Imetukuka, kwa upepo wake
Pwani, pwani, pwani
Imekamilika, njema heba yake
Ndani, ndani, ndani
Imehifadhika, sifa ya upweke
Shani, shani, shani
Bahari tulivu, mawimbi kiasi
Heko, heko, heko
Samaki shupavu, jodari na tasi
Wako, wako, wako
Anga li angavu, ‘mesheheni rasi
Huko, huko, huko
Kwenye Kiswahili, cha kusanifiwa
Safi, safi, safi
Kwenye waswahili, waliosifiwa
Kofi, kofi, kofi
Hizi ndizo mali, tulotunukiwa
Ghafi, ghafi, ghafi
Sasa ni hadithi, za kuhadithika
Aibu, aibu, aibu
Pengine theluthi, imebahatika
Kusibu, kusibu, kusibu
Wa wapi warithi, nafasi kushika
Jaribu, jaribu, jaribu
Ally Hilal,
Wete – Pemba