KISWAHILI KINA WENYEWE

Uhakiki wa Makuwadi wa Soko Huria

KITABU kinachohahikiwa hapa ni Makuadi wa Soko Huria ambacho kimeandikwa na Marehemu Profesa Chachage Chachage. Mchapishaji wa kitabu hiki chenye kurasa 287 ni E&D Limited   na amekipatia namba (ISBN): 9987 622 45 3 katika sekwensia ya vitabu duniani.

Utangulizi

Hii ni riwaya ya kihistoria yenye  ukweli unaodhihirika leo. Inatoa taswira ya mapambano ya Watanzania katika kujipatia uhuru na amani ya kweli.

Na Padri Privatus Karugendo
Na Padri Privatus Karugendo

Ni Mapambano dhidi ya ukoloni na baadaye  dhidi ya baadhi ya watu walioteka nyara uhuru wa wengi na kushirikiana na wageni kupora rasilimali ya nchi kwa kisingizio cha soko huria.

Hadithi inaweka bayana uozo na udhalimu uliojificha katika mfumo wa soko huria: tamaa na pesa na nguvu za kiuchumi, ubinafsi na ukandamizaji.

Pia ni hadithi ya matumaini.  Inatuonyesha jinsi watu wasivyokubali kukandamizwa na wasivyokata tamaa.

Makuadi wa Soko Huria inatukumbusha kwamba utu wa binadamu hauvunjwi kwa pesa wala kwa mabavu.

Tunayoyashuhudia leo hii ya kutoa ardhi yetu kwa wageni ili walime mashamba makubwa na kuwakaribisha wachimbaji wa madini na gesi huku tukitangaza kwamba Watanzania hawana uwezo wa kuwekeza labda kwa kutengeneza togwa, yalitabiriwa kwenye kitabu hiki cha Makuadi wa Soko Huria.

Hata wale waliomchukia mwandishi na kumshambulia kwa kusema uongo na kuwa mzushi, ndio hao sasa wamejionyesha waziwazi kuwa ni makuadi au watumwa wa soko huria, watumwa wa ubepari na mataifa ya ya Ulaya na Amerika.

Mwandishi wa riwaya hii ni Profesa Chachage, Mungu amulaze mahali pema peponi! Mbali na riwaya hii ya Makuadi wa Soko Huria, alishaandika riwaya nyingine tatu ambazo ni Sudi ya Yohana, Kivuli na Almasi za Bandia.

Hata yeye mwenyewe aliona tofauti kati ya riwaya hii na zile nyingine anaposema kwenye riwaya hii kwamba: “Kuna kitu kimoja ambacho ni dhahiri katika masimulizi ya riwaya hii. Tofauti na riwaya za awali, yaani Sudi ya Yohana na Kivuli, matukio mengi ya kihistoria yaliyomo humu yalitokea na kuna watu muhimu wa kihistoria ambao hawakuepukika katika masimulizi haya…”

Hivyo hii ni riwaya iliyofanyiwa utafiti. Ni riwaya inayozungumza! Ni riwaya inayoyagusa maisha ya Mtanzania. Ni riwaya ya kutufumbua macho na kusimama kutetea haki na uhuru wa  taifa letu.

Kutetea utajiri wa taifa letu na kuhakikisha sote tunashiriki utajiri huu na kushirikiana kupambana na kupigana na vibaraka hadi dakika ya mwisho.

Pamoja na ukweli kwamba hii ni riwaya, lakini imeandikwa  kwa aina yake kiasi kwamba inaonyesha hali halisi na mtu anapoisoma ni kama anaiona kabisa filamu ya matukio yote.

Kusema ukweli ni riwaya ya aina yake. Kwa kuishangaa riwaya yake mwenyewe, mwandishi anasema hivi: “Kuna hadithi ambazo mwandishi huziandika kwa nia ya kufungua fundo ambalo si ajabu hata yeye mwenyewe hajui inabainisha kitu gani.

“Hivyo ndivyo ilivyokuwa katika majaribio yangu ya kuandika hadithi siku zote. Nilijaribu sanaa ya uchoraji, ikamezwa na matarajio ya kijamii yaliyonilazimisha kufanya vitu vingine maishani.

“Ushairi nao haukuweza kukidhi matarajio ya kile nisichokijua lakini nilichotarajia. Hivyo, nikajikuta katika hii miaka ishirini nikijitumbukiza katika uandishi wa riwaya.”

Tunavyosema daima kwamba kilichoandikwa kimeandikwa. Kana kwamba Profesa Chachage, alitaka kutuachia wosia, baada ya kuandika riwaya hii iliyotukuka ambayo aliandika kwa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kabarage Nyerere, hakuishi zaidi naye akaenda kule kujiunga na Mwalimu na wahenga waliogangulia.

Utumwa wa kisasa ni utumwa kuliko ule wa kuuzwa sokoni. Walikuuza sokoni wakati ule, lakini sasa hivi wenyewe tunajipeleka kwenye Soko Huria, tukijidanganya kwamba sasa tunaishi kwa utandawazi ambao mwandishi wa kitabu hiki aliubatiza Utandawizi.

Wale waliomfahamu, wanafunzi wake aliowafundisha, marafiki zake waliofundisha pamoja, ndugu jamaa na marafiki walimfahamu Chachage kwamba msimamo wake uliuwa wazi na siku zote aliuonyesha.

Alitaka ukombozi wa mtu mweusi, kujikomboa katika nyanja zote, utamaduni, lugha, uchumi na kujitawala.

Kwa wale ambao hawakupata bahati ya kumfahamu Profesa Chachage, wanafaidi mengi kwenye kitabu chake; mbali na misimamo yake ya kimapinduzi, bado unyenyekevu wake ulikuwa wa juu sana.

Tunamsikia anavyosema kwenye kitabu chake kwenye utangulizi: “Kuna wakati nilikata tamaa kabisa ya kuandika tena.  Lakini kuna watu wawili ambao wamekuwa wakinisukuma na kunipa moyo kwamba inabidi niendelee kuandika, kwani hakuna ainisho jingine la uhai wetu zaidi ya ukweli unaopatikana katika kuwasiliana.

“Kwa sababu hiyo basi,  namtunuku riwaya hii Demere Kitunga. Labda angestahili jema zaidi ya tunuku hii. Lakini sina zaidi na hili. Pili, napenda kumtunuku Elieshi Lema. Yeye ni mwepesi kumfanya mtu aote hata yasiyooteka. Kama si hawa wawili, labda nisingekaa na kuandika tena.”

Ni wazi kwa sote tunaokisoma kitabu ni muhimu kuwashukuru hawa wawili, maana kwa kumtia moyo mwandishi, sasa tuna kitu cha kujivunia katika uandishi wa Tanzania.

Demere Kitunga, ndiye alikuwa mke wa Profesa Chachage na Elieshi,  rafiki wa karibu na mchapishaji wa kitabu hiki.

Mazingira yanayokizunguka kitabu

Taifa letu lilikuwa likipita kwenye kipindi cha mpito. Tulikuwa tumelizika Azimio la Arusha na kufungua milango kwa soko huria na ubinafsishaji. Mashamba yetu makubwa yakabinafsishwa, viwanda navyo vikabinafsishwa.

Tukaanza kuongea lugha ya ubia na wawekezaji. Ndipo ukazuka upepo wa utandawazi. Watu wakaanza kuamini kwamba sasa dunia ni kijiji kimoja na hatuwezi kuishi nje ya kijiji hiki. Baadhi ya Watanzania wakaanza kuutukuza kwa nguvu zote utandawazi na ikafikia kuwaona washamba wale ambao walikuwa wanakwenda pole pole na kuwa na shaka na msamiati huu mpya.

Utandawazi ukawa msamiati wa wasomi na watu wa vijiweni, wengine wakawa hawafahamu wasemacho, kila kitu kigeni kikawa utandawazi.

Ubepari, ubeberu na ukoloni tulivyovikataa miaka ya 1960 na 1970, vikarudi kwa nguvu zote kwa mlango wa utandawazi. Hata wasomi wakachanganyikiwa, wakifikri kwamba Utandawazi ni kitu kipya na chenye manufaa makubwa. Ukapita ushawishi mkubwa wa kuachia ardhi yetu, madini yetu na mazao yetu kama tiketi ya kuingia kwenye Kijiji cha Utandawazi.

Wasomi wakalipwa fedha nyingi na wawekezaji kufanya utafiti na kuwatengenezea njia ya kuingia kwenye nyanja mbalimbali, kwenye biashara na maeneo muhimu ya kuwekeza. Hata na mashirika ya kijamii yakajikuta njia panda yakipata fedha za wafadhili, kwa lengo la kusaidia maendeleo kwa masharti ya kukubali utandawazi wenye kuja na kampuni kubwa za kuwekeza kwenye madini, kilimo na uvuvi.

Profesa Chachage, kabla ya kuandika Makuadi wa Soko Huria, akiwa kwenye semina, alibadilisha msamiati wa utandawazi na kuuita utandawizi, kwamba huu ni ubeberu  na ukoloni mamboleo.

Baada ya kubadilisha maana ya neno hili ambalo lilikuwa linashika kasi kila kona ya taifa letu, watu walipokea mabadiliko haya kwa shangwe kubwa na kuanza kuimba: “Utandawizi”. Hivyo kwa upande wa Profesa Chachage ulikuwa ni mtihani mkubwa wa kuliwekea minofu jambo hili la “Utandawizi”.

Hivyo alitaka kutetea msamiati huu wa utandawizi kwa kuonyesha jinsi utandawazi unavyoendeleza wizi kwa kutunga hadithi ya Makuadi wa Soko Huria. Hivyo alianza kufanya utafiti mkubwa juu ya kitu hiki ili aweze kuwashawishi watu kwamba utandawazi ni utandawizi.

Kwa bahati nzuri au mbaya, mwaka 1996, alipata kazi ya ushauri elekezi kutoka kwa Shirika la Uvuvi ili kuangalia athari zinazoweza kujitokeza kwenye mazingira kwa kuendesha mradi wa uvuvi.

Hivyo alienda Rufiji Delta kufanya utafiti juu ya ufugaji wa kamba. Wale waliompatia kazi ile, walimtaka aandike uongo kwenye matokeo ya utafiti wake. Walitaka kufuga kamba, walishaonyesha jinsi mradi huo ulivyo na fedha nyingi; na kusema kweli ni mradi wenye fedha nyingi, kwa kufuga kamba, kuwavuna na kuwauza nchi za nje.

Kuna soko kubwa na kweli mradi huu ungetengeneza fedha nyingi. Lakini kwa vile Profesa Chachage aliona mradi ule haukuwa na tija kwa wananchi na mazingira yao, aliamua kuandika ukweli. Baadhi ya watu waliokuwa wanategemea faida kutokana na mradi huu, viongozi wa serikali waliotegemea kunufaika kutokana na hongo ya wawekezaji wa mradi huu, walichukia sana juu ya utafiti wa Profesa Chachage.

Profesa Chachage, hakutanguliza maslahi yake, bali aliliangalia taifa la Tanzania. Aliangalia maisha ya watu wa Rufiji Delta. Hivyo akaamua kutoa ukweli kwamba mradi huo haukuwa na tija kwa watu na mazingira.

Kama ungekubalika, basi watu wangepata hasara kubwa na mikoko yote ingefyekwa. Wawekezaji wangefuga kamba, kuvuna na kuondoka wakiacha nyuma yao ardhi isiyokuwa na faida tena kwa wananchi wanaozunguka delta hiyo. Hakupenda kuwasaliti Watanzania, hakupenda kuwa kuadi wa wawekezaji, akaamua kuwa mzalendo.

Baada ya kuona mambo machafu yaliyo kwenye mradi huo wa kamba, Profesa Chachage aliamua kufanya utafiti wake mwenyewe kwenye maeneo hayo, yanayojitokeza kwenye hadithi.

Hivyo alianza utafiti mwaka 1996 na mwaka 1999 akaanza kazi ya kuandika na kumalizia kazi mwaka 2000. Kwa vile alipoanza kuandika ndipo Mwalimu Nyerere, alikuwa hospitali na hatimaye kuaga dunia, akaamua kukiandika kitabu hiki kwa kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (1922-1999). Hivyo ingawa hii ni riwaya ya kubuni, lakini inaongelea matukio halisi na watu wa ukweli, ingawa mwandishi amebadilisha majina yao, lakini wote ni watu na wapo.

Muhtasari wa Kitabu

Kitabu kimegawanyika katika sura kamili 12, lakini  sura hizi zimetanguliwa na sura iitwayo Kifungua pazia na kuhitimishwa na sura Kifunga pazia. Tunaweza kusema kitabu hiki kina sura kumi na nne.

Kitabu hiki ni riwaya ya kihistoria yenye ukweli unaojionyesha leo hii. Inaonyesha mapambano ya Watanzania kujipatia uhuru na baadaye uhuru huu unatekwa nyara na baadhi ya watu ambao kwa kushirikiana na wageni wanapora rasilimali za nchi kwa kisingizio cha soko huria.

TANBIHI: Uhakiki huu umeandikwa na Padri Privatus Karugendo na kuchapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Tanzania Daima la Dar es Salaam. 

1 thought on “Uhakiki wa Makuwadi wa Soko Huria”

  1. Hivi haiwezekani kuchambua kazi ya kifasihi kwa kuzingatia nadharia jaman. Elimu ya sasa hv in nadharia sio fani na maudhui tens kama zamani

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.