KISWAHILI KINA WENYEWE

Usione kwenda mbele kurudi nyuma si kazi

Kama ilivyo taswira ya ulimwengu, ndivyo ilivyo taswira ya maisha ya mwanaadamu anayeishi kwenye ulimwengu huo. Maisha nayo yana misimu kama ilivyo hali ya hewa: kama kulivyo na kaskazi na masika kwenye hali ya hewa, ndivyo kulivyo na hali ziwezazo kufananishwa na kaskazi na masika kwenye maisha ya mwanaadamu: ana siku zake za neema na kubarikiwa, ambapo riziki na satwa humiminika kwa mwanaadamu huyo mithali ya mvua za masika zimiminikavyo kutoka mawinguni na kuirutubisha ardhi.

Lakini pia kuna siku za ukame kwenye maisha ya mwanaadamu, maisha yake yakawa matupu na makavu kama vile jua la kiangazi liikaushavyo ardhi na kuzigeuza tope kuwa vumbi. Ndipo hapo unaposikia wengine wakimsema mwanaadamu huyo: “Kwani kuna tena Mohammed siku hizi: Hana hanani, akiulizwa haungami. Ukimpara yuatoka unga!” Kwa sisi Waswahili, tukisikia hivyo hujua kuwa mwenzetu sasa anapitia kwenye kaskazi za maisha yake.

Hiyo ndiyo hikima ya wahenga wa Kiswahili. Walikuwa na njia za kuyaeleza maisha ya mwanaadamu kwa maneno machache lakini mazito sana unapoyatia kwenye mizani. Kuna mkururo wa methali na misemo ya Kiswahili, ambayo inaelezea kubadilika kwa hali za maisha ya wanaadamu.

Miongoni mwazo, kuna zile zinazotuonya tunapokuwa kwenye kilele cha furaha, raha na pumbao, kwamba tusijisahau kuwa maisha yetu yana majira na miongo yake. Hizo ni kama ule msemo: “Mpanda ngazi hushuka!” ama “Aliye juu mngoje chini” au “Ajidhaniaye kasimama, natazame chini asianguke!”

Kuna ile ambayo inatusuta, baada ya kwamba tumeutumia vibaya muda na jaala yetu wakati wa neema na kuzipuuzia nasaha za hapo juu, kama ule wa “Kusudi hayambwi pole”.

Lakini kuna mingine ambayo haisuti wala haionyi, bali inaelezea tu ukweli wa mambo, kwamba maisha yanakwenda yakibadilika. Hiyo ni kama ule wa “Dunia rangi rangile”, “Dunia mti mkavu”, na hii ambayo leo nimeichagua kuwa kauli ya mada hii: “Usione kwenda mbele, kurudi nyuma si kazi!”

Naam, hata kwenye kilele cha mafanikio na kasi kubwa ya mwendo kwenye safari yetu ya maisha, hikima za Kiswahili zimetufunza kwamba hakuna lisilokuwa. Watu wa falsafa husema kwamba mafanikio ni makosefu yaliyogeuka, basi ndivyo ilivyo pia kwa makosefu kuwa mafanikio yaliyogeuka. Lolote laweza kuwa. Kupata na kukosa, yote ni majaaliwa!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.