Viko vya kufananisha, angani na nchi kavu, lakini si Mungu
Mbona wajiaibisha, mchana jua angavu, kiumbe kumwita Mungu
Dunia imeshakwisha, hali sasa si tulivu, nawambia walimwengu
Uongozi ni wadhifa, anayetoa ni Mungu, hakuna asiyejua
Sio kuleta maafa, kumpa sifa ya Mungu, huku ni kujiumbua
Kukufuru sio sifa, ni madhambi kwa mafungu, dhoruba iso mvua
Polisi si malaika, kamwe yeye hafanani, ni kiumbe mpungufu
Hufanya analotaka, hata kama la dhambini, cheo kipate turufu
Malaika kasifika, hata kwenye Qur-ani, ametajwa na Raufu
Msahafu haufanani, na katiba ya kiumbe, kkitabu kitakatifu
Wala injili yashani, havina kasoro chembe, ni vitabu vya Raufu
Taurati ya zamani, vitabu vyenye ujumbe, mwongozo mbainifu
Na Zaburi ya Daudi, dahari ilidhihiri, ikiwa imetimia
Wapate kuyafaidi, kuyatambua ya kheri, maasi kuyabagua
Vipi unajifisidi, wabadili tafsiri, uzushi watuletea
Mitume si mawaziri, usijitie pumbao, kwa mifano iso macho
Unaona ni fakhari, kuwasifu wenye vyeo, watengeza chakulacho
Jua tu kwenye safari, kaburini ni kituo, utavuna upandacho
Kila ashangiriaye, alichosema mwenzetu, ajuwe hasalimiki
Sote pamoja na yeye, ‘tarudi kwa Mola wetu, kwa shime tujishitaki
Maneno tuyafukie, toba iwe nguzo yetu, Mola atatuafiki
Ally Hilal
Wete – Pemba