Utamu wa lugha haumo kwenye kuizungumza tu kwa minajili ya mawasiliano, bali pia kuihisi haiba na mguso wake. Nakumbuka mwalimu wangu wa isimu aliwahi kuniambia: “Usiongee, ogelea” – kauli iliyonichukuwa muda mrefu kidogo kuielewa, hadi nilipomuomba anifumbulie fumbo lenyewe. Kwamba ukizungumza yahisi maneno yake mithali ya muogeleaji anavyoyahisi maji.
Leo tutie mguu kidogo kwenye bahari hii ya lugha, na ‘tuogelee’ na sio ‘tuongelee’ sehemu nyengine ya upekee wa Kiswahili; nayo ni kutumia kwake maneno yanayojirejea yayo kwa yayo. Maneno kama vile ‘haraka haraka’, ‘kidogo kidogo’, ‘kweli kweli’, ‘sawa sawa’, ‘pole pole’ na mengine kadhaa wa kadha, ndiyo ninayomaanisha hapa.
Swali ni kwamba, je Mswahili huwa anakusudia nini anapoyatumia maneno haya? Je, maana huwa ni moja kwa kila mrejeo wa maneno?
Jawabu la jumla jamala ni kwamba Mswahili hufanya hivyo kwa nia ya kuweka au kupunguza mkazo. Inawezekana ni kwa kupunguza, kuongeza, kulegeza au kusisitiza. Lakini la muhimu kuliko yote ni kwamba, matumizi ya maneno haya yanaongeza utamu wa lugha kando ya kushadidia maana yake.
Hata hivyo, kuna zaidi ya hilo: nalo ni ukweli kwamba – mara kadhaa – maneno haya yanayojirejea yayo kwa yayo, pindi yakiwa peke yake, maana yake huwa si ile iliyomo kwenye hali yake ya kujirejea. Nitafafanua. Mswahili anaposema, kwa mfano, “Nimemshika sawasawa” hukusudia kuwa amemshika barabara au madhubuti kabisa. ‘Sawasawa’ pia inamaanisha mfanano, kama vile tunaposema “Juma na Asha wako sawa sawa” kwa maana aidha ya umri, tabia, au jengine lolote lile tunalowananisha. Ndipo kwenye msingi wa maana hii, panapozaliwa kitenzi ‘sawazisha’, yaani ‘vifanye viwe sawa sawa’.
Lakini pindi likiwa peke yake, neno ‘sawa’ lina maana nyengine zaidi ya moja: miongoni mwao ni ‘sahihi’, ‘ndiyo’, ‘ndivyo’, ‘vyema’ kama katika mfano wa pale unapomfahamisha mtu kitu halafu ukamuuliza: “Sawa hapo!?” ukikusudia amekuelewa, naye akakujibu “sawa” akimaanisha ndiyo amekuelewa.
Waswahili wenyewe huenda mbali zaidi katika maneno haya yanayojirejea yenyewe kwa wenyewe. Sio tu hutumia vielezi kama hivi vya kwelikweli, sawasawa, kidogo kidogo kujenga maana wanayoikusudia, lakini pia hutumia nomino kupunguza au kuongeza msisitizo wao. Kwa mfano, unaweza kumsikia mtu akisema: “Baba siku hizi hatoki nje, ana homa homa”.
Hii ‘homa homa’ hapa ina maana tafauti kidogo na kama angekuwa na homa. Kuwa na homa homa kunamaanisha kuwa si homa kubwa sana. Ni ndogo tu. Angelisema ‘baba ana homa’, basi angelikuwa ni muwele wa kitandani anayepasa kuuguzwa na kujuliwa hali. Hapo ingelikuwa ni wajibu wa anayepewa taarifa hizo kwenda kumjulia hali wakati huo huo. Lakini ‘homa homa’ tu, anaweza kumwambia ‘Basi mpe salamu, mwambie nitampitia baadaye kidogo!”
Unayakumbuka maneno mangapi ya aina hii? Na je, nini tafauti yake pake yanapotumika bila kurejewa kama ulivyo mfano wa “sawasawa” na “sawa”, “homa” na “homa homa”?
Tuchangiane maarifa. Tukisemee Kiswahili.
asanteni kwa kutufunza kiswahili , ila ningependa muongeze mifano.