mahakamni wahalifu wa haki na madalali wa nchi yetu. Usione kwamba nafasi yako kama mtu moja ni ndogo katika kuzuia wizi wa kura. Ukiweza kuzuia wizi wa mtu mmoja tu basi umesaidia pakubwa kwa vile katika wodi yako ni watu ishirini tu wanaweza kubadili matokeo ya uchaguzi kwa ujumla wa wodi zote zilizopo.
Tujipange, uchaguzi ni sawa na mahakama, mwizi anaweza kushinda kesi kwa kukosa ushahidi pamoja na mawakili wazuri wanayoifahamu sheria. Nasi tunaweza kuzuia wizi wa kura kwa kujipanga katika kubeba ushahidi, kuwafichua madhalimu na kuwachukulia hatua za kisheria zitakazoweka heshima kwa wananchi wote.
Imehaririwa na Mohammed Ghassani.