Wananadharia wa lugha wanakubaliana kwamba lugha ni sauti za nasibu, yaani sauti za kubahatisha. Kwa mfano, ni suala la sadfa tu kwamba sauti ‘e’ ikichanganywa na ‘mbe’ inakuwa ’embe’, mojawapo ya matunda matamu ya nchi za joto. Kwa mantiki hiyo, hakuna chochote – nje ya unasibu – zilizofanya sauti hizo zikusanyike pamoja na kutoa neno la lugha linalowakilisha tunda hilo.
Lakini ‘unasibu’ huu wa lugha haumo kwenye sauti tu, kwa maana ya mjengeko na miundo ya maneno. Umo pia kwenye maana za maneno hayo. Hata kwenye hilo neno ’embe, kwa mfano, pana ukweli huo. Ni sadfa tu kuwa embe linaitwa embe, na si kwamba kuitwa kwake embe kuna mashiko mengine zaidi ya unasibu. Kwa nini ndizi isingeitwa embe na embe likaitwa ndizi, ikiwa kulikuwa na mpangilio maalumu wa kimaana katika kutoa majina kwenye lugha?
Nataka nisogee mbele kidogo ya mfano huu wa ’embe’. Katika Kiswahili, tuna kundi maarufu linaoitwa YU-A-WA, ambalo tunaambiwa kuwa huchukua majina yote ya watu, wanyama, ndege, samaki, wadudu – kwa ujumla vyote vyenye uhai visivyokuwa miti na mimea. Mtazamo wa kimapokeo uliliita kundi hili la maneno kuwa ni ngeli ya MTU-WATU, yumkini kwa sababu hiyo hiyo ya kuwa ndani yake munapatikana watu – kama sehemu ya hivyo viumbe vyenye uhai.
Hata hivyo, unasibu kwenye kundi hili la maneno ni wa kustaajabisha zaidi ya makundi mengine yote. Tuangalie mfano wa umoja na wingi: katika hali ya kawaida, wingi huundwa kutokana na umoja kwa kuongeza hicho kipashio cha wa- kutoka m- kama ilivyo kwenye mtoto/watoto, mtu/watu, mzee/wazee. Hapa mtu angeliona uwiano na pengine kuhoji kwamba kanuni inayoongoza umoja kwenye wingi.
Bali vipi ikiwa umoja ni daktari, fundi, jaji – ambao wote huchukuwa wingi wa ma-, yaani daktari/madaktari, fundi/mafundi na jaji/majaji? Je, ni kwa kuwa haya ni majina yanayowakilisha kazi na sio mahusiano? Kama ni hivyo, mbona tunasema mwalimu/walimu na sio alimu/maalimu? Na ni vipi kuhusu shangazi/mashangazi lakini sio jomba/majomba?
Bado kuna unasibu mwengine kwenye kundi hili. Tunapounda sentensi, kwa mfano, zinazohusu aina moja ya umoja na wingi kwa maneno tafauti, tunatumia upatanisho tafauti wa kisarufi. Chukulia mfano wa maneno rafiki na jambazi, ambayo yote yangekuwa na wingi wa ma-, yaani rafiki/marafiki (natambua kuwa pia wingi unaweza kuwa rafiki) na jambazi/majambazi. Tunapoyaweka maneno haya kwenye sentensi, tutapata mifano hii:
i. Rafiki yangu ameondoka na fedha zote/Marafiki zangu wameondoka na fedha zote
ii. Jambazi limeondoka na fedha zote/Majambazi yameondoka na fedha zote
Nataraji umeuona huo unasibu hapo. Kwa nini hatukusema “Rafiki yangu limeondoka…./Marafiki yangu yameondoka…..? Je, ni kwa sababu jambazi/majambazi ina maana mbaya na rafiki ina maana nzuri? Lakini pia, umeona unasibu wa namna ambavyo kwenye umoja wake ‘rafiki’ imehamishiwa kwenye kundi la I-ZI kwa kusema “Rafiki yangu…” na sio “Rafiki wangu…” kama vile ambavyo tungelisema hivyo kwa majina mengine yaliyomo kwenye kundi hili: mtoto wangu, daktari wangu, na kadhalika. Umeona pia ‘jambazi’ ilivyohamishiwa kwenye kundi la LI-YA kama vile ni tunda, jiwe, au dude.
Mswahili mwenyewe, ambaye kwake lugha ni matumizi na sio kanuni za kuzisoma vitabuni na chuoni, hapati tabu kuwapa walio kwenye kundi la YU-A-WA wingi wa MA- au WA-. Kwake ni unasibu unaosadifiana na kuogelea kwake kwenye lugha yake. Hata hahisi kwamba amefanya mabadiliko hayo. Kama wasemavyo Wajapani: “Samaki huwa hajijui kuwa ameroa”.
Kazi i kwa wasiokuwa wenyewe wenye Kiswahili chao.
du sawa ila. ninatka unasib wa lugha na maan ya unasibu