UCHAMBUZI

Sisi ni kizazi cha waliopinduwa na waliopinduliwa

WAKATI Mapinduzi yanafanyika tarehe 12 Januari 1964, baba yangu (Mungu amrehemu) alikuwa ndio kwanza amewasili kisiwani Unguja akitokea Bara, ambako alikuwa ameishi kwa takribani miaka mitano mtawalia.

Katika pirikapirika za Mapinduzi hayo zilizoanza usiku wa Jumamosi, akakamatwa siku ya tatu yake na watu wenye silaha kutokea Bara akiwa mitaa ya Kikwajuni. Jambo la kwanza aliloulizwa lilikuwa ni jina lake. “Naitwaga Massanja!“ Ndilo lililokuwa jibu lake. Lakini rangi yake ya kahawia na nywele zake laini zikamsaliti ingawa alikuwa kweli na lafudhi ya Kimasanjamasanja.

Hakupigwa sana, lakini alifikishwa kwenye kambi ya Raha Leo na pale usuhuba wake wa utotoni na Salim Ghafir, nao pia ukamsaliti, maana alipomuona tu akainuka na kuanza kulia: “Khelef nawe umeletwa huku!?“Baada ya rabsharabsha za Mapinduzi kutulia, baba yangu alirudi kwao Pemba. Akaanzisha maisha yake, akiwa kiongozi si tu wa ukoo wake wa Ghassani, bali pia baadaye akaja akawa balozi wa nyumba kumi kumi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wakati mimi nakua, niliikuta bendera ya CCM ikipepea kwenye paa la makuti la nyumba yetu. Hata tarehe yangu halisi ya kuzaliwa ilibadilishwa kutoka mwezi Januari na kuwa 5 Februari 1977 ili isadifiane na tarehe ya kuzaliwa kwa CCM. Baba yangu hakuwa sehemu ya waliopindua.

Kwa hakika, hakuwahi hata kuwa muumini wa Afro-Shirazi Party (ASP) wala Umma Party – vyama vinavyonasibishwa na Mapinduzi hayo. Ukoo mzima wa baba yangu ulikuwa wanachama wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP ama Hizbu). Lakini baba yangu hakuwa na chuki za kisiasa na ndani ya nyumba yetu kuonesha hisia mbaya za kisiasa dhidi ya mtu mwenye mtazamo tafauti nasi, lilikuwa jambo la haramu.

Nakumbuka sana kwamba mwaka 1993, wakati huo nikiwa bado na miaka 16, alinigombeza hadharani kwa maneno makali, pale nilipokuwa nimetoka kwenye mkutano ulioitishwa na aliyekuwa Waziri wa Elimu na Naibu Waziri Kiongozi wa wakati huo, Omar Ramadhani Mapuri, huku nikiwa natoa maneno mabaya dhidi ya shemegi yangu, Nassor Issa Mazrui (Mungu amrehemu), ambaye kwenye mkutano huo alichukuwa kadi ya CCM na kurejesha ya CUF.

Baba yangu alikuzwa na alitukuza sisi watoto wake kwenye ustahamilivu wa kisiasa. Wakati wa ugonjwa wake wa mwisho mwaka 1994, alilazwa kwenye Hospitali ya Chake Chake na ikasadifiana kuwa kada kijana wa CCM, akiitwa Yussuf Alawi (maarufu kama Yussuf Panzi) naye amelazwa.

Takribani ndugu na jamaa wengi wa Yussuf walikuwa wamemtenga kwa kuwa sio tu alikuwa kada, bali pia alikuwa mtukanaji mzuri wa CUF na viongozi wao akiwa kwenye majukwaa ya siasa, hasa kwenye mikutano iliyokuwa inaitishwa na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Dk. Omar Ali Juma (Mungu amrehemu). Alichokuwa akinihimiza baba yangu kila usiku ukifika ilikuwa ni kumuhudumia Yussuf kwa kila hali, jambo ambalo baadaye lilikuja kuanzisha urafiki wangu na Yussuf hata baada ya baba yangu kutoka hospitalini na kufariki dunia.

Katika Zama za Siasa, baba yangu alikuwa na rafiki yake mkubwa, Bwana Mohammed Fakih wa Kangani Mkoani (Mungu amrehemu), ambaye ukoo wake mzima ulikuwa ASP. Wakati wa msimu wa karafuu, baba aliondoka na aila yake kwenda kupiga kambi kwenye familia ya Bwana Mohammed Fakih Mkoani kwa ajili ya biashara ya mikate ya Ajemi, ambayo ni urithi wa ukoo wetu.

Lakini wiki nzima kabla ya aila ya baba kuwasili Mkoani, wazee wa Bwana Mohammed (Mungu awarehemu) walikuwa wakitoa tangazo kwamba muda wote ambao “Khelef atakuwepo, hakuna kutajwa siasa za vyama.“ Na ndivyo ilivyokuwa pia wakati familia ya Bwana Mohamed ilipokuwa ikitembelea kwetu Pandani. Sisemi kwamba hakukuwa na visa vya karaha na kukomoana kati ya wafuasi wa kambi hizo mbili kwengineko visiwani Zanzibar.

Ninachosema ni kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Wazanzibari wa leo ni wale waliozaliwa na kuishi baada ya Uhuru wa Desemba 1963 na Mapin-duzi ya 1964. Miongoni mwao pia, muna idadi isiyo ndogo ambayo pande mbili za wazazi zimetokea kwenye mitazamo tafauti ya kisiasa, panapohusika dhana hizo mbili za Uhuru na Mapinduzi.

Nadhani familia ya Rais Mstaafu Amani Karume ina hadithi ya kusisimua zaidi katika hili kuliko yangu, kwani mke wake, Bi Shadya, anatokana na kizazi cha waasisi wa siasa za utaifaza Zanzibar, huku Amani mwenyewe akiwa mtoto wa Rais wa Kwanza wa baada ya Mapinduzi. Na wao si peke yao.

Wapo wengi pia ambao ni matokeo ya mchanganyiko sio tu wa wazazi wenye mitazamo tafauti ya kisiasa, bali pia mchanganyiko wa visiwa viwili vikuu vya Unguja na Pemba na pia mchanganyiko wa pande mbili za Muungano, yaani Zanzibar na Tanganyika.

Kuna wengine pia ambao waliinukia wakiwa wafuasi wa kambi moja ya kisiasa lakini wamebadilika sasa na kuwa waumini wa mtazamo mwengine wa kisiasa. Vyama vikuu vya siasa vya Zanzibar hivi sasa sio tena kielelezo cha Zanzibar ya miaka 50 iliyopita nyuma. Kuna ambao walikuwa wafuasi wa ASP na Umma Party, lakini ama wao we-nyewe au watoto wao wamekuwa leo wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF).

Kuna ambao wanatoka kwenye mizizi ya Hizbu na Zanzibar and Pemba People’s Party ZPPP), lakini hivi leo ndio wafuasi namba moja wa CCM. Baraka Muhammed Shamte ni kada mkubwa wa CCM akiwa ndiye mtoto wa kwanza wa muasisi wa ZPPP na Waziri Mkuu wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Muhammad Shamte (Mungu amrehemu).

Kuna pia wasiokuwa na chama chochote cha siasa, na ambao kwao siasa za vyama hazina nafasi katika maisha yao. Wote hawa ndio sehemu ya sisi leo. Sisi Wazanzibari. Binafsi nimeishi kwenye visiwa vyote viwili vikuu vya Zanzibar. Maisha yangu ya kifamilia pia ni mchanganyiko wa visiwa hivi na mitazamo hiyo ya kisiasa.

Ndani ya familia yangu mnatembea damu za walioupokea Uhuru wa 1963 pale Maisara, siku hizo ukiitwa Uwanja wa Coopers na waliokuja kuupindua Uhuru huo Jumamosi, tarehe 12 Januari 1964. Kuna ambao walikuwa viongozi na watumishi wa umma kabla ya Mapinduzi na ambao walikuwa hivyo hivyo baada ya 1964. Zote hizo ni pande zangu. Na wala si peke yangu mwenye pande hizo.

Tuko wengi jumla yetu, maana kila taifa lina historia yake, mazuri na mabaya, kupanda na kushuka. Lakini mwisho wa yote, kila taifa hupaswa kusimama kama taifa, likiitukuza historia yake na wakati huo huo likijifunza kwa matukio na matokeo ya historia hiyo kwa minajili ya kusonga mbele Wakati tukiadhimisha nusu karne ya Uhuru na Mapinduzi ya Zanzibar, hatupaswi hata kidogo sisi kizazi cha sasa kuyachukulia matukio hayo ya kihistoria kama msingi wa kutugawa.

Hatuna sababu ya kuwapa fursa wazee ambao dunia yao inawalizikia, kuturithisha dunia ya matatizo na migogoro kwa msingi wa historia ya kabla na baada ya Uhuru na Mapinduzi. Sisemi kwamba hatuna chochote cha kujifunza kwao, lakini nasisitiza kwamba tuchukue mazuri kutoka kwao na tuwaachie wafe na mabaya yao.

Moja ya mabaya hayo ni kosa walilolifanya wote wawili wakati huo, ambapo upande wa Hizbu/ZPPP ulijisahau kwamba Zanzibar ni ya wote na kupatwa na kiburi cha madaraka na uluwa kwa jina la kuchaguliwa kwenye “uchaguzi wa kidemokrasia“, huku upande wa ASP/Umma Party ukijiona kwamba wao tu ndio wenye haki ya kuitawala Zanzibar kwa msingi wa “wingi wa watu.“ Wote hawakutaka kujua kuwa Zanzibar ni yetu sote.

Matokeo yake, pande zote mbili, ama kwa kujuwa au kutokujuwa, zikachangia kuja kuifanya historia ya kutawaliwa kwa Zanzibar kuwa refu zaidi. Sisi wa leo, tunapaswa kuyatumia mafunzo haya ya kihistoria kupunguza urefu wa nchi yetu kutawaliwa. Si vyenginevyo.

1 thought on “Sisi ni kizazi cha waliopinduwa na waliopinduliwa”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.