Na Mohammed Ghassani
Ijumaa ya tarehe 6 Februari 2015, Rais Joachim Gauck wa Ujerumani na ujumbe wake waliondoka mjini Arusha kurejea kwao baada ya kuwepo ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu usiku wa Jumatatu ya tarehe 2 Februari.

Usiku huo, pale uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam, ujumbe huo ulipokelewa kwa matarumbeta na ngoma nyengine za kienyeji. Siku ya pili yake alipokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete kwenye Ikulu ya Magogoni, ambako mbali ya matarumbeta ya bendi ya jeshi, gwaride na mizinga 21 kwa heshima ya kiongozi wa nchi, uwanja mzima wa Ikulu hiyo ulitanda matarumbeta mengine.
Wakati mkewe Rais Gauck, Bi Daniela Gauck, alipotembelea kituo cha tiba cha CCBRT kilicho kando kidogo ya kitovu cha jiji la Dar es Salaam, wagonjwa wa fistula wanaotibiwa huko walikuwa na muda pia wa kumuimbia nyimbo mwanamke mwenzao huyo, wakisema “Sisi ni tegemeo la akinababa, sisi ni tegemeo la watoto. Sisi ni tegemeo.“
Usiku wa tarehe 3 Februari, Rais Kikwete na mkewe, Bi Salma Kikwete, waliwakaribisha tena wageni wao Ikulu kwenye chakula cha jioni. Ndani ya ukumbi mulivoromboshwa muziki mkali wa bendi ya polisi. Wakati wageni hao wanaondoka kurudi hotelini kwao saa 4:00 usiku, nje kulikuwa na vikundi vya ngoma za kienyeji kuwaaga.

Wakati wanaondoka siku ya Jumatano kuelekea Zanzibar kwa boti ya Azam Marine, bandarini palikuwa na bendi nyengine ya matarumbeta ikitumbuiza kwa zogo na shangwe. Wimbo “Kitororo“ wa msanii nyota wa Tanzania, Naseeb Abdul, maarufu kama Diamond Platinumz.
Zanzibar na Arusha nako ko hali haikuwa tafauti. Kulikuwa na ngoma wakati wa kuwasili na ngoma wakati wa kuondoka. Kwa makisio tu, hadi Rais Gauck na wenzake wanarudi Ujerumani, baada ya kuwepo Tanzania kwa siku zisizozidi tano, tayari walishapigiwa ngoma zaidi ya mara saba.
Wala ujumbe wa Rais Gauck si pekee unaokumbana na “ukarimu“ huu wa kukatikiwa mabuno. Ni utamaduni mkongwe ambao sasa unahitaji kuhojiwa kwa sababu sio tu unaudhi, bali pia unabeba maana kadhaa zisizosema uhalisia ulivyo.
Kitamaduni na kijamii, nafahamu kwamba kwetu Waafrika ngoma si kielelezo cha mikatiko na minyumbuliko ya miili yetu tu, bali pia njia ya mawasiliano. Hata hívyo, ninaamini kuwa nyuma ya ngoma zinazotayarishwa, kulipiwa na kushajiishwa na dola kuchezwa mbele ya wageni kutoka nje, ujumbe unaotumwa una maana mbaya sana.

Chukulia mfano huu halisi. Dhamira ya ziara ya Rais Gauck nchini Tanzania ilikuwa na dhamira mbili kuu: moja ya kisiasa na nyengine ya kiuchumi. Sikiliza hotuba yake, angalia maeneo waliyoyatembelea, utajua kuwa walikuwa wamekuja kwa lengo maalum na lenye uzito wa aina yake. Mikutano ya wafanyabiashara wa pande mbili iliyoangalia fursa za uwekezaji, mazungumzo na asasi za kijamii, waandishi wa habari, wanasiasa na wanasheria. Ujumbe huu una ujumbe ndani yake.
Ongeza ukweli mmoja mchungu sana pia. Ujerumani ilikuwa mkoloni wa Tanganyika na ina historia refu inayorudi nyuma kwenye majilio ya wakoloni kwenye ardhi hii yenye wingi wa rasilimali tangu mwishoni mwa karne ya 19 kupitia wale waitwao wavumbuzi na wamishionari. Miongoni mwa “upotoshaji” uliomo kwenye historia ya kimapokezi ni kwamba wahenga wa Kitanganyika waliweza kudanganywa na “wavumbuzi” akina Karl Peters wa Ujerumani wakawapa ardhi na rasilimali zao kwa shanga na sigara wakati wao wakicheza ngoma na kufanya matambiko.
Si lazima upotoshaji huu uwe na ukweli wa asilimia mia moja, hasa ikikumbukwa kuwa baadaye wazee wa Kitanganyika, wakiwemo Chifu Mkwawa na Bushiri, waliwaongoza wenzao kupambana na Mjerumani kwenye vita vya silaha na umwagaji damu kupigania ardhi zao na kupinga kutawaliwa.

Hivi leo, karne nzima baadaye, Tanganyika na Zanzibar (sasa zikiwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) ni huru na zina watawala wake wazawa. Njia kuu za uchumi na mifumo ya kisiasa imo mikononi mwao wenyewe, angalau kwa maana nyepesi. Bado, hata hivyo, nchi hii ni miongoni mwa mataifa masikini sana duniani, ambayo pato la raia wengi ni chini ya dola moja kwa siku.
Kuna hadithi rasmi ya serikali ambayo wawekezaji kutoka nje husimuliwa na wao wakaisimulia kwa wengine, kwamba ukuwaji wa uchumi ni zaidi ya asilimia 7 kwa mwaka. Lakini pia kuna hadithi ya kisasa ya deni la serikali kupanda katika kiwango kinachotishia kutokopesheka. Kuna hadithi ya machungu ya ukuwaji huo unaoongeza idadi ya wengi wasionacho kabisa na wengi walionacho cha kupitiliza.
Miongoni mwa hao wengi wasionacho kabisa ndio wanaoonekana mbele ya wageni wa kimataifa wakikatika mabuno na kuruka wakitua chini. Ndio wanaopiga matarumbeta na kuimba “Kitorondo, mwendawazimu kaingiaje!”
Tukiri. Tuna tatizo. Na kama hatukujihoji, hakuna atakayetuchukulia kwa umakini, licha ya utajiri tulionao. Tutakuwa watu wa kupiga ngoma kama fursa pekee tuliyonayo mbele ya wageni, maana ni huko ambako hawawezi kushindana nasi. Lakini tukienda mbele ya meza ya mazungumzo na mikataba ya kibiashara na uwekezaji, tunaangushwa chini.
Hapo ndipo uwekezaji unapogeuka ukwapuaji wa rasilimali, si kwa kuwa wageni ni wana dhati ya wizi, bali kwa kuwa ni wafanyabiashara wazuri wanaojua kutengeneza faida, nasi ni wachezaji wazuri wa ngoma tunaojua kukatika mabuno.