Kwenye pita pita zangu, nimeliona suali
Lauliza walimwengu, kati ya hawa wawili
Yupi mroho ndu yangu, muomba huyu awali
Muombwaji aso pingu, huru yeye ni wa pili
Kuna mroho elewa, huyu yule aombae
Aonapo hupagawa, hutaka naye apewe
Yuko radhi kuwagawa, atakacho akitwae
Hakuna la kuambiwa, mpaka nae apewe
Hutamani kiso chake, hutapatapa rohoni
Akili huwa si yake, aonacho hutamani
Atafanya mbinu zake, akitie mikononi
Ataomba akipate, furaha tele moyoni
Aombwae namjua, ana sifa iloyake
Anapogoma kutoa, hutajwa kwa cheo chake
Jina lake alijua, mchoyo ni hadhi yake
Mroho siye tambua, huko si sehemu yake
Kaditamati nangani, fikira nazituliza
Nimekujibu amini, awali ulilouliza
Hamad sitojikhini, hapa mwisho wa kuwaza
Naomba ulithamni, jibu usijelibeza
Ammar Ruwei Nassor
@ammarruweih
Dar es Salaam – Tanzania
20 Aprili 2015