Ushairi ni mchezo. Mchezo wa maneno na hisia za watu. Katika makala haya nataka nieleze machache kuhusu tungo za Mzee Haji Gora Haji anayejulikana pia kwa jina la ‘Mzee Kimbunga’ kutokana na jina la kitabu chake kilichopigwa chapa na kutolewa 1994. Nataka kutoa mifano michache ya sitiari anazozitumia, vipi zinavyohusiana na ‘fikra kuu hiyo inayoshikiliwa na kusisitizwa’ na yeye mwenyewe anatambulika kama mtu gani.
Utungo ufuatao, Jiwe Linasitawi, ameutunga mnamo mwaka 1997:
Na jiwe linasitawi, panapo matumaini
Jiwe lisilositawi, lisiloko aridhini
Ah jiwe husitawi, hilo siyo jambo geniMauwaye yana rangi, tena nyingi naamini
Ni kama mwezi sipingi, humwirika mawinguni
Kama macho hizo rangi, ni yako wangu mwendaniNi macho yenye madaha, kama fikira Moroni
Huingiwa na furaha, ukiwepo muhisani
Ulipo huona raha, kuhisi niko peponiRangi nyingi za mawimbi, yazukayo baharini
Hwenda na kutowa vumbi, kwa upeo wa machoni
Mpenzi kwako sitambi, sijiwezi taabaniAh! jamani linastawi jiwe, bali ajabu sioni
Lasitawi mno jiwe, husitawishwa na nini
Lisilositawi jiwe, nini wake mtihaniLinanukiya upepo, unapasuwa puwani
Miliyo yale ilipo, yapenya masikiyoni
Maisha kimojawapo, kila siku furahaniKama kokwa za fenesi, zinapochomwa jikoni
Ghasiya huja upesi, na kufika mitaani
Kuona hata kuhisi, ni uhuru duniyaniYavutiya vipepeo, vyenye kuruka angani
Rangi nyingi zilo kwao, zinopendeza machoni
Zaghilibu rangi zao, si kwa nani wala naniNdivyo linavyositawi, asiyejuwa ni nani
Lisiloweza sitawi, marejeyo sikiyeni
Ni huwa au haiwi, ilivyo nitajieni
Kwa hakika utungo huo aliotunga Mzee Haji katika bahari ya nyimbo unaonyesha hasa sio ubingwa wake tu, lakini pia mtindo wake na sauti yake Nyimbo hii inatambulika kuwa imetungwa na Mzee Haji kwa sababu ya sitiari anayotumia yenye kiini cha mambo mawili kuhalifiana. Maana jiwe gani linaweza likastawi?
Arudhi ya nyimbo hii, mpigo wake, mdundo wake, mizani na vituo vyake pamoja na vina – hayo yote, jinsi alivyotumia, yanaonyesha kuwa hiyo ndiyo kazi yake Mzee Haji.
Sitiari nyengine anazoweka ni zile zinazotokana na mazingira yake huko Visiwani: mna mawingu na anga, mawimbi na bahmi; kuna vumbi na upepo, mwezi na dunia, jikoni na mitaani; kuna madakha na ghilibu; matumaini na mtihani na maisha.
Haji Gora Haji ni mtu wa kisiwa cha Tumbatu, kaskazini magharibi karibu na Unguja. Tumbatu ina magofu ambayo, pamoja na Unguja Ukuu, ni ya zamani kuliko popote pengine huko Zanzibar, yaani ya karne ya tisa. Ingawa lahaja za Kitumbatu na Kimakunduchi zinahitilafiana, kuna wasomi waliozianisha pamoja katika kikundi cha lahaja za kusini.
Kwa vile Mzee Haji ni Mtumbatu, anatunga kwa Kitumbatu vile vile. Kwa mfano utungo huo “Jiwe Linasitawi” aliutunga katika umbo la shairi kwa Kitumbatu ufuatavyo:
Bwe bila wasi hufana, hufimisha tegemezi
Huwanda hata kugina, ukalyona lijiezi
Bwe halidumbu fana, pasipo mchinjigizi
Hutaka tendelekezi, jibwe ndipo likafanaRangi zakwe za mayuwa, si haba vezo pendezi
Ja mwezi unaoyawa. ukamwilika arizi
Hamba macho rangi huwa, jayako weye mpezi
Huburudika mtima, tondole yangu hakonaMacho yano madaha, ja ya mtima simazi
Huzangiwa ni furaha, hazicheleza pumuzi
Ukawapo hona raha, mrembo mwenye mapozi
Huburudika mtima, tondole yangu hakonaRangi nyingi za mawimbi, yazukayo kibayazi
Bahari inayo dumbi, kwa kusi na kaskazi
Vikubwa vyakwe vitimbi, kingine sifananizi
Kwa upeo usokoma, yanavyozuka kwayonaAhi jamani hufima, tambuyani watambuzi
Hufima mno hukona, kipata naliezi
Bwe velyo lisipofana, huwa lina kizuwizi
Huviya penye nakama, vepo halidumbu fanaUpepo linanukiya, puyani rihi ya fazi
Miliyo yakwe yaliya, mashikiyo kuyahizi
Maisha linaliliya, yasiwe na bumbuwazi
Huviya penye nakama, vepo halidumbu fimaHamba kongwa za fenesi, zikokwa hazitikizi
Hasia huja upesi, wengine kwasana razi
Kona mpaka kuhisi, uhuru wa uwamuzi
Huviya penye nakama, vepo haidumbu fimaZavutiya vitunguja, virukavyo hata pazi
Rangi kwao zizokuja, vezo nacho kivutizi
Zahilibu kula mja, simwana wala mvyazi
Hungiwa ni bumbuwazi, rangi hizo ukazona
Wasifu wa Mzee Gora
Haji Gora Haji amezaliwa mwaka 1933 kijiji cha Kokoni huko kisiwa cha Tumbatu. Alipokuwa na umri wa miaka mitano tu akachukuliwa na kukulia huko Mkunazini, mtaa wa kati kati ya Zanzibar Mjini.
Hapo mjini alikuwa akisoma dini chuoni, lakini hakupata nafasi kwenda skuli ya serikali maana ilimbidi aanze kufanya kazi akiwa bado mdogo. Akafundishwa na mjomba wake, Haji Mjumbe, uvuvi wa nyavu na baadaye baba yake mdogo, Pandu Haji, alimpa ujuzi wa uvuvi wa madema.
Baba yake alikuwa baharia hodari na nahodha wa majahazi yaliyopitia mwambao wote wa Afiika ya Mashariki. Naye Haji Gora mwenyewe tangu alipoanza kuvua, maisha yake yote hadi sasa yamehusiana na bahari akiwa mvuvi, baharia, mpagazi na mchukuzi bandarini, msafirishaji wa karafuu na mwajiriwa wa kampuni ya Kichina huko Tanga aliyoitafutia majongoo ya ufukweni.
Alipokuwa na miaka 16 alijiunga na kikundi cha vijana kilichojiita ‘Ujinga Mewing’ huko Tumbatu na kuanza kujihusisha na ngoma. Kama desturi ngoma za aina hii, hushindana kwa kutungiana mashairi na kuyaimba hadharani, kulumbana na kujibizana.
Fumbo la Kimbunga
Sifa ya tungo za Haji Gora siyo katika umbo tu la upinzani, yaani kujibizana na kuhitilafiana, pia maudhui yake yameelezwa kwa taswira zinazohalifiana. Mwenyewe amesema kuwa mtindo huu “si mbinu wala hekima’, lakini ni siri ndani ya siri’. Kwani ndicho Kimbunga gani kinachoangamiza kila chenye nguvu na kukiachilia kila chenye udhaifu?
Kimbunga mji wa Siyu, kilichowahi kufika
Si kwa yule wala huyu, ilikuwa patashika
Kimeing’owa mibuyu, minazi kunusurika
Nyoyo zilifadhaikaYalizuka majabali, yakibirukabiruka
Zikadidimia meli, ngarawa zikaokoka
Kimbunga hicho kikali, mavumbi hayakuruka
Nyoyo zilifadhaikaNyumba kubwa za ghorofa, siku hiyo zimeruka
Zikenenda kwa masafa, kufikia kwa kufika
Vibanda vyao malofa, vyote vikasalimika
Nyoyo zilifadhaikaChura kakausha mto, maji yakamalizika
Pwani kulikuwa moto, mawimbi yaliyowaka
Usufi nusu kipeto, rikwama limevunjika
Nyoyo zilifadhaikaKuna kikongwe ajuza, viumbe kimewateka
Hicho kina miujiza, kila rangi hugeuka
Watakaokiendekeza, hilaki zitawafika
Nyoyo zikafadhaika
Vipi meli zikadidimia na ngarawa kuokoka, nyumba za ghorofa zikaruka na vibanda kusalimika? Sitiari yake ya Kimbunga ina utata mkubwa, ni fumbo hasa. Je, hicho Kimbunga ni sitiari inayotoa picha ya mtu wa tabia fulani, au kinawakilisha mabadiliko ya ghafla katika jamii ambayo watu wenyewe walikuwa wameathirika kwa namna mbalimbali.
Lakini kilikusudia ‘si kwa yule wala huyu’ mji wa Siyu, kilichowahi kufika, mji ambao hadi siku hizi una jina kwa sababu ya ushujaa wake katika ukinzani wake, pamoja na Waoromo na Wasomali, dhidi ya utawala wa kigeni, yaani wa Kireno na hasa wa Kiomani.
‘Kimbunga’ mwenziwe ‘Maleleji’?
Je, Kimbunga ni hayo mabadaliko ya ghafla ya mwaka 1964 ambayo watu wameyaita ‘mapinduzi’. Na nini hasa kimepinduliwa? Na ikiwa ni hivyo, huu upepo wa ‘malaleji‘ katika shairi la Shuwari alilotunga Haji Gora baadaye unawakilisha mabadiliko gani?
Shuwari ya malaleji, imeshangaza wahenga
Kimya wake uvumaji, tafauti na kimbunga
Lakini popotoaji, sitambuwi zake kunga
lporomosha milima, kugeuza tambarareIlizuka aridhini, kuzagaa kwenye anga
Ushabihi wa tofimi, kila kimoja kugonga
Sinini wala sinini, hakuna kisichotinga
lporomosha milima, kugeuza tambarareHaipulizi vuvuvu, jakusi na mwanashanga
Bali chake kinyamavu, sio mzaha naronga
Kimeleta uokovu, nakupeperusha janga
lpomomosha milima, kugeuza tambarareKwa kote ilifirimba, pwani na kwenye viunga
lkavugika myamba, na mawe yakawa unga
Utahisi kama kwamba, kilobomowa mizinga
lporomosha milima, kugeuza tambarare
Malaleji (au ‘maleleji’) ni upepo unaobadilikabadilika, hasa katika miezi ya Aprili na Novemba, lakini kamusi ya kibaharia ya Prins inaeleza kuwa huko Tumbatau unavuma mwezi wa Juni pia. Ni majira ya upepo shwari ambao hujui unatoka sehemu gani. Hata hivyo ‘iporomosha milima, kugeuza tambarare’ inawezekana ni mtu mkimya mwenye nguvu nyingi za kuweza kuwashawishi watu wengi.
Lakini ikiwa kimbunga ni sitiari ya mabadaliko ya kijamii, kwa nini maleleji isiwe hayo. Mabadiliko tangu mwaka 1985 huko Zanzibar, wakati wa vyama vingi na kulegezwa kwa masharti ya kiuchumi, kulipa soko uhuru fulani, mabadiliko hayo yote yalikuwa yakienda shwari na upepo huu haukuvuma ‘vuvuvu’.
Fikra kuu ya Mzee Haji, dhana anayoshikilia na kusisitiza kila mara ni kupinda na kupindua, kuweka sambamba vitu viwili vinavyogongana na kushindana, kuweka juu chini na chini juu, kuonesha matukio yatukiayo kinyume na matarajio.
Alivyosema, ‘ni siri ndani ya siri’, yaani kimbunga kinavunja yaliyo makubwa, lakini yaliyo madogo hayavunjwi nacho, kumbe malaleji ambayo ni kinyume cha kimbunga, imefika kote na kubomoa kila kitu, hata hivyo imeleta usalama
Baada ya Kimbunga na Shuwari ilikuja Mkasa Namba Mbili:
Kuna kinyozi ambae, kunyowa kiendeleya
Kilofanya nishangae, anyolewae aliya
Hata na kinyozi nae, hajimudu kwa kuliya
Wote wanacholiliya, wala hakijulikaniHawataki kueleza, kilichowafikiliya
Kama utawauliza, kama kwamba wachocheya
Sauti zao hupaza, huzuni kuashiriya
Bali wanacholiliya, wala hakijulikaniPengine yaweza kuwa, kwa ninavyofikiriya
Ambae ananyolewa, labuda anaumiya
Kinyozi anaenyowa, kwa nini mbona aliya
Bali wanacholiliya, wala hakijulikaniHiki ni kitandawili, kinachowategemeya
Wateguzi mbali mbali, jawabu kukipatiya
Nimeifunga kufuli, wafunguzi nangojeya
Kipi kinachowaliza, haraka nitajiyeni
Ajabu kubwa tena mtu mmoja anaumia akinyolewa, lakini anayemnyoa anaumia vivyo hivyo ‘Bali wanacholiliya, wala halijulikani’.
Hatumo tena katika historia, tumefika kwenye siku za Ieo hii hii. Mtu wa tatu anapowakuta watu wawili wakilia katika hali kama hiyo, bila sababu kujulikana, atajaribu kuwapatanisha. Basi inavyosemekana na kutangazwa Maridhiano ya Wazanzibari yamefikiwa karibuni tu.
Taswiria na uhalisia kwenye kazi za Haji Gora
Tungo nyingi za Haji Gora Haji zinaeleza hali ilivyo: hali ya jamii, ya watu, ya historia, kwa kutumia sitiara zinazogongana, kuhalifiana na kuhitilafiana. Ndilo jambo na kinyume chake
Taswira anazotumia zinamfanya msomaji anamtambua kama ni mtu anayejijua nafsi yake. Kwa urahisi anatambulika kama mtu wa pwani, Mtumbatu, Mswahili. Huenda msimamo wake umefichika, hutokea msimamo wake u wazi kabisa kama ulivyo katika mfano huo wa mwisho.
Waswahili husema: ‘kutoa ni moyo’. Kinyume chake ni kunyang’ anya au kupokonya Muyaka bin Haji el-Ghassany ameshughulikia suala hilo katika shairi la Kupewa:
Semani nawapulika, siyo sambe kwamba sivi
Siwi cha mfunda koka, muawa na wavuvi
Unipile sikupoka, sikunyang’anya kwa wivi
Nawauliza wakorofi, mnashika nt’a gani’Nyang’anya hukunyang’anya na kuiba hukuiba
Daima wat’u hufanya kupana vit’u kwa huba
Hilo mimi sikukanya na yangakwisha mahaba
Kupawa ndiyo taliba, kilicho changu mudani
Naye Haji Gora Haji ameendeleza fikra hiyo na kuonesha imani yake katika shairi lake‘Mpewa hapokonyeki’, ambalo limeimbwa na kikundi cha Culture Musical Club na kunaswa sauti kwenye CD yao ya Kidumbaki:
Aliyepewa kapewa, naapa hapokonyeki
Kwa alichojaaliwa, Wallahi hapunguzuki
Ukimlilia ngowa, unajipatisha dhiki
Mpewa hapokonyeki, aliyepewa kapewa
Wewe ukifanya chuki, bure unajisumbuwaMola ndiye atowae, akawapa mahuluki
Humpa amtakae ambaye humbariki
Na kila amnyimae, kupata hatodirikiWa tisa humpa tisa, wa moja haongezeki
Alomnyima kabisa, hata akitaharuki
Atabaki na kunasa, atakwama hanasukiMola hutowa hidaya, tafauti na riziki
Kwa anomtunukiya, huwa ndiyo yake haki
Na asiye mtakiya, huwa si yake laiki.
Tanbihi: Makala hii ambayo kwa mara ya mwanzo ilichapishwa kwa jina la “Tungo za Bwana Kimbunga: Haji Gora Haji” imeandikwa na mtaalamu wa lugha ya Kiswahili mzaliwa wa Uholanzi, PROFESA RIDDER H. SAMSOM, kuelezea kazi za kifasihi za gwiji wa sanaa ya ushairi katika zama hizi visiwani Zanzibar, Haji Gora Haji. Tumeichapisha tena hapa ikiwa imehaririwa kidogo kuakisi wakati wa sasa.