Mengi ya yaliyowahi kusemwa na wahenga wa Uswahilini hayakuwahi kusemwa mahala pengine na yanabeba maana nzito lau yakichambuliwa. Angalia huu msemo: “Mtenda jambo asishe ni kama asiyetenda.
Baba yangu (Mungu amrehemu) alikuwa akipenda kuutumia msemo huu kwangu. Mazingira ambamo msemo huu ukitolewa yalikuwa yakitafautiana kwa maana ya wakati, mahala na hali. Lakini kitu kimoja kilikuwa daima kinafanana: mara zote ilikuwa ni pale ambapo ningelikuwa na kazi ambayo nilishaianza na kisha nikawa nimeamua kuiwacha. Ingeliwezekana kuwa niliiwacha kwa kuchoka, kwa uvivu au kwa kuvunjika moyo. Ingeliwezekana kwamba pia niliiwacha kwa sababu ya kupata jengine la haraka na dharura kulifanya. Lakini hata ninapokuwa nimejipa moyo kwamba ningeimaliza siku ya pili yake au hapo baadaye, bado kauli ya baba yangu ilikuwa ile ile: “Baba, mtenda jambo asishe ni kama asiyetenda!”
Na mara nyingi alinikuta nikiwa nimeshindwa kuimaliza kazi hiyo katika wakati mwengine wowote, na hivyo yeye akawa mshindi nami nikawa nimeshindwa. Miaka mingi sasa baadaye, nikiwa mbali na mazingira ya nyumbani na nikiwa naishi kwenye mfumo tafauti kabisa wa maisha na ule ulionizaa na kunilea, bado msemo huu umekuwa na maana ile ile kwangu. Nilitendalo bila kulisha, huhisabu sikulitenda. Lolote ninalolifanya nusu nusu, basi kamwe silifiki mwisho wake.
Na nimegundua kwamba hili si kwangu tu, bali ndivyo tulivyo wengi wetu. Kwamba mtu anapokuwa ameanza kulifanya jambo fulani, halafu akalikatisha njiani, basi uwezekano wa kuliwacha kabisa jambo hilo ni mkubwa, na ama anapolirejea huwa analazimika kulianza mwanzo kabisa, kama vile huko mwanzo hajafanya chochote.
Baadhi ya wakati, jambo hilo linaweza kuwa limebakia kidogo tu kumalizika, lakini ule wakati unaovunjika moyo na kurudi nyuma, ndio muda unapopoteza kila kile ambacho umekitumia kwa jambo hilo – wakati, fedha na nishati yako. Muda unapoamua kurudi kulifanya tena, unakuta limeshapitwa na wakati, umeishiwa na fedha au pengine nishati na ule moyo wa kulitenda unakuwa haupo tena.
Ndipo misemo mingine kama ule wa kisiasa “Wakati ni huu”, “La leo lifanywe leo,” “Ngoja ngoja utakuta mwana si wako” “Chelewa chelewa utakosa kaa na gando,” na mengineyo – yote kwa pamoja – yanasema kitu kimoja: Mtenda jambo asishe ni kama asiyetenda.