Pumbavu likipumbaa, ‘silache pumbaa nalo
Uwepo linapokaa, likiuka uka nalo
Sijache ukazubaa, lilo silo lambe ndilo
Pumbaa na pumbavulo
Pumbavu likikenua, cheka uavye machozi
Ukiliona lalia, garagara piga kwenzi
Ela lisije kujua, walifanya lipuuzi
Pumbavu pumbaa nalo
Pumbavu likikuita, litike haraka sana
Karibu likikupita, lamkie kwa heshima
Lambe lolo lasifika, kwa mazuri linofanya
Ela hana afanyalo
Hamad Hamad
01 Septemba 2014
Dodoma