UCHAMBUZI

Wanaoapa kutotoa nchi kwa ‘vikaratasi’ wapime kasi ya wimbi

“Amani ni ufunguo wa mafanikio ya kila kitu kwa maisha ya binadamu. Bila ya amani hakuna maendeleo wala mafanikio yatakayopatikana katika nchi,” aliwahi kusema mbunge Mohamed Habib Mnyaa akiwa Dodoma. Miezi michache ijayo kutoka sasa, yaani Oktoba 2015, tunatarajia kufanya uchaguzi mkuu kwa mujibu wa katiba zote za nchi zetu – ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar.

Katika uchaguzi huo, tunatarajia kuwachagua viongozi wapya wa kuongoza mataifa yetu haya mawili kwa kipindi cha miaka mengine mitano ijayo katika ngazi za udiwani, uwakilishi, ubunge na urais, ukiwa ni wa tano kufanyika tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe hapo mwaka 1992.Tayari tangu mwaka huu ulipoanza, joto la uchaguzi limeshuhudiwa kupanda, hususan kwa viongozi wa juu wa nchi yetu.

Rais Ali Mohamed Shein (kushoto) na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad.
Rais Ali Mohamed Shein (kushoto) na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad.

Tumewahi kuwasikia viongozi wa upinzani, hasa Chama cha Wananchi (CUF), wakisema huu ni mwaka wa maamuzi, wakimaanisha kwamba umma umezidi kukiitikia chama hicho na muitikio huo umepelekea wao kupata wanachama wengi zaidi hadi katika mitaa, vijiji, na miji ambayo hapo awali hawakuwa na uungwaji mkono kama vile Donge, Makunduchi na hata Kitope, jimbo na ngome pekee ya Makamu wa Pili wa Raisi wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Mafanikio ya sasa ya CUF yanaambatanishwa pia na historia yake kwenye chaguzi zilizopita, ambapo yenyewe inaamini kuwa ilishinda kila uchaguzi katika ngazi ya urais, lakini ikaporwa ushindi huo kwa msaada wa vyombo vya dola, ikiwemo Tume ya Uchaguzi (ZEC), vikosi vyote vya ulinzi na usalama. Lakini mara hii, kinyume na ilivyokuwa mara zote nne, yaani mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010, CUF iko kwenye nafasi kubwa na nzuri zaidi ya kutowezekana kuibiwa ushindi wake. Kuingia kwake kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa na kusimamia kwake Ajenda ya Zanzibar moja iliyoshikamana na yenye nguvu ndani na nje ya Muungano, kumeijengea CUF ngome isiyovunjika miongoni mwa Wazanzibari wa kila kundi; na hivyo ushindi wa kura inayoutegemea ni mkubwa maradufu na ambao, wengine wanaamini, hautakuwa rahisi kuupora kama ule ambao tafauti huwa ya chini ya asilimia tano.

Hata hivyo, pamoja na kuifahamu nafasi yake hiyo, mara kadhaa CUF imetamka hadharani kwamba ikiwa uchaguzi utafanyika kwenye mazingira ya uhuru, haki na uwazi na kikashindwa kihalali, basi itayakubali matokeo hayo. Akizungumza na wazee wa Kizanzibari katika mkutano wa Bwawani mapema mwezi Machi, Katibu Mkuu wa CUF na anayetarajiwa kugombea tena urais kwa chama hicho, Maalim Seif, alisema ikithibitika kushindwa katika uchaguzi ujao wa 2015 na iwapo uchaguzi utaendeshwa kihalali, atayakubali matokeo hayo.

Lakini pia kwenye mkutano huo Maalim Seif alionya kuwa endapo atashinda, hatokubali tena kuporwa ushindi kama alivyowahi kufanya hivyo mara zote, ukiwemo uchaguzi wa mwisho wa mwaka 2010. Mara kadhaa katika siku za hivi karibuni, mmoja wa waasisi wa serikali ya kwanza ya Zanzibar baada ya Mapinduzi na kiongozi wa Kamati ya Maridhiano, Mzee Hassan Nassor Moyo, amekuwa akitamka bayana kwamba ni yeye ndiye aliyetumwa na Rais Amani Karume mwaka 2010 kumshawishi Maalim Seif akubali matokeo yoyote ambayo yangelitangazwa na ZEC mwaka huo, naye Maalim Seif akakubali kwa kuzingatia umuhimu wa amani ya nchi pamoja na Maridhiano yaliyofikiwa kati ya CUF na CCM.

Kwa upande mwengine, tunawasikia wanachama na viongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakitangaza wazi kuwa lazima watarejea madarakani kwenye uchaguzi huu “kwa vyovyote vile”. Akiwa bungeni Dodoma, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM, Asha Bakari, alisema: “Namwambia (Ismail) Jussa hatutoi (serikali), labda mtupindue. Serikali ya kimapinduzi haichukuliwi kwa karatasi, hilo nawabainishia”.

Tumewahi pia kumsikia aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa CCM kwenye Baraza la Wawakilishi, marehemu Salimini Awadh Salmini, akitamka kwamba hata wapinzani washinde kwa kura, wao CCM hawako tayari kutoa serikali na akafika umbali wa kusema kuwa vifaru na makombora ya kivita yapo kwa ajili ya kuhakikisha hilo. Hizo zimekuwa ndizo kauli za takribani kila kiongozi na kila mfuasi wa CCM kwa takribani muda wote huu.

Kauli hizo za vitisho haziendi kavukavu. Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa kukiripotiwa matukio ya mashambulizi dhidi ya wananchi, uharibifu wa mali za raia na kukamatwa kwa wanachama na wafuasi wa CUF sehemu mbalimbali visiwani Zanzibar. Miongoni mwa matukio hayo ni lile la moto kwa matawi ya CUF huko Tumbatu na Kisauni, kuvamiwa na kushambuliwa kwa msafara wa wanachama wa CUF wakitokea Makunduchi, ambapo watu kadhaa walijeruhiwa, na polisi kuwashambulia kwa mabomu ya machozi na marungu wafuasi wa CUF waliokuwa wanaelekea Kitope kuhudhuria mkutano wa hadhara wa chama chao. Kuna taarifa pia za kamatamakamata inayoendeshwa na jeshi la polisi kwenye maeneo kadhaa ikiwalenga wanachama na wafuasi wa CUF.

Mambo yote haya ni ishara mbaya kwa amani ya nchi. Cha kushangaza ni kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ambayo msingi wake mkuu na uhalali wake pekee ni Maridhiano, imekaa kimya cha mtu aliyepatwa na ugonjwa wa kupooza. Hakuna kemeo wala karipio kwa waliofanya hivi kutoka kwa kiongozi mkuu wa serikali hiyo, Rais Ali Mohamed Shein, wala kwa msaidizi wake wa shughuli za kila siku serikalini, Balozi Iddi. Hakuna hata mmoja kati yao aliyejaribu angalau kutoa mkono wa pole kwa walioathirika na matukio haya. Jeshi la polisi pia limeshasema kuwa matendo hayo yalifanywa na watu wasiofahamika.

Nikiwa kama raia mwema kwa nchi yangu, nimepatwa na mashaka na ningelipenda kufikisha ujumbe wangu moja kwa moja kwa Rais Shein, Makamu wake wa Pili Balozi Iddi, jeshi la polisi Zanzibar, na pia viongozi na kisiasa na wafuasi wao wote. Madhali tumeikubali demokrasia ya vyama vingi, basi hatuna budi tuikubali na misingi yake, ukiwemo ule mkuu wa kukubali matokeo iwapo uchaguzi utakuwa wa uhuru na haki. Hivyo ndiyo demokrasia inavyataka na hivyo ndivyo kutunza amani ya nchi sambamba na kusogea kwenye maendeleo.

Tunapaswa kukaa kitako na kutathmini kauli zetu. Tuzungumze kauli za maslahi na tuacheni kauli za kuwatishia raia wetu. Ukiangalia nchi yetu inategemea utalii kiuchumi, na hakuna utalii iwapo amani ikitoweka. Tuangalie mfano wa karibu katika nchi jirani ya Kenya ambayo kwa sasa utalii umekufa kwa kuwa hakuna amani.

Tuacheni utashi wa maslahi binafsi na tuwekeni mbele utashi wa maslahi ya umma zaidi. Dk. Shein na Maalim Seif, wawili nyinyi ndio tuliowachagua kushika dola mwaka 2010 ili mtuongoze kwa amani na tuende kwa amani katika kila hatua tunayopita. Kaeni kwa pamoja kama wewe Maalim Seif na Rais Karume mulivyokaa awali, na kwa msaada wa Kamati ya Maridhiano, hadi mkafanikiwa kufanya uchaguzi wa aina yake kwa Zanzibar. Ni uchaguzi wa 2010 tu ndio uliokosa kumwaga damu hata tone moja.

Kwa hivyo, kinachotakiwa ni kwa Dk. Shein na Maalim Seif, kabla kuingia katika uchaguz, kutumia nyadhifa zenu hizo za urais na umakamu wa rais kuweka mkakati wa kutunza amani ya nchi. Musikubali kuwaachia mliowachagua waipeleke nchi kombo. Kisha mukumbuke kuwa kuna mkono wa haki na sheria, ambayo kuna siku itasimama hata kama itachelewa. Kauli za kutotoa nchi kwa vikaratasi au kutumia vifaru na mizinga kuzuwia mshindi wa uchaguzi asitangazwe zinaweza kuja kuwa na matokeo mabaya kwa wazitoazo na sio kwa waambiwao tu.

Imehaririwa na Mohammed Ghassani.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.