UCHAMBUZI

‘Karamu’ ya Jumba Maro na chaguzi barani Afrika

Kwa vile Jumba Maro si riwaya yenye hadithi moja refu, bali mkusanyiko wa hadithi nyingi fupi fupi, tutachambua moja tu kati ya hadithi 12 zilizomo, tukiamini kuwa itatusaidia kuuona undani wa ‘Jumba’ lote.   Hadithi iliyopewa jina la Karamu, kama zilivyo nyingine, inaanza na ushairi uitwao ‘Mjumbe Kaemewa’.

Ushairi huu unasimulia masaibu yaliyompata mjumbe aliyetumia kalamu yake kuandika mambo ya kweli ili  watu wake waelewe kile hasa kilichotokea.   Lakini kumbe hakujua kwa kufanya hivyo alikuwa anakosana na wakubwa. Matokeo yake ni kwamba mjumbe huyu aliadhibiwa kwa kuwekwa jela na kukatwa kidomodomo chake.

Katika miaka ya mwanzoni mwa 2000, Zanzibar kulikuwa na mjumbe kama huyu ambaye naye aliamini kuwa kwa kuandika ukweli, alikuwa anaisaidia jamii yake kufahamu mambo na hivyo kuifanya isimamie ukweli siku zote. Lakini naye pia alikuwa anawakera wakubwa. Matokeo yake yakawa ni yaleyale ya mjumbe wa Jumba Maro.

Huyo alikuwa ni gazeti la Dira, ambalo lilijitolea kuandika na kuchambua masuala mbali mbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yaliyohusu khatima ya Zanzibar. Lakini nalo likaandamwa hadi likafungiwa moja kwa moja na serikali, huku mhariri wake mkuu, Marehemu Ali Nabwa, akigeuzwa mkimbizi kwa kutangazwa si raia katika nchi ya mababu na mabibi zake. Mjumbe kaemewa.

Kitendawili cha Nyoka

Baada ya ushairi huo kuifungua hadithi, mwandishi ameanza kwa kitendawili cha kuingia nyoka katika chumba cha Bwan’ Tajir, ambacho kwa namna kilivyojengwa hakukuwa na uwezekano wowote wa nyoka huyo kufika huko. Kuingia kwa nyoka huyu kulimshtua sana Bwan’ Tajir kiasi ya kwamba alimtoa kazini nokoa wake mkuu kwa kuwa uchunguzi wa barza aliyoiunda kuchunguza mkasa wenyewe ulibaini kuwa nyoka aliingia kwa uzembe wa nokoa huyo.

Tafrani ya kuingia kwa nyoka katika chumba cha Bwan’ Tajir ndiyo inayotuunganisha na kiini cha hadithi yenyewe. Kwamba sio tu kuwa Bwan’ Tajir alikuwa akimuogopa nyoka huyu binafsi, lakini pia alikuwa amekusudia kupika karamu kubwa na kuwaalika watu wazima wote wa mji kuja kula kwake, katika kasri lake.

Kwa hivyo, kwa upande, mmoja kujitokeza kwa habari hii kungelisababisha watu wengi kusita kuja katika karamu hiyo kwa kukhofia usalama wao na, kwa upande, mwingine kujitokeza habari hii ingewapa watu picha halisi kwamba naye Bwan’ Tajir ni mwoga na kwake kunapenyeka,. Na fahari ya Bwan’ Tajir ni “kuwa watu wote kabisa washiriki katika karamu yake, wale wanywe fadhila zake” (uk. 92), bila ya kuushuku woga wake na ugoigoi wa himaya yake.

Hata hivyo, mwandishi anatuonesha kuwa Bwan’ Tajir si mtu wa fadhila kiasi hicho.  Kupitia nong’ono za watu, tunajifunza kuwa huyu ni mtu bakhili na mwenye tabia ya uchoyo mno kiasi cha kwamba “hutia ndizi na dagaa katika mifuko yake ya suruali ili asiombwe.” Swali ambalo watu walikuwa wakijiuliza ni vipi angeliweza kuwakirimu watu wa mji mzima?

Karamu yenyewe ya mji

Hatimaye, karamu inapikwa na kuliwa, lakini kama ilivyokhofiwa tangu mwanzo karamu hiyo ilikuwa na mapungufu mengi sana kiasi cha kwamba haikuwa halali hata kidogo kusema kuwa ilikuwa ‘karamu ya mji’. Wengi wa watu walikosa hata tonge moja ya biriani huku wachache wakiwa wamekula zaidi ya sahani moja. Na hata hao waliopata kula, wengi wao walikuwa ni watoto na sio watu wazima wa mji kama ilivyoahidiwa mwanzoni.

Hao watu wazima waliokoseshwa walikuwa wamekoseshwa katika mazingira ya kutatanisha na kusikitisha kabisa. Kwa mfano, mwandishi anatwambia kuwa kuna wengi waliokataliwa kuingia katika ukumbi wa dhifa kwa kuwa bawabu hakuzitambua kadi zao za mwaliko. Ati zilikuwa na rangi tafauti na kadi alizoagizwa kupokea.

Kuna wengine walikuwa na kadi zenye rangi sahihi, lakini walikataliwa kuingia kwa kuwa herufi za majina yao ni tafauti na wanavyoyatamka.   Mahala pamoja bawabu anamuuliza mwenye kadi: “Mbona umeniambia jina lako Ahmed na humu limeandikwa Ahmad?” Mwenye kadi anajitetea kuwa si yeye aliyeandika kadi hiyo, bali ni karani wa Bwan’ Tajir. Anasema kwamba hata yeye alimwambia na mapema karani huyo juu ya kukosewa  kwa herufi moja kwenye jina lake, lakini karani alimhakikishia Ahmed kuwa hapatokuwa na taabu yoyote ile: siku ya karamu, atakula tu. Lakini leo hii bawabu anamwambia Ahmed: “…hutaramba karamu….saa ya kutazama makosa imekwisha. Kazi yangu ni kutazama kadi sahihi. Asiyekuwa nayo haingii”. Na kweli Ahmed, na wenziwe wa mfano wake, hawakuruhusiwa kuingia kwenye ukumbi wa karamu. (uk. 93)

Kwa hali hii watu wazima wengi wa mji wakakosa kula karamu waliyoandaliwa. Ilikuwa kana kwamba huu ulikuwa ni mpango uliofanywa makusudi na Bwan’ Tajir na wasaidizi wake, maana hata watu hawa walipolalamika kuwa wamekoseshwa karamu, hakuna mwenye mamlaka aliyewasikiliza.

Hata Shawishi Mkuu, ambaye ndiye aliyekabidhiwa jukumu la uandazi, alipoambiwa kuhusu hilo, alisema haiwezekani kuwe na watu waliokosa chakula ilhali biriani huko ndani ilikuwa ya ‘kupigia mbwa’.

Watu walipomuapia kuwa wao hawajaramba kitu, aliwanuka viganja vyao. Alipoona ni kweli havinukii harufu yoyote ya machopochopo, akawaruka hapo hapo: “Waongo hawa. Wamekula kisha wakaenda kunawa na wanataka kudanganya kula mara mbili”. (uk. 94)

Masikini watu wazima wale, wakasawijika kwa kuambiwa kuwa wanazua ili wajilie mara mbili ilhali hata hiyo moja hawakuipata. Hivi ndivyo karamu ya Bwan’ Tajir ilivyoishia.

Karamu ya Jumba Maro na Chaguzi za Afrika

Baada ya kuangalia kilichomo kwenye ‘Karamu’ ya Jumba Maro, sasa tuirejeshe kazi hii ya kifasihi ‘watuni’, yaani kwa jamii ya Zanzibar, kwa uchache wake, na jamii nzima ya Kiafrika, kwa upana wake, ili kuzisaidia jamii kujisoma kupitia kazi hii ya mwandishi Ally Saleh. Maoni ya mhakiki huyu ni kwamba ‘Karamu’ inaakisi moja kwa moja chaguzi zetu katika mfumo wa vyama vingi visiwani Zanzibar, nchini Tanzania na eneo zima la Afrika, ambako bado demokrasia haijaimarika.

Pana mfanano mkubwa baina ya maandalizi, uendeshaji na matokeo ya chaguzi zetu ndani ya mfumo wa vyama vingi na karamu hii ya Bwan’ Tajir, ambaye ana khulka zile zile za serikali za vyama tawala vya baada ya uhuru barani Afrika.

Ule mkasa wa kuingia kwa nyoka katika chumba cha Bwan’ Tajir unawakilisha kipindi cha kuja kwa siasa za vyama vingi katika nchi hizo, ambazo zilijipenyeza bila ya ridhaa ya dhati ya watawala.

Siku zote watawala barani Afrika walikuwa wakiuogopa upinzani kwani unahatarisha maslahi yao ya kuwapo madarakani, kama vile Bwan’ Tajir anavyomuogopa nyoka kumfichulia aibu zake za woga na ugoigoi. Kwa hakika, katika baadhi ya misamiati ambayo ilikuwa ikitumika Zanzibar (ambako mwandishi na mhakiki wanatokea) kuwaita wapinzani miongo mingi baada ya Mapinduzi ya 1964 ni hilo la ‘nyoka.’

Kupitia mdomo wa Bwan’ Tajir, serikali ya chama tawala inamkaripia mtu inayedhani kuwa amechangia kurudi kwa nyoka, yaani vyama vingi: “Usiniambie mie habari ya (nyoka) kutoka wapi…mie nilikwambia naogopa nyoka. Nilikukabidhi kazi ya kuhakikisha nyoka sio tu hawaonekani, lakini pia wasikaribie nilipo”. (Uk. 91)

Ukweli ni kuwa, laiti serikali barani Afrika zingelikuwa na uwezo wa kuzuia vyama vingi visije, zingelifanya hivyo. Lakini kilichotokea ni kuwa wakati ulikuwa umeshafika, na hakuna ambaye angelikinzana na matakwa ya wakati, kama vile anavyosema Nokoa Mkuu, ambaye alituhumiwa na kuhukumiwa kwa kumruhusu nyoka kupita hadi chumbani kwa Bwan’ Tajir, kwamba: “Sina uwezo wa kuzuia kudra”. (uk. 91)

Wasemavyo wamalenga: “Muda na kudura hazina zisubirio”, ndivyo ambavyo wakati ulivyolazimisha kuja kwa vyama vingi hata kama wakubwa walikuwa hawavitaki. Kwa hivyo, nyoka (upinzani kupitia siasa za vyama vingi) hakuweza kuzuilika kuingia katika chumba cha Bwan’ Tajir (barani Afrika).

Watawala na mawakala wao katika vyombo vya habari, vyombo vya dola, taasisi za kijamii na kwengineko, hawakuwa na uwezo wa kuvizuia vyama vingi visirudi, kwa kuwa hayo yalikuwa ni matakwa ya wakati.

Wameshindwa kumzia ‘nyoka’ lakini wamebakia kwenye nyumba

Lakini ikiwa walishindwa na hicho, kuna chengine ambacho waliweza kukifanya: nacho ni kuandaa mikakati na mbinu za kuvizuia vyama hivi kuwaondoa wao madarakani. Mikakati na mbinu hizo inafumbatwa na mwandishi Ally Saleh kwenye fumbato moja la ‘Karamu’, ambayo inawakilisha chaguzi za magube na varange, ambazo zimekuwa zikifanyika kwenye mataifa mengi barani Afrika kwa takribani miongo miwili sasa, lakini kwa sehemu kubwa zikiwa zimeshindwa kuwaondoa watawala madarakani. Chaguzi zimekuwa njia ya watawala hao kujihalalishia kuendelea kubakia madarakani huku wakiudanganya ulimwengu kuwa na wao wana demokrasia ya vyama vingi.

Ndivyo ‘Karamu’ ilivyoandaliwa katika Jumba Maro. Bwan’ Tajir alimtafuta Shawishi Mkuu kuwa muandaaji na mpishi wake. Shawishi huyu akawa na jukumu moja tu: kwa upande mmoja, kuhakikisha kuwa watu wengi zaidi wenye haki ya kula karamu hiyo hawapati fursa na, kwa upande mwingine, wale wasio na haki hiyo, lakini ambao kula kwao kutakuwa kwa faida ya Bwan’ Tajir, wanaila kwa matonge na kwa kufuta sinia mbili mbili. Kwa ufupi, Shawishi Mkuu alikuwa na dhima ya kuifuja karamu.

Ndivyo ilivyo katika uhalisia. Kwamba katika kuandaa mazingira ya kuendelea kubakia madarakani, watawala wanawatafuta akina mashawishi wakuu na kuwafanya wawe na mamlaka ya kuandaa na kusimamia chaguzi ziitwazo za vyama vingi. Kwa maana nyengine ni kuwa watawala wanajiundia mitandao inayohawakikishia kuwepo kwao madarakani dumu daima, hata pale umma (watu wazima wa mji) utakapokuwa umeshawakataa.

Kwa mfano, hiki ndicho kinachofanyika hadi leo Zanzibar, ambako mtandao madhubuti wa masheha, vyombo vya dola na Tume ya Uchaguzi, unahakikisha kuwa Wazanzibari wengi wenye haki ya kupiga kura hawaandikishwi kuwa wapiga kura, kwa upande mmoja na, kwa upande mwingine, wale wasiokuwa na sifa, lakini ambao wanatumiwa kukipigia kura chama tawala wanaandikishwa ikibidi hata zaidi ya mara moja. (Rejea ripoti ya TEMCO/REDET: The Politics of the PVR, 2005)

Mkasa wa ‘Karamu’ ya Jumba Maro kuliwa na watoto wadogo huku watu wazima wakitazama macho tu, ndio mkasa wa kura za majimbo kadhaa ya Zanzibar ambako kura zinazoambiwa zimemchagua mgombea fulani hupigwa na watu wasiotimia umri huku washaotimia wakilia machozi.

Mkasa wa watu wachache kula sahani mbili mbili za biriani huku wengine wakienda miayo kwa njaa, ndiyo mkasa wa upigaji kura zaidi ya mara moja katika maeneo kadhaa ya Zanzibar, huku zaidi ya Wazanzibari 20,000 kila uchaguzi wakipingwa na masheha kuwa si wapigakura halali, maana masheha hao “hawawatambui kuwa wakaazi wa shehia“ zao. (Pitia ripoti ya National Democracy Institute-NDI, 2005).

Mkasa wa akina Ahmed kukataliwa kuingia kwenye chumba cha karamu kwa kuwa kadi yake imeandikwa Ahmad, ndio mkasa wa Wazanzibari wanaojikuta ama majina yao yameshapigiwa kura au wanaambiwa hawamo katika orodha ya wapiga kura katika siku yenyewe ya kupiga kura. (Rejea makala za Christian Science Monitor, 2005).

Hitimisho: ‘Karamu’ na Uchaguzi Mama mmoja Baba mmoja

Kwa hivyo, kwa kila hali, ‘Karamu’ ya Jumba Maro inafanana sana na chaguzi zetu ziitwazo za kidemokrasia. Ni njia ya akina Bwan’ Tajir kuutangazia ulimwengu kuwa na wao wana ukarimu wa kutosha wa kualika watu kuja kula katika makasri yao, lakini kumbe hawana uhodari huo. Kutoa na kujitolea kwataka moyo, na moyo huo akina Bwan’ Tajir (watawala wetu) hawanao.

Watawala wetu, kama alivyo Bwan’ Tajir, huomba pesa za kugharamikia chaguzi ati kuwapa raia fursa ya kuwaweka madarakani viongozi wawatakao, lakini kwa hakika huwa ni kwa kujionyesha tu.

Katika vyembe vya nafsi zao, watawala hawa huwa wameshajiwekea kabisa kwamba hawataondoka madarakani kwa vyovyote vile, ikibidi hata kwa kutumia mtutu wa bunduki, ili waendelee kusalia pale walipo.

Hufanya mbinu, visa na mikasa, alimradi tu utimu muradi wao. Ya chaguzi barani Afrika na ya Jumba Maro ni mama mmoja, baba mmoja.

3 thoughts on “‘Karamu’ ya Jumba Maro na chaguzi barani Afrika”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.