KISWAHILI KINA WENYEWE

Kata pua uunge wajihi

Maisha yana mafunzo mengi, kazi ni kwa mwanaadamu anayeishi maisha hayo kuyachukua mafunzo hayo na kuyatia njiani yakawa sehemu ya hayo maisha wenyewe. Moja ya mafunzo yaliyomo kwenye hikima za wahenga wetu wa Uswahilini ni huu msemo “Kata pua uunge wajihi”, ambao umebeba kurasa kwa kurasa za ilimu ndani yake.

Maisha yanatufunza kupitia msemo huu kwamba hiyari ni chache ulimwenguni, na zinapotokea zenyewe huwa si hiyari kwa mwanaadamu. Mara kadhaa kwenye maisha yetu hukabiliwa na hali ambapo hupaswa kuliharibu moja kwa kulitengeneza jengine.

Kazi kubwa, kama nilivyosema, ni kwa mwanaadamu kuchagua lipi la kuliharibu – au angalau la kuliwacha liharibike lenyewe – kwa minajili ya kulitengeneza jengine lililo muhimu zaidi. Hapa mfanano na mpishano upo baina ya hicho unachokizingatia kuwa muhimu zaidi (wajihi, uso) kwa kile unachoona kwamba kinaweza kutolewa sadaka ya kukatwa (pua).

Ni lipi uso na lipi pua, kwa mfano, katika muktadha wa mtu aliyekabiliwa na haja ya kusoma na kutunza familia yake, huku mkononi akiwa rasilimali haba zisizoweza kuyafanya yote kwa wakati mmoja? Kipi akitoe sadaka ili atimize kipi na kwa wakati upi? Huko ndiko kukata pua kwa kuunga wajihi.

Lakini si kila wakati mwanaadamu anaweza kuujua upi ni wajihi na ni ipi pua. Baadhi ya wakati kile anachokichukulia kuwa ni wajihi, yaani cha muhimu zaidi, huwa ndicho pua, yaani kisicho na umuhimu wa juu kwa wakati huo. Ndipo unapokuja msemo mwengine wenye hikima tele – “Fikiri ndipo utende”. Wachina wana msemo usemao “Pima mara 10 kata mara moja”, ambao sasa ni kanuni ya kiufundi. Na sio kupima mara moja na kukata mara 10.

Basi ni pale unapoweza kupima mara 10 kabla ya kuikata pua mara moja, ndipo unapoweza kunufaika na kitendo chako cha kujiumiza pamoja kwa kujijenga pengine. Lakini inageuka kuwa hasara isiyoweza kufidiwa, pale unapopima mara moja na kukata mara 10, maana hutabakia tu umeuharibu kabisa wajihi wako, bali unaweza hata kujikuta umekata mashavu, midomo, macho, kidevu na masikio.

Kata pua uunge wajihi lakini kwa kwanza kufikiri ndipo ukatenda.

2 thoughts on “Kata pua uunge wajihi”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.