Leo tuangalie ukweli mmoja kuhusu semi za Kiswahili – kuwa kwake kauli za hikima zinazojitegemea, kwa mintarafu ya kwamba kila kauli inajitosheleza kwenye muktadha wake na haina uhusiano wala utegemezi kwa kauli nyengine ya hikima. Kwa mfano msemo “La kuvunda halina ubani“ ni kauli ya kuvunja moyo na kusuta kwa upande wake, lakini inajitosheleza kwenye muktadha itakaotumika bila ya kujali msemo “Subira huvuta kheri!“ kwa upande mwengine.
Pale Mswahili anapokuwa amezimaliza jitihada zake zote kwa jambo fulani, akawa ameshavipenya vipenu na vipembe vyote vya jambo hilo, na mwisho wa siku jua likamtulia akiwa hana alilolifanikisha, basi hujifariji na au kufarijiwa na waliomzunguka kwamba “Hebu liwache tena hilo. Umeshajitahidi pa kujitahidi, lakini ndilo la kuvunda lilivyo, halina ubani!“
Mwengine, kwa kuwa Waswahili wanakulia na kukuzwa kwenye mazingira ya kumjua na kumtukuza Mungu, anaweza kusema “Jitihada haiondoshi kudura“, kwa maana ya la mja ni kujitahidi kutaka na kufanya jambo, lakini wa kulikadiria jambo hilo kuwa ni Mungu mwenyewe tu. Ukweli wa hikima iliyomo kwenye msemo huo, hata hivyo, haitegemei wala haiiharibu ile iliyomo kwenye msemo “Mgaagaa na upwa hali wali mkavu“ ama “Haba na haba hujaza kibaba!“
Ukweli huu kuhusu hikima za Kiswahili ndio unaosababisha Waswahili kuwa na shehena kwa shehena za kauli hizi, ambazo hata kama nyengine zinagongana zenyewe kwa wenyewe, bado hazimchanganyi Mswahili mwenyewe kuzitumia na kunufaika kwa busara zilizomo ndani yake.
Unajua kwa nini!? Kwa sababu semi – ikiwa moja ya tanzu za lugha – zipo kwa ajili ya kumtumikia mwanaadamu, na sio kwamba mwanaadamu yupo kuzitumikia. Lugha – kama vilivyo vyengine vyote kwenye manzili hii ya ulimwengu – ni miliki ya mwanaadamu. Mungu aliyaumba yote yaliyomo yaje yatutumikie na sio sisi kuyatumikia, basi kwa hivyo, mwanaadamu si mtumwa wala mmilikiwa wa lugha!
Basi itwae, ivae, iingie, ioge ukiiogelea upendavyo, utakavyo! Japokuwa nalo haliondoshi kuwa kila lugha ina wenyewe! Kiswahili nacho, kinao wenyewe, na ndio wenye satwa na jiha hiyo.